"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, November 8, 2018

JINA LAKO NI LA NANI?

Bwana Mungu alipowaumba Adamu na Hawa, tunafahamu hakuwaumba wote kwa wakati mmoja, bali alianza kumuumba Adamu kwanza kisha Hawa baadaye, Ndoa ya Adamu na Hawa  ndio ndoa ya kwanza  kabisa kufungishwa, na ilifungishwa na Mungu mwenyewe.

Lakini jambo la kujifunza mara tu baada ya mtu wa kwanza kuumbwa Bwana Mungu, alimpatia jina “Adamu” na baadaye alipomfanya Hawa kutoka katika ubavu wa Adamu hakumpatia jina lolote lile badala yake Adamu ndiye aliyekuja kumpatia jina mkewe na kumwita Hawa..kwasababu alisema yeye ndiye mama wa wote walio hai (Mwanzo 3:20), Lakini jina hilo Hawa halikutoka kwa Mungu bali kwa Adamu. Kwanini Mungu hakumpa Hawa jina hilo tutakuja kuona sababu tutakavyozidi kusoma.

Lakini hebu tutazame kwa ufupi nguvu iliyopo katika jina, katika maisha ya kawaida ukilitaja jina la Raisi wa nchi ni tofauti na jina la Waziri wa nchi, na ni tofauti na jina  la mbunge au balozi, kila jina lina nguvu yake na heshima yake. Jina lenye cheo kikubwa ndilo lenye  nguvu zaidi na heshima kubwa zaidi. Barua ikiandikwa kwa jina la Raisi itaheshimika zaidi kuliko kuliko ikiandikwa kwa jina la Balozi.  Kadhalika biashara yenye jina kubwa ni raisi kupata mapato mengi kuliko, yenye jina lisilojulikana, Kwahiyo unaweza ukaona kuwa jina la mtu au kitu au bidhaa linaweza likabeba nguvu kubwa sana ndani yake.

Sasa Bwana Mungu alimpatia jina mtu wa kwanza, akamwita ADAMU, jina hilo lilikuwa na nguvu ya kutosha na heshima ya kutosha ya kuweza kutiisha na kumiliki fahari  na milki zote za mwilini na za rohoni Bwana Mungu alizompa Mwanadamu. Na ndio maana tunaona mwanamke hakupewa jina lingine lolote na MUNGU,  lilikuwa ni jina moja tu walilopewa na Mungu Adamu na Mkewe, liwapasalo wao kufanyia mambo yote. Tunaweza tukasoma jambo hilo katika kitabu cha Mwanzo..
Mwanzo 5:1-2 “Hiki ndicho kitabu cha vizazi vya Adamu. Siku ile Mungu alipoumba mtu, kwa sura ya Mungu alimfanya; 2 mwanamume na mwanamke aliwaumba, akawabariki AKAWAITA JINA LAO ADAMU, siku ile walipoumbwa.”
Unaona hapo? Akawaita jina lao ADAMU!!, hakumuita mwanamume peke yake ADAMU bali pia alimwita mwanamke ADAMU. Ikiwa na maana kuwa ni Jina moja tu walilopewa liwapasalo wao kutawala na kumiliki milki zote za ulimwengu huu. Heshima yao na nguvu yao ilikuwa ndani ya hilo jina.  Jina Hawa lilitoka kwa Adamu tu kama utambulisho kwa mkewe, lakini mbele za Mungu jina lao lilikuwa ni moja tu nalo ni ADAMU!

Lakini tunaona baada ya Adamu na mkewe kuasi kwa kutokutii maagizo ya Mungu, na kula matunda  waliyoagizwa wasiyale, heshima yao ilishuka, wakafukuzwa  kutoka katika ile bustani ya Edeni. Na hapo ndipo jina lao likashuka thamani. Nguvu ya lile jina ikashuka. Hata simba akawa hamwogopi tena mwanadamu, baadhi ya wanyama badala ya kumwogopa na kumkimbia mwanadamu, wakaanza kutafuta  kumla, ardhi badala umzalie Adamu na mkewe vyakula vizuri ikaanza kumzalia michongoma na miiba n.k

Hivyo Heshima ya mwanadamu ikapotea, na Bwana Mungu kwa kulijua hilo na kwa kumuhurumia mwanadamu, akamleta Adamu wa pili, ambaye angempa jina lisiloweza kuharibika, ili kwa jina hilo aweze kurudisha heshima na milki zote ambazo mwanadamu wa kwanza kazipoteza,

 Adamu huyu wa pili naye pia anaye mke wake aliyetwaliwa kutoka ubavuni mwake lakini mke wake sio wa mwilini bali wa rohoni.  Na Adamu huyu wa pili ni YESU KRISTO ambaye mkewe wake NI KANISA LAKE TEULE ALILOLITOA KUTOKA UBAVUNI MWAKE PALE KALVARI, walipomchoma mkuki ubavuni kulitoka MAJI na DAMU, ikifunua kuwa kanisa lake linazaliwa kwa DAMU YAKE iliyomwagika pale Kalvari na Linazaliwa kwa MAJI..Haleluya..

2Wakorintho 11: 1 “Laiti mngechukuliana nami katika upumbavu wangu kidogo! Naam, mchukuliane nami. 2 Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; KWA KUWA NALIWAPOSEA MUME MMOJA, ILI NIMLETEE KRISTO BIKIRA SAFI3 Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo”.

Unaona hapo? Na kama vile Mungu hakumpa mkewe Adamu jina lingine vivyo hivyo na Mke wa Bwana Yesu Kristo hakupewa jina lingine lolote isipokuwa jina la Yesu.

Matendo 4: 12 “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, KWA MAANA HAPANA JINA JINGINE CHINI YA MBINGU WALILOPEWA WANADAMU LITUPASALO SISI KUOKOLEWA KWALO”.


Hivyo jina la bibi-arusi(mke) wa Yesu Kristo linalojulikana mbinguni ni moja tu nalo si lingine zaidi ya YESU. Ndilo alilopewa na Baba,  Yohana 17: 6 “Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu; walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika”.

Ukisoma Yohana 1:25-26 utaona tena jambo hilo:

 “Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua; lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma. Nami naliwajulisha JINA LAKO, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.”

Hivyo malaika au mapepo wakimwona bibi-arusi wa Kristo popote  pale ni sawa na wamemwona Yesu Kristo mwenyewe, Sasa Katika hilo Jina bibi-arusi wa Kristo anaokolewa,  hilo hilo anabatiziwa, anaponywa magonjwa yake, anafanya miujiza yote na zaidi ya yote amepewa mamlaka ya kufanya chochote  atakacho kwa jina hilo.

Wakolosai 3.17 “na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote KATIKA JINA LA BWANA YESU, MKIMSHUKURU MUNGU BABA KWA YEYE”.

SASA BIBI-ARUSI WA KRISTO NI NANI?

Bibiarusi wa Kristo ni mtu yeyote aliyemwamini na kumkubali Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yake, aliyetubu dhambi zake zote kwa kumaanisha kuziacha, na kusafishwa kwa DAMU yake na kusafishwa kwa MAJI ambalo ni Neno lake, ambao ni UBATIZO wa Maji MENGI katika Jina LAKE, yule anayeishi maisha matakatifu na ya kujichunga wakati wote huyo ndiye bibi-arusi wa Bwana Yesu au mke wa mwanamkondoo.

Je! wewe ni bibi-arusi wa Kristo? Kumbuka huwezi ukamiliki chochote kama jina lako halijabadilishwa, je! mbinguni unajulikana kama nani? Adamu na Mkewe walijulikana kama ADAMU, Kadhalika Kristo na wateule wake wanajulikana kwa jina moja nalo ni Jina la Yesu, je! na wewe ni miongoni mwa kundi  lililobadilishwa jina na kupewa jina la Yesu?? kama hujazaliwa mara ya pili na kuwa bibi-arusi wa Kristo huwezi kuwa na jina hilo. Heshima yako katika ulimwengu wa roho bado haipo,hofu itakusumbua,  magonjwa yatakutesa, nguvu za giza zitakutesa, mauti itakuandama, na mambo yote mabaya yatakuwa sehemu yako. Kwasababu haupo chini ya Jina moja lililoadhimishwa na Mungu kwa ukombozi.

Wafilipi 2: 9 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, AKAMKIRIMIA JINA LILE LIPITALO KILA JINA;  ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;”
11 na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.”

Ni maombi yangu kuwa huyu Bwana Yesu, asikupite leo hii, kama hujampokea Yeye umpokee leo, ayageuze maisha yako, na akuingize katika milki ya watu wa Mungu, na kwa jina lake akulinde, upate ushindi angali muda bado upo. Kwasababu jina hilo ni ngome IMARA. Kumbuka Jina la YESU linakaa ndani yako na sio ulimini mwako. Likiwepo humo basi lolote utakalolitamka kwa ulimi wako litafanikiwa sawa na mapenzi yake. Lakini ikiwa hautaokolewa au upo vuguvugu jina la YESU halina nguvu yoyote ndani yako.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na Mungu atakubariki.

No comments:

Post a Comment