Inaaminiwa na wengi wetu kuwa Mariamu, mama,
aliyemzaa Bwana wetu Yesu Kristo, alikuwa ni mwanamke wa kipekee sana, na
aliyebarikiwa zaidi ya wanawake wengine wote, na kabla hajapata Neema ya kumzaa
Bwana wetu Yesu Kristo alikuwa ni mtu mkuu sana, na anayependwa sana na
aliyeheshimika sana...Lakini je! ni kweli maandiko yanasema hivyo?
Tukisoma maandiko kitabu cha Luka 1: 1.42 inasema “akapaza sauti kwa nguvu akasema, UMEBARIKIWA
WEWE KATIKA WANAWAKE, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa”.
Maneno hayo
yalizungumzwa na Elizabeth, mama yake Yohana Mbatizaji baada ya kukutana na
Mariamu, Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu akambariki na kumwambia UMEBARIKIWA WEWE
KATIKA WANAWAKE.
Sasa jambo la muhimu
la kuzingatia hapo ni hilo neno “KATIKA” Hakusema “kuliko wanawake wote” hapana
bali “katika”
Ikiwa na maana kuwa katika wanawake
waliobarikiwa na yeye (Mariamu) ni mmoja wapo..na sio kwamba yeye kabarikiwa
kuliko wote..
Wakati Fulani mwanamke mmoja alimtaja Mariamu
kuwa kabarikiwa sana, mbele ya umati mkubwa wa watu na mbele ya Bwana Yesu,
lakini Bwana alimrekebisha pale pale na kumwambia HERI walisikiao Neno la Mungu
na kulishika..
Sasa maana ya neno heri ni “amebarikiwa yeye”
Luka 11:27 “Ikawa alipokuwa akisema maneno hayo, mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia, Heri {limebarikiwa} tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya. Lakini yeye alisema, Afadhali, heri{wamebarikiwa} walisikiao neno la Mungu na kulishika”.
Kwa lugha nyepesi katika mstari huo tunaweza
kusema “...Mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake akamwambia; amebarikiwa
mwanamke Mariamu aliyekuzaa, lakini Bwana akasema amebarikiwa zaidi mwanamke
Yule alisikiaye Neno la Mungu na kulishika”
Kwahiyo unaweza ukaona hapo ingekuwa Mariamu
amebarikiwa kuliko wanawake wote, Bwana Yesu asingemkosoa huyu mwanamke
aliyekuja Kumtangaza Mariamu hadharani kuwa ni mbarikiwa.
Na pia kumbuka Bwana Yesu hakutabiriwa kutokea katika ukoo wa
Mariamu, bali ukoo wa Yusufu Mumewe Mariamu..ndio maana ukisoma pale mwanzo wa
kitabu cha Mathayo utaona ukoo wa Bwana Yesu Ulianzia kwa Ibrahimu na ukaishia
kwa Yusufu mumewe Mariamu, na haukuanzia kwa Ibrahimu na kuishia kwa wazazi wake
Mariamu. Hivyo unaweza ukaona ni neema tu Mariamu kumzaa Bwana.
Kwahiyo ni muhimu kufahamu hilo ili tusije
tukamwona Mtu Fulani ni wa kipekee sana katika maandiko zaidi ya mwingine, Imefikia
wakati watu wanamaabudu Marimu, bila hata hofu ya Mungu, mwanamuhisisha katika
ibada zao na kumtolea shukrani kana kwamba yeye ni Kristo. Hata Nabii Eliya
biblia inatuambia alikuwa ni mtu mwenye tabia moja na sisi (Yakobo 5:17). Mfano
kama biblia isingeandika vile leo hii si
ajabu tungewaona watu wamemfanya leo kuwa ni mtu wa nne katika uungu wa Mungu.
Ni
YESU KRISTO, peke yake aliye Mfalme wa
wafalme, na Bwana wa mabwana ndiye aliyekuwa wa kipekee zaidi ya wengine wote
duniani...
Sasa tukirudi kwenye kiini cha somo ambacho
tutaona ni jambo gani lililomfanya
Mariamu, apate neema ya kumzaa Mwokozi wa Ulimwengu Yesu Kristo.
Awali ya yote Biblia takatifu haijaelezea
maisha ya nyuma ya Mariamu kabla ya kumzaa Bwana wetu Yesu Kristo..Lakini tukiyachunguza
maandiko kwa undani tunaweza tukapata
dondoo chache za maisha yake ya nyuma jinsi yalivyokuwa..
Sasa kabla ya kumsoma Mariamu hebu tuwasome
kidogo Wanawake wachache kwenye maandiko waliopewa neema ya kuzaa baadhi ya MASHUJAA..
Tukianza na mwanamke wa Kwanza wakati wa
kipindi cha Waamuzi, aliyekuwa (Mke wa mtu mmoja aliyeitwa Manoa) Tunasoma hivi..
Waamuzi 13: 2 “Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; NA MKEWE ALIKUWA TASA, hakuzaa watoto.3 Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini UTACHUKUA MIMBA, NAWE UTAMZAA MTOTO MWANAMUME.4 Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi;5 kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti”.
Mwanamke huyu ndiye
aliyemzaa shujaa Samsoni...Sasa ukiyachunguza kwa makini maisha yake utagundua
alikuwa ni Mwanamke aliyekuwa MNYONGE kwa sababu alikuwa tasa..wakati wanawake wengine wana watoto yeye hakuwa na
mtoto hata mmoja na umri wake umeshakwenda...Na inaelekea alikuwa katika hali
hiyo kwa muda mrefu akimwomba Mungu usiku na mchana, na pengine alimwekea
nadhiri Bwana kwamba endapo atapata mtoto wa kiume atampatia Bwana kama sadaka.
Hivyo aliendelea kubakia katika hali
hiyo hiyo paka siku malaika wa Bwana alipomtokea na kumwambia atazaa mtoto wa
kiume (Samsoni) ambaye atawaokoa watu wake Israeli na maadui zao. Huyu Samsoni
biblia inasema alikuwa ni Mnadhiri wa Bwana tangu tumboni mwa mama yake.
Tukirudi tena kwenye
maandiko tunamwona mwanamke mwingine aliyezaa Shujaa..Na huyu si mwingine zaidi
ya Hana mke wa Helkana. Huyu naye hakuwa na mtoto kwa muda mrefu na zaidi ya
yote, mke mwenza alikuwa akimtesa na kumchokoza mara kwa mara kutokana na hali
yake ya utasa..Hivyo kwasababu ni mcha Mungu na alikuwa mwenye haki alimwekea Bwana
nadhiri kwamba endapo atapata Mtoto wa kiume atamweka wakfu kwa Bwana maisha
yake yote...na Bwana alimkumbuka akampa Neema ya kumzaa Nabii Samweli, aliyekuja
kuwa nabii mkubwa sana Israeli na Mwamuzi. Na hivyo Bwana akautoa UNYONGE wake
akampatia Faraja yake dhidi ya dhiki na mateso aliyokuwa anayapitia kwa muda
mrefu.
Hivyo Hana alifurahi sana mpaka akazungumza
maneno haya..
1 Samweli 2: 1 “Naye Hana akaomba, akasema, Moyo wangu wamshangilia Bwana, Pembe yangu imetukuka katika Bwana, Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu; Kwa kuwa naufurahia wokovu wako;2 Hakuna aliye mtakatifu kama Bwana; Kwa maana hakuna ye yote ila wewe, Wala hakuna mwamba kama Mungu wetu.2 Samwli 2:3 “Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani.4 Pinde zao mashujaa zimevunjika, Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu.5 Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula, Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha. Naam, huyo aliyekua tasa amezaa watoto saba, Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika.6 Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu.7 Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu.8 HUMWINUA MNYONGE KUTOKA MAVUMBINI, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake”.
Ukisoma mstari wa 8 unasema “HUMWINUA MNYONGE KUTOKA MAVUMBINI” Ikifunua kuwa hapo kwanza Hana alikuwa mnyonge lakini Bwana
alimwinua kutoka mavumbini, alikuwa chini na sasa Bwana kamwinua juu sana..alikuwa hana mtoto
lakini sasa kamzaa shujaa Samweli n.k
Tukimtazama mwanamke wa Mwisho katika
maandiko ambaye naye pia alizaa Shujaa...alikuwa ni Elizabethi aliyekuwa ndugu
yake Mariamu. Huyu Elizabeth naye alikuwa ni Tasa, hakuwa na Mtoto mpaka
alipokuwa mzee, yeye pamoja na Mume wake Zakaria walikuwa ni wacha Mungu.. Na
zaidi ya yote mume wake alikuwa ni Kuhani hivyo walikuwa wakiomba dua usiku na
mchana kuhusu hali yao..Siku moja malaika alimtoke Zakaria na kumwambia mkewe
aliye Tasa atachukua Mimba, na atazaa mtoto ambaye atawarejesha wengi kwa
Bwana.. Na huyu mtoto tunakuja kumwona si mwingine zaidi ya YOHANA MBATIZAJI,
ambaye alitabiriwa kuja kwa roho ya Eliya..Shujaa wa Bwana aliyetabiriwa
kuitengeneza njia ya Bwana. Habari yake inapatikana katika (Luka mlango wa
kwanza wote).
Sasa tabia za wanawake wote hawa watatu,: Yaani
Mke wa Manoa, Hana, pamoja na Elizabethi utaona kuwa walikuwa ni wanawake
wanyonge na wacha Mungu, na watulivu, na waliodharaulika... Hakuna hata mmoja
aliyekuwa na heshima katika jamii ya watu wake wanaowazunguka, walikuwa ni
wanawake wasio na uzao, kwa mfano Hana, hakuwa na watoto lakini bado alikuwa
anamcha Mungu, alikuwa hakosi zamu za kwenda kuabudu Yerusalemu...Hivyo kwa
mienendo yao inayompendeza Bwana na ya utulivu, na ya kusubiri kwa muda mrefu,
Bwana akawapa neema ya Kuzaa MASHUJAA..
Na sio hao tu, tazama maisha ya Sara ambaye
alikuwa mgumba kwa miaka mingi, mwanamke aliyemcha Mungu na mume wake mpaka
kufikia hatua ya kumwita mumewe bwana. Mwanamke aliyedharauliwa na wanawake
wengine wote lakini yeye ndiye alikuyekuja kumzaa Isaka. Vivyo hivyo tunaowaona
akina Rebeka mambo yale yale, Raheli ambaye alikuja kumzaa Yusufu, mambo yale
yale n.k.
Sasa mpaka hapo tumeshaanza kupata picha ya
MWANAMKE MARIAMU jinsi alivyokuwa naye alikuwa ni mwanamke wa dizaini gani??
Kwa kuwasoma maisha ya hao wanawake watatu waliotangulia unaweza ukapata picha
kuwa Mariamu naye sio kwamba alikuwa ni mwanamke aliyekuwa na kila kitu, au
aliyekuwa na heshima...Hapana! Utaona tabia yake na maisha yake ni lazima itakuwa
yanafanana na hao wanawake watatu waliomtangulia... Inawezekana yeye hakuwa
Tasa kwasababu alikuwa ni Bikira lakini alikuwa ni mjonge mahali Fulani..
alikuwa ni mwanamke aliyedharaulika...pengine familia yao ilikuwa inajulikana ni
duni tu, na pengine ilikuwa haina jina...Pengine wabinti wenzake walikuwa
wanafanikiwa na kuzaa watoto wenye sifa, yeye alijitunza tu! Alikuwa anachekwa
kama Hana, alikuwa ni mdhaifu, na alikuwa hana umaarufu wowote, pengine alikuwa
hana uzuri sana wa kuvutia kama mmojawapo ya wanawake wa kidunia waliokuwepo
kipindi kile, lakini alikuwa mcha Mungu...
Lakini ulipofika wakati. Bwana akautazama
unyonge wake..akamkirimia kumzaa SHUJAA WA MASHUJAA, na MFALME WA WAFALME
haleluya!! Malaika wa Bwana akatumwa kama alivyotumwa kwa mke wa Manoa,
akatumwa kama alivyotumwa kwa Zekaria Mume wa Elizabethi, akaambiwa atachukua
mimba kwa uwezo wa Roho na kumzaa Bwana Yesu. Hivyo Bwana akawa amemwondolea
unyonge wake, na yeye akajihisi ni mwanamke kati ya wanawake waliobarikiwa..ndio
maana utakuja kuona akisema...
Luka 1: 46 “Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,47 Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu;48 Kwa kuwa ameutazama UNYONGE WA MJAKAZI WAKE. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa;49 Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu.50 Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi Kwa hao wanaomcha.51 Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao;52 Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; NA WANYONGE AMEWAKWEZA.53 WENYE NJAA AMEWASHIBISHA MEMA, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu”.Unaona anasema hapo “wanyonge amewakweza” ikiwa na maana kuwa hapo kwanza naye pia alikuwa mnyonge.
Ni jambo gani la kujifunza kwa Mariamu na
wanawake hawa wengine?
Katika hali zao za Unyonge walimngojea Bwana
na kumtumainia kwa saburi, na pili walijua Bwana ndiye anayeshusha na ndiye
anayepandisha...Walipoona tabu nje! Bwana ndiye aliyekuwa kimbilio lao, Hana
hakuzunguka kwa wapunga pepo kupata utatuzi wa tatizo lake, wala Elizabethi
hakuwatafuta waganga wamtatulie tatizo lake la kukosa mtoto, walijua ni Bwana
ndiye aliyewafunga matumbo yao na ipo siku yatafunguka..hivyo waliendelea kukaa
katika njia zake..
Hakuna hata mmoja unaona akimlaumu Mungu
katika hali yake ya unyonge aliyokuwa anapitia, wote walikuwa katika hali ya
utulivu mpaka ulipofikia wakati wa Ahadi zao kutimia wote walizaa
mashujaa..Ukimsoma pia Sara na Rebeka na Raheli na Ruthu aliyekuwa bibi yake
Daudi..utaona jambo hilo hilo, wote walikuwa ni wanawake wavumilvu na
hawakuiacha njia yao ya haki na mwisho wakazaa mashujaa.
Hivyo Dada/Kaka unayesoma ujumbe huu, ukitaka
kuzaa Shujaa katika maisha yako epuka manunguniko, epuka njia za mkato, kubali
kudharauliwa na kuwa mnyonge, kubali kuonekana sasa wewe ni mshamba katika
Kristo,kubali kuonekana tasa usiyeweza kufanya chochote maadamu unamcha Mungu
usiogope. kwasababu utafika wakati Bwana atalikumbuka teso la kijakazi wake
kama Mariamu alivyosema.
Unapokosa kitu sasa usiwalaani waliokuwa
nacho, wabariki,ukikosa mtoto sasa usiwalaani wanaokulaani, usizunguke kwa
waganga, wala usiuache UTAKATIFU wako, ishi maisha yanayompendeza Mungu kila
siku,ukijiepusha na mambo yote mabaya ya ulimwengu, kwasababu Mungu anao wakati
wake na majira yake, na ukifika wakati Bwana atakufurahisha kama
alivyomfurahisha Mariamu , atautoa unyonge wako kama alivyoutoa wa Mariamu na
wengine.
Isaya 54: 1 “Imba, wewe uliye tasa, wewe usiyezaa; paza sauti yako kwa kuimba, piga kelele, wewe usiyekuwa na utungu; maana watoto wake aliyeachwa ni wengi kuliko watoto wake yeye aliyeolewa, asema Bwana”.
Bwana akubariki.
Tafadhali “share”
ujumbe huu kwa wengine.
No comments:
Post a Comment