"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, November 19, 2018

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 43


SWALI 1: BWANA YESU awabariki ndugu......naswali ndugu zangu hivi KUFUKIZA UVUMBA ndio kufanyaje? Na tena wana wa Israel walimfukizia uvumba Malikia wa mbinguni ndio yupi huyo?

JIBU: Uvumba ni aina Fulani ya manukato, yanayotengenezwa kwa viungo mbalimbali ambavyo baada ya kutengenezwa pamoja, huwa yanachomwa na kutoa harufu Fulani iliyo nzuri.

Sasa katika biblia (Agano la Kale) wana wa Israeli walipokuwa jangwani kabla ya kufika nchi ya Ahadi, walipewa maagizo na Mungu mwenyewe watengeneze UVUMBA, na makuhani watakuwa wanauchoma huo kila siku ndani ya ile Hema waliyoambiwa waitengeneze..Na ni makuhani peke yao ndio waliokuwa wanaruhusiwa kufanya hiyo kazi ya kuvukiza uvumba.



Hivyo Makuhani waliuchukua huo uvumba na kuuchoma kila siku ndani ya ile hema ya kukutania katika madhabahu ndogo iliyokuwemo kule ndani, Na ilikuwa ni amri ya daima ni lazima wafanye hivyo kila siku..Na Bwana aliwaagiza wana wa Israeli wasitengeneze uvumba wowote kwa viungo hivyo kwa ajili ya mambo yao..Fomula ya kutengeneza huo uvumba ni kwa ajili ya Bwana tu!



Kutoka 30: 34 “Bwana akamwambia Musa, Jitwalie MANUKATO MAZURI, yaani, natafi, na shekelethi, na kelbena; viungo vya manukato vizuri pamoja na ubani safi; vitu hivyo vyote na viwe vya kipimo kimoja;

35 nawe UTAFANYA UVUMBA WA VITU HIVYO, manukato ya kazi ya ustadi wa mtengenazaji manukato, yatakuwa yamekolea, safi, matakatifu;

36 nawe baadhi yake utayaponda sana, na kuyaweka mbele ya ushuhuda ndani ya hema ya kukutania, hapo nitakapokutana nawe; nayo yatakuwa kwenu matakatifu sana.
37 Na uvumba utakaofanya, hamtajifanyia uvumba wenye viungo sawasawa na uvumba huo; utakuwa kwenu mtakatifu kwa ajili ya Bwana”.

Sasa swali ni kwanini Bwana aliwapa hayo maagizo ya kuchoma uvumba ndani ya nyumba yake??

Jibu ni kwamba kila kitu kilichokuwemo ndani ya ile Hema ya kukutania kilikuwa ni lugha ya picha ya jambo linaloendelea rohoni....kwamfano kile kinara cha taa saba ndani ya nyumba ya Mungu kiliwakilisha makanisa saba katika ufunuo sura ya 2 na ya 3, kadhalika Yule kuhani mkuu anayeingia patakatifu pa patakatifu na Damu ya mwanakondoo ili kufanya upatanisho, anamwakilisha Yesu Kristo, ambaye ndiye kuhani wetu mkuu aliyeingia patakatifu pa patakatifu kwa damu yake mwenyewe mara moja tu!



Kadhalika na ule UVUMBA, kwa jinsi ulivyokuwa unachomwa ndani ya Nyumba ya Mungu, na moshi wake kukijaza kile chumba, na kupaa juu mbinguni..Jambo lile lilikuwa linafunua jinsi gani maombi ya watakatifu yanavyomfikia Mungu, kwanza yanakuwa yameandaliwa kulingana na Neno lake, pili yanapaa juu kama moshi na kumfikia Mungu mbinguni, kwani tunajua kitu pekee kinachopaa juu chenyewe ni moshi..Hivyo kwasababu yametengenezwa na viungo vinavyoendana na Neno la Mungu, maombi ya watakatifu yanakuwa ni harufu nzuri ya kuvutia mbele za Mungu, yanakuwa kama perfume mbele zake. Na ndio maana Daudi alisema maneno haya..



Zaburi 141: 2 “SALA YANGU IPAE MBELE ZAKO KAMA UVUMBA, Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.”


Kwasababu hiyo basi katika agano jipya hatuchomi ubani tena, wala hatuvukizi uvumba kwasababu hayo yalikuwa ni mambo ya mwilini yanayofunua mambo ya rohoni, HIVYO UVUMBA WETU NI MAOMBI YETU TUNAYOMWOMBA MUNGU KILA SIKU YANAYOENDANA NA NENO LAKE.

Ndio maana pia tunasoma hayo katika kitabu cha Ufunuo..


Ufunuo 5:8 “Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, NA VITASA VYA DHAHABU VILIVYOJAA MANUKATO, AMBAYO NI MAOMBI YA WATAKATIFU.”


Ufunuo 8: 4 “ NA MOSHI WA ULE UVUMBA UKAPANDA MBELE ZA MUNGU PAMOJA NA MAOMBI YA WATAKATIFU, kutoka mkononi mwa malaika.”

Lakini pamoja na hayo shetani naye huwa anapenda kuiga na kugeuza mambo, na kuwadanganya watu kuwa mambo hayo kwasasa yanapaswa yaendelee kufanyika, kama anavyowadanganya watu kuwa kwasababu agano la kale kondoo na mbuzi walikuwa wanachichwa kwa ajili ya upatanisho, vivyo hivyo na sasa kondoo na mbuzi wanapaswa wachichwe kwa ajili ya kuondoa mikosi katika mtu, au jamii au ukoo, hivyo watu badala wapone ndio wanajiongezea roho juu ya roho.. Vivyo hivyo leo hii Bado shetani anawadanganya watu juu ya kuvukiza uvumba, ndio utasikia watu wanaambiwa wakachome ubani manyumbani mwao kufukuza mapepo, na zaidi hata makanisani watu wanavukiza uvumba, jambo ambalo ni machukizo kwa Mungu wa mbinguni....

Na kuhusu MALKIA WA MBUNGUNI. Hakuna mahali popote biblia imesema kuna malkia mbinguni, isipokuwa imeeleza miungu ya kipagani, inayojulikana kama malkia wa Mbinguni, hivyo biblia ilipotaja malkia wa mbinguni mahali popote ilikuwa inamaanisha miungu ya kipagani inayojulikana na watu kama malkia wa mbinguni, Ni sawa na leo atokee mtu atengeneze kinyago chake halafu akiite Malkia wa mbinguni, kiuhalisia sio kweli kwamba ni malkia wa mbinguni, mbinguni Mungu aliko hapana bali kimeitwa vile kutokana na watu wanakiita chenyewe malkia wa mbinguni.


SWALI 2: Ndugu zangu Huyu Mariamu MAGDALENE"..Magdene ni jina la baba yake au ni Jina la ukoo wake?.

JIBU: Hapana aliitwa mariamu Magdalene kuonyesha asili yake ili kumtofautisha na Mariamu wengine kwenye biblia…Kumbuka hili jina Mariamu limetumika mara nyingi kwenye biblia..Hivyo ili kuwatofautisha hawa Mariam wote, huyu aliitwa mariamu Magdalene kuonyesha na Mariam aliyetokea huko mji wa MAGDALENE uliokuwa kando kando mwa bahari ya Galilaya huko kaskazini mwa Israeli. Lakini hilo sio jina la Baba yake au ukoo wake..Hapana ni jina la mji aliotokea.
Ni kama Yule mwanamke Msamaria, hilo jina Msamaria sio jina la baba yake, hapana bali ni jina la mji anaotokea unaoitwa SAMARIA uliopo katikati ya Israeli.

SWALI 3: Shalom Ndugu, Jana nilipomaliza kusali nilipumzika kidogo kitandani Hapo Ikanijia Ndoto, katika hiyo ndoto nilikuwa na SIMU mkononi mbele yangu kulikuwa na daraja la kuvuka sikujuwa hilo, Macho yangu yalikuwa bize kuangalia Simu nikajikuta nimepita pembeni ya hilo DARAJA lililokuwa mbele yangu nikiwa katika hatari yakushushwa na hayo MAJI MENGI Nikajitahidi kujishika huku na huko kwenye mbao za daraja nikasalimika,kilichoninyima Amani niliona Biblia yangu ilibaki ikishushwa na maji, kuifuata sikuweza tena kwa kuogopa hatari ya wingi wa maji Ni kitu gani hapo ndugu zangu?Karibuni...


JIBU: habari yako ndugu yetu. Ili kupata tafsiri iliyo sahihi na bora zaidi ni vizuri ukamwomba Mungu kwanza akufunulie huku ukiyachunguza maisha yako kwa ukaribu. Sasa kwa ndoto kama hiyo kwa jinsi nionavyo mimi katika mazingira ya hiyo ndoto, ni kwamba kuna baadhi ya mambo yanayokusonga ambayo yanaweza kukupeleka kudondoka katika Imani. Na mambo hayo si mingine zaidi ya simu. Jaribu kuchunguza mwenendo wako kwenye mitandao, kumbuka mitandao sio mizuri sana sana kwa sisi mkristo kwasababu ina mambo mengi, sisi tunaingia humo kwa lengo la kupeleka injili na sehemu kidogo kujifunza, lakini sehemu kubwa kumejaa uovu. Hivyo angalia unapoingia kule, ni kitu gani kinakupeleka kule, je ni kuchat? Au kujifunza na kuondoka...Epuka kukaa muda mrefu huko mpaka unakosa muda wa kusoma biblia na kumtafakari Mungu, epuka kuzungumza na watu wasio na maana mitandaoni, epuka kusoma soma kila post inayojitokeza mitandaoni isiyo na maana, ..Usipoteze muda wako mwingi huko hata ukashindwa kufanya mambo yako mengine ya msingi,  ili kukifanya kile ulichoshikilia kisianguke.Na Bwana akusaidie..Ndivyo nionavyo mimi ndugu yetu.


SWALI 4: Je! kuangalia televisini(tv) ni kosa naomba unisaidie ndugu?

JIBU: Shalom, kuangalia tv hakuna tatizo lolote, inategemea tu unaangalia kipindi gani katika hiyo tv, kama unasikiliza habari, au unafuatilia vipindi vya kujiendeleza mwenyewe kimaisha hakuna tatizo lolote..Lakini inapotumika kuangalia mambo yasiyostahili kama movie zisizofaa, pornography, Vipindi vya udadisi wa maisha ya watu(umbea) ndio tatizo.. Na sio tv peke yake bali hata mitandao ya kijamii kama hii.. Unapokuja huku kutafuta mambo yanayokusaidia katika ukuaji wako wa kiroho kama hivi ni vizuri, lakini ukija huku kwa nia nyingine kutafuta mambo yasiyofaa ni kosa. Mambo yote tunatakiwa tufanye kwa utukufu wa Mungu.  Ubarikiwe!

No comments:

Post a Comment