"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, October 25, 2018

TUZIJARIBU HIZI ROHO.

Biblia inatuambia katika 2Timotheo 3:1 kwamba siku za mwisho kutakuwa na NYAKATI ZA HATARI SANA, na kama ni nyakati za Hatari tunapaswa tuchukue tahadhari kubwa zaidi kuliko hata za watakatifu waliokuwa wanaishi nyakati za kale kabla yetu, kwasababu biblia pia inasema shetani angali akijua kuwa muda wake ni mchache anafanya juu chini awaangushe wengi kwa njia yoyote ile. Mkristo ni kuwa makini huu sio wakati wa kuamini kila “roho” inayodai kuwa ni ya Mungu, biblia imetuonya na kutuambia,

1Timotheo 4:1 "Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani"
Sasa mambo ya duniani yanatufundisha nini?, kwamba tunajua hakuna mtu yeyote asiyependa kununua kitu kilicho katika uhalisia wake (original), na kama kitu hicho kitasifika kweli kuwa ni original basi hakitakosa kuwa na feki yake baada ya muda fulani,

Lakini utakuta kwa mwanzo kilipoanza kutolewa masokoni labda tuseme ni simu utaona kuwa karibia simu hizo zote zilikuwa ni original, lakini kwa jinsi siku zilivyokuwa zinazidi kwenda, kidogo kidogo utashangaa kuona feki chache zipo humo humo zikifanana kabisa na zile original, na kwa jinsi siku zitakavyozidi kuendelea kwenda, hata zile original huwa zinazidiwa na feki sokoni, Feki zinakuwa ni nyingi, na matokeo yake huuzwa kwa bei rahisi, na hizo ndio watu hupenda kuzikimbilia kwasababu ni bei nafuu..Lakini baadaye wanajikuta wanaangukia katika majuto pale wanapogundua kuwa hazidumu, halafu bado hazikidhi mahitaji yale ambayo aliyoyatarajia kuyaona kutoka katika hizo simu..

Na ndio hapo inampelekea mtu kuhangaika kutoka kwa fundi huyu hadi fundi yule,na kutumia gharama kubwa zaidi hata ya ile aliyoinunulia, akiona tatizo bado lipo anachukia kabisa kuwa na simu na kujuta ni kwanini alinunua simu na mwisho wa siku kuitupa..tatizo sio AINA YA ILE SIMU bali tatizo ni U-FEKI wa simu.

Kadhalika katika ukristo hakuna kitu ambacho shetani hajafanikiwa kukiundia feki chake, biblia inasema, anao wachungaji wa uongo (Yer 23:1), anao mitume wa uongo (2Kor 11:3), anao waalimu wa uongo, watumishi wa uongo na manabii wa uongo (2Petro 2:1). Kama vile tu Bwana alivyokuwa na watumishi wake wanaomtumikia, Sasa shetani kuwa na watumishi wa uongo tu haitoshi ni vema pia kujua hao watumishi wanamtumikia nani, au wanamtangaza nani, au wanamuhubiri nani?.

Kama vile tu mitume, wainjilisti, waalimu, na manabii wa Bwana walikuwa wanafanya kazi moja ya kumtangaza YESU KRISTO ili watu wote wamwamini yeye, kadhalika hawa nao wanafanya kazi moja ya kumtangaza “yesu” wao ambaye siye yule YESU tunayemwambudu wa kwenye maandiko, na wanafanya hivyo ili watu tu wamwamini huyo waangamie siku za mwisho.

Biblia ilishaweka wazi kabisa, kuwa yupo “yesu” mwingine, yupo “roho” nyingine, kadhalika ipo nayo “injili nyingine” ambayo sio ile Bwana aliyoitoa kupitia mitume wake watakatifu tangu mwanzo, soma

2Wakorintho 11:4 “Maana yeye ajaye akihubiri YESU MWINGINE ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea ROHO NYINGINE msiyoipokea, au INJILI NYINGINE msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye!”
Unaona hapo? Kazi ya hawa watumishi wa uongo ni kumtangaza yesu mwingine anayoonekana kama ni YESU halisi, na roho mwingine anayeonekana kama ni ROHO wa Mungu halisi ya Mungu na Injili nyingine ineyoonekana kama ni injili halisi ya Mungu lakini kumbe ni yesu-FEKI, roho-FEKI, na injili-FEKI. Lakini tunajua kitu feki kwa mwonekano wan je! ni ngumu kugundua kwasababu vyote vitaonekana kuwa ni sawa lakini utendaji kazi wake, na udumuji wake ndio vitakavyowatenganisha..wote watalijata jina la YESU katika shughuli zao za ibada, watatolea mapepo na kutabiri n.k..

Na ndio maana Bwana alisema mtawatambua kwa MATUNDA YAO, hicho tu!.

Mathayo 7.15-23 “ Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.
16 Mtawatambua kwa MATUNDA YAO. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?
17 Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya.
18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.
19 Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni.
20 Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.
21 Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?
23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu"
Ndugu kumbuka ili uwe na uhakika YESU uliyempokea katika maisha yako, ni HALISI, ni lazima ujiulize, JE! UNAUHAKIKA UMEOKOLEWA NA KUSAFISHWA DHAMBI ZAKO KWA DAMU YAKE?, Kiasi kwamba hata ukifa sasa bila shaka yoyote utakwenda mbinguni moja kwa moja?. Kwasababu kumbuka kiini cha Kristo kuja duniani mpaka kufikia hatua ya kuitoa nafsi yake sio wewe kuwa bilionea hapana bali ni suala la UKOMBOZI, je! wewe tangu umfahamu YESU, alishawahi kuyabalisha maisha yako, na kupata uhakika wa wokovu ndani ya nafsi yako?. Jana yako inatofauti na leo yako? Kama sivyo basi! Ujue ulimpokea YESU mwingine ambaye siye aliyehubiriwa na mitume.

Kadhalika unasema unaye ROHO MTAKATIFU, je! huyo Roho aliyeko ndani yako anakufanya kuwa MTAKATIFU kama jina lake lilivyo?, na Je! anakuongoza katika kuijua kweli yote kama maandiko yanavyosema (Yohana 16:13)?, na Je! anakushuhudia kila siku katika maisha yako kuwa wewe ni mwana wa Mungu?(Warumi 8:16). Kama sio basi ufahamu kuwa ulipokea roho nyingine ambayo sio ROHO MTAKATIFU. Kadhalika ulihubiriwa injili nyingine ambayo sio injili iliyohubiriwa na watumishi wa Mungu hao mitume (yaani biblia).

Na ndio maana hauwezi kudumu katika IMANI, ni kwasababu gani? Ni kwasababu hukumpokea Kristo HALISI katika maisha yako, leo unasimama kesho unaanguka, Huyo ni yesu mwingine ulimpokea asiyeweza kukupa wokovu wa uhakika katika maisha yako. Dhambi inakutawala, unashindwa kuitawala dhambi na bado unasema umeokoka, unashidwa KUJILINDA hapo ndugu hujaokoka, biblia inasema wote waliozaliwa na Mungu hawatendi dhambi, ikiwa na maana kuwa dhambi haiwatawali 1Yohana 5.18 “Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu HUJILINDA, wala yule mwovu hamgusi.”
Na ndio sababu huwezi kudumu katika imani kwasababu ni yesu-feki ulimpokea ukidhani ni BWANA YESU KRISTO. Kumbuka kazi ya Mungu haiwezi kuwa na kasoro, Kristo akimwokoa mtu kamwokoa kweli kweli wala habahatishi kwasababu msalaba una nguvu kuliko kitu chochote kilichowahi kusikika chini ya jua hili.

Ulikuwa hivyo ni kwasababu ulikuwa radhi kusikiliza injili isiyo ya gharama,(unayoweza kuipata sokoni muda wowote), ile ambayo manabii wa uongo wanayoifundisha kwamba unaweza ukawa ni mkristo bado pia ukawa ni wa kidunia, unaweza ukawa mkristo bado usijikane nafsi yako usiishe kama mitume walivyoishi kujikana nafsi zao, bado uwe unaishi maisha kama mfano wa watu wa ulimwengu huu na huku umeokoka, ukristo usioweza kuachana anasa, ukristo ambao unaruhusu mwanamke kuvaa suruali na vimini, pamoja na mawigi, na Kupaka lipsticks na wanja, ukristo unaosema Mungu siku zote ni wa rehema, hawezi kuwaangamiza watu wake aliwaumba hivyo ishi tu atakurehemu kwa neema zake maadamu umemkiri kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako inatosha.

Injili ambayo haina muda kusisitiza mtu kuishi maisha ya kujilinda roho yako kila siku, bali unasisitiza kila siku kuulinda mfuko wako. Ukristo unatoa tu mafundisho ya mafanikio ya kidunia na kupuuzia mafanikio ya kimbinguni..

Hizo zote ni INJILI nyingine zisizoweza kumwokoa mwanadamu, na zinatumia jina la “yesu” mwingine linalofanana na BWANA YESU KRISTO kuwatumainisha watu wajione kuwa wapo salama kumbe Kristo hawatambui!, Kinachowatambulisha kwamba wao sio WA-KRISTO ni matunda yanaonekana ndani ya maisha ya watu wanaowahubiria.

Ndugu shetani ni wa HILA tangu mwanzo, alimdanganya ADAMU na kufanikiwa. hashindwi kutundanganya sisi na kufanikiwa kama hatutathamini roho zetu. Tusijipe matumaini ya bure kwamba tumeokoka na huku maisha yetu hayauhakisi wokovu. Ukristo halisi sio rahisi kuupata kama vile kitu original kisivyo rahisi kukipata, Ukristo wa YESU KRISTO MWOKOZI wa ulimwengu una gharama zake.

Ikiwa umekubali kweli ayaokoe maisha yako dhamiria kweli kweli kutoka moyoni, kwamba upo tayari kumwishia yeye, kwa gharama zozote zile atakazokuambia, na yeye akishaona hiyo nia yako na utayari wako basi moja kwa moja ATAKUPA UWEZO WA KUFANYIKA MTOTO WA MUNGU (Yohana 1:12 Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;).

Sasa UWEZO huo wa kufanyika mtoto wa Mungu hauji kwa kila mtu tu ambaye anasema kampokea YESU bure bure, hapana bali unakuja kwa wale tu! waliodhamiria kwa dhati ndani ya mioyo yao kuanzia huo wakati na kwendelea kumwishia BWANA kwa gharama zozote zile, hapo ndipo yule Roho Mtakatifu sasa anaushusha huo uwezo, na hapo ndipo utakapoweza kuishinda dhambi na kudumu katika Imani ya YESU KRISTO BWANA wetu.

Ni maombi yangu kuwa ikiwa tunatamani kweli tuponywe roho zetu, basi tumtafute YESU HALISI, bila kukwepa vigezo vyote vitakavyoambatana na kumfuata yeye. Vinginevyo tutajikuta tumeangukia katika matumaini ya uongo ya manabii na watumishi wengi wa uongo ambao hawana huruma na hatma ya maisha ya mtu bali mambo ya ulimwengu huu tu, na katika siku ile tukajikuta tunaanza kumwambia Bwana mbona nilinena kwa lugha?, mbona niliongozwa sala ya toba?, mbona nilibatizwa? mbona nilikuona wewe kwenye maono? Na yeye atakwambia “Sikukujua kamwe; ondoka kwangu, wewe utendaye maovu”!!.

Ni hali gani utajisikia siku hiyo ukingundua kuwa ulimpokea yesu mwingine ambaye siye yeye HALISI?. Hizi ni nyakati za mwisho za HATARI mtafute YESU KRISTO wa kwenye Biblia, ambaye hasa lengo lake la kwanza ni kuigeuza roho yako kukupa uzima wa milele, na si kitu kingine.SIMAMA IMARA! BWANA ATAKUIMARISHA.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.

No comments:

Post a Comment