"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, December 15, 2018

NADHIRI.


Kumbukumbu 23: 21 “Utakapoweka nadhiri kwa Bwana, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako; nayo hivi itakuwa dhambi kwako.
22 Lakini ukijizuia usiweke nadhiri, haitakuwa dhambi kwako.
23 Yaliyotoka midomoni mwako yashike kuyafanya; kwa mfano wa ulivyomwekea nadhiri Bwana, Mungu wako, ni sadaka ya hiari uliyoahidi kwa kinywa chako”.

Nadhiri, ni kitu chochote unachoweza kukiahidi kumtolea Mungu kwa ihari yako mwenyewe. Na kitu hicho kinaweza kuwa sadaka mfano mali, fedha, shamba n.k..Lakini pia nadhiri ni ahadi mtu anayoweza kuiahidi ya maisha Fulani mbele za Bwana mfano mtu anaweza akaahidi mbele za Bwana kumtumikia yeye endapo atafanyiwa kitu Fulani na Mungu..Mfano tunamwona Yakobo wa kwenye maandiko.. wakati ambapo anamkimbia Esau Ndugu yake kwasababu aliuchukua mbaraka wake maana Esau alimkasirikia kwa hilo…Hivyo ikamlazimu Yakobo aende nchi ya mbali katika ukoo wa baba yake na mama yake huku akiwa mikono mitupu hana kitu kabisa… Na wakati akiwa njiani akamwekea Mungu nadhiri kwamba endapo Mungu atamlinda njia aiendayo na kumfanikisha katika chakula na mavazi ndipo Yehova atakuwa Mungu wake na atamtolea yeye fungu la kumi la kwa kila alichopewa.. Tunasoma hayo katika..
Mwanzo 28: 18 “Yakobo akaondoka asubuhi na mapema, akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake.
19 Akaita jina la mahali pale Betheli; lakini jina la mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu.
20 Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae;
21 nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu. 22 Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi”.
Na tunaona baada ya kumwekea Mungu hiyo nadhiri, Bwana Mungu kweli alimfanikisha Yakobo alimpa utajiri mwingi katika mifugo na mali na wakati anamrudia ndugu yake Esau kutoka kwa Labani mjomba yake, aliikuwa amepata mali nyingi sana na utajiri , na ndipo Yakobo akaitoa nadhiri ile, akamtumikia Mungu siku zake zote na kumtolea fungu la kumi.

Mwanzo 31: 13 “Mimi ni Mungu wa Betheli, huko ulikotia mafuta nguzo, na kuniwekea nadhiri. Sasa ondoka, toka katika nchi hii, urudi mpaka nchi ile uliyozaliwa”.

Kwahiyo hiyo ni moja wapo ya nadhiri, nadhiri ya kumtumikia Mungu, endapo atakufanyia kitu Fulani. Na kama tunavyoona hapo Mungu anakumbuka kila nadhiri mtu anayoiweka mbele zake, alikumbuka ya Yakobo siku aliyomwekea na mahali alipomwekea..hivyo anamkumbusha.

Kuna usemi unaosema kwamba AHADI ni DENI, lakini NADHIRI ni ZAIDI YA DENI..ni kifungo, biblia inatuonya kabla hatujaweka nadhiri, tujitafakari kwanza mara mbili mbili mbele za Mungu kabla ya kuchukua uamuzi huo.. Inasema

Hesabu 30: 1 “Kisha Musa akanena na wale vichwa vya kabila za wana wa Israeli, na kuwaambia, Neno hili ndilo aliloliagiza Bwana.
2 Mtu atakapomwekea Bwana NADHIRI, au, atakapoapa kiapo ili kufunga nafsi yake kwa kifungo, asilitangue neno lake; atafanya sawasawa na hayo yote yamtokayo kinywani mwake”.
Na pia inarudia kusema kitu hicho hicho katika kitabu cha…
 
Mhubiri 5:4 “Wewe ukimwekea Mungu NADHIRI, usikawie kuiondoa; KWA KUWA YEYE HAWI RADHI NA WAPUMBAVU; basi, uiondoe hiyo uliyoiweka nadhiri.
5 Ni afadhali usiweke nadhiri, Kuliko kuiweka usiiondoe”.

Mistari yote hiyo inaonyesha jinsi gani Mungu anafuatiliza kila Neno linalotoka katika kinywa cha mtu, Neno lolote linalotoka vinywani mwetu mbele za Bwana.

Kitu kimoja wengi wasichojua ni kwamba, NDOA NI NADHIRI. Na kwanini Mungu anachukia kuachana sio kwasababu tu Mungu anachukia uasherati! Hapana zaidi ya hilo anachukia sana mtu anapoivunja nadhiri aliyoitoa kwa kinywa chake. Wakati wa ndoa kufungwa mtu anaahidi mbele za Mungu kuishi kwa upendo, na mwenzake na kwa uvumilivu, kutoachana katika hali yoyote ile watakayoipitia katika maisha, aidha katika umaskini au katika utajiri, katika uzima au ulemavu, katika huzuni au furaha n.k..Na wanaahidi kuwa Kifo ndicho kitakachowatenganisha…

Sasa kwa wanandoa kama hawa pasipo kufikiri wanaweza wakadhani kuwa wameahidiana wao hizo ahadi, kumbe hawajui na nadhiri wamemwekea Mungu..kwasababu wamekwenda kuziweka mbele zake..Na endapo ikitokea wameachana kwasababu yoyote mojawapo ya hizo hapo juu, Biblia inasema “Bwana hawi radhi na wapumbavu”..inasema ni afadhali mtu kutokuiweka kabisa kuliko kuiweka asiiondoe..Hicho ni kifungo cha maisha.

Kumuacha mke wako au mume wako kwasababu tu amekuwa maskini, au mlemavu…ni tiketi kamili ya kwenda katika lile ziwa la moto hakuna msamaha juu ya hiyo dhambi, ukimwacha mume wako au mke wako kwasababu tu mmegombana siku moja au kwasababu amekuwa mnene, au kwasababu amekuwa mzee au havutii tena..hakuna neema juu ya hilo, suluhisho pekee ni kumrudia tu!!.

Bwana anasema katika Hesabu 30:2 “ Mtu atakapomwekea Bwana NADHIRI, au, ATAKAPOAPA KIAPO ILI KUFUNGA NAFSI YAKE KWA KIFUNGO, ASILITANGUE NENO LAKE; ATAFANYA SAWASAWA NA HAYO YOTE YAMTOKAYO KINYWANI MWAKE”.

Hii ina maana kuwa kabla ya kuamua kuoa, au kuolewa..yatafakari hayo yote kwanza na upige gharama kabisa..endapo ikitokea atakayekuja kuwa mume wako/ mke wako kafilisika utaendelea kumpenda na kuishi naye…endapo ikatokea kawa mlemavu utaendelea kumheshimu na kumpenda,..endapo mmegombana utakuwa tayari kumsamehe n.k, utakuwa tayari kumtunza kama mwili wako mwenyewe?? Kama hayo yatakushinda ni afadhali USIWEKE HIYO NADHIRI KABISA. Ni afadhali usioe wala kuolewa kabisa.

Mhubiri mmoja wa kimarekani anaitwa William Branham, wakati Fulani Alienda kumwombea mtu mmoja aliyekuwa anaumwa sana karibia na kufa…na kwasababu Bwana amemkirimia karama ya kinabii, wakati akiwa katika hatua ya kumwekea mikono Yule mgonjwa ili amwombee…Ono likamjia kutoka kwa Mungu, akamwona Yule mtu akiwa katika hali ya Kuzama maji, na wakati akiwa katika kuzama…akamlilia Mungu amwokoe asife maji, akiwa katika ile hali akamwekea Mungu nadhiri na kumwambia endapo, atamwokoa na MAUTI ILE YA KUZAMA MAJI basi atamtumikia yeye siku zote za maisha yake..na Bwana akamsikia akamwokoa na mauti ile ya kufa maji..Lakini Yule mtu alipotoka pale akaisahau ile nadhiri aliyomwekea Mungu..akaendelea na maisha yake ya kawaida…Na Bwana akamwambia katika ono ndugu William Branham kwamba huyo mtu hatapona ugonjwa uliompata bali atakufa..kwasababu alimwekea Mungu nadhiri na hakuitimiza…Na alipomwambia Yule mtu, mambo hayo Bwana aliyomwonyesha Yule akakiri ni kweli alimwekea Mungu nadhiri wakati anakaribia kuzama maji..Lakini alilolisema Bwana amelisema, baada ya siku kadhaa Yule mtu alifariki.

Ipo mifano kadha kadha katika maandiko, ambayo watu walifanya mchezo na nadhiri, Mmojawapo wa watu hao tunamwona ni Anania na Safira mkewe. Hawa wakiwa katika vyumba vyao vya siri waliahidi kuuza shamba lao na kiasi chote cha fedha kitakachopatikana basi watakipeleka madhabahuni kwa Bwana…ndivyo walivyoahidi mbele za Bwana na Bwana akasikia, akawajalia kufanikisha haja ya mioyo yao, lakini walipoona Bwana amewafanikisha na wameuza lile shamba kwa kiwango kizuri walichokitarajia tamaa ikawaingia wakasahau kuwa walimwahidi Mungu kiasi chote, lakini wao wakaficha sehemu ya fedha, na kumpelekea Mungu kiasi kidogo…Biblia inasema kwa kosa hilo hawakudanganyana wao bali walimdanganya Mungu mwenyewe na walikufa wote wawili ndani ya siku moja.
 Matendo ya Mitume 5 : 1-42
“1 Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali,
2 akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume.
3 Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja?
4 Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu.
5 Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya.
6 Vijana wakaondoka, wakamtia katika sanda, wakamchukua nje, wakamzika.
7 Hata muda wa saa tatu baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea.
8 Petro akamjibu, Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema, Ndiyo, kwa thamani hiyo.
9 Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe.
10 Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana wakaingia wakamkuta amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe.
11 Hofu nyingi ikawapata kanisa lote na watu wote walioyasikia haya”.
Ndio maana Zamani katika agano la kale, Bwana aliwakataza kabisa watu waliomwekea Mungu nadhiri, wasinywe mvinyo wa aina yoyote, wala divai,wala hata mzao wa mzabibu usifike vinywani mwao, unajua ni kwasababu gani?..Ni kwasababu mtu aliyemwekea Mungu nadhiri kila wakati anapaswa awe katika akili yake timamu, ili asiisahau ile nadhiri aliyomwekea Mungu…Mvinyo unamfanya mtu ajisahau, unamfanya mtu atoke katika akili yake ya kawaida.. Na pia Bwana alitoa maagizo mtu yoyote aliyejiweka kuwa mnadhiri wa Bwana asikate nywele zake sharti ataziacha ziwe ndefu mpaka siku atakapoitimiza nadhiri yake? Unajua ni kwasababu gani?..Ni kwasababu kila atakapoziona nywele zake kichwani nyingi akumbuke kuwa alimwekea Mungu nadhiri, inakuwa ni kama kitu cha kumkumbusha kuwa ana deni sehemu Fulani katika maisha yake. Ndio maana Samsoni alionywa asikate nywele zake,wala wazazi wake wakati wa ujauzito wake alionywa asinywe divai. Kwasababu yeye alikuwa ni mnadhiri wa Bwana biblia inasema hivyo.

Hesabu 6: 1 “Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Nena na watu wa Israeli, uwaambie, Mtu mume au mtu mke atakapoweka nadhiri kubwa, nadhiri ya Mnadhiri, ili ajiweke wakfu kwa Bwana;
3 ATAJITENGA NA DIVAI NA VILEO; hatakunywa siki ya divai, wala siki ya kileo, wala asinywe maji yo yote ya zabibu, wala asile zabibu, mbichi wala zilizokauka.
4 Siku zote za kujitenga kwake asile kitu cho chote kilichoandaliwa kwa mzabibu, tangu kokwa hata maganda.
5 Siku zote za nadhiri yake ya kujitenga, wembe usimfikilie kichwani mwake; hata hizo siku zitakapotimia, ambazo alijiweka wakfu kwa Bwana, atakuwa mtakatifu, ataziacha nywele za kichwani mwake zikue ziwe ndefu”.

Ni hatari sana kuweka nadhiri na kutoitimiza..Katika maandiko matakatifu nyakati za Waamuzi kulikuwa na mwamuzi mmoja anayeitwa YEFTHA, huyu alimwekea Mungu nadhiri kwamba endapo ataenda vitani na kushinda, basi Yule atakayetokea wa kwanza mbele yake kumpokea basi atamfanya sadaka ya kuteketezwa, lakini kwa bahati mbaya alitegemea kije kitu kingine, pengine ng’ombe zake lakini alikuja binti wake wa pekee na alikuwa hana mwingine…lakini kwasababu anajua madhara ya kuahidi nadhiri na kutoitimiliza, akamteketeza binti wake kwa moto, ili kuiondoa ile nadhiri, na Mungu hakumhesabia makosa.

Waamuzi 11: 29 “Ndipo roho ya Bwana ikamjilia juu yake Yeftha, naye akapita katika Gileadi na Manase, akapita na katika Mispa ya Gileadi, na kutoka hapo Mispa ya Gileadi akapita kuwaendea wana wa Amoni.
30 Naye Yeftha akamwekea Bwana nadhiri, akasema, Kwamba wewe utawatia wana wa Amoni mkononi mwangu kweli,
31 ndipo itakuwa ya kwamba, kile kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na amani kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha Bwana, nami nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa.
32 Basi Yeftha akavuka kuwaendea wana wa Amoni ili kupigana nao; naye Bwana akawaua mkononi mwake.
33 Akawapiga kutoka Aroeri hata kufikilia Minithi, miji ishirini, na mpaka Abel-keramimu, akawapiga kwa machinjo makuu mno. Basi hivyo wana wa Amoni walishindwa mbele ya wana wa Israeli.
34 Kisha Yeftha akafika Mispa nyumbani kwake, na tazama, binti yake akamtokea kumlaki, na matari na machezo; naye alikuwa ni mwanawe pekee; hakuwa na mwingine, mwana wala binti, ila yeye.
35 Ikawa alipomwona akayararua mavazi yake, akasema, Ole wangu! Mwanangu, umenitweza sana, nawe u mmoja miongoni mwahao wanisumbuao; KWA KUWA MIMI NIMEMFUNULIA BWANA KINYWA CHANGU, NAMI SIWEZI KUREJEA NYUMA”.
Kumbuka Bwana hajawahi kuagiza watu wamtolee yeye sadaka ya kuteketezwa, na yeyote afanyaye hayo alikuwa anakwenda kinyume na maagizo yake, lakini kwasababu ya NADHIRI Bwana hakumhesabia YEFTHA makosa. Na Yefha alitambua kabisa endapo asingetimiza maneno aliyoyazungumza kwa kinywa chake basi yangeweza kumtokea mambo mabaya sana..mfano wa Anania na Safira.

Ndugu unayesoma haya, ulimwahidi Mungu nini alipokuponya? Ulimwahidi Mungu nini alipokufanikisha katika mambo yako? Ulimwahidi nini siku alipokuokoa?...Ulimwekea Nadhiri gani, kama ipo je! Unaikumbuka bado? Au umeisahau? Kama wewe umeisahau kumbuka Mungu hajaisahau?..uliahidi kumtolea fungu la kumi je unafanya hivyo?..uliahidi kutoa kitu Fulani kwa ajili yake..je! ulifanya hivyo?? Uliahidi endapo akikuponya, au akikufanikisha, au akikufaulisha au akikufikisha salama utamtumikia? Je! Umefanya hivyo?..Wakati mwingine upo katika hatari nyingi na unapitia mambo magumu ni kwasababu uliweka nadhiri na haukuitoa.

Bwana akujalie kuyaona hayo!. Ili uukwepe mkono wa Mungu.
 
Tafadhali “share” kwa wengine na Bwana akubariki.

No comments:

Post a Comment