Lakini ili uonekane kuwa umestahili kupokea URITHI huo utakaokuja kufunuliwa kwa wana wote wa Mungu siku ile ya mwisho ya unyakuo, ni lazima kwanza kwa namna moja au nyingine upitie njia kama aliyopitia BWANA YESU KRISTO alivyokuwa hapa duniani. Ni lazima Bwana aisafishe kwanza nyumba yake, na mambo yote machafu. Hatuwezi kuwa warithi na tabia zetu chafu tulizotoka nazo huko ulimwenguni. Hatuwezi kuwa wasengenyaji, halafu kule tukawe warithi wa uzuri Mungu aliwaandalia watakatifu wake, hatuwezi tukawa na viburi halafu tuingie uzimani hivi hivi kiwepesi, hatuwezi tukawa watukanaji, wawakaji wa tamaa, waabudu sanamu, waongo halafu tukamilikishwe mambo matukufu makuu namna ile kiwepesi wepesi tu. Ni sharti kwanza hayo yote yasafishwe. Na yakishasafishwa sasa hatuna budi kukionja kikombe cha mateso kama kile alichokinywa Bwana.
Kama YESU alikuwa ni mkamilifu bila dhambi yoyote [yeye aliyekuwa mti mbichi] lakini alionja sehemu ya HUKUMU YA MUNGU kwa ajili ya makosa yetu, itakuwaje kwa sisi tulio miti mikavu?. Hatuwezi kuikwepa hukumu yake. Hivyo kwa mtu yeyote aliye mwaminio wa kweli HUKUMU hii pia lazima ipite juu yake. Ambayo hiyo inakuja hapa hapa duniani. Tofuati na Hukumu ya watu waovu, yao itakuja baada ya kifo. Ambapo huko hakuna kutubu, mtu akishaonekana amesimama mbele ya Kiti cheupe cha Enzi cha mwanakondoo basi jua mtu huyo moja kwa moja ni kwenye ziwa la moto, kwasababu huko hakuna tena msamaha.
Hivyo hukumu hii ya Mungu itakuja juu ya mwaminio kwa namna zote mbili: Yaani pale ATAKAPOFANYA KOSA kadhalika na pale ATAKAPOISHI MAISHA MASAFI YA HAKI. Katika zote mbili hukumu ya Mungu lazima itamfiikia.
1) MTAKATIFU ATAKAPOISHI MAISHA YA HAKI:
“1Petro 4: 4.13 Lakini kama MNAVYOYASHIRIKI MATESO YA KRISTO, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.14 MKILAUMIWA KWA AJILI YA JINA LA KRISTO NI HERI YENU; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia.15 Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine.16 Lakini ikiwa kwa sababu ni Mkristo asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo.17 KWA MAANA WAKATI UMEFIKA WA HUKUMU KUANZA KATIKA NYUMBA YA MUNGU; na ikianza kwetu sisi, mwisho wao wasioitii injili ya Mungu utakuwaje?18 NA MWENYE HAKI AKIOKOKA KWA SHIDA, YULE ASIYEMCHA MUNGU NA MWENYE DHAMBI ATAONEKANA WAPI?19 Basi wao wateswao kwa mapenzi ya Mungu na wamwekee amana roho zao, katika kutenda mema, kama kwa Muumba mwaminifu".
Unaona? Kama vile Bwana Yesu alivyopitia makwazo, na majaribu mazito namna ile mpaka kufikia hatua ya kudhihakiwa na kutukanwa, na kutemewa mate, na huku hajafanya jambo lolote listahililo kutendewa mambo hayo, hakutenda dhambi yoyote kustahili msalaba, hakumdhulumu mtu yeyote kustahili kupigwa makofi, lakini aliyapitia hayo, sio kwamba alimkosea Mungu, hapana, bali Mungu aliridhika kumfanya ayapitie yale, ili aitimize HUKUMU ile juu yake ili mbele zake aonekane kama amestahili kuzipokea Ahadi zote alizokuwa amemwahidia za kumfanya awe mrithi wa vyote. Biblia inasema..
Isaya 53: 4 “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; LAKINI TULIMDHANIA YA KUWA AMEPIGWA, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.
5 Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu;..
9 Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.
10 LAKINI BWANA ALIRIDHIKA KUMCHUBUA; AMEMHUZUNISHA; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi, Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake;
11 Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki Atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao”.
Kama tunavyoona maandiko yanasema “TULIMDHANIA KUWA AMEPIGWA NA MUNGU”..Bwana Yesu kupitia majaribu kama yale mpaka kusulibiwa kwa aibu msalabani watu walidhani kuwa Mungu ndiye aliyemlipizia maovu yake, ya kujifanya kuwa yeye ni sawasawa na Mungu. Lakini Mungu alimuhukumia adhabu ile kwa ajili yetu, “Mungu aliridhika kumchubua na kumuhuzunisha” ili mwisho wa siku aje kuona wingi wa uzao Mungu alimwandalia kwa kupitia yeye, ili baadaye aje kuona matunda ya taabu yake biblia inasema hivyo, jinsi atakavyomiliki mataifa mengi na wafalme wengi. Na ndio maana mpaka sasa unaweza kuona ni jinsi gani KRISTO anamiliki kila kitu sasa hivi, Jina lake linaitwa kila mahali duniani kote, katika vizazi vyote na hapo bado ufalme wake haujaanza, siku ukija kuanza duniani ndipo tutamwelewa vizuri yeye ni kwanini anaitwa BWANA WA MABWANA na MFALME WA WAFALME.
Vivyo hivyo na sisi ambao tutakuwa warithi pamoja na yeye. Kusudi kwamba tuonekane tumestahili kuzirithi hizo ahadi nono ambazo Mungu kawaandalia watoto wake, yapo mambo tutayapitia kwa ajili ya imani yetu. Ni kweli inajulikana kila mahali kuwa mtu akiwa mwenye haki, hawezi kuudhiwa au kushitakiwa kwa namna yoyote ile, lakini kwa mkristo ni kinyume chake. Mungu kaiweka hivyo kwa makusudi yake, hiyo ndiyo HUKUMU yake kwa wana wake.
Kwa mfano unaweza ukashangaa hapo mwanzo ulikuwa ni fisadi, lakini ulipomwamini Kristo tu na kuacha ufisadi, badala ya wale wanaoupinga wakufurahie ghafla unashangaa ndio wanaanza kukuchukia, ulikuwa ni mhubiri feki, wa injili za juu juu tu, za kuwachekesha watu madhabahuni, lakini ulipoamua kuchukua uamuzi wa kusimama katika imani, na kuanza kuihubiri ile injili ya mitume,sasa badala ya kufurahiwa ghafla makasisi wenzako wanaanza kukuangalia vibaya na kukutenga, na kukukataza kuhubiri mbele ya makanisa yao. Ulipokuwa katika dhambi ndugu na marafiki hawakuwa na neno lolote juu yako. Lakini siku ulipoamua kumfuata Kristo badala wakufurahie umekuwa mtu mwema, ndio kwanza wanaanza kukuzungumzia vibaya, wanaanza kukuchukia bila sababu, wanaanza kukuwekea vinyongo, wanaanza kukuwekea mitego isiyo na sababu ukitazama kosa lako hulioni.
Mtume Paulo aliliona hilo tangu zamani na kusema 2Timotheo 3:12 “Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu WATAUDHIWA”.
Wafilipi 1: 29 “Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake;”
Hivyo ndugu mkristo, usishangae wala usiogope unapoyapitia haya, kwasababu ya Imani yako, unapopigwa, unapofungwa, unapotengwa, unapoachwa jua tu hiyo ni hukumu ya Mungu inapita juu yako, hata mitume walipitia kadhalika na wakristo wenzako duniani wanapitia hivyo hivyo ili siku ile uonekane kuwa umestahili kupata vinono vya ufalme ule usikuwa na mwisho kama Bwana Yesu yalivyomkuta ni sharti upitie hapo..Jua tu hivyo ni vya kukutengenezea TAJI bora utakapoingia katika ufalme ule. Wakati mwingine utashangaa kuona misiba ya watu wako wa karibu, au utapoteza vile uvipendavyo kwasababu umeamua tu kumfuata Kristo, utapitia njaa, utapitia shida, n.k. Lakini kuwa na uhakika kuwa hujapoteza lolote, hiyo ni hukumu ya Mungu itakayopita juu yako kwa muda.
Sasa biblia ndio inakuja kusema IKIWA MWENYE HAKI ATAOKOKA KWA SHIDA NAMNA HIYO?. Asiye mcha Mungu na mwenye dhambi ataonekania wapi?. Ndugu hukumu za Mungu si za kuzitamani kabisa. Ikiwa huyu ambaye anamcha Mungu leo hii unamwona yupo katika dhiki,na pengine taabu. Ikiwa watakatifu ndio unawaona kuwa wenyewe ndio watu wa bahati mbaya. Wewe ambaye sasa huna habari na Mungu siku ile utaonekania wapi? Ni nani atakayasimama badala yako kukutetea siku ile?.
Leo hii watu wanaowadhihaki watakatifu na kusema hawana uelekeo wowote, wana shida, wamepoteza dira ya maisha, maisha yao ni ya dhiki, hawana mbele wala nyuma, hawajui hata wale wayahudi walimwambia hivyo hivyo Bwana Yesu. Walisema ngoja sasa tumuue tuone huyo baba yake kama atakuwa na uwezo wa kumshusha msalabani, . Na walipoona hajashushwa msalabani waliendelea kudhihaki, hakisema huyo Mungu mbona hamsaidii? lakini hawakujua kuwa Mungu ndiye aliyeridhika kumchubua,.Ikiwa Bwana Yesu ambaye hakuwa na dhambi aliupata ule ufalme kwa taabu vile, sisi ambao leo hii tunaudharau wokovu na njia ya msalaba tutaonekania wapi siku ile.?.
2) MTAKATIFU ATAKAPOMKOSEA MUNGU.
Leo hii watakatifu wakimkosea Mungu kwa kosa linaloweza kuonekana kuwa dogo, inawagharimu adhabu kubwa sana hata wakati mwingine kupoteza maisha yao kama ilivyokuwa kwa Hanania na safira (Matendo 5), kwa kosa kutokutimiza tu nadhiri zao walikufa wote wawili pale pale.
Kumbukumbu 8: 5 “Nawe fikiri moyoni mwako, ya kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo Bwana, Mungu wako, akurudivyo”.
Sasa hao walio waasherati, na waabudu sanamu, na washirikina, na wenye dhambi wote ambao hawataki sasa kuyasalimisha maisha yako kwa Bwana. siku ile watastahimili vipi ile hukumu?. Pengine utatoka leo kuzini na usione chochote, utatoka leo kuua na jambo lolote baya lisikutokee, utakwenda kulawiti na ubaya wowote usikupate. Utakwenda kuloga na usikutwe na ubaya wowote, Sio kwasababu Mungu hakuoni au wewe ni mtu wa kipekee sana kwake zaidi ya Yule anayemcha yeye na kupitia mabaya. Hapana fahamu tu jambo moja, Hukumu ya waovu sio sasa. Bali ni baada ya dunia hii yote kuisha. Siku ile mataifa yote yatakaposimama mbele ya kiti cha huku cheupe cha enzi cha mwanakondoo na kila mmoja atakapotoa hesabu ya mambo yake yote aliyokuwa anayafanya hapa duniani. Sio kutamani kuwepo siku hiyo. Kumbuka watakatifu wale walimwamini Kristo wakati huo hawatakuwepo.
Huu si wakati wa kuchekezea maisha yako, Kila mtu anajua kuwa haya ni majira ya kurudi kwa Bwana Yesu mara ya pili duniani, Kila mtu anajua kuwa dhiki kuu ipo mlangoni kuanza, na Yule mpinga-kristo kunyanyuka. Sasa unasubiri nini usitengeneze maisha yako sasa?.
Ikiwa mwenye haki akiokoka kwa shida, yule asiyemcha Mungu na mwenye dhambi ataonekana wapi?.
Ni furaha yangu, ukigeuka sasa angali muda upo.
Tafadhali hubiri habari njema hizi kwa wengine.
No comments:
Post a Comment