"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, November 5, 2018

TUNAYE MWOMBEZI.

Maombolezo 3:22 Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi.
23 NI MPYA KILA SIKU ASUBUHI; Uaminifu wako ni mkuu.
24 Bwana ndiye fungu langu, husema nafsi yangu, Kwa hiyo nitamtumaini.
Jina la Bwana na mwokozi wetu YESU KRISTO lihimidiwe milele. Leo ni siku mpya ambayo Bwana aliibuni tangu zamani kwa ajili yangu mimi na wewe ili tuiishi, tulipoamka asubuhi leo tumebahatika kupewa neema ya kusikia sauti nzuri ya milio ya ndege ikimsifu Mungu kwa furaha mitini, Tukikumbuka kuwa Leo tu ya tarehe hii yenyewe zaidi ya watu 151,600 watakufa ulimwenguni kote hiyo ni kulingana na takwimu za sensa ya dunia, lakini mimi na wewe Bwana ametukirimia neema zake za kipekee, sio tu kuamka salama bali pia kupata nafasi ya kufungua simu zetu na kuingia mitandaoni na kutazama yaliyojiri huko, mpaka unapokutana na ujumbe huu..

Unadhani utakuwa umefanya jambo gani jema mbele za Mungu mpaka uifikie siku ya leo?. Jaribu kifikiri juu ya hilo, je! Ni utakatifu wako?, je! Ni kwasababu unayo afya? Je! Ni kwasababu wewe ni kijana?.

Utagundua ni huruma tu za Bwana kwamba hatuangamii..Mungu anatuhurumia ndugu yangu, rehema zake ikishaitwa tu LEO asubuhi zinakuwa mpya tena kana kwamba hazikuwepo jana na juzi, zinakuwa mpya kama vile leo ndio mara ya kwanza kuachiliwa juu yetu..Mara nyingi tunamkosea Mungu wetu kwa namna zote lakini REHEMA zake ni nyingi kwa watu wote. Yaani Kwa waliookolewa na kwa wale ambao hawajaokolewa, wote rehema za Mungu zinakaa juu yako kwasababu yeye mwenyewe alisema anawaangazia jua na kuwanyeshea mvua yake wote waovu na wema.

Hivyo kwa sisi TULIOOKOLEWA pale tunapokaribia kuzama katika maji ya mauti kutokana na mapungufu yetu au madhaifu yetu na majaribu mazito hakika tunaye mwombezi wetu naye ni YESU KRISTO Bwana wetu, yeye pekee ndiyo hiyo hizo REHEMA YA MUNGU KWETU, na HURUMA yake Mungu kwetu. Biblia inasema katika 1Yohana 2:1 Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki...

Unaona yeye Bwana kila ikiitwa Leo anatupelekea dua zetu kwa Baba, hakika sifa na heshima na utukufu tunamrudishia yeye kwa upendeleo huu wa ajabu..Na kama sio yeye leo hii sisi tunaoitwa watakatifu tungeshaangamia siku nyingi. Siku ile tungewezaji kusimama kwa haji yetu?. Hakika Wana AMANI tele wote walio katika Kristo YESU siku zote. Haleluya.

Lakini kwa ambaye hajaokolewa naye pia rehema za Mungu zipo juu yake: Lakini ni kwasababu gani haangamii?. Sio kwamba Bwana YESU yupo anamwombea juu mbinguni hapana?, yeye hilo halimuhusu kwasababu wakati Bwana angali akiwa hapa duniani hakudhubutu kufanya jambo kama hilo kwa yeyote Yule asiyeupande wake bali yeye mwenyewe alisema katika Yohana 17: 9 "Mimi nawaombea hao; SIUOMBEI ULIMWENGU; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako;".

Unaona hapo mtu mwenye dhambi haombewi lolote na Bwana YESU, ni mtu aliye katika hukumu siku zote akisubiria siku ile kusimama mbele ya kiti cheupe cha enzi cha Mungu ahukumiwe kisha atupwe katika lile ziwa la moto, lakini kama ni hivyo basi ni kwanini haangamii?.Ni kwanini mpaka leo anaishi, anapumua, ana afya, anafanikiwa, angali YESU hamwombei juu mbinguni?. Ni kwanini mpaka leo shetani hatamwangamiza?

Ni kwasababu moja tu ambayo hiyo tunayoisoma katika,
Ezekieli 33: 11 Waambie, Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa, Enyi nyumba ya Israeli?
Ezekieli 18: 23 Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? Asema Bwana MUNGU; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi?

Unaona ni kwasababu gani huangamii ewe mtu mwovu?..Ni kwasababu Rehema za Bwana zimekushikilia mpaka sasa ili UTUBU. Unafahamu kabisa maisha unayoishi nje ya Kristo huna raha nayo,unastahili kwenda kuzimu, lakini bado unazidi kuishi hivyo!, unafahamu kabisa uzinzi na ukahaba unaoufanya utakupeleka jehanum lakini bado unazidi kudumu katika mambo kama hayo, unafahamu kabisa ukiwa nje ya YESU KRISTO hutaweza kusalimika, hutaweza kuikwepa hukumu ya Mungu, lakini ni kwanini unaendelea kufanya hivyo?. Idadi kubwa ya watu wanaokufa leo haumo katikati yao, unadhani hao waliokuwa na dhambi nyingi sana kuliko wewe?.

Siku ya leo ni mpya, rehema za Bwana zipo juu yako, zikikuvuta utubu, lakini usipofanya hivyo leo, ipo siku mauti itakukuta kwa ghafla na kule uendapo utaufichia wapi uso wako? utakuwa ukijutia siku zile zote neema ya Mungu ilipokuwa inakupigia kelele masikioni kila siku asubuhi utubu lakini hukutaka. Yatakuwa ni majuto makubwa kiasi gani?

Ndugu kwa haya maneno machache, ikiwa Kristo hayupo ndani yako leo, fanya uamuzi wako binafsi sasa. Unachopaswa kufanya ni wewe mwenyewe utubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kabisa kuziacha, uamue kabisa kuanzia sasa unaanza maisha mapya ndani ya Kristo YESU. Kumbuka toba ni kugeuka na sio kuongozwa sala Fulani tu. Wewe peke yako chukua uamuzi wa kugeuka hiyo ni bora zaidi ya sala yoyote unayoweza kuongozwa, na ikiwa toba yako imetoka moyoni kweli kweli na sio kidesturi za kidini au kimazoea. Basi uwe na uhakika Bwana amekusamehe.

Lakini hiyo peke yake haitoshi, Biblia inasema “aaminiye na KUBATIZWA ataokoka (Marko 16:16)”. Hivyo unaukamilisha wokovu wako kwa kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na uwe katika jina la YESU KRISTO..hapo utakuwa na uhakika wa kupata ondoleo la dhambi zako, na kisha kuanzia huo wakati Bwana atakupa Roho wake MTAKATIFU akulinde mpaka siku ya ukombozi wa mwili wako, yaani unyakuo (Matendo 2:38).

Kumbuka ubatizo sahihi ni muhimu, ikiwa ulibatizwa ulipokuwa mchanga, au ulibatizwa kwa kunyunyiziwa maji, au ulibatizwa kidini tu, au kimazoea na haukutubia dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha siku ulipobatizwa, basi ni sharti ukabatizwe tena kwa ubatizo wa maji tele na kwa jina la YESU KRISTO, na sio kwa jina la Baba na mwana na Roho Mtakatifu kama inavyofanyika kimakosa kwa watu wengi, bali kwa jina lake Yesu Kristo ili upate ondoleo la dhambi zako, Hiyo ni kulingana na vifungu hivi vya maandiko (Mdo 2:38, mdo 8:16, ,mdo 10:48, na mdo 19:1-5).

Hivyo ukiwa utazingatia hayo yote, na kuyaishia maisha matakatifu Bwana akubariki kwa kuwa hapo utakuwa umezaliwa mara ya pili. Na ndio kuanzia huo wakati wewe nawe unakuwa na MWOMBEZI mbinguni, ambaye hapo kwanza haukuwa naye..Naye si mwingine zaidi ya BWANA YESU KRISTO kuhani wetu mkuu aliyetupatanisha sisi na Mungu kwa damu yake. Utukufu na heshima na enzi vina yeye milele na milele AMINA.

Ikiwa utatenda dhambi pasipo kujijua, au dhambi ya kutokukusudia au dhambi ya madhaifu yeye yupo siku zote kukuombea mbele za BABA, akulinde na Yule mwovu kwa Kuwa Kristo ameshakuwa mtetezi wako basi mbele za Mungu ukiwa chini hiyo neema hauhesabiwa kuwa na hatia makosa yako yanasitiriwa kwasababu rehema zake hazitakoma juu yako milele na milele. Na hatuhesabiwi haki kwa matendo ya sheria bali kwa Neema;

Ndio lile neno lililosemwa na manabii hapo linatimia..

Warumi 4:6 "uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo,
7 Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao.
8 Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi."

Hivyo ubarikiwe wewe uliyechagua uamuzi huu bora wa kumwamini YESU KRISTO.

Tafadhali “share” habari hizi kwa wengine.

No comments:

Post a Comment