"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, December 19, 2018

VIFUNGO VYA GIZA VYA MILELE.

Luka 8: 30 “Yesu akamwuliza, Jina lako nani? Akasema, Jina langu ni Jeshi; kwa sababu pepo wengi wamemwingia.
31 Wakamsihi asiwaamuru WATOKE KWENDA SHIMONI.
32 Basi, hapo palikuwa na kundi la nguruwe wengi wakilisha mlimani; wakamsihi awape ruhusa kuwaingia wale. Akawapa ruhusa.
33 Pepo wakamtoka mtu yule wakawaingia nguruwe, nalo kundi lilitelemka gengeni kwa kasi, wakaingia ziwani, wakafa maji”.
Shalom! Mtu wa Mungu, ni siku nyingine Bwana ametupa neema ya kuliona jua lake, sifa na utukufu ni vyake milele, karibu tujifunze pamoja maneno ya uzima ya Yesu Kristo Bwana wetu, leo tukilitazama kwa undani tukio hilo walilokutana nalo Yesu na wanafunzi wake, mara baada ya kuvuka bahari ya Galilaya pale walipokutana na Yule mtu mwenye jeshi la mapepo waliomsumbua sana kwa muda mrefu, lakini tunaona jambo la kwanza kabisa kama tunavyosoma wale mapepo walichofanya, ni kumsihi Bwana kwa nguvu asiwapeleke SHIMONI..Swali la kujiuliza hapo ni kwanini shimoni na sio sehemu nyingine, na huko shimoni ni wapi?.

Ni wazi kabisa kama tukichunguza mawazo ya hayo mapepo tunaona kuwa yalikuwa yanafahamu kabisa hilo eneo, lakini hayakuwepo kwa wakati huo , na ndio maana jambo la kwanza walipokutana tu na mtu anayewatambua vizuri na makao yao wastahiliyo kuwepo kwa wakati huo moja kwa moja waliona ni heri wajisalimishe na kuomba sharti ya amani mapema, kabla ya mambo mabaya kutokea ya kuamriwa kurudi Shimoni, waliona ni heri wapitie nusu shari kuliko shari kamili.

Mfano leo hii ukiona mtu mwenye akili timamu anachagua kwenda kuishi porini sehemu isiyo na huduma zozote za kijamii kuliko kuishi Mogadishu Somalia, utajua kuwa anazosababu zake za msingi kuchagua hivyo. Jambo la kwanza utajua aidha alishawahi kuishi katika mazingira yote mawili na kuona kule porini ni bora zaidi ya Mogadishu, au alishawahi kusikia habari za kule Mogadishu kwamba sio sehemu salama ya kuweka makazi ya kudumu kwa mtu yeyote kutokana na vita au vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kutokea huko mara kwa mara, hivyo akaona bora achague mahali penye unafuu zaidi..

Hali Kadhalika na haya mapepo vivyo hivyo, yalifahamu kabisa hali halisi ya huko shimoni jinsi kulivyo, na ubaya wake, na shida zake na mateso yake, kutokana na kwamba aidha walishawahi kuwepo huko kwa kipindi Fulani au waliwaona wenzao wakiteseka katika makao hayo ya shida, na hivyo wao nao hawataki kwenda huko.

Biblia inasema.

2Petro 2: 4 “Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, BALI ALIWATUPA SHIMONI, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu”;


Unaona? Kama tunavyosoma hapo, makao ya malaika wote ambao hawakuilinda enzi yao, malaika wote ambao hawakuisimamia kweli, malaika wote ambao hawakudumu katika mipaka ya msingi waliyowekewa na Mungu, malaika wote waliokaidi kanuni za Mungu walizopewa waziendee walikuja kutupwa wote shimoni baadaye, katika vifungo vya giza wakae huko mpaka siku ile ya mwisho ya hukumu.

Kama tunavyofahamu mtu akitumbukia katika Shimo refu basi mtu huyo anakuwa katika hali ya mashaka na ya kukosa matumaini, kwasababu makao yake yatakuwa ni pale pale daima isipokuwa labda mtu amekuja kumtoa. Hivyo malaika wote walioasi makao yao yanapaswa yawe ni shimoni kwa sasa, kwenye vifungo vya milele wakingojea hukumu ya mwisho. Lakini pia si wote walio humo kwasasa biblia inasema hivyo, wapo baadhi wanaozunguka zunguka duniani pamoja na mfalme wao ibilisi, Sababu za Mungu kuwaruhusu wao wawe hivyo hatujui Bwana anazijua, lakini wakati utafika Shetani naye atatupwa katika shimo hilo kwa muda wa miaka 1000 akiungana na wale waliokuwa wamefungwa tangu zamani, kisha baadaye ataachiliwa kwa muda mfupi kwa kutimiza kusudi Fulani duniani. Na baada ya hapo ndipo kwa pamoja watatupwa wote kwenye lile ziwa la moto.

Ufunuo 20:1” Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake.
2 Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu;
3 akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache”.


KAMA KUNA BAADHI YA MAPEPO AMBAYO HAYAPO SHIMONI KWA SASA, BASI MAKAO YAO YAKO NI WAPI ?

Hakuna pepo lolote lenye makao ya kustarehe duniani, hakuna mahali popote pepo anapata unafuu isipokuwa ndani ya mtu tu! basi. Nje ya hapo, ni dhiki kubwa na mateso. Na ndio maana wanafanya bidii sana kila mmoja walau apate mahali pa kujiegesha ndani ya mtu duniani. Sasa mara baada ya pepo kumtoka mtu baada ya kuombewa au baada ya mtu kumpa Kristo maisha yake haliendi kustarehe mahali Fulani tu, hapana linakwenda mahali pa jangwa, mahali penye ukame. Bwana Yesu alisema hivi.

Mathayo 12:.43 “Pepo mchafu, amtokapo mtu, HUPITIA MAHALI PASIPO MAJI, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate.
44 Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa.
45 Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya”.


Unaona hapo linakwenda mahali pasipo maji ni sawa na kusema linakwenda mahali pa jangwa pasipo na uhai, mahali pa shida na dhiki pasipo kuwa na kiburudisho chochote. Sasa pepo linapomtoka mtu ndipo katika roho linakuwa katika hali kama hiyo ya mtu aliyeachwa jangwani mwenyewe pasipo na msaada wowote. Kumbuka Hapo ni tofauti na shimoni, na kwa jinsi atakavyoendelea kukosa mahali pa kutulia ndivyo hali yake itakavyozidi kuwa mbaya zaidi, sawasawa tu na wale walioko shimoni. Ataendelea hivyo hivyo mpaka siku ile ya mwisho ya Hukumu ambayo wote kwa pamoja na wale walio vifungoni kwenye mashimo sasahivi watakapotupwa kwenye lile ziwa la moto.

Hivyo unaweza ukuona ni shida nyingi kiasi gani hivi viumbe vilivyolaaniwa vinapitia vinapokosa mahali pa kustarehe, lakini sasa pale mtu anapovipa makao katika mwili wake, mtu huyo naye anafanyika kuwa mwana wa laana, Mungu anamwona mtu kama huyo naye anastahili kutupwa shimoni. Naye pia anashiriki laana zile zile walizowekewa hayo mapepo tangu zamani.

Na ndio hapo sasa mtu mwovu akifa, pindi tu anapokata roho moja kwa moja anajikuta anashuka kwenye shimo refu la giza, kwenye vifungo vya milele sasa huko chini kuna taabu na mateso yasiyoneneka Mahali ambapo baadhi ya hayo mapepo yalipo sasahivi, mateso ya huko ni makubwa jaribu kifikiria hata mapepo yaliyopo duniani hayataki kupelekwa huko, ni mahali pabaya kiasi gani.

Sasa wote kwa pamoja wataendelea kukaa huko wakisubiria hukumu ya siku ile ya mwisho kisha watupwe kwenye lile ziwa la moto. Hayo ndio mambo yaliyowakuta hata watu wa kipindi cha Nuhu na watu wa kipindi cha Sodoma na Gomora biblia inasema sasahivi wapo katika vifungo hivyo vya milele, wapo shimoni wakingojea hukumu ya mwisho na ndipo wahukumiwe na kutupwa kwenye lile ziwa la moto.

Yuda 1:6 “Na malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu, amewaweka katika vifungo vya milele chini ya giza kwa hukumu ya siku ile kuu.
7 Kama vile Sodoma na Gomora na miji iliyokuwa kando-kando, waliofuata uasherati kwa jinsi moja na hawa, wakaenda kufuata mambo ya mwili yasiyo ya asili, imewekwa kuwa dalili, wakiadhibiwa katika moto wa milele”.


2Petro 2: 4 “Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu;
5 wala hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki, na watu wengine saba, hapo alipoleta Gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu;
6 tena akaihukumu miji ya Sodoma na Gomora, akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya;”


Unaona hapo? Kuna hatari nyingi sana leo hii tukiifanya miili yetu kuwa makao ya mashetani, mtu yeyote ambaye bado hajasafishwa kwa damu ya YESU KRISTO na kupata ondoleo la dhambi zake na kubatizwa ipasavyo na kupokea Roho Mtakatifu, basi mtu huyo yeye ni makao na kimbilio la roho chafu za mashetani zilizoasi.. Mtu yeyote ambaye ni mwasherati na mzinzi basi yeye ni hifadhi wa makao ya mapepo, mtu yeyote ambaye ni mwabudu sanamu, kadhalika yeye naye ni makao ya mapepo, mtu yoyote aliye mshirikiana na mchawi, na anayejihusisha na masuala ya waganga wa kienyeji, mwili wake ni makao ya mapepo wachafu..mwanamke yeyote ambaye anavaa nguo za uchi, na vimini na suruali basi huyo ni makao ya mapepo. Na akiendelea hivyo hivyo mpaka siku atakapokufa naye moja kwa moja atajikuta kwenye vifungo vya shimo hilo la kuzimu pamoja na watu wa sodoma na gomora na watu wa kipindi cha Nuhu pamoja na yale mapepo wakisubiria hukumu ya siku ya mwisho. Kisha wakatupwe kwenye lile ziwa la moto.

Zamani katika agano la kale mtu mwenye pepo hukumu yake ilikuwa ni kifo.

Walawi 20: 26 “Nanyi mtakuwa watakatifu kwangu mimi; kwa kuwa mimi Bwana ni mtakatifu nami nimewatenga ninyi na mataifa, ili kwamba mwe wangu.
27 TENA MTU MUME AU MTU MKE ALIYE NA PEPO, au aliye mchawi, hakika atauawa; watawapiga kwa mawe; damu yao itakuwa juu yao”.


Tukiyajua hayo, na tukifahamu kuwa shetani na mapepo yake yanazunguka kila siku duniani yakitafuta hifadhi ndani ya wanadamu. Basi tutaishi maisha ya kujichunga kila siku. Tutazijaribu hizi roho zote zinazokuja mbele yetu na mafundisho yake ya uongo. Tutaishi maisha ya uangalifu huku tukimruhusu Roho Mtakatifu achukue sehemu yote ya maisha yetu. 


Bwana akubariki.

Tafadhali “share” kwa wengine ujumbe huu. Na Mungu atakubariki.

No comments:

Post a Comment