"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, October 19, 2018

MTETEZI WAKO NI NANI?

Mwinjilisti mmoja maarufu wa Marekani aliyeitwa Danny Martin, katika jitihada zake nyingi za kumtumikia Mungu siku moja usiku alijiona kwenye ndoto kwamba amekufa,na huko upande wa pili alijikuta yupo safarini kuelekea mbinguni, kwa mbali aliyaona malango makubwa sana, lakini alipokaribia mahali pale alisikia mtu mmoja akimwambia “Ni nani huyu anakaribia hapa?” Kwa ujasiri akajibu ni “mimi Martin Muhubiri wa Injili” lakini wale watu wakamwambia kabla hujaingia ndani subiri kwanza hapo mlangoni tuliangalie jina lako kama lipo kwenye KITABU au la!.

Hivyo walipoangalia na kulikosa wakasema “Jina lako halimo huku”…Lakini Danny akasema “Haiwezekani jina langu kukosekana humo mimi ni mtumishi wa Mungu” wale watu wakamwambia hiyo haijalishi ulikuwa nani duniani ukishafika hapa kama jina lako halipo huku, hatuna cha kukusaidia huwezi kuingia ndani ya malango haya ya mbinguni.

Ndipo Danny akawaomba wale watu wamsaidie afanye nini? Lakini wale watu wakamwambia sisi hatuwezi kukusaidia labda kama unataka kukata rufaa kwa Mungu mwenyewe katika kile KITI CHAKE CHEUPE CHA ENZI . 
Ndipo Danny akasema sina namna inanipasa nifanye hivyo. Basi wakamruhusu kuelekea mahali kilipo kiti cheupe cha Enzi cha Mungu, juu sana. (Anaeleza Danny) kwa jinsi nilivyokuwa ninizidi kuelekea juu ndivyo mwanga mkali ulivyokuwa unazidi sana, nilikuwa ninakwenda kwa haraka lakini ilinibidi nipunguze mwendo na baada ya muda kidogo nikasimama kabisa. Ndipo nikasikia sauti ikisema ni nani huyu anayekikaribia kiti changu cha hukumu cha haki?..Ndipo nikasema ni mimi Danny, mwinjilisti wa Kimarekani niliyevuna roho nyingi sana za watu kwako, lakini nilipofika getini wale walinzi walinizuia nisiingie.

Ndipo ile sauti ikamwambia “Vema mimi ninapenda haki”..”Mimi ninazo AMRI”..Je! Danny katika maisha yako yote hujawahi kusema uongo? . Danny anaelezea akisema “nilidhani mimi nimekuwa mtu mwaminifu siku zote lakini nilipofika mbele ya ule uwepo wa ajabu wa Mungu nilijiona kuwa kumbe sikuwa hivyo”..Ndipo nikasema …”Hapana Bwana nimekuwa nikisema uongo”…Akaniuliza tena…Danny ulishawahi kuiba?...Danny anasema: hapo nyuma nilidhani kuwa mimi ni mwaminifu sana lakini mbele zake siku hiyo niliona mapungufu mengi sana ndani yangu..Ndipo nikamwambia “Ndio Bwana nilishawahi kuiba”…

Akaniuliza tena, Danny ulishawahi kutenda dhambi?..Nikamjibu Ndio Bwana..

Akaniuliza..ulishawahi kufanya hivi, ulishawahi kufanya vile?.....Nikasema Ndio Bwana nilishafanya..

Danny anazidi kuelezea ( wakati huo nilisikia kama mifupa yangu inachomoko kwenye maungio yangu, nikitazamia tu kusikia lile neno Bwana alilolisema katika Mathayo 25: Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake;))..

Lakini muda huo wakati nayatazamia hayo yafuate nyuma yangu nilisikia sauti nzuri ya unyenyekevu na ya kupendeza,ikizungumza na nilipogeuka nikaona sura nzuri ya tabasamu ambayo sikuwahi kuiona hapo kabla katika maisha yangu..Akasema:

Baba ni kweli Danny kwa bidii zake alijitahidi kufanya kilicho kizuri japo alishindwa, lakini kipo alichokifanya alipokuwa duniani, yeye alitia juhudi zote kusimama kwa ajili yangu Hivyo mimi nami nipo hapa kusimama kwa ajili yake.
Ndugu yangu Je! Bwana hakusema? Katika Luka 9: 9.23 Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.
24 Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha.
25 Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?
26 KWA SABABU KILA ATAKAYENIONEA “HAYA” MIMI NA MANENO YANGU, MWANA WA ADAMU ATAMWONEA HAYA MTU HUYO, ATAKAPOKUJA KATIKA UTUKUFU WAKE NA WA BABA NA WA MALAIKA WATAKATIFU.
Ipo siku imbayo Bwana atatukiri mbele za Baba yake, pia ipo siku ambayo Bwana atatukana mbele za Mungu.

Leo hii tunamwoneaje Kristo HAYA?. Ni pale tunapokataa kujikana nafsi zetu kwa Kristo kila siku, pale tunapoambiwa tutubu tukaoshwe dhambi zetu sasa wakati muda angali bado upo lakini sisi tunaona kama siku tukiwa hivyo watu watatuona kama washamba, pale unapoona siku ukiwa mkristo, pombe hutakunywa tena, pale unapoona siku ukiwa mkristo disco hutakwenda tena, unapoona siku ukiwa mkristo uasherati hutafanya tena, pale unapoona siku ukiwa mkristo kampani zako mbovu hutaongozana nazo tena, unakataa kufanya hivyo sasa kwasababu unaupenda ulimwengu kuliko Mungu…Hapo ni sawa na kumwonea HAYA Kristo na maneno yake. Biblia inasema katika 1 Yohana 2 “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.”

Ndugu kama ukifa leo hii utaenda kuwa mgeni wa nani huko? Ni nani atakayesimama huko kukutetea mbele ya kile kiti cheupe cha hukumu cha Mungu?. Bwana anasema KWA SABABU KILA ATAKAYENIONEA “HAYA” MIMI NA MANENO YANGU, MWANA WA ADAMU ATAMWONEA HAYA MTU HUYO, ATAKAPOKUJA KATIKA UTUKUFU WAKE NA WA BABA NA WA MALAIKA WATAKATIFU.

Unakataa kuchukua msalaba wako sasa umfuate Kristo, kwasababu unajua ukristo hauhitaji mwanamke anayevaa nguo zinazoshora maungo, na suruali, unajua mwanamke wa kikristo havai mapambo ya kikahaba na kiasherati, unaogopa utaonekana wa kale, hivyo unaona ni bora uwe vuguvugu, huko ni kumwonea HAYA KRISTO. Ni kweli leo utafanikiwa kukwepa hayo kwa kitambo sasa lakini siku ile ambayo utasimama kwa nafsi yako, mahali ambapo utahitaji mtetezi utakosa, utagundua kuwa ulivyoipenda nafsi yako wakati ulipokuwa duniani ndivyo ulivyokuwa unaipoteza, na siku hiyo ndiyo utagundua kuwa Bwana hakudanganya alivyosema “”Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha.

Ndugu yangu maisha haya yanapita, unatafuta mali kupita kiasi unamsahau Mungu muumba wako, unapendezwa na mambo ya ulimwenguni hata muda na Mungu wako huna, kuna siku itafika utamuhitaji sana Kristo awe mtetezi wako lakini yeye atasimama kando asikujibu lolote kwasababu hataona la kukujibu, Badala yake atakukana na kusema sikujui wewe. Utajisikiaje siku hiyo?, mbele ya mahakama ya haki ya Mungu?

Hizi ni nyakati za hatari biblia ilizozisema, ni heri ujisalimishe kwake, kwa hii miaka sabini themanini uliyopewa hapa duniani kuliko ukawe na majuto ya milele baada ya kufa. Isikie sauti ya YESU KRISTO leo na usiyaonee haya maneno yake. Anza maisha yako upya uchukue msalaba wako sasa umfuate, uwe radhi kuipoteza nafsi yako kwa ajili yake ili uwe na uhakika siku zinazokuja kwamba utaipata kuliko kuipata sasa kwa anasa na raha za kitambo za dunia kisha siku ile uipoteze milele.

Tubu dhambi zako muda huu, na ikiwa bado hujabatizwa katika ubatizo sahihi wa maji tele katika JINA LA YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako,(kulingana na matendo 2:38,8:16, 10:48 na 19:5 na Mathayo 28:19) fanya bidii ufanye hivyo, naye Mungu aliyemwaminifu atakugawia kipawa cha Roho Mtakatifu. Ili uwe na uhakika wa kuzaliwa mara ya pili.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali wape ujumbe huu na wengine.

Kwa mpangilio mzuri wa masomo haya tembelea website yetu >>> www.wingulamashahidi.org

No comments:

Post a Comment