"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, November 9, 2018

JE! UNAMPENDA BWANA?


Bwana Yesu alisema “MTU AKINIPENDA  ATAZISHIKA AMRI ZANGU (Yohana 14:15)” lakini tunaona hiyo pekee haitoshi kwasababu kama  ingekuwa inatosha Bwana asingemwambia tena Mtume Petro mahali pengine  maneno haya…

Yohana 21:15 “Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia simoni petro, je! simoni wa yohana, WEWE WANIPENDA KULIKO HAWA? akamwambia , naam ,bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. akamwambia, LISHA WANA-KONDOO WANGU.
16 akamwambia tena mara ya pili, simoni wa yohana, wanipenda? akamwambia, ndiyo, bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. akamwambia, CHUNGA KONDOO ZANGU.
17 akamwambia mara ya tatu, simoni wa yohana, wanipenda? petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, wanipenda? akamwambia, bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. yesu akamwambia, LISHA KONDOO ZANGU”.Kwahiyo tunaona licha ya kuzishika amri zake, kuna mambo mengine matatu ya yatakayokamilisha upendo wetu kwa Kristo.  Nayo ni (1) KULISHA WANA-KONDOO WAKE, (2) KUCHUNGA KONDOO ZAKE (3) KULISHA KONDOO ZAKE.

KUZISHIKA AMRI:

Kuzishika Amri za Mungu ni kuzielewa, kuzipenda na kuziishi, na sio kuzikariri  na yeyote aziishie amri za Mungu  amri hizo zinapaswa zisiwe nzito kwake, Maagizo ya Mungu yanapaswa yawe ni mepesi kwake kuyashika kwasababu Roho wa Mungu anakaa ndani yake, hivyo Nira ya Kristo kwake inakuwa ni laini, na mzigo unakuwa mwepesi,hajisikii uzito wala hajilazimishi kuzitimiza sheria za Kristo ndani yake..Hatatumia nguvu nyingi kujizuia kutenda dhambi, hivyo anakuwa anazitimiza pasipo kujiweka katika utumwa, hawi chini ya utumwa wa sheria, kwasababu Nia ya Mungu sio sheria zake ziwe mzigo mzito kwetu, nia yake sio tuzishike amri zake kwa uchungu na mateso na utumwa ..hapana na ndio maana alisema katika..

Kumbukumbu 30: 10 “ukiwa utaifuata sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa kuyashika maagizo yake, na AMRI ZAKE zilizoandikwa katika chuo hiki cha torati; ukimwelekea Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote.
11 Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, SI MAZITO MNO KWAKO, WALA SI MBALI.
12 Si mbinguni, hata useme, Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya?
13 Wala si ng'ambo ya pili ya bahari, hata useme, Ni nani atakayetuvukia bahari, akatuletee, aje atuambie, tusikie, tupate kuyafanya?

Unaona ili kuzishika Amri za Mungu,  ni lazima Kuwepo na wepesi ndani yako ambao Mungu ameuweka, ili Sheria zake zisiwe nzito mno kwako. Hivyo kwa kuishi maisha kama hayo ya kutimiza sheria za Mungu pasipo utumwa. Huko ndiko kuzishika Amri za Mungu. Na huko ndiko kumpenda Bwana. Lakini kufanya hivyo pekee hakutoshi kuonyesha upendo wetu kwa Bwana. Lipo jambo lingine la ziada la kufanya ili kutimiza upendo wetu kwake.

Na jambo hilo si lingine zaidi ya kulitazama kundi la Mungu kwa kulilisha na kulichunga.Ndio maana Bwana alimwuliza Petro mara tatu swali lile lile? Je! wanipenda?

 NINI MAANA YA KULISHA KONDOO WAKE:

 Kama neno lenyewe lilivyo “kondoo wake”  ikiwa na maana kuwa sio kondoo wa mtu Fulani, bali ni kondoo wa Kristo. Hivyo mtu hawezi kujiamulia tu, njia au namna ya kuwalisha,  kwa lugha nyingine Petro aliambiwa yeye ni  mchungaji aliyeajiriwa kuwachunga na kuwalisha kondoo, hivyo kondoo hata mmoja asipolishwa inavyopaswa ataulizwa na aliyemwajiri, kwasababu kondoo sio wake, bali ni wa mtu mwingine.

Kondoo wanawakilisha watu wa Kristo waliomwamini yeye, na wachache wanaohitaji kumwamini.. hao ndio kondoo wa Kristo, biblia inasema tuwalishe hao, na chakula chao sio nyasi bali ni NENO LA MUNGU lisilochanganywa na chochote..  Kazi kubwa ya mchungaji ni kwenda huku na huko kutafuta mahali penye nyasi zinazowafaa kondoo.. Kadhalika Sisi kama wakristo tuliookolewa tunalo jukumu la kuwaongoza wenzetu, au kuongozana sisi kwa sisi mahali panapopatikana Neno la Uzima.

Ukimwona ndugu yako anahangaika huku na kule, ni wajibu wako kama mkristo kumwelekeza kwa upendo mahali ambapo anaweza kuishibisha nafsi penye Neno la Uzima. Huko ndiko kumpenda Kristo. Maadamu ndani yetu kuna nuru kidogo ambayo haimo ndani yao.

KUCHUNGA KONDOO WAKE.

Kama neno lilivyo “kondoo wake” ikiwa na maana kuwa “sio kondoo wa  mtu fulani” bali ni kondoo wa Yesu Kristo, hivyo hatuwezi kujichagulia njia ya kuwachunga..Tunapokea maagizo kutoka kwake namna ya kuwachunga.

Sasa Bwana Yesu alisema “Tujihadhari na mbwa mwitu wakali” na pia alisema “tujihadhari na mbwa mwitu wanaokuja na mavazi ya kondoo”…Sasa dhumuni la mbwa mwitu kuvaa mavazi ya kondoo ni ili na yeye aonekane kama kondoo ili asitumie nguvu nyingi kuwakamata kondoo. Sasa hao Bwana ndio aliosema tujichunge nao sana, na tukiisha kujihadhari nao, tuwachunge na ndugu zetu dhidi yao.. HUKO NDIKO KUCHUNGA KONDOO WAKE.

Sasa hawa mbwa-mwitu ndani ya mavazi ya kondoo ni wakina nani?

Mathayo 7: 15 “Jihadharini na manabii wa uongo, WATU WANAOWAJIA WAMEVAA MAVAZI YA KONDOO, WALAKINI KWA NDANI NI MBWA-MWITU WAKALI. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?”


Unaona, Manabii wa uongo ndio mbwa-mwitu ndani ya mavazi ya kondoo.  Na manabii wa uongo sio tu manabii, hapana bali hata waalimu wa uongo, wachungaji wa uongo, watumishi wa uongo, wainjilisti wa uongo, maaskofu wa uongo, mashemasi wa uongo, wapendwa wa uongo, waimbaji wa uongo n.k hawa wote kwa pamoja wanaunda kundi linalojulikana kama manabii wa uongo. Yaani watu wote ambao kwa nje wanajulikana kama ni wakristo lakini ndani katika maisha yao ya siri sio wakristo hata kidogo, ni watu wa ulimwengu huu, walevi, watukanaji, vuguvugu, waasherati, walaji rushwa n.k…Na bado wanahubiri na kushuhudia na kuimba. Wengine wanajiita PAPA wakiwapoteza watu waabudu sanamu Mungu alizozikataa.Hiyo ndio roho  ya mpinga-kristo.

Hao ndio Bwana, aliotuonya tulichunge kundi lake dhidi yao, ikiwa tumeona mtu ajiitaye mkristo halafu ni mwasherati au mlevi au mwabudu sanamu,tunapaswa tujihadhari naye Hatupaswi kuwashauri watoto wa kiroho(kondoo wa Kristo) kuambatana nao, ni lazima tutawachunga kondoo wa Mungu dhidi yao..Na zaidi ya yote tutawafundisha hila za hao manabii wa uongo, na Roho ya Mpinga Kristo inavyotenda kazi, Biblia inasema

1Wakoritho 5: 9 “Naliwaandikia katika waraka wangu, kwamba msichangamane na wazinzi.
10 Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang'anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia.
11 Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba MSICHANGAMANE NA MTU AITWAYE NDUGU, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang'anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye.
12 Maana yanihusu nini kuwahukumu wale walio nje? Ninyi hamwahukumu hao walio ndani?
13 Lakini hao walio nje Mungu atawahukumu. NINYI MWONDOENI YULE MBAYA MIONGONI MWENU.”
Hivyo tunapoona ndugu yetu, anapotea na uongo wa adui ni jukumu letu sisi,  kumwokoa, hatuwezi tukasema tunampenda Kristo na tukaacha kulipenda na kundi lake, Popote pale tulipo katika hatua yoyote ile ya kiroho, ni wajibu wetu kuwasaidia walio chini yetu..Hata katika familia jukumu la kulea watoto sio la wazazi peke yake, lakini utakuja kukuta kwamba hata watoto wana jukumu la kuleana wao kwa wao..kaka au dada anawalea wadogo zake na hao wadogo wanawalea walio wadogo zaidi. Na katika familia ya Mungu ni hivyo hivyo, ndio jukumu tulilopewa kulishana na kuchungana.

Kuchunga kondoo wa Kristo sio jukumu la mchungaji kanisani tu au muhubiri bali ni jukumu la Kila Mkristo.

Bwana atusaidie sote tuweze kumpenda yeye kweli kweli, KWA KUZISHIKA AMRI ZAKE na KULICHUNGA KUNDI dhidi ya mbwa mwitu wakali lake na KULILISHA chakula cha Neno la Uzima.

Mungu akubariki.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine…

No comments:

Post a Comment