"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, November 30, 2018

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 44

SWALI 1: Ni sahihi mtu kubatizwa kwenye maji ya KISIMANI?.

JIBU: Kwanza ni muhimu kufahamu maana ya hili neno UBATIZO.Hili ni neno la kiyunani lijulikanalo kama (BAPTIZO), lenye maana ya"KUZAMISHWA". Kwahiyo kama tafsiri ya jina lake ilivyo, mtu anapobatizwa ni lazima azamishwe mwili wake wote katika maji, Na kumbuka haisemi ni katika mto, bahari, ziwa, au kisima, n.k. La! Maagizo yametolewa ni kuzamishwa.

Kwahiyo Hakuna tatizo lolote mtu kubatizwa/kuzamishwa kisimani, ili mradi tu, maji yawe mengi ya kuweza kumzamisha mwili wake wote, hivyo iwe kwenye mto, kisima, chemchemu, pipa au baharini au kwenye dimbwi, popote pale la muhimu ni azamishwe mwili wote uzame usionekane na abatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Ubatizo mwingine wowote tofauti na huo ni Batili. Hivyo Mtu huyo anapaswa akabatizwe tena.Kumbuka Nyakati za mtume Paulo kulikuwa na watu waliokuwa wanaujua ubatizo tu wa Yohana wa Toba, hawakuufahamu ubatizo uletao ondoleo la dhambi, Lakini Paulo alipowahubiria na kuamini wakabatizwa tena kwa ubatizo sahihi soma..

Matendo 19: 1 "Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko;
2 akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia.
3 Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana.
4 Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu.
5 Waliposikia haya WAKABATIZWA KWA JINA LA BWANA YESU.
6 Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.
7 Na jumla yao walipata wanaume kumi na wawili. "

Na wewe pia unaweza ukawa umebatizwa kwa ubatizo usio sahihi, hivyo usione aibu kwenda kubatizwa tena, ili kufanya imara wito wako na uteule wako.

Ni muhimu kufahamu kuwa hakuna ubatizo wa kunyinyuziwa kulingana na maandiko...Na ubatizo sahihi ni muhimu mno haupaswi kuupuziwa kwa namna yoyote ile. Kadhalika hakuna chuo chochote cha kupitia ndipo ukabatizwe, pale mtu tu anapoamini na kutubu kabisa kwa kumaanisha kuziacha dhambi zake moja kwa moja anapaswa aende akabatizwe kwa ajili ya ondoleo la dhambi zake na kupokea kipawa cha ROHO MTAKATIFU.

Matendo 2: 37 "Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu".

Ukipata muda pia pitia mistari hii ,( Matendo 8:16, 10:48)
SWALI 2: Asante mwalimu .lakini swali langu kuhusu ubatizo, kwa nini naona si sahihi kufanya ubatizo kwa maji ambayo yanasimama tu kama kisima, kidimbwi n.k maana maji yanayosimama inaashiria hayana uhai. Maji yanayoteremka kama mtoni ilivyo sahihi kimaandiko ama unasemaje unielimishe kidogo. Kwa kuongeze inadaiwa kwamba aina hizi za ubatizo inatokana kwa yule mpinga kristo . Kwa nini naonelea sharti ubatizo ni kwa maji inayoteremka?
JIBU: Ubarikiwe kwa swali lako, Kinachohitajika na cha muhimu ni maji mengi ya kumzamisha mtu, kwasababu maana yenyewe ya neno "ubatizo" ni "kuzamisha", na maji yote yana uhai, yawe yanatembea au yamesimama, na ndio maana maji yaliyosimama ukiyachukua na kuyamwagilia kwenye mmea wako unakua tu vizuri, haufi, maji yaliyosimama yana uhai sawa tu na maji yanayotembea. Kwahiyo ubatizo ni popote penye maji mengi. Ubarikiwe!SWALI 3: Kuandika vi- notes ( kuhusu kitu ninachofundishwa kanisani au kujifunza biblia) sasa kitu kinachonishangaza sipati muda wa kuvipitia ? Sijui tatizo liko wapi ? Nisaidie hapo ndugu.
JIBU: Tatizo lipo kwako, unapaswa uonyeshe BIDII, kuyapitia yale unayofundishwa, kwa kujiundia wewe mwenyewe utaratibu wako binafsi, ambao utakuwezesha kupata muda wa kutosha wa utulivu kila siku kukaa chini na kuyapitia yale uliyofundishwa, vinginevyo utakuwa katika hatari ya adui kuyanyakuwa yale unayofundishwa kila siku, unafanana na ile mbegu iliyotupwa katika njia,(Marko 4:15) ambapo unalisikiaa lile Neno lakini hulitendi kazi hivyo adui adui anakuja na kulinyakua haraka…

Biblia inatuonya tuwe na bidii katika kusoma 1Timotheo 4:13 “Hata nitakapokuja, ufanye BIDII KATIKA KUSOMA…”.Unaona, hivyo tatizo kama la kwako sio la kuombewa, ni jambo la kurekebisha ratiba yako, na kutenga muda wako binafsi na Mungu wako kila siku. Upate kujifunza Neno la Mungu kwa bidii, na sio kwa ulegevu.
 

SWALI 4: Ndugu naomba unifungue akili kidogo juu ya hili? Katika wakorintho wa 1wakoritho5 :5. ' KUMTOLEA SHETANI MTU HUYO, ILI MWILI UADHIBIWE, ILI NA ROHO IOKOLEWE katika siku ya Bwana Yesu." .......ndugu zangu hapo pamenichanganya naomba mnisaidie ?.

JIBU: Shalom, Awali ya yote utaona kuwa waraka huo Mtume Paulo aliwaandikia watakatifu waliokuwa wanaishi Korintho, haukuandikwa kwa watu wote, hapana bali ni kwa “watakatifu tu”. Sasa adhabu za watakatifu zinatofautiana, zipo dhambi za mauti na zipo dhambi zisizo za mauti.

1Yohana 5:16 “Mtu akimwona ndugu yake anatenda dhambi isiyo ya mauti, ataomba, na Mungu atampa uzima kwa ajili ya hao watendao dhambi isiyo ya mauti. Iko dhambi iliyo ya mauti. Sisemi ya kwamba ataomba kwa ajili ya hiyo.
17 Kila lisilo la haki ni dhambi, na dhambi iko isiyo ya mauti.”

Hivyo dhambi zisizo za mauti ni dhambi ambazo mtu yeyote aliye mkristo akifanya anaweza akaomba au akaombewa na kusamehewa, lakini dhambi za mauti ni dhambi ambazo ukizifanya hata uombeweje au uombeje adhabu za mauti zipo pale pale.Ukitubu utasamehewa hapa duniani lakini adhabu ipo pale pale, Na moja ya dhambi hizo ndio mfano wa ile alioyoifanya Anania na Safira mke wake.

Kadhalika Mungu alitoa mamlaka kwa kanisa pia kutoa adhabu kama hizo, kwa makosa yale yaliyopitiliza, kwamfano juu ya habari hiyo utaona kuwa kulikuwa na watu wanajiita ni wakristo lakini wanafanya mambo ya aibu ambayo hata hayawezi kuonekana kwa watu wa mataifa wasiomjua Mungu, yaani mtu analala na mke wa baba yake na bado anajiita ni mkristo na anafanya ushirika na watakatifu, sasa watu wa  namna hiyo dhambi wazifanyazo adhabu yake ni mauti, na kanisa limepewa mamlaka ya kumtoa mtu huyo kwa shetani aadhibiwe, kusudi kwamba roho yake baadaye ije kupona, vinginevyo kama asipoadhibiwa hapa duniani, kwa uovu kama huo ni wa kuelekea moja kwa moja katika ziwa la moto..

Sasa akishakabidhishwa kwa shetani, jambo lolote linaweza kutokea juu yake, anaweza kutokewa na mambo ya ajabu, pengine hata ajali, ugonjwa, kifo cha ghafla n.k. lakini mwisho wa siku ni lazima afe. Hata atubu kwa namna gani hawezi kusamehewa hapa duniani. Hivyo sisi kama wakristo tunapaswa tuwe makini ni mambo tuyafanyayo tukijua kabisa sio kila dhambi tutapata rehema..nyingine zitatugharimu maisha yetu  hata kama tutatubu vipi kwa kumaanisha. Kwa urefu zaidi kuhusu dhambi ya mauti unaweza ukasoma kupitia link hii >>> dhambi ya mauti

Lakini pia ndugu ... Naomba unifungue akili kwa hili ... Mfano mko katika mazungumzo mazuri tu ghafla mwenzio akaanza KUMSENGENYA ndugu mwingine ? Sasa kwa upande wako unajua kwamba KUSENGENYA ni dhambi sasa utachukua maamuzi gani?

JIBU: Unayakatisha hayo mazungumzo na kuzungumza habari nyingine..usipoonyesha ushirikiano leo na kesho yule mtu atatambua kuwa wewe hupendi kuzungumza vibaya habari za watu wengine, hivyo siku nyingine hatakuja kukuletea habari hizo..Lakini kama utakuwa unakubaliana naye, na kuonyesha ushirikiano naye atakuona kuwa wewe ni mwenzake na hivyo kila siku utakuwa katika mazingira ya usengenyaji.

Kadhalika ni wajibu wako pia kujionyesha kuwa wewe ni mkristo. Watu wakishakufahamu kuwa wewe upo hivyo, wataogopa kukuletea habari za usengenyaji kwasababu watajua kuwa wewe huzipendi.

SWALI 5: Shalom ndugu nataka unisaidie katika hili kwa siku za hivi karibuni nimekuwa na changamoto mpya najikuta nawaka tamaa isiyo ya kawaida najikuta nina tamaa kali ya kutaka kuzini ila nachoshukuru kwa sasa naweza kujizuia hofu ni je?? haita ni shinda huko mbeleni..?
 
JIBU: Dalili  mojawapo inayoonyeshwa kuwa umezaliwa mara ya pili ni kutokushindwa na dhambi. Ukishaona mtu anasema kazaliwa mara ya pili halafu kaenda kuzini ni wazi kuwa bado hajazaliwa kwa Roho wa Mungu..

1Yohana 5:18 “Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu HATENDI DHAMBI; bali yeye aliyezaliwa na Mungu HUJILINDA, wala yule mwovu hamgusi.”

Unaona hilo Neno HUJILINDA..Ikiwa na maana kuwa dalili zozote za kutenda dhambi  za makusudi  zinaponyemelea maisha yake hutafuta suluhisho haraka kabla ya kuingia katika mtego huo. Sasa kwa hali kama ya kwako, ni wazi kuwa nguvu zako za rohoni zimepungua. Na inawezekana ni moja ya mambo haya au yote..

     1)     Huombi
     2)     Hufungi
     3)     Hufanyi ushirika
     4)     Hutafakari Neno la Mungu.

Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mathayo 26:40 “Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami HATA SAA MOJA?
41 KESHENI, MWOMBE, MSIJE MKAINGIA MAJARIBUNI; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.
Unaona, mtu anaingia majaribuni kama mtu sio mwombaji. Na kiwango cha chini tunapaswa tuombe kwa siku ni walau lisaa limoja..Hivyo kama wewe sio mwombaji tamaa zitakutawala tu, na pia utakosa raha ya wokovu wako. Maombi ni silaha moja kubwa sana, na shetani ndio anayopenda kuishambulia, kwasababu anajua akimtoa mtu katika mstari wa maombi ameshammaliza.

Yakobo 4: 4.1 Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu?
2 Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa HAMWOMBI! “

PILI, KUFUNGA: Kufunga kwa mkristo kuna umuhimu sana, kwanza, kunakusaidia kuutiisha mwili chini, na kuifanya roho yako kuja juu,..hivyo inakupa wepesi wa kusali na kuutawala mwili kirahisi. Na pia ukiwa ni mfungaji tamaa za mwili zinadidimia zenyewe ndani yako. 

TATU: kama sio mtu wa kujumuika na wengine kufanya ushirika, kuabudu na kumsifu Mungu. Hali mbaya za adui zitakusumbua kila siku. Jijengee tabia ya kuhudhuria ibadani, hata kama vingine havitakusaidia lakini ule ushirika u wa kumsifu na kumwabudu Mungu ni muhimu sana kwa mkristo yeyote aliyeokolewa.. Ni ahadi ya Mungu wanapojumuika wawili au watatu kwa jina lake, huwa anashuka katikati yao…Hivyo usipendelee sana kukaa mwenyewe kama upo mwenyewe..

NA LA MWISHO. NI UTAFAKARIJI WA NENO: Neno lenyewe linaweza kukupa nguvu, na maonyo juu ya maisha yako, na kukufariji. Kwa jinsi utakavyokuwa mtafakariji wa Neno zaidi ndivyo utakavyokuwa na uwezo wa kumshinda adui na njama zake, kwasababu mitego yote ya shetani na namna ya kuitatua ipo katika maandiko,Kwasababu huko huko katika kutafari Roho Mtakatifu ndipo anaposema na wewe.

Hivyo ukizingatia hayo, huwezi kuanguka leo na katika siku zinazokuja. Bwana akubariki sana.


No comments:

Post a Comment