"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, December 20, 2018

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 47


 SWALI 1: Kutoka 10:1 “BWANA anasema atampa Farao moyo Mgumu, asimtii, je! hapo Bwana Atamhukumu Farao kama mkosaji?”.
JIBU: Ndio atamuhukumu kama mkosaji, na ndio maana utaona zile adhabu zote zilimpata!! Hata kufiwa na mtoto wake wa kwanza…Na baada ya kufa kama hakupewa moyo wa kutubu, basi bado ataenda jehanamu ya moto.

Kumbuka Moyo wa kutubu na moyo wa kumtafuta Mungu, ni Mungu mwenyewe ndio anaotoa sio sisi tunaoamua kwa juhudi zetu..ndio maana Bwana Yesu alisema katika “Yohana 6: 44 Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka;”..Umeona hapo? Nguvu ya mtu kumfuata Mungu ni Mungu mwenyewe ndiye anayekujalia..vinginevyo haiwezekani kumtafuta Mungu wala kumfuata.

Sasa Kwanini Mungu amjalie Musa moyo mlaini wa kumkubali na Farao ampe moyo mgumu wa kumkataa??..hatujui na wala hatuwezi kumuuliza Mungu hayo maswali, ndivyo ilivyompendeza yeye, ni sawa na tumuulize Mungu alitokea wapi?? Hayo ni maswali tusiokuwa na majibu nayo….Yapo juu ya upeo wa fikra zetu.

Na ndio maana mtume Paulo alisema katika..

Warumi 9.13 “Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia.
14 Tuseme nini basi? Kuna udhalimu kwa Mungu? Hasha!
15 Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye.
16 Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.
17 Kwa maana maandiko YASEMA JUU YA FARAO, ya kwamba, nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote.
18 BASI, KAMA NI HIVYO, ATAKAYE KUMREHEMU HUMREHEMU, NA ATAKAYE KUMFANYA MGUMU HUMFANYA MGUMU.
19 Basi, utaniambia, MBONA ANGALI AKILAUMU? Kwa maana NI NANI ASHINDANAYE NA KUSUDI LAKE?
20 La! Sivyo, Ee binadamu; WEWE U NANI UMJIBUYE MUNGU? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi?
21 Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?”

Unaona hapo? Biblia inasema pia wapo watu ambao hawajakusudiwa uzima wa milele, watu ambao majina yao hayajaandikwa katika kitabu cha uzima kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu (ufunuo 17:18 na Ufunuo 13:8)..Swali ni Ni wakina nani hao?? Jibu ni kwamba Hatuwajui, Mungu ndie anayewajua…sisi sio kazi yetu kuwafahamu, jukumu tulilopewa ni kuhubiri injili kwa kila kiumbe kana kwamba wote wote wamekusudiwa uzima wa Milele,…Na kujitahidi kuishi kulingana na maagizo yake na amri zake,ili tuwe na uhakika sisi sio miongoni mwa hilo kundi lililoandikiwa kupotea milele.Kwasababu dalili kuu inayotambulisha kuwa umekusudiwa uzima wa milele ni pale mtu anapoitii na kubadilika, kadhalika dalili kubwa inayoweza kumtambulisha kama mtu huyo hajakusudiwa uzima wa milele, ni pale anapoupinga wokovu ndani ya moyo wake.

SWALI 2: Shalom Naomba unisaidie hapa Sanduku la Agano kwenye Agano jipya, lilikua linawakilisha nini?.
JIBU: Shalom!, Kwa hali ya kawaida tunafahamu sanduku kazi yake huwa ni kuhifadhi vitu Fulani, inaweza ikawa ni fedha,vito,nguo, hazina, miili n.k. na ndio maana tukirudi kwenye biblia tunaona biblia inataja masanduku ya aina mbali mbali, kwa mfano pale Yusufu alipokufa biblia inatuambia mwili wake waliuweka kwenye sanduku (Mwanzo 50:26), hivyo kuna masanduku ya miili. Hali Kadhalika kulikuwa na masanduku ya kuhifadhia sadaka, ambayo yaliitwa masanduku ya sadaka au masanduku ya hazina, mahususi kwa kazi ya sadaka tu!.(Marko 12:41).Vivyo hivyo na masanduku mengine yalikuwepo, ya fedha, ya vito n.k..

Sasa tukirudi kwenye sanduku la agano lililokuwepo Israeli katika agano la kale, mpaka limeitwa sanduku la agano ni wazi kuwa ndani yake lilikuwa limehifadhi maagano Fulani. Na kama ukisoma biblia utaona ndani ya sanduku lile ambalo Musa alipewa maagizo alichonge lilikuwa na vitu vitatu: kimoja ni zile mbao zenye zile amri 10 Mungu alizompa Musa akiwa mlimani, zilizoandikwa kwa kiganja cha Mungu mwenyewe, cha pili ni ile mana, na cha tatu ni ile fimbo ya haruni iliyochipuka.

Na kila mojawapo hapo ilikuwa na maana yake. Musa aliagizwa avitunze vitu hivyo vitatu kwenye sanduku lile liwe kama kumbukumbuku la agano Mungu alilofanya na wana wa Israeli tangu walipotoka Misri mpaka walipoingia katika nchi ya ahadi. Vitu hivyo aliagizwa vikae kwenye sanduku kwa vizazi vyote kama ukumbusho.

Waebrania 9:2 “Maana hema ilitengenezwa, ile ya kwanza, mlimokuwa na kinara cha taa, na meza, na mikate ya Wonyesho; ndipo palipoitwa, Patakatifu.
3 Na nyuma ya pazia la pili, ile hema iitwayo Patakatifu pa patakatifu,
4 yenye chetezo cha dhahabu, na sanduku la agano lililofunikwa kwa dhahabu pande zote, mlimokuwa na kopo la dhahabu lenye ile mana, na ile fimbo ya Haruni iliyochipuka, na vile vibao vya agano;
5 na juu yake makerubi ya utukufu, yakikitia kivuli kiti cha rehema; basi hatuna nafasi sasa ya kueleza habari za vitu hivi kimoja kimoja”.

Fimbo ile ikimaanisha ukombozi wao waliopewa na Mungu kwa njia ya mti ule, Mungu alitumia kipande kile cha mti ule kumwadhibu Farao mpaka kuwaachilia watoke katika utumwa ule mgumu ambao kwa namna ya kawaida ilikuwa haiwezekani wao kutoka (Kwahiyo fimbo ya Haruni ndio ile ile fimbo ya Musa).

Kadhalika amri zile kumi zikufunua sheria zote na maagizo yote Mungu aliowapa wana wa Israeli walipokuwa jangwani kwamba waziendee hizo siku zote za maisha yao.
Na mana, inafunua chakula cha kiroho Mungu alichokuwa anawapa kule jangwani kilichoshuka kutoka mbinguni, ambacho kiliwapa nguvu ya kusonga mbele katika hali zozote walizokuwa wanapitia.

Sasa tukirudi katika agano jipya kama swali lilivyoulizwa Sanduku la agano linawakilisha nini katika agano jipya?. Jibu ni kuwa mambo yote yaliyotendeka katika mwili kwenye agano la kale yalikuwa yanafunua mambo yanayoendelea katika roho kwenye agano jipya sasa. Hivyo sisi sote tunaoishi katika agano jipya, Na sisi pia Mungu aliingia agano na sisi na kutugawia FIMBO, AMRI, na MANA. Na hizo zote akazihifadhi katika sanduku lake moja litembee nasi. Na sanduku hili si lingine zaidi ya BIBLIA neno la Mungu. Fimbo yetu ni msalaba ule ambao kwa huo Mungu aliutumia kumpiga shetani siku ile pale Golgotha, siku ile Bwana aliposema IMEKWISHA! Baada ya damu yake kumwagika Basi siku hiyo ulikuwa mwisho wa kila kitu kwa shetani, Bwana aliyotuweka huru mbali na utumwa na vifungo vya shetani (Farao).

Kadhalika amri zile ni maagizo yote tuyasomayo katika Biblia Bwana aliyotupa,kila siku tuyafuate na Mana na ufunuo wa Roho ambao huo unashuka moja kwa moja kutoka mbinguni kwa Baba kutupa sisi nguvu ya kudumu katika IMANI.

Hivyo vitu hivyo vitatu vinakamilisha agano jipya na vyote hivyo vipo katika sanduku moja nalo ndio BIBLIA TAKATIFU.

Na kama vile mahali popote wana wa Israeli walipoenda sanduku la agano lilifuatana nao kadhalika mtu yeyote aliye mkristo na anakaa mbali na biblia maneno ya Mungu ni wazi kabisa bado hajaingia kwenye hili agano jipya la damu ya Yesu Kristo.

Ubarikiwe!
        

No comments:

Post a Comment