"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, December 15, 2018

KWANINI TUWE WENYE BUSARA KAMA NYOKA?


Mathayo 10:16 “Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.”
Sentensi hiyo imekuwa ikiwatatiza wengi, wakijiuliza ni kwanini Bwana YESU alisema maneno kama hayo: IWENI NA BUSARA KAMA NYOKA. Kwani nyoka anayobusara gani, kwanini hapo asingesema iweni na busara kama simba au mnyama mwingine wa mwituni na sio nyoka?. Tunafahamu katika biblia nyoka ni mnyama aliyepoteza sifa kuliko wanyama wote aliowaumba Mungu, kadhalika ni mnyama aliyelaaniwa kuliko wanyama wote, katika biblia mnyama anayefananishwa na shetani ni nyoka peke yake, tofauti na wanyama wengine kama njiwa ambaye anaonekana akimwakilisha Roho Mtakatifu na wanyama wengine kama kondoo, ng’ombe, na simba lakini nyoka hastahili hata kutamkwa kwenye vinywa vya wakristo kwa sifa njema lakini hapa Bwana kamtaja.

Na zaidi ya yote Bwana wetu YESU anatuonya na kutumbia; basi iweni na busara kama nyoka, Leo hii tutafunza ni busara gani nyoka aliyokuwa nayo.

Awali ya yote ukisoma kuanzia ule mstari wa 1 utaona kuwa maneno hayo Bwana Yesu alikuwa anawaambia wale wanafunzi wake 12. Muda huo alikuwa anawapa maagizo ya msingi ya kuzingatia katika kwenda kufanya kazi ya utumishi. Ni mahusia ya msingi kabisa ambayo walipaswa wazingatie na sio tu katika kile kipindi walichokuwa na Bwana Yesu pindi walipotumwa bali pia hata baada ya kuondoka kwake. Na ndio hapo tunakuja kusoma huo mstari wa 16, akiwaambia maneno hayo akisema: “Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu;”.. Umeona hapo? Mpaka hapo tumeshafahamu kuwa maneno hayo yanawahusu wale tu WANAOTUMWA!, na si watu wengine.

Sasa hao ndio walioambiwa katika kutumwa kwao wanapaswa wawe na tabia kama kondoo katikati ya mbwa-mwitu, na sio kama simba katikati ya mbwa-mwitu, hii ikiwa na maana kuwa watakapotendewa mabaya au watakapopigwa au watakapoudhiwa wasirudishe baya kwa baya, bali wajifanye kama kondoo wasioweza kufanya lolote. Bwana alikuwa anayomaana ya msingi kabisa kuwaambia hivyo, kwasababu alijua umuhimu wake katika kuziokoa roho za watu. na ndio tabia tuliokuja kuiona kwanza kwa Bwana wetu YESU Kristo kisha kwa mitume wake baadaye..Sasa baada ya hapo, ndipo akawapa maagizo haya kwamba huko mtakapokwenda IWENI NA BUSARA KAMA NYOKA. NA KUWA WATU WAPOLE KAMA HUA.

Ni busara gani aliyonayo NYOKA?

Nyoka anavyozungumziwa hapa ni nyoka jinsi alivyokuwa katika asili yake pale Edeni.Embu jaribu kifikira Adamu na Hawa watu ambao Mungu alikuwa anazungumza nao uso kwa uso wakiisikia sauti yake kila siku kwa kipindi cha muda kirefu sana, wakiyatimiza maagizo yake yote aliyowapa kwa muda mrefu kwamba wasile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, halafu kirahisi rahisi tu ndani ya siku moja wakate shauri waache kuyatii maagizo ya Mungu na kuasi..Usidhani ni jambo jepesi jepesi kufikia hatua ya kula lile tunda, ushawishi wa namna hiyo unahitaji maarifa na busara ya hali ya juu sana..

Nyoka alijua kabisa ili kuwapata wale watu sipaswi kutumia nguvu ya aina yoyote, kama angejaribu kufanya hivyo basi yeye mwenyewe angejikuta kwenye hali mbaya sana kwasababu Adamu asingemvumilia. Alijua kabisa hapaswi kutumia maneno ya kufuru kwa Mungu wao, kama angefanya hivyo basi Adamu asingemvumilia pia kwa hilo, alijua kabisa kuzungumza na Adamu ni ngumu hivyo akatafuta njia mbadala mahali palipo dhaifu ili afanikishe mpango wake wa kuwadondosha. Alitumia busara nyingi kuupindua mpango wa Mungu uliokuwa ndani ya wanadamu. Hivyo japo aliruhusu busara yake itumiwe vibaya na shetani lakini bado mbele za Mungu alionekana kuwa ni mnyama mwenye busara nyingi..

Hata baada ya kulaaniwa, unamwona katika mawindo yake, hatumii papara, huwa unatulia sana, na kukamata mawindo yake kwa ghafla, hana mikono, hana miguu, lakini anamkamata panya mwenye uwezo mkubwa wa kusikia, na kuponyoka.

Unaukumbuka ule mfano Bwana alioutoa katika Luka 16:1-9, wa Yule wakili aliyekuwa mwizi, lakini katika wizi wake alikuwa na busara?...Kama hukuwahi kuupitia basi kaupitie tena, naamini utajifunza kitu.

Vivyo hivyo na wale wanaotumwa na Bwana kupeleka injili, Bwana YESU anawaambia IWENI NA BUSARA KAMA NYOKA. Alimaanisha kuwa huko waendako watakutana na watu waliojikita katika misingi ya imani zao potofu, hata ufanyeje huwezi kuwang’oa mahali walipo..Shetani ameshawahubiria kwa miaka mingi, kwamba akitokea mtu mwingine anawaletea habari za Imani nyingine zaidi ya hiyo waliyofundishwa hawawezi kuwaamini wala kuwapokea. Hivyo kama huyo anayetumwa kupeleka Injili hataweza kutumia busara kuwahubiria habari mpya ya wokovu katika Kristo Yesu basi anaweza kujikuta anampoteza kondoo Yule au anajitafutia matatizo yeye mwenyewe yasiyo ya lazima.

Leo inasikitisha kuona mtu anasema ni mtumishi wa Kristo na ni mhubiri lakini mambo anayoyafundisha kwa watu ambao wapo katika misingi ya imani nyingine mbali na Kristo, haina busara kabisa..Utamkuta anakutana na mtu labda pengine haamini katika kula nyama ya nguruwe. Lakini yeye kwasababu anajua kuwa nguruwe si kitu mbele za Mungu, badala ya kumfundisha mambo ya msingi, halafu kwa jinsi atakavyoendelea kukua kiiamini baadaye ndipo amwambie na habari hizo pia, jambo la kwanza ataanza kwa kumwambia nguruwe si dhambi!, ataanza kuwaambia dini yenu ni ya kigaidi, ataanza kuwaambia mnaabudu majini n.k. Unadhani itakuwa ni rahisi kumvuta huyo mtu kwa Kristo? Jibu ni hapana Kinyume chake utazua migongano na malumbano na kusababisha jina la Mungu kutukanwa.

Mtume Paulo katika safari yake ya kutangaza injili alikutana na watu wengi tofauti tofauti, lakini alifanikiwa kuwageuza wengi wao kwa busara ya Roho iliyokuwa ndani yake. Tunasoma hayo katika

1Wakorintho 9: 20 “Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria, nalikuwa kama chini ya sheria, (ingawa mimi mwenyewe si chini ya sheria), ili niwapate walio chini ya sheria.
21 Kwa wale wasio na sheria nalikuwa kama sina sheria, (si kwamba sina sheria mbele za Mungu, bali mwenye sheria mbele za Kristo), ili niwapate hao wasio na sheria.
22 Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu.
23 Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya Injili ili kuishiriki pamoja na wengine”.

Wakolosai 4:5 “Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati.
6 Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.

Unaona hapo?. Tukikosa busara, tutazua mashindano ya dini badala ya wokovu kwa watu. wengine wanapotukanwa tu kidogo wao nao wanarudisha matusi, hawajui kuwa wale ni mbwa-mwitu ni kawaida yao kutukana, sasa na wao kwa kukosa busara wanarudisha na wao dhihaka, sasa hapo ni mtu gani unatazamia aupokee wokovu?. Matokeo yake badala ulete faida katika ufalme wa mbinguni unaleta hasara kwa jambo dogo tu la kukosa busara. Upo mitandaoni, badala ya kuwavutia watu Kristo wampokee ndani yao, unakwenda kutafuta sehemu za madhaifu yao na kuanza kuwakasirisha kwa maneno ya hasira, hujui kuwa ipo siku utaulizwa na Bwana kwa hiyo huduma unayoifanya: Sisemi kuwa hupaswi kukosoa mabaya, lakini katika ukosoaji wako tumia busara. Angalia mwisho wa siku unamshawishi nani?. Au malengo yako ni nini? kukoa au kuonyesha kuwa wale hawako sahihi na wewe upo sahihi?. Jichunguze lengo lako ni nini? kujenga au kutaka kuonyesha kuwa una ujuzi mwingi?..Biblia inasema upendo hujenga, bali ujuzi huleta majivuno (1 Wakoritho 8:1)

Luka 12:42 “Bwana akasema, Ni nani, basi, aliye wakili mwaminifu, MWENYE BUSARA, ambaye bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake?
43 Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo.
44 Kweli nawaambia, atamweka juu ya vitu vyake vyote.
45 Lakini, mtumwa yule akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia kuja, akaanza kuwapiga wajoli wake, wanaume kwa wanawake, akila na kunywa na kulewa;
46 bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini.”

Unaona?. Ni maombi yangu kwa kusoma haya sisi sote hatutaanza kuwa mawakili wenye busara wa Kristo, ambao tutawapa posho wale walio nje kwa wakati, na sio kuwapiga, na kuwaudhi, na kuwadharau ili Bwana atakapokuja atupe thawabu iliyostahili, na tufanikiwe kuleta matunda mengi kwa Bwana.
 
Ubarikiwe sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na Bwana atakubariki.

No comments:

Post a Comment