"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, November 1, 2018

NGUVU YA MUNGU YA UUMBAJI

Katika kitabu cha mwanzo tunasoma, baada ya Bwana Mungu kuumba mbingu na nchi na viumbe vyote alistarehe siku ya saba, biblia inasema hivyo katika..

Mwanzo 2: 1 “Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. 2 Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. 3 Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya. 4 HIVYO NDIVYO VIZAZI VYA MBINGU NA NCHI ZILIPOUMBWA. Siku ile Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi”.


Lakini kuna mambo kadhaa ya kujiuliza kuhusu uumbaji wa Mungu, Jambo la kwanza la kujiuliza ni kwanini Mungu hakuumba vitu vyote ndani ya dakika moja? Maana anao huo uwezo na badala yake akachukua siku saba kukamilisha uumbaji wake?

Swali la pili la kujiuliza, Ni hapo aliposema… “HIVYO NDIVYO VIZAZI VYA MBINGU NA NCHI ZILIPOUMBWA” Hivyo vizazi vilivyoumbwa ni vipi?

Na yapo maswali mengine mengi sana ya kujiuliza juu ya kitabu cha mwanzo, lakini leo tuyatazame haya mawili kwa msaada ya Bwana. Kwasababu tukiweza kumwelewa Mungu katika uumbaji wake tutaweza kumwelewa Mungu katika uumbaji wake anaotufanyia sisi kila siku katika maisha yetu, kwasababu Mungu ni yeye yule hajabadilika jana, leo na hata milele hatabadilika. Njia alizozitumia kuumba mwanzo ndizo hizo hizo zinazoendelea leo katika uumbaji na utengenezaji wa maisha yetu.

Ni wazi kuwa Mungu anao uwezo wa kuumba kitu kufumba na kufumbua lakini, tunaona hakuutumia huo uwezo wake katika uumbaji wa Mbingu na nchi pamoja na uumbaji wa wanadamu na viumbe.. Hakuiumba dunia kufumba na kufumbua, bali ilimchukua muda kidogo katika utengenezaji, kwanini alifanya hivyo..kwasababu ndivyo ilivyompendeza.

Kwahiyo tunaweza kujifunza kuwa sio mpango wa Mungu, mambo kuzuka haraka haraka, sio mpango wa Mungu kwamba jambo ameliahidi leo na leo leo litimie kama lilivyo, ingawa huo uwezo anao, lakini hautumii sana na ndio maana tunasoma pale mwanzo baada ya Bwana Mungu kuiumba dunia, hakuiumba pamoja na miti wala bustani siku ile ile bali aliiumba kwanza yenyewe pamoja na mbegu kisha akizinyeshea mvua, ndipo baada ya kipindi Fulani zile mbegu zikaota, zikawa miche midogo ya miti, mingine pengine ilichukua miezi kadhaa kuwa mikubwa, mingine miaka, lakini baada ya kipindi Fulani ndipo ikatokea misitu mikubwa..Lilikuwa ni jambo la pole pole, ingawa Mungu hakushindwa kuiumba dunia ikiwa na misitu tayari kwa dakika moja.

Kadhalika alipoviumba vizazi vya nchi (yaani wanadamu na wanyama) hakutokeza mamilioni ya wanadamu ndani ya siku moja, au mamilioni ya wanyama ndani ya siku moja, bali alimwumba mwanadamu mmoja kama mbegu duniani, akamwekea ndani yake vizazi vyake, vizazi vyote vya wanadamu akaviweka ndani ya mtu mmoja , ili kwamba baada ya muda Fulani labda baada ya miaka 1,000 au 2,000 ndipo wanadamu wawe wameijaza dunia yote.

Kwahiyo unaweza kuona kwamba mpango wa Mungu, wa wanadamu kuijaza dunia yote, ulikuwepo Edeni lakini haukutimia ile ile siku ya kwanza Mungu alipomuumba mwanadamu, hivyo unaweza ukaona jambo ni lile lile kwamba sio mpango wa Mungu kutimiza kusudi lake lote katika ile siku ya kwanza aliyozungumza.

Kadhalika sio mpango wa Mungu, leo tuzaliwe kesho tuwe na watoto, haitawezekana kwasababu nguvu ya Mungu ya uumbaji haiendi kasi hivyo, inapasa kwanza mwanadamu akamilike kwa miaka kadhaa ndipo awe na uwezo wa kupata mtoto.

Na vivyo hivyo, katika maisha yetu, sio mpango wa Mungu leo tukapande mbegu shambani na leo leo tukavune,sio mpango wa Mungu kutupa mali kwa haraka haraka, ingawa anao uwezo wa kufanya hivyo, ila ni mara chache chache sana na kwa watu wachache tena kwa ajili ya utukufu wake, lakini mpango wa Mungu hasa ni kuchuma kidogo kidogo. Mithali 13: 11 “Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa”..Kwahiyo tukitaka Bwana aumbe jambo jipya katika maisha yetu tunapaswa tuwe watu wenye subira na wavumilivu.

Kadhalika tukitaka Bwana atuponye, sio lazima atuponye siku hiyo hiyo tuliyomwomba, wakati mwingine itachukua muda, wiki, miezi au wakati mwingine hata miaka, lakini mwisho wa siku atatuponya. Mtu akipata jeraha tunajua hawezi kupona siku ile ile, itamchukua wiki, au miezi, au wakati mwingine miaka jeraha lile kupona, na kufunga, na ngozi kurudia kama ilivyokuwa..Sasa ile hatua ya kidonda kupona taratibu taratibu kwa namna ambayo hatuwezi kuona, ndio ile ile nguvu ya uumbaji iliyokuwa pale Edeni, Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi, na ndio hiyo hiyo nguvu inayoponya maisha yetu leo.

Nguvu hii ya uumbaji ipo taratibu sana haiwezi kuonekana kwa macho lakini baada ya kipindi Fulani inaleta matokeo, ndio hiyo hiyo inayolisogeza jua na mwezi, huwezi kuona jua likisogea kwa macho isipokuwa baada ya masaa Fulani ukitazama juu utaona limehama kutoka pale lilipokuwepo kwanza.

Vivyo hivyo huwezi kuona mti ukikua kutoka hatua moja hadi nyingine kwa kuudadisi kwa macho, ukifanya hivyo hutaona chochote, utasubiri na kusubiri pasipo kuona chochote ila mfano ukiondoka na kurudi baada ya siku kadhaa utashtukia tu umeongezeka urefu, hivyo ndivyo nguvu ya Mungu ya uumbaji inavyotenda kazi.

Ndivyo Mungu, anavyotenda kazi hatuwezi kumchunguza kwa akili za kibinadamu, tunachopaswa kufanya ni kumuamini tu, na kisha kuiachia ile nguvu yake ya uumbaji itende kazi, kwa uvumilivu wote pasipo kunung’unika.

Leo Bwana akikuahidia kukuponya unachopaswa kufanya ni kumwamini, usiangalie umekaa na ugonjwa siku ngapi au miezi mingapi au miaka mingapi, usijaribu kumdadisi Mungu jinsi gani anaponya…wewe mwamini tu, na kusubiri, kwa uvumilivu wote, na kushukuru kwasababu ile nguvu yake ya uumbaji inatenda kazi ndani yako kwa namna ambayo wewe huwezi ukajua. Itafika wakati utajikuta tuu, unaanza kuona unafuu kidogo kidogo, na hatimaye kupona kabisa, ukiona umeombewa na bado hali yako bado iko vile vile..sio wakati wa kuhama kanisa hili kwenda lile au mtumishi huyu kwenda yule, sio wakati wa kupanic huku na kule, tulia mahali ulipo mngoje Bwana, kwasababu Bwana anatenda kazi kwa namna usioijua wewe.

Vivyo hivyo na riziki nyingine za ulimwengu huu kama mali, sio za kuzihangaikia huku na huko, kwenda kwenye maombi haya na yale pale unapoona hakuna mabadiliko, tulia mahali ulipo tekeleza wajibu wako Bwana atakupa kidogo kidogo, kwanza yeye alisema “hata tusitie shaka” BWANA Mungu hakuijaza dunia hii watu ndani ya siku moja, ilichukua maelfu ya miaka vivyo hivyo hawezi kukujaza wewe mali nyingi ndani ya siku moja, atakupa kidogo kidogo mpaka utakapojaa kiwango anachokitaka yeye. Ndivyo nguvu yake ya uumbaji inavyotenda kazi.

Na zaidi sana na lililo kuu ni “KUWA MKAMILIFU”…Huwezi kuzaliwa mara ya pili leo na leo leo kuwa mkamilifu kwa kiwango kile Mungu anachotaka, Baada ya kuzaliwa mara ya pili Bwana anatutakasa kidogo kidogo ule uchafu uliopo ndani yetu ambao tulikuwa tunautumikia tulipokuwa kwenye dhambi, anauondoa mpaka tunakuwa wakamilifu kwa viwango vile anavyotaka yeye. Siku baada ya siku tunadumu katika ushirika, fundisho la mitume, kuumega mkate, na kusali ili tukue viwango vya kumzaliwa Mungu matunda.(Matendo 2:42)


Dada/Kaka..Je! umeiruhusu hii nguvu ya Mungu ya uumbaji itende kazi ndani yako leo?..Nguvu ambayo itakutengeneza na kukuumba upya uwe mtakatifu katika vile viwango vya kwenda mbinguni?, biblia inasema waasherati, wazinzi, walevi, waabudu sanamu, watukanaji sehemu yao ni katika lile ziwa la moto, na inasema pia katika “Waebrania 12:14 kwamba hakuna mtu atakayemwona Mungu asipokuwa Mtakatifu” Je wewe unao? Una uhakika kwamba Kristo akija leo utakwenda mbinguni? Kama huna huo uhakika ni wazi kuwa atakapokuja utaachwa..na kukumbana na dhiki kuu na siku ya Bwana inayowaka kama moto,na maandiko yanasema katika 2 Petro 1:10 kwamba tujitahidi kuufanya imara uteule wetu na wito wetu,..

Ndugu tunaishi katika siku za hatari ambazo Kristo yupo mlangoni kurudi, siku sio nyingi waovu wote wa huu ulimwengu wataomboleza na kujuta watakapojua kwamba Kumbe Kristo alikuwa ni Kweli, na wakati huo watakuwa wameshachelewa, ni maombi yangu usiwe mmoja wao. Tubu leo ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kukamilisha maagizo ya Bwana Yesu Kristo naye Bwana ataanza kuyaumba upya maisha yako, kwa kupitia Roho wake Mtakatifu.

Bwana Yesu akubariki sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na Bwana atakubariki.

No comments:

Post a Comment