"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, December 5, 2018

WEWE NI HEKALU LA MUNGU.

Mwili wa mwanadamu au mnyama yoyote ni makazi ya roho, hakuna mtu asiyekuwa na roho ndani yake wala hakuna mnyama asiyekuwa na roho ndani yake. Kwahiyo mwili ni kama mavazi ya roho. 

Kwahiyo mtu aliyempa Yesu Kristo maisha yake, aliyetubu kabisa dhambi zake, na kubatizwa na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu, ndani yake kunakuwa na roho mbili, {Roho yake binafsi na Roho wa Mungu(Roho Mtakatifu)}. Roho Mtakatifu kazi yake anapoingia ndani ya mtu, kazi yake ni kuwa msaidizi, anaisaidia roho ya mtu aliyempa Bwana maisha yake ili itende mapenzi ya Mungu aliye mbinguni. Anaingia katika vyumba vya ndani kabisa vya moyo na anafanya kazi kwa namna ya kipekee ambayo haiwezi kuchunguzika kirahisi. 


biblia imesema katika:

1Wakorintho 6: 19 “ Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu”.
Sasa kumbuka hapo inasema kuwa mwili wenu ni HEKALU LA ROHO MTAKATIFU, haijasema miili yenu ni NYUMBA YA ROHO MTAKATIFU. Na kama unavyojua hekalu ni tofauti na nyumba ya kawaida, nyumba ya kawaida inaweza ikawa na matumizi mengi, inaweza ikageuzwa ikawa ya kupangishwa, inaweza ukauzwa, inaweza kutumika leo kama nyumba ya familia kesho ikawa nyumba ya kulala wageni, inaweza ukageuzwa ikawa sehemu ya biashara n.k Lakini tunapozungumzia hekalu, haliwezi likawa kwa jinsi mtu anavyotaka…Hekalu kazi yake ni moja tu “NI MAHALI PA KUFANYIA SALA NA IBADA BASI!”

Kwahiyo Unaweza ukaona hekalu ni sehemu nzito kidogo, na ina sheria kali kidogo kuliko nyumba ya kawaida. Hivyo mtu anapopokea kipawa cha Roho Mtakatifu mwili wake siku ile ile unageuka, na kuwa HEKALU LA ROHO MTAKATIFU. Kuanzia huo wakati na kuendelea shughuli zinazofanyika ndani yake ni shughuli za Ibada na sala tu!.

Ndio maana Roho Mtakatifu anazidi kusisitiza jambo hilo hilo kwa kinywa cha Mtume Paulo na kusema…1Wakorintho 3: 16 “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa HEKALU LA MUNGU, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi”.

Kama pia ni mfuatiliaji wa maandiko utagundua kuwa Hekalu ni tofauti na Sinagogi, Sinagogi ni mahali palipokuwa pameandaliwa na wayahudi wa zamani kwa ajili ya kujifunza sheria na torati, kwasasa tunaweza tukasema ni mahali kama kanisani. Na haya masinagogi yalikuwepo mengi, sehemu kadha wa kadha katika Israeli, Lakini Hekalu lilikuwa ni moja tu! duniani, na hekalu Lilikuwa na sehemu na sehemu kuu tatu 1) UA WA NDANI, 2) PATAKATIFU na 3) PATAKATIFU PA PATAKATIFU.

Kwa lugha nyepesi UA wa ndani ni UANI, Tengeneza picha nyumba yenye uzio wa ukuta, NA Ina sebule na chumba kimoja,sasa kule uani, ndipo palipoitwa UA WA NDANI katika Hekalu la Mungu, na sehemu ya pili paliitwa PATAKATIFU…Sehemu hii kwa sasa tunaweza tukapaita SEBULENI, na sehemu ya tatu na ya mwisho paliitwa PATAKATIFU PA PATAKATIFU..kwasasa tunaweza kusema ni kile chumba cha ndani cha MASTER.

Sasa Bwana aliagiza sehemu zote hizi zinapaswa ziwe safi. Kusiwepo mtu yoyote wa kulitia unajisi HEKALU LA MUNGU. Na sio kila mtu aliyekuwa na ruhusa ya kuingia ndani ya hekalu la Mungu, isipokuwa makuhani peke yao wana wa Lawi.. Lakini sehemu nyingine kama kwenye masinagogi watu wote walikuwa wanaruhusiwa kuingia kusali na kujifunza torati.

Sasa kama biblia inasema sisi ni Hekalu la Roho Mtakatifu basi ni wazi kuwa ndani yetu kuna sehemu kuu tatu ambazo zinapaswa ziwe takatifu sana.

Sehemu ya kwanza ni Miili yetu kwa nje(ambayo inafananishwa na ule UA WA NDANI), Sehemu ya pili ni ndani ya miili yetu ambapo kuna Nafsi (panapofananishwa na PATAKATIFU) Na sehemu ya tatu ni ndani kabisa mwa vyumbwa vya roho zetu (ambapo ndipo PATAKATIFU PA PATAKATIFU). Sehemu zote hizi tatu zinapaswa ziwe takatifu. 


Bwana Yesu alipofika Yerusalemu, alikuta watu wanauza njiwa, na kufanya biashara kwenye Hekalu la Mungu, na ndipo Hasira ya kimungu ikawaka ndani yake.. na kuanza kuangusha kila kitu ndani ya Hekalu na kusema maneno haya… “Imeandikwa, NYUMBA YANGU ITAITWA NYUMBA YA SALA; bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.Mathayo 21:13”

Unaona hapo, sio kwamba hakukutana na watu katika masinagogi mengine mbali mbali waliokuwa wanafanya biashara, alikutana nao wengi hata alipokuwa Nazareti lakini hakuchukizwa nao sana kama alivyochukizwa na wale waliokuwa wanafanya biashara katika HEKALU TEULE MOJA TU LA MUNGU MWENYEZI lililokuwa Yerusalemu…

Kumbuka hawa wafanya biashara hawakuwa wanafanya biashara ndani kule PATAKATIFU PA PATAKATIFU. Hapana! Walikuwa wanafanya biashara zao maeneo ya UA WA NJE, ndani wasingeweza kufika kwasababu ni kuhani mkuu tu! peke yake ndiye aliyekuwa anaingia kule.

Sasa hayo yana maana gani? Tunapokuwa tumeokoka, na Roho Mtakatifu anakaa ndani yetu, moja kwa moja, miili yetu inabadilishwa na kuwa Hekalu la Mungu, kumbuka sio kila mtu ni hekalu la Mungu, hapana! Bali ni wale tu waliompa Bwana Yesu maisha yao, hao ndio miili yao inafanyika Hekalu la Roho Mtakatifu. Wengine ambao hawajampa, miili yao sio hekalu la Mungu kwasababu ndani yao hawana Roho Mtakatifu, wana roho nyingine…Hivyo miili yao ni mahekalu ya hizo roho nyingine ambazo ni za mashetani.

Kwasababu hiyo basi, tunaweza kufahamu kuwa MIILI YETU, na NAFSI ZETU na ROHO ZETU zinapaswa ziwe katika hali ya USAFI kila wakati kwasababu, NDIVYO VIUNGO VITATU vinavyounda Hekalu la Roho Mtakatifu. 

1Wathesalonike 5: 23 “Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi NAFSI ZENU na ROHO ZENU na MIILI YENU mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo”.
Unaona hapo, usafi unaanza Nje ya Mwili, kisha kwenye Nafsi ya mtu, na mwisho unaishia ndani katika roho ya Mtu.

Sasa hebu tujifunze kidogo usafi wa nje wa mwili unaohitajika ni upi? 

Inaaminika na wengi kuwa “Mungu huwa haangalii mwili na badala yake anaangalia roho tu” Nataka nikuambie kwa upendo kabisa ndugu yangu unayesoma haya, Mungu haangalii mwili, au nafsi yako, wala roho yako, Mungu anaangalia Hekalu lake kwa ujumla. Na hekalu lake ndio limeundwa na hivyo vitu vitatu mwili, nafsi na roho.

Kumbuka tena waliokuwa wanafanya biashara katika Hekalu la Mungu, ambao Bwana Yesu aliwafukuza walikuwa hawafanyi biashara hizo ndani ya patakatifu, au patakatifu pa patakatifu, hapana! Walikuwa wanafanya karibu na UA WA NDANI. Na jambo hilo bado lilimchukiza sana Bwana.. 

Na kadhalika leo, jambo lile lile Biashara inapofanyika katika UA WA NDANI (juu ya mwili), jambo hilo ni baya sana na linamchukiza Mungu, kuliko mambo mengine yote!! Na jambo hilo linaweza kumsababishia mtu hata mauti ya kimwili. Yafuatayo makuu mawili yasiyotakiwa kabisa kufanyika juu ya Hekalu la Mungu.

1 ) UASHERATI
Uasherati ndio jambo la kwanza kabisa linaloweza kumwangamiza mtu anayesema amempa Bwana maisha yake, Na uasherati/uzinzi ndio dhambi ya kwanza inayoliharibu Hekalu la Roho Mtakatifu..Mtu mzinifu na bado anasema ameokoka..anafanya dhambi mbaya kuliko hata mtu mwuaji ambaye hajampa Bwana maisha yake.

* 1 Wakorintho 6:17 “Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye.

18 IKIMBIENI ZINAA. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe”.

* Mithali 6: 32 “Mtu aziniye na mwanamke HANA AKILI KABISA; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake”.

Ningependa nikukumbushe kitu kimoja mwana wa Mungu, Hasira ya Mungu haiji kwanza kutokana na maovu ya watu wasiomwamini, hapana! Ghadhabu ya Mungu duniani inaletwa kwanza kutokana na maovu ya watu wanaomwamini…Kumbuka gharika ya kwanza ilikuja kwasababu gani? “Ni kwasababu wana wa Mungu waliwatamani binti za Binadamu” yaani Watoto wa Mungu waliwatamani binti wa ulimwengu huu, ndipo ghadhabu ya Mungu ilipopanda.

Na kadhalika katika siku hizi za mwisho, watu wengi wanaosema wameokoka lakini ni vuguvugu ndio watakaochangia pakubwa kuivuta ghadhabu ya Mungu duniani…Ukisoma pia biblia agano la kale utaona, Bwana Mungu alikuwa akichukizwa na maovu ya wana wa Israeli, sio kwamba wana wa Israeli ndio waliokuwa watu waovu kuliko wote duniani, hapana ni kwasababu wao ndio waliokuwa wana wa Mungu. Hivyo maovu wanayoyafanya wao yanaonekana sana machoni pa Mungu, kuliko watu wa mataifa.

Shetani anachofanya katika siku hizi za mwisho, ni kuwadanganya watu wanaosema wamempa Bwana maisha yao, wakike na kiume kujiingiza katika mahusiano..kwa kisingizio kwamba watakuja kuoana wakati Fulani mbeleni, hivyo wanaingia katika dhambi ya uasherati, pasipo kujua njama za shetani. 


Kaka/Dada..usidanganyike, uashetari kabla ya ndoa, ni sawa na kujiwekea kitanzi mwenyewe shingoni na kwenda kujiua. Ni sawa na ndege anayeenda mtegoni peke yake biblia inasema hivyo katika (Mithali 7:23-27). 

Biblia inasema pia “unafanya jambo litakalokuangamiza nafsi yako”. Bwana hawezi kuridhia huo uovu juu ya Hekalu lake, ambalo lingepaswa kuwa Takatifu, na sehemu ya sala. Ni heri uwe umeamua kuwa mtu wa ulimwengu kuliko kusema umeokolewa na YESU KRISTO halafu unafanya uasherati. Ni hatari sana.

2 ) Jambo la Pili ni MAPAMBO
Mapambo yoyote ambayo yanaweza kuning’inizwa juu ya mwili wa mtu, ni machukizo mbele makubwa mbele za Mungu, Wengi hawapendi kusikia haya lakini ni afadhali usikie leo hii ubadilike, ili siku ile usije ukasema “mbona sikupata mtu aliyeniambia ukweli”.

Nataka nikuambie UKWELI ndugu/Dada yoyote unayevaa wigi, au unayevaa herein au unayevaa nguo fupi (yaani vimini, pamoja na suruali kwa wadada)..au unayevaa mambo yoyote ambayo hujui maana yake, na bado umesema umempa Bwana maisha yako..kama unafanya hayo pasipo kujua, leo hii nakuambia ukweli yaache mambo hayo yanapeleka mamilioni kuzimu. Mwili wako tangu ulipompa Bwana maisha yako ulifanyika Hekalu lake, sio nyumba yake…zingatia hilo Neno HEKALU!!

Utauliza kuvaa herein kuna shida gani? Historia ya kutobolewa masikio ipo kwenye biblia..Katika agano la kale kitabu cha kutoka Mlango wa 21 tunasoma..

1 Basi hukumu utakazoziweka mbele ya watu ni hizi2 Ukimnunua mtumwa wa Kiebrania, atakutumikia muda wa miaka sita; mwaka wa saba atatoka kwako huru bure.3 Kwamba aliingia kwako peke yake tu, atatoka hivyo peke yake; kwamba ameoa, mkewe atatoka aende pamoja naye.
4 Kwamba ni bwana wake aliyempa huyo mke, naye amemzalia wana, wa kiume au wa kike; yule mke na wanawe watakuwa ni mali ya bwana wake, naye mume atatoka peke yake.
5 Lakini huyo mtumwa akisema waziwazi, Mimi nampenda bwana wangu, na mke wangu na watoto wangu; sitaki mimi kutoka niwe huru;
6 ndipo hapo huyo bwana wake atamleta mbele ya Mungu na kumleta mlangoni, au penye mwimo wa mlango; na bwana wake ATALITOBOA SIKIO LAKE KWA UMA; NDIPO ATAMTUMIKIA SIKUZOTE."
Unaona hapo? Mtumwa aliyekataa uhuru ndiye aliyetobolewa sikio? Ishara kwamba amekataa kupewa uhuru..kwahiyo leo hii mtu yoyote awe mwanaume au mwanamke anayetobolewa masikio katika roho ni “mtumwa aliyekataa uhuru” na uhuru tunaopewa leo ni uhuru wa dhambi, kwahiyo mtu anayetoboa masikio na kuweka hereni ni ishara ya mtumwa aliyekataa kuwekwa huru mbali na dhambi na Bwana wake.

Ndugu au dada unayetoboa masikio na kuvaa hereni, jiepushe na hayo mambo…pengine ulifanya pasipo kujua, tubu tu na ujirekebishe kwasababu ulikuwa hujui..huwezi kuziba lile tundu kwenye sikio lakini acha kuvaa hizo hereni kwasababu ukifanya hivyo unakuwa unatilia muhuri lile agano la kukataa uhuru.

Kadhalika pia uvaaji wa WIGI na upakaji wa UWANJA pia upo katika biblia.. Ukisoma kitabu cha 2 Wafalme 9: 30 “Hata Yehu alipofika Yezreeli, Yezebeli akapata habari; AKATIA UWANJA MACHONI MWAKE, AKAPAMBA KICHWA CHAKE, akachungulia dirishani”.

Huyu mwanamke Yezebeli ndiye mwanamke pekee katika maandiko aliyekuwa anapaka uwanja, hakukuwa na mwanamke yoyote aliyekuwa anapaka wanja katika Israeli, sasa huyu Yezebeli alikuwa ni mke wa Mfalme Ahabu, asili yake hakuwa mwisraeli bali alikuwa ni mwenyeji wa nchi inayojulikana leo kama Lebanoni. Huyu mwanamke hakuwa anamwabudu Mungu wa Israeli, bali alikuwa anamwabudu Baali miungu ya kipagani.

Mfalme Ahabu alipomtoa katika hiyo nchi ya Lebanoni, alikuja Israeli na manabii wake wa kipagani (manabii wa Baali) kumsaidia kufanya shughuli zake za kuabudu miungu, mwanamke huyu Biblia inasema pia alikuwa ni MCHAWI !!! Na hivyo uchawi wake ulizidi mpaka kwenye mwili wake, alikuwa anapaka UWANJA kama desturi ya miungu yao, kuongeza nguvu zake za kiroho.

Mwanamke huyu ndiye aliyewakosesha sana Israeli na kuwafundisha baadhi ya waisraeli kushiriki ibada za sanamu, ndiye aliyemsumbua sana nabii ELIYA, Na alikuwa mkatili sana,kwa ufupi alileta machafuko makubwa sana Israeli. Na roho yake utakuja kuona inatajwa tena katika kitabu cha ufunuo. 

Ufunuo 2: 20 “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia YULE MWANAMKE YEZEBELI, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu.
21 Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake”.

Kwahiyo nataka uone dada roho iliyopo ndani ya hayo mapambo (wanja,wigi na hereni)..wanawake wachawi wa kimataifa ndio waliokuwa wanafanya hivyo ili kuchochea nguvu za giza ndani yao, ni sawa sasahivi wachawi wanavyovaa hirizi viunoni, kujichanja chale, na kujichora na machaki usoni na kutembea uchi miaka Fulani mbeleni ije kuwa fashioni watu wote wafanye hivyo…hicho ndicho kilichotokea kwa wigi na uwanja, na uchoraji wa tatoo zamani wachawi ndio waliokuwa wanafanya lakini nyakati hizi ni watu wanaojiita watu wa Mungu…Uchoraji wa Tatoo zilikuwa zinafanyika kwenye ibada za wafu na zilikuwa ni desturi za kipagani..

Walawi 19: 28 “Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, WALA MSIANDIKE ALAMA MIILINI MWENU; mimi ndimi Bwana”.

Kwahiyo dada au kaka unayesoma ujumbe huu, fahamu kuwa tangu siku ulipompa Bwana maisha yake, Roho Mtakatifu alikugeuza wewe kuwa Hekalu lake takatifu, usiliharibu ili naye asikuharibu. Kama ulikuwa unafanya hayo pasipo kujua, Mungu ni mwenye huruma, leo hii umeujua ukweli ukitubu kwa kusudia kutokufanya hayo tena yeye ni mwaminifu atakusamehe kulingana na Neno lake, tupa leo hizo suruali ulizokuwa unavaa, tupa leo hizo wigi, na hereni ulizokuwa unavaa, acha kupaka uwanja na lipstick…weka nywele zako katika uhalisia wake, zitunze tu, na la muhimu kabisa Acha uasherati. Usitamkwe kabisa! Litakase Hekalu la Mungu.

Bwana akubariki, na kama hujampa Bwana maisha yako, ni vyema ukafanya hivyo leo, angali mlango wa Neema haujafungwa, mgeukie yeye kwamaana biblia inasema “mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, kabla hazijakaribia siku zilizo mbaya”.

Bwana akusaidie katika hilo na aikamilishe safari njema aliyoianza moyoni mwako.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na Mungu atakubariki.

No comments:

Post a Comment