"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, November 16, 2018

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 42


SWALI 1: Mimi nimeokoka lakini kuna siku niliota ninasalimiana na mtu na ghafla katika mkono wake nikahisi kuna vitu vinakata, na nilipoamka nikahisi maumivu kiganjani na baada ya kuchungumza kwa makini niligundua nimechanjwa. Ninaomba ushauri wako nifanye nini?

JIBU: Ingekuwa ni ngumu kwa mtu ambaye sio mkristo kumshauri lakini kwasababu umesema wewe umeokoka basi ukijikuta katika mambo kama hayo huna haja ya kuwa na hofu biblia ilishatupa mwongozo katika

Marko 16: 17” NA ISHARA HIZI ZITAFUATANA NA HAO WAAMINIO; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;
18 WATASHIKA NYOKA; HATA WAKINYWA KITU CHA KUFISHA, HAKITAWADHURU KABISA; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”

Mstari wa 18 unasema “WATASHIKA NYOKA, hata wakinywa kiu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa”. Jiulize ni kwanini hakusema “, hawatakunywa kabisa kitu cha kuwafisha(kuwadhuru) kwasababu wao ni waaminio?”.

Unaona kuna mazingira mengine Mungu anaruhusu mkristo yeyote akumbane nayo japo hastahili kukutana nayo ili nguvu za Mungu zionekane, ili Ishara hizo zionekane. Mtu anakuwekea sumu ya mamba kwenye chakula unakula, sumu ambayo hazipiti dakika 10 unakuwa umeshakufa, lakini Mungu anaruhusu uile kusudi kwamba wale waliokufanyia hivyo wapate kusadiki kuwa Mungu wako ndiye Mungu ikiwezekana wao nao waokoke.

Mtume Paulo alipokuwa katika kisiwa kimoja kiitwacho Melita akiwa kama mfungwa wakati anaota moto usiku NYOKA alitokea na kumuuma, wenyeji wa kijiji kile walimwona Paulo kama mtu mwenye LAANA kwa kuona kitendo kile cha kuumwa na nyoka, lakini baada ya muda kidogo walipogundua kuwa sumu ya yule nyoka haikuwa na madhara yoyote katika mwili wa Paulo, wakageuka wote na kumwamini Mungu aliyekuwa ndani yake. Lakini je! tuliona Paulo akianza kukemea? au kuanza maombi ya mkesha? au kuhangaika huku na kule kutafuta suluhisho? Hapana, kinyume chake tunaona alimtupa nyoka kwenye moto na kuendelea na shughuli nyingine.

Lakini jiulize Paulo kama Mtumishi wa Mungu ni kwanini Mungu hakumwepusha na hatari kama zile? Kwanini Mungu hakumwepusha yule nyoka asimng’ate kabisa? Lakini badala yake aliruhusu amng’ate Unajuaje kama yule nyoka alikuwa ni wa-kichawi ametumwa ili kumdhuru Paulo?.

Vivyo hivyo na wewe pia, ikiwa ni mkristo, huna haja ya kuwa hofu, ikiwa umekuta hirizi ndani kwako, zikusanye kazichome moto, unasikia paka wanalia darini toka nje wafukuze, umekuta nyoka ndani mtoe nje mchome moto, umelala usiku na umeamka asubuhi umekuta wamekuchanja, mikononi, au usoni, au masikioni au mwili mzima, ikiwa wamechukua nywele zako, au nyayo zako, au nguo zako wewe waongezee na mashuka kwasababu uwe na uhakika kuwa hakuna madhara yoyote yatakayokuja juu yako kwasababu wewe ni mwaminio [MKRISTO], na ishara zile zinafuatana na wewe. Kinyume chake mambo hayo yatabadilika kuwa ushuhuda kwao, na kumtambua Mungu aliyeko ndani yako NDIYE MUNGU, na itakuwa fursa ya wao kuokoka.

Hivyo uwe na amani tu.
Ubarikiwe

SWALI 2: Ndugu zangu Mtume Paulo alikuwa na maana gani kusema 1Wakorintho 15:31"...,NIKAKUFA KILA SIKU?

JIBU: Katika ukristo KUFA kupo kwa namna mbili:

>Aina ya kwanza ni kufa kwa habari ya dhambi.

>Aina ya pili ni kufa kwa ajili ya Ndugu: Yaana kuwa tayari
kuiponza roho yako, mpaka kufikia hatua ya kuweza kuitoa roho yako kwa ajili ya injili na kwa ajili ya Kristo.

Ukristo sio wa leo na kesho halafu basi, Tunapokuwa wakristo inamaanisha tunajikana nafsi zetu kila siku, na kumwishia Mungu siku zetu zote zilizobakia na ndio maana Bwana YESU alisema: “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake KILA SIKU, anifuate.
24 Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. (Luka 9:23-24).

Unaona hapo, ni kuchukua msalaba wako na kumfuata KILA SIKU na sio siku moja au mbili kisha basi,.Kwa lugha iliyo rahisi ni kwamba kila siku unapaswa UFE kwa habari ya ulimwengu na uwe hai kwa habari ya Kristo. Unakufa kila siku kwa habari ya fashion za ulimwengu huu, unakufa kila siku kwa kampani za marafiki wabovu, unakufa kila siku kwa habari ya matusi, kila siku unakufa kwa habari ya uasherati na tama zake kwa kujiweka mbali nazo, unakufa kwa habari ya rushwa, unakufa kwa habari ya usengenyaji, na anasa n.k.

Kadhalika pia tunapoona ndugu zetu walio wachanga na wanahitaji msaada wa kiroho wa injili kutoka kwetu nasi tunajua kabisa tusipofanya hivyo wataangamia, hapo pia tunagharimika kuwaendea kwa gharama zozote zile bila kujali ni hatari gani tutakumbana nayo huko mbeleni kama vile mtume Paulo alivyokuwa anasema..Bila kujali jamii itakutenga vipi, bila kujali serikali itapingana nawe vipi, bila kujali watu wenye chuki watakuvizia muda wowote kukuua, bila kujali watu wa dini wanakuchuliaje n.k.

Sasa huko ndio KUFA KILA SIKU WA AJILI YA KRISTO. Lakini ikiwa maisha yetu kila siku yatakuwa hivyo hayana mabadiliko yoyote, kila siku tunaonakena hatuna tofuati na watu wa ulimwengu. Hiyo ni dalili tosha kutuonyesha kuwa bado hatujamfauta Kristo..

Ubarikiwe.

SWALI 3: Biblia inasema Unapo soma usipunguze wala usiongeze neno, JE? huko kuongezea au kupunguza ni kama vipi.ambako tunakatazwa?

JIBU: katika hali ya kawaida mtu anapozungumza maneno mengine ya uongo ambayo wewe hujasema mtu huyo ni sawa na kakuongezea maneno… Kwamfano mtu anapokwenda kutoa ushahidi mahakamani ya kwamba amekusikia ukisema maneno Fulani na angali wewe hujasema hayo maneno,na anafanya vile kwa makusudi mtu huyo atakuwa ni kama amekuongezea maneno, Vivyo hivyo na kwa Mungu mtu anapotoa ushuhuda wa uongo kuhusu Mungu, au anapofundisha jambo la uongo kinyume na Neno la Mungu na anafanya vile makusudi kwa nia ya kupotosha, mtu huyo ni sawa na ameongeza neno katika maneno ya Mungu na Biblia inasema ataongezewa mapigo katika siku ile (Ufunuo 22:18).

Kwamfano maandiko yanasema “Mtu ameandikiwa kufa mara moja na baada ya kifo ni hukumu Waebrania 9:27” Lakini inatokea mwalimu au mtumishi analijua hilo andiko na maana yake lakini badala ya kuwafundisha watu hilo, anawapotosha na kuwaambia hakuna hukumu baada ya kufa, au mtu baada ya kufa anakwenda toharani kutakaswa kisha mbinguni baadaye hata kama alikufa katika dhambi, Hivyo anaendelea kuwafariji watu wazidi kudumu katika dhambi zao..huyo ni sawa na ameongeza Neno katika maneno ya Mungu..

Kadhalika kupunguza maneno inatokea pale mtu anapoujua ukweli na hauhubiri wote kama inavyopaswa, pengine kwa hofu Fulani, au kwasababu anaogopa kutengwa, au kuchukiwa…mtu kama huyo ni sawa na amepunguza Neno kati ya maneno ya Mungu, na hivyo atapunguziwa sehemu yake (yaani thawabu yake) katika ule mti wa Uzima, na katika ule mji Mtakatifu Yerusalemu ya Mungu katika siku ile.(Ufunuo 22:19).

Kwamfano Maandiko yanasema { Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; KWA MAANA KILA AFANYAYE MAMBO HAYO NI MACHUKIZO KWA BWANA, MUNGU WAKO. (Kumbu.22;5}, sasa kwamfano Mwalimu, au muhubiri au mchungaji, akilijua hili na hawafundishi wanafunzi wake , au washirika wake,mambo kama hayo kwa hofu Fulani labda watamchukia, au watamkimbia sasa mtu kama huyu ni sawa na amepunguza Neno katika Maneno ya Mungu na hivyo sehemu yake pia itapunguzwa katika mji ule.

Kwahiyo tunapaswa tulichukue Neno la Mungu kama lilivyo bila kupunguza makali yake, au kuongeza shuhuda zipinganazo na Neno la Mungu kwa lengo la kuwapotosha watu.

Ubarikiwe.

No comments:

Post a Comment