YOHANA 3:3 “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.6 Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.7 Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.8 Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho.”
Jina la Bwana wetu Yesu Kristo
lisifiwe daima, Ni siku nyingine tena Bwana aliyotupa kwa neema zake na leo
tutaangalia vifungu hivyo ni kwanini Yesu aliifananisha hali ya mtu aliyezaliwa
kwa Roho na kama UPEPO UVUMAO.
Yapo mambo matatu hapo Bwana
aliyoyasema kuhusu Upepo,
1) La kwanza ni Upepo Huvuma upendako
2) La pili ni: Sauti yake waisikia (lakini hauuoni)
3) Na la tatu ni Hujui utokako wala unakokwenda.
Na mwisho
akamalizia kusema “NDIVYO ILIVYO HALI YAKE MTU ALIYEZALIWA NA ROHO”. Hii ina
maana gani? Ni wazi kuwa inamaanisha pale Roho wa Mungu anapoingia ndani ya mtu kwa
mara ya kwanza basi hali yake inabadilika na kufanana na tabia inayoweza
kulinganishwa na tabia ya upepo.
Tabia hizi ni
mara tu baada ya mtu kuzaliwa kwa Roho, kwahiyo tunaweza kusema Upepo huo ni
Roho mtakatifu ndani ya mtu. Kwasababu ndiye aliyemfanya kuwa hivyo. Kama
tunavyofahamu tabia ya upepo, kwanza ni kitu kisichoweza kuonekana kwa macho lakini utaisikia sauti yake pale
unapovuma, au utauhisi katika mwili wako pale unapopita karibu na wewe, lakini
usijue chanzo chake ni wapi na hatma ya
safari yake itaishia wapi!!.
Kadhalika Roho Mtakatifu anapoingia ndani ya mwamini
tabia hizi za upepo wa Roho huingia ndani yake. Pale mtu alipoamua na
kudhamiria kweli kumpa Kristo maisha yake. Basi kuanzia huo wakati na kuendelea
ndani yake kunakuwa na nguvu isiyojulikana chanzo chake ni nini kwa nje! Watu wa
nje wanaweza kushangaa mbona huyu mtu tabia yake imebadilika kwa ghafla
hivi,wasijue ni nani aliyembadilisha, wakijaribu kachunguza labda ni dini
hawaoni, labda ni dhehebu hawaoni, labda ni mwanadamu hawaoni, na ndio hapo
utaona maisha ya yule mtu yanabadilika, pengine mambo aliyokuwa anapenda
kuyafanya hapo mwanzo yanageuzwa ghafla, maisha aliyokuwa anaishi nyuma
yanageuka ghafla, mara nyingine atajikuta anachukia hata kufanya baadhi ya vitu
alivyokuwa anavifanya nyuma, anajikuta kiini cha maisha yake ni kumwangalia
Bwana YESU tu mahali popote alipo…Baadhi ya mambo yasiyokuwa na maana yataanza
kumkera, anaanza kutokujiona kuwa huru akiwa katika vikao vya usengenyaji,
tofauti na alivyokuwa hapo mwanzo..
Hii yote
inatokea ni kwasababu yule Roho aliye ndani yake humsukuma kufanya vitu ambavyo
hata pengine yeye mwenyewe hajui ni kwanini anavifanya, saa nyingine anaweza
akadhani ni kwa akili zake anafanya hivyo.Au ni kwasababu ametokea tu kupenda
mwenyewe Lakini ukweli ni kwamba sio yeye anafanya hivyo bali ni Roho wa Mungu
ndani yake atembeaye kama upepo usioonekana anamwelekeza asikojua yeye.
Atajikuta
anaanza kuchukia kupenda pombe, ambapo hapo mwanzo alikuwa anazitamani,
anajikuta kuvaa vimini na suruali anajiona kama yupo uchi au anajiaibisha mbele
za watu hivyo anajikuta anaanza kupenda kuvaa sketi ndefu ambazo hapo mwanzo
alikuwa akivaa anajiona kama mshamba. Anajikuta anatamani kusoma biblia, au
kusikiliza Neno la Mungu sana, ambapo hapo kwanza alikuwa hana mpango navyo.
Anajikuta kampani za marafiki wa kidunia ni mzigo mkubwa kwake tofauti na jinsi
alivyokuwa nyuma. Anajikuta hata akipitia dhiki kubwa kiasi gani kwa ajili ya
imani hapepesuki mpaka watu wa nje! Wanashangaa huyu mtu ni wa dizaini gani.
N.k.
Na hata baada
ya muda mrefu kupita ukimuuliza ilikuwaje kuwaje ukaweza kuacha dhambi na mambo
ya kidunia pamoja na majaribu mazito kiasi kile atakwambia kwa kweli sifahamu
nguvu hiyo ilitoka wapi,nilijikuta tu ninamsimamo na maamuzi yangu..nilijikuta
tu kuna nguvu fulani ndani yangu ikinisukuma kunipeleka sehemu Fulani,sasa huo
ulikuwa ni ule upepo wa Roho ambao ulikuwa unampeleka asikotazamia yeye
kwenda,.ataishia kukwambia ni neema za Mungu tu.
Na ndio maana
katika siku ile ya Pentekoste Roho aliposhuka kwa watu kwa mara ya kwanza Ishara
ya kwanza aliyoshuka nayo ni ishara ya UVUMI
WA UPEPO uendao kwa kasi, sio kwasababu Mungu alikuwa anataka kuwaonyesha watu uweza
wake wa kuamuru tufani, hapana, bali Upepo ule ulifunua jambo kubwa sana katika
roho kwa waumini wa kweli waliokuwa
Yerusalemu..na ndio maana ukichunguza kwa makini baada ya pale maisha na
mienendo ya mitume ilibadilika ghafla
tangu ule wakati, walipokea ujasiri usio wa kawaida kuhubiri injili, walijawa
na Imani kwa Mungu, hawakuwaogopa maadui zao tena, na kwenda kujificha kama
ilivyokuwa pale mwanzo.. Mara nyingi roho alikuwa akiwatwaa na kuwapeleka
wasikojua, na huko wanapofika wanalihubiri Neno la Mungu kwa ushujaa
mwingi..Tunamwona mtu kama Filipo alitwaliwa na Roho na kupelekwa kule Roho
alipopenda kumpeleka.
Matendo 2:1 "Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote
mahali pamoja.
2 KUKAJA GHAFULA TOKA MBINGUNI UVUMI KAMA UVUMI WA UPEPO WA NGUVU UKIENDA KASI, UKAIJAZA NYUMBA YOTE WALIYOKUWA WAMEKETI.
3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.
4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka".
2 KUKAJA GHAFULA TOKA MBINGUNI UVUMI KAMA UVUMI WA UPEPO WA NGUVU UKIENDA KASI, UKAIJAZA NYUMBA YOTE WALIYOKUWA WAMEKETI.
3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.
4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka".
Unaona kulikuwa na Upepo
wasiojua ulipotoka ,Ule ulifunua UPEPO WA ROHO, ambao ndio ulioathiri maisha
yao kuanzia ule wakati na kuendelea.
Unaona umuhimu kwa kuzaliwa kwa
Roho? Leo hii ni kwasababu gani huwezi kushinda tamaa, na dhambi, ni kwasababu
moja tu, nayo ni hii HAUJAZALIWA MARA YA PILI hivyo ule upepo wa Roho hauwezi
ukawa na nguvu juu ya maisha yako. Haujamkaribisha Roho ndani ya maisha yako.
Kama ungekuwa umezaliwa kwa Roho ile nguvu ingekusukuma mahali usipojua kama
vile UPEPO uvumapo na usingeona kuwa dhambi ni jambo gumu kuliacha kwasababu ni
Roho mwenyewe angekuwa anatenda kazi ndani yako.. Nguvu ile Ingekusukuma kule
usikoweza kufika, ingekusukuma kutenda mapenzi ya Mungu na kumtazama Kristo
kila wakati.
Kumbuka
Nikodemo alikuwa ni Farisayo wa mtu dini
sana, anayejua maandiko sana lakini hakuwa amezaliwa mara ya pili, unaona? kumbe
unaweza ukawa wa kidini na usiwe na Roho Mtakatifu ndani yako. Ndugu Usiridhike
na dhehebu lako, au kanisa lako ukajiona kuwa tayari umekamilika na huku unaona
kabisa maisha yako ya kikristo yanadorora siku baada ya siku..Na ndio maana
maandiko yanasema, MTU ASIPOZALIWA KWA MAJI NA KWA ROHO HAWEZI KUUINGIA UFALME
WA MBINGUNI hapo hata kama uwe unayafahamu maandiko kiasi gani, huwezi kuuingia
ufalme wa mbinguni, Bwana Yesu anasema hivyo.
Lakini Mtu
anazaliwaje kwa Roho na kwa Maji?
Ni kwa
kukudhamiria kabisa kutubu na kuacha dhambi na maisha ya kale.Wengi hawafanyi
hivyo, toba haitoki moyoni bali midomoni na ndio maana inakuwa ngumu Roho wa
Mungu kukaa ndani yao. Na maana ya toba sio kuomba msamaha tu, bali ni KUGEUKA
AU KUACHA. Hivyo unapogeuka na kukusudia kuacha dhambi hata usiposema kwa mdomo
hiyo tayari ni TOBA, Hivyo ukizingatia hayo na Mungu akishaona nia yako yeye
mwenyewe atakuosha “roho yako”, kwa maji
(ambayo ni DAMU yake na Neno lake) na kukugawia Roho wake ndani yako
atakayekuweza kukusaidia kuishinda dhambi siku zote za maisha uliyopo hapa
duniani..
Kama maandiko
yanavyosema:
Ezekieli 36: 24 “Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa
katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe.
25 Nami NITAWANYUNYIZIA MAJI
SAFI, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu
vyote.
26 Nami nitawapa ninyi moyo
mpya, NAMI NITATIA ROHO MPYA NDANI YENU, NAMI NITATOA MOYO WA JIWE ULIOMO NDANI
YA MWILI WENU, NAMI NITAWAPA MOYO WA NYAMA.
27 NAMI NITATIA ROHO YANGU
NDANI YENU, NA KUWAENDESHA KATIKA SHERIA ZANGU, nanyi mtazishika hukumu zangu,
na kuzitenda.
28 Nanyi mtakaa katika nchi ile
niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.”
Hivyo mambo hayo hayatimiliki
pasipo kuambatana na ishara ya wazi ya nje kuonyesha kuwa hicho kilichotendeka
nje ndicho kilichofanyika rohoni mwako. Kwahiyo ni lazima mtu akazamishwe
kwenye MAJI mengi akabatizwe kwa maji tele,kama Bwana alivyoagiza na ni katika
JINA LA YESU, kuonyesha kuwa ameoshwa dhambi zake kwa maji ya Roho, kisha ndipo
awe na uhakika kuwa amepokea ubatizo wa Roho Mtakatifu ndani yako.
Hivyo ikiwa haujachukua uamuzi huo
fanya hivyo haraka, ili neema hii ipate kuwa juu yako. Na ule UPEPO wa ROHO
MTAKATIFU utakuvumisha na kukupeleka usikojua wewe, Na mwisho wake utashangaa
umetulia mahali Mungu ambapo alikusudia..na utakuwa na uhakika siku ile
kunyakuliwa juu kwenda mbinguni kumlaki Bwana, katika upepo huo wa kisulisuli
kama Nabii Eliya.
Chukua muda
wako kuwahubiria habari njema za wokovu, ndugu zako, marafiki zako na jamaa
zako popote pale ulipo, ili na wao wapone, shetani asipate mazao.
Mungu
akubariki.
No comments:
Post a Comment