"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, November 9, 2018

KITENDAWILI CHA SAMSONI

Waamuzi 14: 13”......... Basi wakamwambia, Haya, tega kitendawili chako, ili tupate kukisikia. 14 Naye akawaambia, KATIKA HUYO MWENYE KULA KIKATOKA CHAKULA, KATIKA HUYO MWENYE NGUVU UKATOKA UTAMU
 

Kitendawili hichi Samsoni alisukumwa kukisema baada ya kukutana na tukio la ajabu katika safari yake alipokuwa akishuka kwenda Ufilisti yeye pamoja na wazazi wake kwa ajili ya kumchumbia binti aliyekuwa amemwona huko katika kijiji kimoja kilichoitwa Timna. Sasa wakati akiwa njiani alikutana na Simba mwenye nguvu ambaye alitaka kumrarua, lakini Samsoni alipomwona alinyanyuka na kumshambulia kama biblia inavyosema jinsi alivyo mpasua haraka sana ni kama vile mtu anavyompasua mbuzi, Samsoni hakutumia silaha yoyote mkononi, ni kitendo kilichochukua sekunde chache tu, na shughuli yote ilikuwa imekwisha, akaendelea na safari yake.,hilo lilikuwa jambo la kawaida kwake halikumwingia sana moyoni mwake, lakini jambo lililomshangaza ni baada ya kurudi kutoka huko Timna yeye pamoja na wazazi wake na kukuta ule mzoga wa simba umezungukwa na nyuki wengi sana na ndani yake kuna Asali.

Ni jambo la kushangaza! Hata sisi sote tunajua Moja ya wadudu walio wasafi na hawatui katika vitu vilivyo na uozo au uchafu wowote ni NYUKI. Nyuki huwa utawakuta sana sana kwenye maua, mazuri, na kwenye miti yenye matunda na yenye harufu wakitafuta vimelea vizuri vingi tofauti tofauti kwa ajili ya kutengeneza asali yenye ubora ule tunaouna..na kamwe haijajawahi kutokea nyuki kutua kwenye mizoga na miozo, tena cha kushangaza zaidi ndani ya muda ule mfupi kwenye mzoga wa Yule Simba walikuwa tayari wameshatengeneza asali nyingi, na wakati nyuki kutengeneza asali iliyotayari kulika tunajua inachukua sio chini ya miezi 6 na kuendelea.

Hivyo Samsoni kuona jambo lile ilimshtusha sana, mpaka kugundua kuwa lipo somo kubwa ndani yake anapaswa ajifunze, na baada ya kutafakari kwa utulivu sana ndipo akatunga kitendawili kile na kuwapelekea wafilisti.

Akawaambia: “Katika huyo mwenye kula kikatoka chakula, Katika huyo mwenye nguvu ukatoka utamu.(Waamuzi 14:14)”

Samsoni akijua kabisa hakuna hekima yoyote ya kibinadamu inayoweza kukitegua kitendawili kile isipokuwa Mungu au yeye peke yake awafunulie. Na ndio maana ukisoma hiyo habari utaona wale wafilisti walipoona muda wao waliopewa wa kurudisha majibu unakaribia kuisha na bado majibu hawana, wakatumia hila ya kumshawishi Yule binti wa kifilisti aliyekuja kumchumbia amulize Samsoni tafsiri ya kitendawili kile..Na baada ya Yule binti kumbembeleza sana ndipo Samsoni akawafunulia tafsiri yake. Lakini alikasirika sana kwasababu walitumia hila kupata majibu na tafsiri yake ilikuwa ni hii:

Wakamwambia:,NI KITU GANI KILICHO TAMU KULIKO ASALI? NI KITU GANI KILICHO NA NGUVU KULIKO SIMBA?

Kwa lugha rahisi tunayoweza kuielezea kitendawili hicho kwa sasa ni hii “CHAKULA KITAMU KULIKO VYOTE MFANO WA ASALI, HUWA KINATOKA KWA WANYAMA WAKALI NA WENYE VITISHO KAMA SIMBA”...Pia haijabadili maana tukisema “HAZINA KUBWA ZA MAFANIKIO YOTE, HAZIPATIKANI PENGINEPO ISIPOKUWA KATIKA MAZINGIRA YA MAJARIBU MAZITO, AU VITISHO AU MAADUI WAKALI”.

Samsoni hakutazamia kuwa katika yule Simba aliyekuwa anataka kumrarua ndani yake kuna ASALI. Hakutazamia kuwa kutoka kwa Yule adui yake ambaye alikuwa anataka kummeza huyo huyo ndiye atakayeweza kumtolea chakula chake cha kila siku.. Na ndio maana ukisoma habari za Samsoni maisha yake kuanzia huo wakati na kuendelea hakuwahi kuwaogopa maadui zake walipokuja kushindana naye..Ilifika wakati alikuwa anajiona salama zaidi kwenda kulala katikati ya hema za wafilisti [maadui zake] zaidi hata ya alipokuwa nyumbani kwao Israeli ni kwasababu gani? Ni kwasababu alijua kuwa “ katika huyo mwenye kula, ni lazima kitoke chakula tu, na katika huyo mwenye nguvu utatoka utamu nao”.

Ujasiri huo huo aliokuwa ndani ya Samsoni tunaweza kuuona pia ukijidhihirisha ndani ya Manabii wa Mungu miaka mingi baadaye baada ya kufa Samsoni. Ule ujasiri tunauona tena juu ya huyu nabii aliyeitwa ELISHA. Tunasoma habari zake katika 2Wafalme 6. Siku moja mfalme wa Shamu alikasirika sana baada ya kuona siri zake zinafichuliwa na Elisha huko Israeli, Kila alipopanga njama dhidi ya waisraeli Elisha alifunua siri zao na mikakati yao.

Hivyo huyu mfalme wa Shamu akaamua siku moja kupanga majeshi yake yote kuenda kuuhusuru huo mji aliokuwa anaishi Elisha, Na walipoamka asubuhi kumbe jeshi lote la Shamu limewazunguka kama tunavyosoma habari Yule mtumishi wake Elisha aliogopa sana kwasababu alijua siku hiyi ndio mwisho wake umefika, Lakini Elisha alimwambia usiogope simba hawa..Ndipo Yule kijakazi akafunguliwa macho yake na kuona jeshi kubwa la malaika limewazunguka kuwapigania na kuwashindania.

Vivyo hivyo ilitokea wakati huo huo hilo jeshi la shamu liliuzunguka tena mji wa Samaria ili kutaka kuungamiza mji wote na vitu vyao vyote, Elisha naye akiwa humo humo ndani, Hao washami waliuzingira mji wote kwa muda wa siku nyingi, kiasi kwamba hakukuwa hata na mtu wa kuingiza na kutoa chakula mle mjini, matokeo yake kupelekea chakula kupungua sana na uchumi wa mji kuporomoka kwa kiwango kikubwa, njaa ilikuwa kali kiasi kwamba hata mavi ya njiwa yalikuwa ni chakula kinachouzwa kwa kugombaniwa na kwa bei ya juu sana.. Kichwa cha punda nacho kiliuzwa kwa bei ya juu sana, watu walikuwa wanakufa kwa njaa na Elisha naye yupo ndani yake.

Mfalme wa Israeli alipoona Elisha ndiye wakati wa nyuma aliwaombea rehema hao hao maadui zao waliokuja kuwahusu wasiangamizwe, akakasirika sana na kutuma mtu aende kumuua lakini Elisha, hakuwa na wasiwasi wowote wala hofu yoyote, kwasababu alilitambua lile neno kama la Samsoni:

KATIKA HUYO MWENYE KULA, KITATOKA TU CHAKULA, NA KATIKA HUYO MWENYE NGUVU NI LAZIMA UTOKE UTAMU”.

Hivyo Elisha akasubiri mpaka dakika ya mwisho, hakudhubutu kufungua kinywa chake na kumkufuru Mungu kwamba kwanini Mungu amewaacha mpaka wamefikia hatua hiyo? kama walivyokuwa wananung’unika wana wa Israeli kule jangwani. Bali yeye alitulia kimya mpaka Yule mjumbe aliyetaka kuja kumuua alipofika.Na ndipo Neno la BWANA likamjia Elisha na kumwambia Yule mtu.
2Wafalme 7: 1 “Elisha akasema, Lisikieni neno la Bwana; Bwana asema hivi, Kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa Samaria.
2 Basi yule akida, ambaye mfalme alikuwa akitegemea mkono wake, akamjibu yule mtu wa Mungu, akasema, Tazama, kama Bwana angefanya madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akamwambia [Elisha], Angalia, wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula.”.
Unaona? Watu hawakusadiki maneno yale, ni sawa leo hii mtu aseme bei ya gari lililokuwa linauzwa milioni 20 sokoni, kuanzia kesho na kuendelea litakuwa linauzwa kwa shilingi elfu 50...Kwa namna ya kawaida hilo haliwezi kuwezekana, na ndio maana hata Yule mjumbe kutoka kwa mfalme akamdhihaki Elisha na kumwambia hata kama MUNGU angefungulia madirisha ya ngano kutoka mbinguni hilo jambo lisingewezekana..hata kama magari yote ulaya yangetupwa Tanzania kama nguo za mitumba, hilo jambo lisingewezekana unaona?.

Lakini hawakujua kuwa Mungu si wanadamu..Hawakujua kuwa Yule SIMBA aliyekuwa anataka kupambana nao kumbe ndiye aliyewaletea ASALI NYINGI..Wale waliowahusuru pande zote ndio waliowaletea wao chakula.

Angalia jambo Mungu alilofanya. Kumbuka wale nao wasingeweza kuwazunguka wayahudi siku hizo zote bila kuwa na chakula, na nyara, na wanyama wengi na maghala ya nafaka pamoja nao. HIVYO KITU ALICHOFANYA BWANA NI KUWASIKILIZISHA SAUTI YA VITA USIKU WA MANANE, NA VISHINDO VIZITO VYA FARASI NA TETEMEKO la nchi kiasi kwamba wale Washami wakayeyuka mioyo wakidhani kuwa Israeli imekwenda kukodi mataifa jirani ili waje kuwasaidia..Hivyo jambo la haraka haraka ambalo wangeweza kufanya ni kuondoa maeneo yale kwa kasi sana wao kama wao pasipo kuchukua kitu chao chochote.

WALIACHA MAGHALA YAO YA CHAKULA, NYARA ZAO, HAZINA ZAO, FEDHA ZAO, WANYAMA WAO WENGI SANA. Na asubuhi ilipofika wayahudi walishangaa wasione mtu, hivyo wakaenda kuchukua zile nyara zao zote, chakula siku ile kikawepo kingi kiasi kwamba bei ya chakula ilishuka ghafla na kuuzwa kwa bei ile ile Elisha mtu wa Mungu aliisema. Hivyo njaa iliyoikumba mji ilikoma ndani ya siku moja. Na uchumi wa Israeli wote kunyanyuka ndani ya siku moja.

Ni kwasababu gani? Ni kwasababu Elisha alijua katika huyo mwenye kula, kitatoka tu chakula, na katika huyo mwenye nguvu ni lazima utoke utamu”.

Nataka nikutie moyo wewe uliyeamua kuchukua uamuzi wa kumfuata Kristo kwa gharama zozote zile, isitishwe na majaribu yatakapokujia, usitishwe na hila za maadui, usitishwe na vikwazo, fahamu tu huko ndiko utajiri wako ulipo, huko ndiko chakula chako kilipo.. Wana wa Israeli walipokuwa wanapita katika hali ngumu kwa kitambo tu badala ya kuusubiria wokovu wa Mungu wao moja kwa moja walianza kumnung’unikia kana kwamba Mungu anawatesa..

Na ndio maana Mungu hakupendezwa nao kwasababu walikosa ufahamu kuwa mara nyingine kwa kupitia njia zile ndio Mungu alikuwa anawaletea hazina zao. Wakristo tunaomsubiria Bwana tukijifunza kanuni hizi hatutakuwa watu wa manung’uniko tunapokutana na vikwazo, na maadui badala yake ndio tutafahamu kuwa wakati wa mbaraka wetu ndio umekaribia. Yusufu alipopelekwa katika gereza la wafalme mahali ambapo alikuwa anasubiria wakati wowote kukatwa kichwa, kama tu vile alivyomtabiria Yule muokaji wa mfalme kuwa atakatwa kichwa si zaidi yeye aliyekuwa anashutumiwa kwa kulala na mtumishi wa mfalme..alifahamu kabisa yupo pale kusubiria siku ya kukatwa kichwa, lakini hakunung’unika na kulalamika akisema ni kwa nini Mungu mimi ninataeseka huku muda wote huu angali ninalicha jina lako? Hakudhubutu kusema vile, yeye aliongojea tu kwasababu alitambua kuwa

katika huyo mwenye kula, kitatoka tu chakula, na katika huyo mwenye nguvu ni lazima utoke utamu”. Na tunasoma Kutoka kwa Farao ulitoka utamu.

Na kweli ulipofika wakati, Yule Yule aliyekuwa anamtazamia amuue, alikuja kumfanya kuwa waziri wake mkuu.

Hivyo kaka/dada uliyekombolewa kwa damu ya Bwana Yesu, usihangaike huku na kule jaribu linapotokea mbele yako, wala usilione ni kubwa, tulia na utauona wokovu wa Bwana katikati ya hatari, utiwe nguvu katika jaribu lolote unalopitia siku moja Mungu atakuthibitisha kwasababu huko ndiko kutokako utamu wa maisha yako ya sasa na ya baadaye.

Amen!

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.

No comments:

Post a Comment