"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, December 18, 2018

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 46


SWALI 1: Ni uthibitisho upi unaoonyesha kuwa kuna MBINGUNI na KUZIMU.

JIBU: Ili kupata jibu ya swali hilo, ni vizuri pia tujiulize baadhi ya maswali ambayo ni rahisi kabisa kuyajibu yanayoonekana katika maisha yetu ya kila siku. Tuchukulie mfano Leo hii nikimuuliza daktari je! Utanithibitishiaje kuwa kama kuna kitu kinachoitwa kirusi au bacteria.?.. Tunafahamu hataniita na kuniambia angali kwa makini utaviona hewani , vikielea, vinginevyo nitamuona ni mwendawazimu lakini yeye kama daktari atajua kabisa kwa macho yangu ya asili siwezi kuviona virusi au bacteria hivyo jambo yeye atakalolifanya ni moja kwa moja kunichukua na kunipeleka mahabara na kunionyesha KIFAA maalumu kinachoitwa HADUBINI (Microscope), ambacho hicho kimeundwa mahususi kwa ajili ya kuvuta vitu visivyoonekana kwa macho. Hivyo pale  nitakapoitazama labda tusema damu kwenye hadubini hiyo na kuona vijidudu vidogo vidogo vikitembea ndipo hapo nitakapoamini kuwa kuna viumbe vinaitwa Bacteria au virusi.

Kadhalika leo hii mtaalamu wa masuala ya Anga, akaniambia kuna sayari inayoitwa Pluto inayofanana na dunia, ni wazi kuwa siwezi kuamini kwasababu kwa macho yangu hayalithibitishi  hilo lakini pindi atakapotumia kifaa chake maalumu kinachoitwa DARUBINI (Telescope). Ambacho hicho ni mahususi kwa kuvuta magimba yote yaliyo angani ndipo nitakapoamini kuwa kweli kuna sayari inayoitwa Pluto kwasababu ninaiona kwenye darubini.

Vivyo hivyo na mambo ya rohoni, hatuwezi kuyatambua kwa jinsi ya mwilini biblia inatuambia hivyo katika 1Wakoritho 2: 14 “Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni”.

Hivyo ili sasa tuweze kujua kuwa kuna mbingu au kuzimu basi yatupasa nasi pia tutumie kifaa maalumu kinachoweza kuvuta mambo ya rohoni na hicho si kingine zaidi ya BIBLIA TAKATIFU.

Tatizo linakuja ni pale watu wasipotaka kuliamini NENO LA MUNGU na huku bado wanataka wamwone Mungu, ni sawa na mtu anayetaka kuona kirusi na huku bado haiamini Hadubini. Iamini kwanza biblia, ndipo utakapopata uthibitisho kweli kama kuna mbingu au kuzimu vinginevyo hata mtu atoke mbinguni au kuzimu akuambie hutaamini wala hutaweza kulithibitisha hilo.

 
SWALI 2: Shalom!.Ndugu zangu  Biblia inatuambia kuhusu kazi yakutoa jasho aliyopewa Nuhu ya"KUVIINGIZA KATIKA SAFINA"VIUMBE VIRUKAVYO-Vya kiume na vyakike kwa jinsi yake" "KILA NAMNA YA WANYAMA-Wakiume na Wakike kwa jinsi yake'' . Swali Ni je! Nuhu Alipata wapi ujuzi huo wa kuvitambua hivyo viumbe vyote, na je! Hao wanyama wote aliwatolea wapi?


JIBU: Ukisoma mstari wa 20 sura ya 6 wa kitabu kile cha Mwanzo  inasema : 20 Katika vyote virukavyo kwa jinsi yake, na kila namna ya mnyama kwa jinsi yake, kila kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake, wawili wa kila namna WATAKUJA KWAKO ILI UWAHIFADHI.
Unaona hapo, hilo neno WATAKUJA KWAKO ILI UWAHIFADHI , hii ikituthibitishia kuwa sio wanyama wote Nuhu alikwenda kuwachunguza  kujua jinsia zako au kuwakamata, hapana wengine walikuja wenyewe Mungu ndiye aliyewaleta,isipokuwa wale wa kufungwa, kazi ya Nuhu ilikuwa ni kuwaingiza tu ndani.


SWALI 3: Luka21 18"Walakini hautapotea hata Unywele mmoja wa Vichwa vyenu."Hapo anamaanisha nini ndugu zangu?..


JIBU: Hii ni kuonyesha kuwa Bwana hakuja kukomboa roho zetu tu basi, bali hata miili yetu pia..Na aliposema hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea, alikuwa anaamanisha kuwa hata kile kinachoonekana kuwa hakina thamani katika mwili wetu hakitapotea..vyote vitarejeshwa tena, ..Ikiwa ni mwamini alikufa hana mguu, basi siku ile ya ufufuo mguu wake utarejeshwa ikiwa alikufa na upara juu ya kichwa chake, basi nywele zake zote zitarejea katika siku ile na kuwa kama kijana.

 Na baada ya kurejeshwa ndipo miili mipya ya utukufu kutoka mbinguni ambayo asili yake ni mbinguni na sio ardhini  itakuja kuivaa hii miili yetu ya ardhini. Kuonyesha kuwa hakuna kilichopotea hata kimoja...

1Wakoritho
15:51 “Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,
52 kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.
53 MAANA SHARTI HUU UHARIBIKAO UVAE KUTOKUHARIBIKA, NAO HUU WA KUFA UVAE KUTOKUFA.
54 Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda.
55 Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako?”

Lakini pia ikiwa Bwana anasema “Walakini HAUTAPOTEA hata Unywele” alimaanisha kuwa wapo ambao UTAPOTEA..Na hao ndio wale wanampinga YESU mfalme wa uzima sasa hivi wakijua kabisa yeye pekee ndiye mwenye uwezo wa kuokoa roho zao na miili yao. Siku ile wakifa katika dhambi basi miili yao na roho zao vyote kwa pamoja zitateketea katika lile ziwa la Moto milele. Watapotea milele wala hakutakuwa na kumbukumbu kama hata hao watu walishawahi kuishi duniani.

Ubarikiwe

No comments:

Post a Comment