"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, December 17, 2018

TUSIFUNGWE NIRA PAMOJA NA WASIOAMINI.

2 Wakorintho 6:14 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, KWA JINSI ISIVYO SAWASAWA; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?”
Biblia inasema tusifungiwe Nira pamoja na wasioamini..NIRA ni KIFAA kinachowekwa katikati ya wanyama wawili wa jamii moja, kinachowafunga pamoja...ili kutimiza kusudi la kazi Fulani, kama vile kulima, kusafirisha mizigo n.k mfano ng’ombe wawili wanaweza kufungwa nira pamoja kwa kazi ya kilimo, na kulivuta lile jembe nyuma yao...kadhalika farasi wawili wanaweza kufungwa nira moja ili kulivuta gari la kubebea watu au vitu nyuma yao..Punda nao wanaweza kufungwa nira pamoja ili kusaidia kuvuta mzigo Fulani nyuma yao...
    


Tukirudi katika maandiko biblia inatuonya tusifungwe nira pamoja na wasioamini, Kumbuka haikumaanisha tukae mbali kabisa na wasioamini, au tusizungumze nao, au tusifanye nao kazi, au tusiishi nao, au tusisome nao au tusile nao, au tusisalimiane nao...hapana haikumaanisha hivyo... ukisoma kwa makini huo mstari unasema “msifungiwe nira pamoja na wasioamini kwa jinsi isivyo sawasawa”..Sasa zingatia hilo neno “kwa jinsi isivyo sawasawa”... Ikiwa na maana kuwa kumbe kuna jinsi iliyo sawasawa ambayo tunaweza tukafungwa nao nira, unaweza ukafanya kazi ofisi moja na mtu asiyeamini, unaweza ukasoma darasa moja na mtu asiyeamini, unaweza ukala sahani moja ya chakula na mtu asiyeamini kama Bwana alivyofanya n.k...Lakini kuna mipaka ambayo hatupaswi kufungiwa nao Nira.

Kwa mfano, mtu asiyeamini anaweza akawa ni mwizi, au mwasherati, au mtukanaji sasa kama ni shuleni tunaweza tukawa naye darasa moja, tukazungumza naye kwa upendo na kujaribu kumvuta kwa KRISTO lakini, kukaa naye katika mazingira yake ya utukanaji, au ya uasherati, au ya wizi au ya usengenyaji hayo tumeonywa tujiepushe nao...kushirikiana naye katika anasa, au ulevi hivyo vyote tumeonywa tukae mbali navyo..tukiwa shuleni tutashirikiana nao katika masuala ya shuleni tu basi, lakini masuala ya kwenda disko, au kwenye starehe za kidunia, au kutazama picha chafu, au kufanya nao mustarbation hayo tumeonywa..vivyo hivyo kazini tutashikamana nao kwa masuala ya kazini tu basi..lakini katika eneo la maisha ya rohoni hilo tumeonya tujiepushe nao.

Sasa kwanini Bwana alituonya tusijifunge Nira nao kwa jinsi isivyopaswa?. Kwani tukiishi nao hivyo hivyo kuna shida gani??..si tutajiepusha nao tu!!

Hekima ya Mungu ni kuu kuliko hekima ya mwanadamu... Umewahi kujiuliza kwanini watu wa ukanda Fulani wana lafudhi zinazofanana? Au wana tabia zinazofanana?..Unadhani wote walipenda wawe wanalafudhi zinazofanana? Au walishauriana wawe vile?..Utakuja kugundua kwamba ni “kule kukaa pamoja kwa muda mrefu” ndiko kuliko wafanya wote wafanane tabia na lafudhi bila hata wenyewe kujijua kuwa wapo hivyo.

Kwahiyo unaweza ukaona kuwa kuna nguvu Fulani ya kumbadilisha mtu ipo katika ya jamii anayojiunganisha nayo..hata kama yeye hataki lakini kwa jinsi anavyokaa na ile jamii atajikuta tu kwa muda Fulani ameshafanana na jamii ya wale watu kiusemi, na kifikra.

Ndio maana katika agano la kale Bwana alitoa maagizo punda na ng’ombe wasifungwe nira pamoja...punda afungwe na punda mwenzake na ng’ombe afungwe na ng’ombe mwenzake... Kumbukumbu 22: 10 “Usilime kwa ng'ombe na punda wakikokota jembe pamoja”.

    

Unajua ni kwasababu gani?


Sababu ni kwamba watakapofungwa nira pamoja punda na ng’ombe..kuna tabia ng’ombe alizo nazo punda atakazoanza kuziiga na kadhalika kuna baadhi ya tabia za punda ng’ombe ataziiiga hivyo itazaliwa tabia moja ambayo haifai katika shughuli zozote za kazi..

Fuatilia utaona kuwa mahali palipo na mchanganyiko wa kuku na bata, utaona bata kuna wakati wanaonyesha tabia Fulani kama za kuku na kuku vivyo hivyo kuna wakati wanaonyesha tabia kama za Bata..Mimi nimewahi kushuhudia hilo na pia kitafiti limethibitishwa...Pia kwa wanyama wengine wote ndio hivyo hivyo, wakichanganyikana pamoja wanakuwa wanaingiliana tabia...

Hivyo ndivyo Bwana alivyoviumba viumbe vyake vyote ikiwemo wanadamu kwamba...tabia ya mmoja inaweza kumuathiri na kumgeuza mwingine endapo wakikaa pamoja kwa muda mrefu.

Ndio maana maandiko yanazidi kusema katika ..


Mithali 22: 24 “Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira nyingi; Wala usiende na mtu wa ghadhabu nyingi; .. USIJE UKAJIFUNZA NJIA ZAKE; NA KUJIPATIA NAFSI YAKO MTEGO”.

Unaona hapo?..inasema usije ukajifunza njia zake? HIYO KUJIFUNZA sio kujifunza kwa kutaka hapana! Hakuna mtu yoyote anapenda kujifunza njia mbaya...hiyo kujifunza ni tabia ambayo inaingia ndani ya mtu pasipo hata yeye kujijua, kama alikuwa sio msengenyaji na akakaa na mtu ambaye ana tabia ya kuzungumzia habari za watu wengine kila wakati..na yeye baada ya muda Fulani atajikuta tu anaanza anazungumzia habari za wengine kila mahali...

Kama alikuwa hana hasira nyingi lakini akajiunganisha na mtu wa hasira nyingi na anaye kufoka foka..mara ya kwanza ataishangaa ile tabia lakini baada ya muda Fulani, ataona ile hali ni ya kawaida tu! Kutukana na kukasirika ni kawaida...hivyo na yeye atakapoudhiwa kidogo tu hasira zitamjia na kuanza kufoka na kutukana kama mwenzake anavyofanya, kwasababu moyo wake ulishakufa ganzi siku nyingi..Hata mara ya kwanza ukipita mahali penye kelele nyingi na harufu nyingi tofauti tofauti siku ya kwanza utaona kuna usumbufu mkubwa na harufu nyingi lakini kwa jinsi utakavyoendelea kupita hapo kila siku, unakuja kuona ile sehemu ni ya kawaida tu! Unapazoea!! Harufu zinapotea na kelee huzioni tena kuwa ni nyingi..Watu wanaoishi machinjioni ukiwauliza hivi huwa hamwisikii hiyo harufu mbaya ya damu, watakujibu hawasikii kitu wanaona kawaida tu! Ni kwasababu gani ni kwasababu wameshakufa ganzi katika yale mazingira.


Kwahiyo ni kujihadhari kama Bwana anavyotuonya..Yeye ndiye aliyetuumba sisi, ana hekima kuliko sisi, unajua madhaifu yetu yapo wapi, na ndio anatuambia “tusifungwe nira pamoja nao kwa jinsi isivyopaswa” Kinyume chake tujifunge nira na wanaoamini, maana hao nao watatuambukiza tabia zao njema zinazompendeza Mungu..ndio maana Bwana alipowatuma wanafunzi wake aliwatuma wawili wawili..kuonyesha kwamba Bwana anatufunga nira yake kuanzia wawili na kuendelea? Kwasababu na yeye Bwana anayo Nira yake, anayotufunga sisi watoto wake pamoja, lakini anasema Nira yake ni laini na mzigo wake ni mwepesi..Maagizo yake sio mazito tunapokuwa wawili au watatu kwa jina lake, tunakuwa tuna uwezo wa kushinda kwasababu tumefungwa nira yake pamoja.

Ni matumaini yangu, kuanzia leo utaangalia mazingira yanayokuzunguka, na watu unaojishughulisha nao, je! ni kwa mambo ya maana tu, au wanaingilia mpaka utaratibu wako wako Imani. TUJILINDE!

Bwana akubariki.


Tafadhali tangaza habari njema za ufalme popote ulipo, kama umeshampa Bwana maisha yako, na pia kama hujamkabidhi Bwana maisha yako, ni vyema ukafanya hivyo leo kabla nyakati za hatari hazijaanza, maana tunaishi katika kipindi cha siku za mwisho, ambacho Bwana yupo karibu sana kurudi.

2 comments: