"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, November 1, 2018

IKO NJIA IONEKANAYO KUWA SAWA MACHONI PA MTU.

Mwanzoni kabla sijaokoka nilidhani ndani ya moyo wangu kuwa Mungu hataweza kunihukumu mimi, nilidhani ndani ya moyo wangu kuwa ijapokuwa ninamuudhi Mungu sasa lakini mwisho wa siku ataniokoa tu, kwasababu mimi sina dhambi nyingi zaidi ukilinganisha na watu kama wauaji, na wachawi, nilidhani kuwa pombe nilizokuwa ninakunywa kwa kiasi sizingeweza kuniletea madhara makubwa kiasi cha kutupwa jehanum kama wale wanaokuwa walevi wa kupindukia, uasherati niliokuwa ninafanya na disco nilizokuwa ninakwenda zisingekuwa ni kosa kubwa sana kunifanya mimi niangamizwe kabisa mfano wa wale wanaoigiza mikanda ya ngono.

Nilidhani kuwa matusi niliyokuwa ninatukana Mungu atayafumbia macho siku ile kwasababu Mungu ni wa rehema atanirehemu, kadhalika usengenyaji niliokuwa ninauzungumza niliona pia ni hali tu ya kibinadamu kwamba kila mtu huwa anafanya hivyo, kila kitu niliona kama si dhambi sana, nusu nusu maadamu mimi simdhulumu mtu, siui, wala siendi kwa waganga, isitoshe mimi ni mkristo na nina dhehebu langu, ninawapa kitu maskini hiyo inatosha,Mungu kunihurumia katika siku ile .

Sikuwa najali sana habari za Mungu, niliona kukaa hapo katikati ni sawa tu niliona kama YESU ni kitu cha ziada katika maisha yangu lakini sio msingi wa maisha yako. Hayo yote yalikuwa ndani ya moyo wangu Mpaka siku Bwana alipokuja kuniokoa kwa neema zake, na kunifungua macho ndipo nilipogundua kuwa nilikuwa katika hali ya HATARI SANA pasipo kujijua.
Biblia ipo wazi kabisa inasema;


Mithali 14: 12 Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.
        


Ni wazi kila mtu ndani ya nafsi yake ataona kuwa kile anachokifanya au anachokiamini kuwa ni sawa hata kama watu wengine watakiona vipi, mwingine ataona kuwa kushika amri kumi tu za Mungu inatosha, hakuna haja ya kumjua Kristo YESU, mwingine ataona kunywa pombe huku upo kwenye dini yako ni sawa tu!. Mungu atasema Mungu haangalii nje anaangalia vya ndani hivyo kuvaa vimini, na suruali kwa mwanamke wa kikristo sio tabu, Mwingine atasema mimi naamini hakuna ziwa la moto bali tukifa tunapotea tu, mwingine atasema tukifa tunakwenda kwanza toharani kisha mbinguni baadaye, mwingine atasema kusaidia tu yatima na wajane na kuishi maisha ya kujitunza hiyo inatosha kukupeleka mbinguni. Mwingine atasema mambo ya Mungu yametungwa hakuna kitu kama hicho fanya biashara tengeneza pesa enjoy maisha siku ukifa umepotea hakuna maisha baada ya kifo..n.k. Kila mtu akiwa na mawazo yake mwenyewe moyoni akijitumainisha kuwa ni sawa..

Biblia inaendelea kusema.



Yeremia 17: 9 “MOYO HUWA MDANGANYIFU KULIKO VITU VYOTE, UNA UGONJWA WA KUFISHA; NANI AWEZAYE KUUJUA? 10 Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.”

Unaona hapo, shetani ni mdanganyifu, lakini MOYO wako ni mdanganyifu zaidi ya shetani. Kwasababu shetani naye hakuwa na mtu wa kumdanganya kabla yake bali moyo wake ndio uliomdanganya, vivyo hivyo na wewe pia kinachokudanganya kwanza ni moyo wako kisha baadaye shetani atakusaidia kufanya hivyo. Na ndio maana biblia inazidi kusisitiza na kusema katika Mithali 4: 23 LINDA MOYO WAKO KULIKO YOTE UYALINDAYO; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.
Kaka/Dada haijalishi ni kitu gani unachokiamini kuwa ni sawa, haijalishi unajiona upo katika njia iliyonyooka kiasi gani, haijalishi ni sifa gani umeipata mbele za watu kwa matendo yako mema na ya kiasi, lakini Neno la Mungu na kanuni za Mungu zitabakia kuwa pale pale, Biblia inasema katika,


Yohana 14: 6 Yesu akamwambia, MIMI NDIMI NJIA, NA KWELI, NA UZIMA; MTU HAJI KWA BABA, ILA KWA NJIA YA MIMI.

Usidhani kuwa dini inatosha, yupo aliyekuwa mtu wa dini na kushika amri zote lakini hakuwa na uzima ndani yake unaotoka kwaYESU KRISTO peke yake. Tunamsoma huyo katika

Mathayo 19: 16

“Na tazama, mtu mmoja akamwendea akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ILI NIPATE UZIMA WA MILELE? 17 Akamwambia Kwani kuniuliza habari ya wema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri.
18 Akamwambia, Zipi? Yesu akasema, Ni hizi, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo,
19 Waheshimu baba yako na mama yako, na, Mpende jirani yako kama nafsi yako.
20 Yule kijana akamwambia, Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena?
21 Yesu akamwambia, UKITAKA KUWA MKAMILIFU, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; KISHA NJOO UNIFUATE.
22 Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
23 Yesu akawaambia wanafunzi wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni.
24 Nawaambia tena, Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.

Kadhalika aliwaambia mafarisayo na masadukayo wale washika dini maneno haya:


Yohana 8:24 "kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu.”


Unaona hapo? Usikubali kuuruhusu moyo wako kukudanganya kuwa YESU hana umuhimu sana katika maisha yako, usiruhusu kuona njia zako kuwa ni sawa mbele za Mungu na huku bado haujasafishwa dhambi zako katika damu ya YESU KRISTO. Leo hii unaweza ukawa na ujasiri mwingi na kiburi kingi cha kujiona hivyo, lakini ngoja siku utakayokaribia kufa hapo ndipo utajiona kuwa wewe si kitu, unahitaji uzima ndani yako na wakati huo utakuwa umeshachelewa.


Ni maombi yangu usitumainie akili zako kukuongoza popote katika njia za uzima, usitumainie nguvu zako, usitumainie elimu yako, usitumainie matendo yako, usitumainie uzuri wako, usimtumainie mwanadamu, usitumainie kile unachoamini bali tumainia kile Mungu anachosema kuwa kitakuokoa hiyo ndio salama yako ndugu. Siku ile kutakuwa na majuto makubwa sana pindi utakapogundua moyo wako ulikudanganya, kuupinga wokovu unaopatikana katika YESU KRISTO peke yake.
Huu ni wakati wa kubadili mwelekeo wa njia zako, na kukubali kuitii INJILI, Bwana Yesu anasema

Yohana 6:44 Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho.

Unaona hapo wote walio nje ya neema wapo katika giza, na wewe usitie moyo wako ugumu ukaipinga hiyo sauti inayokuita UOKOKE, kwasababu hiyo ni sauti ya neema ili umwendee akupe uzima wa milele, sio wote watakoikubali isipokuwa wale waliochaguliwa na Mungu tangu kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu. Leo hii uwe nawe mmojawapo kwa kuitii, Inawezekana ulisharudi nyuma, au haukutambua umuhimu wa YESU maishani mwako, leo anza upya.
Mithali 28: 13 Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.

Tubu sasa kwa kumaanisha kabisa kuacha dhambi zako mbele zake YESU KRISTO, Kisha baada ya kufanya hivyo hatua inayofuata upaswa ukabatizwe katika UBATIZO SAHIHI kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako. Kumbuka wale wote walio nje ya Kristo hawana ondoleo la dhambi zao, hata iweje. Hivyo ili kuukamilisha wokovu wako unapaswa ukabatizwe kwa maji mengi na uwe ni kwa jina la YESU KRISTO, kama ulibatizwe ubatizo mwingine nje ya hapo pasipo kujua ni batili unapaswa ukabatizwe tena, kisha Bwana mwenyewe atakupa Roho wake mtakatifu kuanzia huo wakati na kuendelea atakayekupa uwezo wa kushinda dhambi. Na hapo utakuwa umeuokolewa mwenye tumaini la uzima wa milele. Kisha Damu ya YESU Kristo ndipo itaanza kunena mema juu ya maisha yako.

Hizi ni siku za mwisho YESU KRISTO yupo mlangoni kurudi, usiruhusu njia za udanganyifu wa mali zikakusonga usiufuate uzima ulio kwa BWANA YESU.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.


Ukiwa umetubu na unautahitaji wa kubatizwa, tuwasiliane kwa namba hizi 0679804471.

No comments:

Post a Comment