Kuja kwa Bwana duniani kulikuwa kwa kitofauti sana, wakati ambapo Israeli ilimtazamia aje kipindi ambacho uzao wa Daudi unaonekana wazi kwa wafalme waliokuwa wanatawala Yuda zamani za wafalme. Lakini yeye hakutokea hicho kipindi, walipotazamia labda pengine angetokea wakati ambapo wamerudishwa kutoka Babeli lakini hakuonekana hata katika hicho kipindi, wengine walizani utawala wa Umedi hautaisha hata ajapo lakini hakutokea pia ndani ya utawala ule mpaka ulipoisha, Wengine walitazamia labda ingekuwa ni katika utawala wa Uyunani, lakini hata huo nao hakutokea, mpaka ulipoanza utawala mwingine mpya uliojulikana kama Rumi ya kipagani, na ndipo akaja kuzaliwa mwokozi wa ulimwengu Bwana Yesu Kristo, Ni siku ambazo Israeli tayari imeshapoa sana, siku ambazo Israeli tayari imeathiriwa na tamaduni za kigeni za kipagani , siku ambazo Israeli imeshasahau hata kama kuna masihi mkombozi wao anayetakiwa kuja isipokuwa kwa wayahudi wachache tu ndio waliokuwa wanamtazamani, lakini taifa lote lilishalala na ndio maana hata siku ile Mamajusi kutoka mashariki walipoleta taarifa za kuzaliwa mfalme wa wayahudi, biblia inasema habari zile sio tu zilimfadhaisha Herode peke yake bali na Yerusalemu yote pia. Alishuka wakati viwango vya maovu katika Israeli na dunia nzima vipo juu, Bwana alikiita kizazi kile, kizazi cha zinaa na uzinzi , Lakini huo ndio wakati Mungu aliouchagua kumleta mwanae duniani.
Biblia inasema alikuwa kama mche mwororo kwenye nchi kavu, alikuwa kama mzizi mbichi katika nchi kame, siku ambazo watu hawakuwa na habari na Mungu, siku ambazo viongozi wa kidini walikuwa ni wapenda fedha kupindukia, kuliko kumpenda Mungu (Luka 16:14) tofauti na ilivyokuwa hapo zamani, ambapo walawi waliokuwa wanahudumu katika nyumba ya Bwana, hawakujiuhusisha na mambo ya kidunia, bali fungu lao lilitengwa kwa ajili yao, lakini wahudumu wa kipindi cha Yesu, sio tu walikuwa ni wapenda fedha, bali pia walikuwa wafanyaji wa biashara katika sehemu takatifu hekaluni mwa Mungu. alikuja kipindi ambacho unafki umejaa katikati ya viongozi wa kidini (Mathayo 23:13-15), kipindi ambacho viongozi wa kidini wamejaa kutokuwa na kiasi na dhihaka biblia inasema hivyo (Mathayyo 23:25). kipindi ambacho watu wote wenye haki na manabii pindi walipojaribu kusema ukweli walikuwa wanapigwa hadharani kwenye masinagogi yao na kuuliwa na hao hao viongozi wa kidini. Na tunaona ndivyo walivyokuja kufanya hata kwa Bwana(Mathayo 23:33).
Lakini huo ndio uliokuwa wakati wa Mungu aliouchagua kuleta wokovu duniani. Bwana Yesu Alikuwa kama jani bichi jangwani, alikuwa kama mizizi mibichi kwenye ardhi ya ukame, alikuja wakati usiostahili wa yeye kuja, kipindi ambacho Israeli haijawahi kuona nabii kwa muda wa miaka 300 kwa maana nabii wa mwisho alikuwa ni Malaki...Kipindi ambacho watu wa mataifa wanalimiliki taifa la Israeli, wakiamrishwa kana kwamba wapo nchi ya ugenini. Kipindi ambacho kila mtu anajiamulia mambo yake. Lakini ndio wakati wa Masihi kutokea, kutengeneza tena upya mambo yote.
Isaya 53: 1 "Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?2 Maana alikua mbele zake kama MCHE MWORORO, NA KAMA MZIZI KATIKA NCHI KAVU; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.3 Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.4 Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.5 Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, NA KWA KUPIGWA KWAKE SISI TUMEPONA".
Maandiko yanasema ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta?. Inaamanisha kuwa kuzaliwa kwa Kristo duniani lilikuwa ni jambo lisilosadika kwa yeyote Yule aliyelisikia, eti katikati ya ouvu atokee masihi?..afadhali ingekuwa wakati wa kipindi cha waamuzi au kipindi cha wafalme wa Israeli. Lakini sio kwa wakati ule aliokuja..
Hivyo pamoja na ukame wote huo wa kiroho uliokuwa Israeli kwa wakati ule. Hapo ndipo Kristo alipotokea, Hapo ndipo wale wenye nguvu wachache ambao hawakukata tamaa walitambuka kuja kwa Kristo, walisadiki habari za kuja kwake, Mkono wa Mungu ulifunuliwa kwao..Mfano wa hao kwenye biblia tunamwona HANA, mwanamke aliyekuwa amejitoka kikamilifu kwa Mungu, Licha ya kufiwa na mume wake katika siku za ujana wake, lakini hakuona sababu ya kwenda kuolewa tena bali alichagua kudumu hekaluni usiku na mchana akimwomba Mungu, auharakishe wokovu aliowaahidia wayahudi tangu zamani, wakati wayahudi wengine wameshakata tamaa na kuendelea na mambo yao, na kusahau kitu kinachoitwa mwokozi duniani, lakini Hana hakuwa hivyo yeye alidumu hekuluni kwa miaka 84. usiku na mchana akimtafakari Mungu na wokovu uliokuwa unatarajiwa Israeli tangu zamani. Mpaka siku moja wakati Yesu anaenda kuwekwa wakfu Hekaluni na wazazi wake ndipo Mungu akamwonyesha huyu ndiye aliyekuwa anamtazamia...
Kadhalika alikuwepo mzee mwingine naye vivyo hivyo alikuwa anatazamia faraja ya Israeli yaani kuja kwa mwokozi kwa muda mrefu, mpaka ikafikia wakati Mungu akamshuhudia kwamba hatakufa mpaka atakapomwona mwokozi duniani.
Habari hizo tunazisoma katika Luka 2:25-38
"25 Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake.26 Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana.27 Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria,28 yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema,29 Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema;30 Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako,31 Uliouweka tayari machoni pa watu wote;32 Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.33 Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake.34 Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa.35 Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.36 Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake.37 Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba.38 Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, NA WOTE WALIOKUWA WAKIUTARAJIA UKOMBOZI KATIKA YERUSALEMU AKAWATOLEA HABARI ZAKE".
Embu leo hii jaribu kufikiria ungekuwa na wewe upo katika kipindi kile je! Ungeweza kutambua kuzaliwa kwa Bwana duniani? Je! Hata ungehadhithiwa ungeweza kusadiki habari hizo?, kati ya mamilioni waliokuwa Yerusalemu ni watu wachache sana walioweza kufunuliwa tukio hilo la kuja kwa mwokozi duniani. Alikuja kama MWIVI, hakuja kwa kujionyesha onyesha, au kwa kupigwa parapanda angani ili dunia nzima itazame, bali alikuja kama mwivi. Alizaliwa zizini.
Na ndivyo itakavyokuwa kuja kwake mara ya pili. Kama ilivyokuwa katika kuja mara ya kwanza, wakati ambao watu wameshakata tamaa ya kuja Masihi duniani ndipo alipokuja na kujifunua kwa wale wachache ambao hawakuzimia mioyo yao katika kumsubiria mfano wa ANA na SIMEONI. Wakati ambao unafki mwingi na upendaji fedha umekithiri katika kanisa la Kristo na kwa watu wanaojiita watumishi wake,kama ilivyokuwa kipindi kile, ndipo Kristo atakaposhuka. Wakati ambapo manabii wengi wa uongo wamezagaa kila mahali na wale wa ukweli wanatengwa na kanisa ndipo Kristo anaposhuka .
Hivyo ndugu mambo tunayoyaona sasahivi ni dalili madhubuti inayotutambulisha kuwa tunaishi katika majira ya kuja kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Siku hiyo itakapofika siku ile ya UNYAKUO, dunia haitajua chochote, wakristo vuguvugu wanaodai wanamngojea Bwana na huku mguu mmoja upo nje, mambo ya kidunia yakiwasonga siku hiyo hawatajua chochote, bali atakuja kwa watu wachache sana, mfano wa Ana na Simeoni watu waliojazwa Roho Mtakatifu, watu ambao usiku na mchana wanautazamia wokovu na macho yao yapo mbinguni siku zote ndio watakajua, watu ambao ni wacha Mungu kama Simeoni, watu ambao wanadumu madhabahuni pa Mungu, hawataki kutoka katika mstari wa Neno ndio watakaojua lakini wengine wote watabaki wakisubiria hukumu ya Mungu mwenyezi.
Bwana atatokea kwao kama mche mwororo, kama jani bichi katika dunia chafu, katika jamii ya watu wenye dhihaka wanaosema huyo Yesu mnayengojea kwa miaka 2000 sasa yuko wapi, tulidhani angekuja wakati wa mitume hakutokea, tulidhani angekuja wakati wa kipindi cha matengenezo ya kanisa mbona hakutokea, wakati wa kipindi cha upentekoste hakutokea mpaka millennium mpya imeanza hajaja bado, huyo sio wa kuja leo wala kesho. Nyie mnapoteza mida yenu, badala ya kufikiria mambo ya muhimu mnawaza juu ya kuja kwa YESU hichi ni kizazi kipya...
Unaona? Hao watu wa kudhihaki biblia inasema watatokea katika siku za mwisho. Lakini wewe kaka/dada, unayemngojea Bwana sasa. Usikatishwe tamaa, siku ya wokovu wetu ipo karibu kushinda hata sisi tunavyodhani. Usiache kumtazama Kristo, majira haya dunia inayoona kuwa hakuna uwezekano wa kuja kwa Bwana, lakini ndio haya haya atakayokujia kama mwivi. Ndio haya Mungu aliyoyachagua. Siku yoyote hatutakuwepo hapa duniani.
Ni matumaini yangu utaufanya uteule wako na wito wako imara sasa kabla siku ile haijafika.
Amen.
Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine. Na Mungu akubariki!
This comment has been removed by a blog administrator.
ReplyDelete