"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, October 26, 2018

TAFUTA KUJUA MAMBO YAJAYO:

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, aliye Mfalme wa wafalme, na mkuu wa uzima, libarikiwe!

Karibu tujifunze Neno la Mungu, leo tutajifunza umuhimu wa kutaka kutafuta kujua mambo yajayo, Kwasababu biblia inasema katika..
Mathayo 7: 7 “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;
8 KWA MAANA KILA AOMBAYE HUPOKEA; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa’.
Umeona! Bwana amesema kila aombaye hupokea, na kila atafutaye ataona ikiwa na maana kwamba, chochote mtu atakachokihitaji kama akikitafuta kwa bidii atakipata, kama atakitamani na kukihangaikia kwa bidii atakipata, na sheria hiyo haipo tu kwa wakristo bali hata kwa watu wasio wa Kristo, na viumbe vyote mtu yeyote hata asiye mcha Mungu akiamua kutafuta kitu chochoe katika ulimwengu huu kwa bidii atakipata tu! kwasababu ndivyo ilivyo “kila atafutaye atapata”…

Lakini leo hatuzungumzii namna ya kutafuta vitu vya ulimwengu huu, kwasababu Bwana Yesu mwenyewe alisema…”itatufaidia nini kuupata ulimwengu mzima na kupata hasara ya nafsi zetu ?”

Akimaanisha kuwa tusiwekeze nguvu zetu kubwa kutafuta mambo ya ulimwengu huu yanayopita badala yake tuwekeze nguvu kubwa kutafuta kujua mambo ya ulimwengu ujao yasiyoweza kuharibika. Na sheria ni ile ile kwamba “tukitafuta kwa bidii tutapata”

Lakini kama tunavyojua zipo gharama za kutafuta kitu, katika maisha ya kawaida hakuna mtu yeyote anayetafuta elimu ya kidunia katika hatua za awali akajihusisha na mambo ya ulimwengu huu, kwanza kabisa wengi wa wazazi huwa wanawapeleka watoto wao shule za bweni, na shuleni kule wanazuiliwa kuwa na vitu vyovyote vitakavyoweza kuathiri taaluma ya watoto wao, ndio hapo mwanafunzi atazuiliwa kuwa na simu, redio, atazuiliwa pia kuwa mzururaji, zaidi ya yote atazuiliwa hata kuingia jikoni,au kujishughulisha na kazi yoyote ya kujipatia kipato, yeye kazi yake iliyompeleka pale ni moja tu!! yaani kutafuta elimu. Kwahiyo waalimu wanafahamu endapo mwanafunzi akijihusisha na mojawapo ya mambo hayo, wanajua kabisa mwanafunzi yule hatapata kile alichoenda kukitafuta pale.

Hivyo analazimika kufungiwa shuleni, ananyimwa uhuru kwa asilimia kubwa, anakuwa ni sawa na kama yupo gerezani hivi, ananyimwa kujihusisha na mahusiano yoyote yale,tena wakati mwingine analazimika kupelekwa shule ya jinsi moja tu! isiyo ya mchanganyiko, Na zaidi ya yote kama mwanafunzi yule anajielewa atazidi kujiweka kwenye utumwa mwingine ulio mkali zaidi ya ule, ndio hapo masaa yake mengi atatumia kusoma hata ya usiku wa manane, muda anaolala utakuta ni masaa machache sana…ataendelea kwenye hicho kifungo kwa muda wa miaka kadhaa akitafuta tu! kilicho bora na hatimaye atakipata! Lakini je! asingeingia gharama za kuingia kwenye hicho kifungo kikali na cha kijitaabisha hivyo je! angekipata kilicho bora??

Ndio maana Bwana Yesu alisema katika Mathayo 17: 21 “[Lakini namna hii haitoki ila kwa KUSALI NA KUFUNGA.]”

Unaona hapo aliposema kufunga hakumaanisha kuacha kula tu! bali alimaanisha kuacha kujishungulisha na mambo mengine ya kando ambayo yanaweza kuathiri kile kitu unachokitafuta. Hiyo ndio maana ya “kufunga” Kama vile mwanafunzi anavyofunga kwa kujizuia na mambo mengi ili apate anachokitafuta, anafunga kuwa mzururaji, kumiliki simu, kuangalia tv n.k

Mfano mzuri tunaweza kujifunza kwa kiumbe kama kuku, yeye atakapofika wakati wa kuyahatamia mayai yake, analazimika kufunga siku 21, lengo la yeye kufunga sio kwasababu anataka kuutesa mwili wake bila sababu, au kwasababu kapewa masharti ya kufanya hivyo, au kwasababu anatimiza wajibu Fulani, hapana bali ni kwasababu anajua endapo akienda kutembea huko na huko yale mayai aliyokuwa akiyahatamia yatapoteza lile joto na hivyo kuwa viza, na aambulie kutoata kile alichokuwa anakitafuta.

Kadhalika na tunapoutafuta ufalme wa mbinguni, tunapaswa tufunge! Na kufunga sio kuacha kula tu, hiyo ni moja, maana kuu pale ya kufunga ni tunatakiwa tufunge mambo ya ulimwengu huu yanayotuzuia tusifikie malengo yetu, kama vile kuku anavyolihifadhi joto lake kwa siku 21 kwa uvumilivu wote, na sisi vivyo hivyo tunapaswa tulihifadhi joto letu, kwa Roho Mtakatifu tuliyepewa kwa kipindi chote tunachoishi hapa duniani, Bibli inasema katika Luka 12: 35 “taa zenu ziwe zinawaka;…nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao,” hivyo tunapaswa tufunge uasherati, tufunge anasa, tufunge kiburi, tufunge kuzurura huku na kule kutafuta mambo ya ulimwengu huu yanayoharibika na utafutaji wa mali uliopitiliza…zaidi tuelekeze macho yetu mbinguni..kwasababu muda uliobaki ni mchache sana.

Kadhalika na maana ya kusali pia sio tu kujifungia ndani tu, na kupeleka mahitaji mbele za Mungu, hapana ni zaidi ya hapo, maana ya kusali pamoja na kupeleka mahitaji yetu na haja zetu mbele za Mungu ni kukaa katika uwepo wa Mungu muda mrefu ukitafuta kujua na kujifunza huku na kule kuhusu mahali ulipotoka, ulipo sasa na unapoeleka. Hiyo ndio maana ya sala.

Kaka/Dada tafuta mambo yajayo kwa “KUFUNGA NA KUSALI” wafunge marafiki wasio na maana wanaokuvuta katika mambo ya ulimwengu huu, ni afadhali uwe peke yako lakini unaenda mbinguni kuliko kuwa miongoni mwa kundi kubwa linalokwenda Jehanamu ya moto. Rafiki anayekudharau wewe unapomtafuta Mungu au anayekushauri namna ya kumtafuta Mungu wakati yeye mwenyewe hamtafuti ni Mlevi, msengenyaji, mla rushwa huyo atakupeleka jehanamu, tangu lini kipofu akamwongoza kipofu mwenzake? Bwana Yesu alisema wote watatumbukia shimoni..

Dada unayesoma hapa usipotaka kufunga mambo ya ulimwengu huu na kutazama macho yako..usipotaka kufunga uvaaji mbaya, usipotaka kufunga uvaaji wa mawigi, na kupaka wanja na lipstick, usipotaka kufunga usengenyaji wako, usipotaka kufunga tamaa za kuwa maarufu kama wanawake wa ulimwengu huu Kristo atakapokuja hutajua chochote…Hebu jifunze kwa mwanamke Ana wa kwenye biblia aliyefunga mambo yake yote na kuamua kutazama na kutafuta mambo yanayokuja ya mbinguni..

Mwanamke Ana, alifiwa na mume wake akiwa na umri mdogo, na akaamua kutokuolewa tena akafunga mambo yote na kuanza kujishughulisha katika kutafuta mambo yanayokuja tu…Wakati huo Masihi (Yesu Kristo) bado alikuwa hajazaliwa, lakini kwa jinsi alivyokuwa anatia bidii kutafuta sana…Bwana akamfunulia MAJIRA YA KUJA KWAKE, akashuhudiwa kumwona Bwana uso kwa uso. Hivyo wakati wakuu wa dini, hawajui majira ya kuzaliwa Bwana, Mwanamke Ana tayari alikuwa anajua kalenda ya Mungu. Wakati wanawake wengine wanafurahia fashioni za ulimwengu mwanamke Ana, alikuwa anajua Kristo yupo mlangoni kuja ulimwenguni. Tunasoma habari hiyo katika..
Luka 2:36 “Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake.37 Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana KWA KUFUNGA NA KUOMBA.38 Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake”
Na mambo haya haya yatatokea katika siku hizi za mwisho, wakati wewe dada unaendelea kujifurahisha na mambo mabovu ya ulimwengu huu, wapo wanawake wenzako mahali fulani Bwana ameshawapa kalenda yake ya kurudi kwake mara ya pili, wakati wewe unasema Kristo haji leo wala kesho wapo wanawake wenzako mahali Fulani ambao dunia inawaona washamba leo, wanazungumza na Bwana uso kwa uso, na wameshuhudiwa mambo mengi.

Kadhalika ndugu unayesema Kristo, haji leo wala kesho, hivyo ni wakati wa kuishi unavyotaka, ni vizuri ukafahamu kuwa ni maelfu wanaowaza kama wewe, lakini wapo wachache wanaofahamu nyakati za kujiliwa kwao, wapo wachache ambao wameamua kweli kufunga mambo ya ulimwengu huu na kuamua kumtafuta muumba wao, ambao tayari wameshapewa kalenda yote ya kurudi kwa Bwana..wakati ulevi wako unastawi, rushwa yako inastawi, kiburi chako kinastawi, anasa zako na uasherati wako unastawi..wenyewe wanainua vichwa vyao juu wakiitazama jinsi ile siku inavyokaribia…

Jifunze kwa Simeoni ndugu yangu, mtu aliyeishi wakati mmoja na mwanamke ANA, yeye naye Roho alimshuhudia kwamba hatakufa hata atakapomwona Kristo akifika ulimwenguni.. Wakati dunia nzima haielewi chochote..Tunayasoma hayo katika..

Luka 2:25 “Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu MWENYE HAKI, MCHA MUNGU, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake.
26 Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana.
27 Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria,
28 yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema,
29 Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema;
30 Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako,
31 Uliouweka tayari machoni pa watu wote;”

Ni maombi yangu kuwa Bwana ataigeuza nia yako na mtazamo wako kuanzia leo na kuendelea, uanze kutamani kujua mambo yajayo, Roho yule yule aliyemfunulia ANA na SIMEONI kuja kwake, mara ya kwanza, Roho huyo huyo anaweza kuyafunua macho yako leo ukaona jinsi kuja kwake mara ya pili kulivyo karibu, endapo tu utakusudia KUFUNGA mambo yote ya ulimwengu na kujitenga kumtafuta Mungu kama Ana na Simeoni.

Kama hujampa BWANA YESU maisha yako, ni vizuri ukafahamu kuwa Hakuna Uzima nje ya yeye, wasanii maarufu wamepita, maraisi washupavu wamepita,.Raisi tu wa Marekani aliyemaliza muda wake, leo hii umeshaanza kumsikia anafifia lakini huyu YESU mpaka leo hii anatangazwa, habari zake hazichakai na ndivyo ilivyo kwa wale wote wanaomcha yeye, hivyo nakushauri kama hujampa maisha yako, tubu leo na ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo upate ondoleo la dhambi zako nawe utakuwa na uhakika wa uzima wa milele.

Mungu akubariki.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na Bwana akuongezee Neema yake.

No comments:

Post a Comment