Moja ya dhambi zinazowaangusha wengi ni “kutokusamehe”. Na hii inatokana mara nyingi na kutokuelewa nini maana ya msamaha. Ni rahisi kujilazimisha kusamehe lakini kama msamaha haujatoka ndani basi huo sio msamaha.
Ili kuelewa vizuri, tuchukue mfano una mtoto mdogo labda wa umri wa miaka 6 hivi, ukamkuta siku moja kachukua takataka kaweka ndani ya Friji, kwa namna ya kawaida ni lazima utakasirika na kuamua kumuadhibu ili kwamba siku nyingine asirudie...lakini je! Baada ya kumwadhibu utamwekea kinyongo?..Ni wazi kuwa hutamwekea kwasababu unajua ni mtoto tu! Laiti angefikia umri Fulani wa kujielewa asingefanya hivyo. Kwahiyo unamsamehe tu! Kwasababu unaelewa ni utoto tu ndio ulio ndani yake! Ndio unaomsumbua. Huwezi kwenda huku na kule na kwenda kutangaza kila mahali kwamba mwanao ni mbaya na kuanza kumchukia na kumwekea uadui.
Sasa usingeweza kuamua kumsamehe kabisa kutoka ndani ya moyo wako kama usingeelewa sababu ya kina ya yeye kufanya vile. Na ulipogundua kwamba sababu ni UTOTO ndipo ulipoamua kumsamehe kabisa kabisa.
Kadhalika tunapokuwa wakristo hatuwezi kusamehe watu wanaotuudhi au wanaotufanyia ubaya kutoka ndani ya mioyo yetu,kama hatutaelewa sababu ya wao kutufanyia huo ubaya ni ipi.
Leo tutajifunza sababu kubwa ya watu kutufanyia ubaya, au kutuudhi, au kutuumiza, au kutupangia mabaya, au kutuonea au kutufanyia chochote kile ambacho hakistahili kufanyiwa. Ambayo ukiielewa hiyo itakufanya uweze kumsamehe mtu kutoka ndani ya moyo wako kabisa.
Na sababu hiyo si nyingine zaidi ya DHAMBI ndani ya Mtu.
Mtu yoyote ambaye hajampa Bwana Yesu maisha yake, anakuwa ni milki ya shetani asilimia 100, Na kama anakuwa ni milki ya shetani, tunajua matunda ya shetani ndani ya mtu, ni yapi, Mwovu akiwa ndani ya mtu, Yule mtu lazima atakuwa ni mtu wa chuki, ni lazima atakuwa ni mtu wa kiburi, ni lazima atakuwa ni mtu wa hasira, ni lazima atakuwa ni mtu wa matusi, ni lazima atakuwa mtu wa kujipenda mwenyewe na kujijali nafsi yake, na kujiona yeye ni bora kuliko mwingine,ni lazima atakuwa ni mtu wa mashindano, ni lazima atakuwa mtu wa shari siku zote, mtu wa majivuno na wa dharau, na wakati mwingine atakuwa hata muuaji, n.k Kwa ufupi tabia zote mbaya ambazo zinajulikana zitakuwemo ndani ya huyo mtu ambaye hajampa Kristo maisha yake.
Sasa kama vile mtoto anapokosa, moja kwa moja unaelewa kabisa tatizo la Yule mtoto ni UTOTO uliopo ndani yake na laiti kama angekuwa mtu mzima asingefanya vile, Vivyo hivyo mtu yoyote ambaye hajampa Yesu Kristo maisha yake anapokutendea ubaya, anapokuonea wivu, anapokutukana pasipo sababu, anapokudharau, anapotafuta kukuangusha, anapokutegea mitego ya kila aina ili uanguke, anapokuchukia bure, anapokusengenya huku na huku, anapokuonea hasira, anapokuumiza kwa njia yoyote ile n.k Unapaswa uelewa kwamba tatizo sio yeye bali ni DHAMBI iliyo ndani yake, unapaswa uelewe laiti angekuwa Mkristo kweli kweli kama wewe asingefanya vile, laiti angekuwa amempa Bwana maisha yake asingekuwa na chuki,asingekulaani,asingekutukana, asingekuonea wivu n.k...
hivyo sio yeye bali ni ile dhambi iliyo ndani yaki, Kama vile unavyoielewa hali ya mtoto mdogo anapofanya kosa vivyo hivyo unapaswa uielewa hali ya Mtu asiye ndani ya Kristo anapokukosea.
Ndio maana pale Kalvari Bwana Yesu hakutusamehe sisi kwasababu tu aliamua kutusamehe, au alituvumilia,hapana! bali alitusamehe kwasababu alijua hatujui tutendalo, Alijua laiti tungemjua yeye ni nani kwa wakati ule Tusengelimsulibisha pale msalabani. Alijua laiti tungefunguliwa macho yetu tusingefanya yale mambo...Hivyo alitusamehe katoka ndani ya moyo wake kabisa.
Sasa ukishindwa kuelewa haya, utajikuta kila mtu anakuwa adui yako, utashinda kuelewa tofauti ya mtu aliye ndani ya Kristo na mtu asiye ndani ya Kristo, utajikuta unakesha katika maombi ya kuangamiza maadui zako, utajikuta na wewe unaanza kulipiza mabaya badala ya mema. Utajikuta na wewe shetani amekuingia unaanza kuwa na chuki, unaanza kuwa msengenyaji, unaanza kulipiza visasi n.k
Hakuna sababu ya mtu kuwa adui yako, anapokutukana, hakuna sababu ya mtu kuwa adui yako anapokusengenya, hakuna sababu ya mtu kuwa adui yako anapokuchukia, hakuna sababu mtu kuwa adui yako anapokusaliti, hakuna sababu mtu kuwa adui yako anapokutendea ubaya wowote ule, kwasababu unaelewa kabisa kwamba tatizo sio Yule mtu, TATIZO NI DHAMBI ILIYOPO NDANI YAKE, laiti angekuwa mkristo kweli kweli asingefanya vile, hivyo unachopaswa kufanya ni kuchukua hatua ya wewe kumwombea Bwana ampe wokovu ile Dhambi hizo ziondoke ndani yake, lakini sio kushindana naye...Kwasababu ukishindana naye huwezi kumbadilisha kuwa kama wewe, wala hawezi kuvutiwa na kile kilichoko ndani yako. Suluhisho pekee ni kumwombea Rehema na Neema mbele za Mungu.
Ndugu jifunze kusamehe kutoka ndani ya moyo, kwa kuelewa hali ya mtu aliyopo. Kama kuwa na maadui hakuna mtu aliyekuwa na maadui kama Bwana wetu Yesu Kristo, na maadui zake namba moja tulikuwa ni mimi na wewe. Tulimtemea mate...je! wewe katika maisha yako ulishawahi kutemewa mate kama yeye?.. tulimtukana na kumdhihaki, na zaidi ya yote tukampeleka msalabani na kumwaibisha..je! wewe katika maisha yako ulishawahi kuaibishwa hivyo? Lakini yeye hakuwahi kutuita sisi maadui zake.. zaidi sana alisema “Baba wasamehe kwa kuwa hawajui watendalo” na zaidi ya yote akatuita sisi tuliokuja kumwamini baadaye rafiki zake.
Kama Bwana Yesu alitusamehe madeni makubwa kama hayo, unadhani sisi tunapaswa tuwafanyieje wanaotukosea?..tunapaswa tufanye zaidi ya hapo. Bwana alisema mwenyewe kwamba sisi tusipowasamehe waliotukosea hata Baba yetu wa mbinguni hatatusamehe makosa yetu. Ikiwa na maana kuwa kama kuna mtu yoyote ambaye hatujamsamehe kwa dhati kabisa kutoka ndani ya mioyo yetu, na sisi hatutasamehewa dhambi zetu, hivyo ni ziwa la moto litakuwa linatungoja, na Kristo hawezi kuzungumza uongo.
Ndugu yangu, epuka maombi yakupiga maadui zako, epuka kupeleka mashtaka mabaya mbele za Mungu juu ya watu wanaokuudhi, au kukuumiza, usimtaje ndugu yako kwa ubaya mbele za Mungu, wala usimtakie shari, bali mwombee rehema..ili atubu awe mkamilifu, Biblia inasema katika
Mithali 24: 17 “Usifurahi, adui yako aangukapo; Wala moyo wako usishangilie ajikwaapo; Bwana asije akaliona hilo, likamkasirisha; Akageuzia mbali naye hasira yake”.
Unaona? Hapo Bwana hafurahii, kuanguka kwake mtu mwovu, wala hafurahii mashataka mabaya tunayompelekea dhidi ya watu wengine, maombi tunayopaswa kuomba mbele zake ni Bwana atuepushe na madhara yao lakini sio awapige, au awaue, au awalaani. Adui yetu mkubwa ni shetani na sio watu.
Ni maombi yangu kuwa Bwana atakupa Moyo wa Rehema na Toba dhidi ya ndugu wanaotukosea.
Ubarikiwe sana.
Tafadhali “Share” ujumbe huu kwa wengine
Tembelea pia tovuti yetu hii >>> www.wingulamashahidi.org
No comments:
Post a Comment