"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, November 20, 2018

JE! UMEFUNDISHWA?

Wafilipi 4.10 “Nalifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifikiri hali yangu lakini hamkupata nafasi.
11 Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo.
12 Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, NIMEFUNDISHWA kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa.
13 Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”.
 Katika maandiko haya Mtume Paulo, anasema AMEFUNDISHWA kushiba na kuona njaa…Hebu litafakari hilo neno kwa undani “NIMEFUNDISHWA”. Kufundishwa maana yake ni kupewa maarifa ambayo ulikuwa huyajui, hivyo ni wazi kuwa Mtume Paulo kuna wakati alikuwa hajafundishwa baadhi ya mambo mpaka ulipofika wakati Fulani wa kupokea mafundisho za dizaini hiyo..

Na moja ya mambo hapa ambayo Mtume Paulo anasema amefundishwa ni hili la “KUSHIBA NA KUONA NJAA”. Ikiwa na maana kuwa kuna wakati Mungu alimpitisha katika kipindi cha uhitaji mkubwa (kipindi kikali cha kuona njaa) ili amfundishe huko.. Na kuna wakati pia Mungu alimpitisha katika kipindi cha kushiba ili pia ajifunze.


 Kwahiyo tunaona kuwa mojawapo ya tabia ya Mungu ni kumpitisha Mtu katika VIPINDI VIWILI, vya KUSHIBA na KUONA njaa. Vipindi vya KUPUNGUKIWA na KUWA NA VINGI, Vipindi vya kupandishwa juu na vipindi vya kushushwa.(Mhubiri 3). NIA NA MADHUMUNI YA MUNGU..NI ILI TUFIKIE MAHALI TUWE RADHI NA VITU TULIVYONAVYO. Tufikie mahali tusipepesuka na hali yoyote tutakayokutana nayo katika siku za usoni.

Unajua kuna tabia moja Fulani ambayo baadhi ya majeshi mengi duniani wanayo,  pindi wanapomsajili mwanachama mpya katika jeshi huwa wanamchukua Yule mtu kwasababu ndio kajiunga kwa mara ya kwanza,hajui kanuni cha jeshi, wanamchukua na kuanza kumwonea au kumfanyia mambo ya kumuudhi…utaona kafika tu kesho yake, anaanza kupigwapigwa pasipo sababu, pengine ametulia tu hajafanya kosa lolote anajikuta  mtu anatokea na kuanza kumtukana pasipo sababu na kumshurutisha kufanya jambo Fulani, utakuta kalala na mtu anakuja kumwamsha na kumpiga bila sababu, na mambo mengi mabaya ya kuudhi hapo hakuna wa kumsaidia. Sasa huo ndio umekuwa utaratifu wa majeshi mengi duniani kufanya hivyo, nia na makusudi yao sio kumtesa Yule mgeni, au kumwonea hapana bali kumtolea ndani yake “ile hasira ya asili (kupanic) ambayo kila mtu anakuwa amezaliwa nayo ” Ili kumpa uwezo wa kustahimili mambo magumu atayoweza kukutana nayo katika vita.

 Kwahiyo utaona mara za kwanza anapigwa, na kuanza kunung’unika saa hiyo hiyo, na wakati mwingine kurudisha mapigo au matusi au kununa kwa muda mrefu, na kutengeneza kinyongo lakini siku zinavyozidi kwenda anakuwa anazoea zile hali hivyo hata akifanyiwa hayo mambo mara nyingi vipi  anajikuta  hapaniki tena kama zamani, anakuwa kawaida, haumii moyo tena kama alivyokuwa anaumia..Hiyo inamsaidia Yule mwanajeshi akiwa vitani atumie AKILI ZAIDI KULIKO HISIA. Kwahiyo hayo ni moja ya mafundisho tu ya majeshi ya watu wa Ulimwengu huu. Hicho ndicho kinachomtofautisha mwanajeshi na raia wa kawaida. Utashangaa ni kwanini anaweza akaona ndugu yake  mpendwa vitani labda kaka yake kapigwa risasi na kuuliwa, badala ya kuvunjika moyo na kulia pale, yeye ndio atambeba na kumuhifadhi kisha kuendelea na vita kana kwamba hajafiwa..Lakini ukirudi kwa watu wa kawaida mfano msiba umetokea kidogo tu utaona watu wanaanza kupiga mayowe  na wengine hata kukufuru..Ni kwasababu gani? Ni kwasababu hawajafundishwa. Hilo tu.
Lakini Kristo naye ana mafunzo yake, kabla ya kumpeleka mtu, katika vita vya kiroho..Na mojawapo ya mafundisho ndio hayo “KUFUNDISHWA KUONA NJAA na KUSHIBA”.
Wana wa Israeli kabla ya kufika nchi ya Ahadi, Bwana aliwapitisha jangwani na wakati mwingine alikuwa anawaacha waone njaa na kiu kwa muda mrefu ili awafundishe. Ili Watakapoingia nchi ya Kaanani wasilalamike watakapopitia mitikisiko kidogo tu. Walikuwa wanatembe jangwa masiku hawaoni maji.


Kumbukumbu 8: 1 “Amri hii ninayokuamuru leo mtaishika kuitenda, mpate kuishi na kuongezeka, na kuingia katika nchi ile ambayo Bwana aliwaapia baba zenu; nanyi mtaimiliki.
2 Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako ALIYOKUONGOZA MIAKA HII AROBAINI KATIKA JANGWA, ili akutweze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo.
3 Akakutweza, AKAKUACHA UONE NJAA, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa MWANADAMU HAISHI KWA MKATE TU, BALI HUISHI KWA KILA LITOKALO KATIKA KINYWA CHA BWANA”.


Unaona! Wana wa Israeli kuna kipindi Mungu aliwaacha makusudi waone njaa lakini walikuwa hawafi wala hawaumwi, Ili wajue tu kuwa Mtu anaweza kuishi bila kula vyakula vya kimwilini na asife bali akaishi kwa Neno la Mungu tu.

Na ndio maana Bwana Yesu naye vivyo hivyo alipokwenda mlimani alifunga siku 40 usiku na mchana bila kula, na mwovu alipomjia na kumjaribu ageuze  jiwe kuwa mkate..alimpa jibu lile lile kuwa “MTU HATAISHI KWA MKATE TU BALI KWA KILA NENO LINALOTOKA KATIKA KINYWA CHA BWANA”..Kwasababu gani alimjibu vile ni kwasababu “HUKO NYUMA ALISHAFUNDISHWA KUSHIBA NA KUONA NJAA” kwahiyo kwake yeye AWE NACHO au ASIWE nacho vyote ni sawasawa. Awe na chakula asiwe na chakula kwake yeye ni sawa sawa..Anayaweza mambo yote kwa yeye AMTIAYE Nguvu. Anachojua ni kwamba Mungu hatamtupa kabisa.

Na ndio Mtume Paulo naye, hakuwahi kutamani fungu kutoka kwenye makanisa aliyoyazaa yeye kiroho, ingawa angestahili kupata fungu kutoka huko, lakini badala yake ndio anawaambia watu wa kanisa la Filipi ambalo walitamani sana kumuhudumia kwa mali zao..

Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; MAANA NIMEJIFUNZA KUWA RADHI NA HALI YO YOTE NILIYO NAYO. 
12 Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, NIMEFUNDISHWA kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa.
13 Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”.

Hiyo ina maana kuwa HAHUBIRI INJILI YA KRISTO kwasababu anataka FEDHA, au kwasababu ANA FEDHA, hapana Bali anahubiri injili ya Kristo kwasababu ana NIA YA KRISTO NDANI YAKE, AWAVUTE WENGI KWAKE…AWE NACHO ASIWE NACHO KWAKE YEYE NI SAWASAWA Injili ya KRISTO ataendele kuihubiri.

Na sisi je! Tumefundishwa KUWA RADHI NA VITU TULIVYO NAVYO? Kwamba ifikie mahali hatumfuati Bwana Yesu kwasababu tunatafuta utajiri, au mali kutoka kwake, au hatumfuati kwasababu Tuna mali., Yaani ifikie hatua tunasema TUMEFUNDISHWA KUWA RADHI NA VITU TULIVYO NAVYO. Tumefundishwa kuridhika na vitu tulivyo navyo..viwe vingi au vichache tutamtumikia Bwana, tuwe tuna  Elimu tusiwe na Elimu kwetu iwe ni mamoja, tuwe matajiri tuwe maskini Thamani ya Kristo Kwangu ni ile ile. Niwe na chochote nisiwe na chochote tutaihubiri injili ya Kristo.

Kama hatujafunzwa hivyo Basi tumwombe Bwana atufundishe masomo hayo ili tuweze kutembea naye pasipo manung’uniko wala malalamiko Kama alivyotembea na Mtume Paulo..Hiyo itatusaidia sisi tunapopitia vipindi vya kupungukiwa tusijione wanyonge, na kuanza kutanga huku na huko, bali tujue ni vya muda tu, sisi tusonge mbele na Imani mpaka kuja kwake YESU KRISTO ambapo yeye mwenyewe atatufariji kwa taabu zetu hapa duniani.

Tafadhali wahubirie wengine habari njema ya Msalaba kwa kadri uwezavyo.

Ubarikiwe.

1 comment:

  1. Barikiwa Sana naitwa
    Pastor ADERICK KALUGILA. NI kiudumu kutoka Maswa Mungu akubarikia kwa mafundisho yako NI mazuri endelea

    ReplyDelete