"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Sunday, January 20, 2019

KAENI NDANI YANGU NAMI NDANI YENU.

Shalom mwana wa Mungu, karibu tujifunze Neno la Mungu, ambapo leo tutajifunza kwa ufupi juu ya somo lenye kichwa kinachosema “KAENI NDANI YANGU NAMI NDANI YENU”..Maneno hayo aliyazungumza Bwana Yesu, alipokuwa anazungumza na Wayahudi wakati Fulani kabla ya kusulibiwa kwake, Aliwaambia
Yohana 6: 53 “Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.
54 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.
55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.
56 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu YANGU HUKAA NDANI YANGU, NAMI HUKAA NDANI YAKE”.
Sehemu nyingine pia alisema.. Yohana 15:4 “ KAENI NDANI YANGU, NAMI NDANI YENU. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu”

Sentensi hiyo ni ngumu kidogo kuilewa, lakini hebu tutafakari mfano huu tunaweza tukauelewa zaidi..

Mfano mtu achukue ndoo na aijaze maji hadi juu na kisha achukue glasi aiweke ndani ya ile ndoo, unadhani kitu gani kitatokea hapo?..Ni wazi kuwa ile glasi itajaa maji ikiwa ndani ya ile ndoo…hivyo kwa ufupi tunaweza kufupisha na kusema.. “glasi ipo ndani ya maji na maji yapo ndani ya glasi” Ili kuifikia glasi lazima uyakute maji, na ndani ya glasi pia kuna maji.

Na kwa Mungu ndio hivyo hivyo, “aliposema kaeni ndani yangu nami ndani yenu” alimaanisha kuwa Munguatakuwa nje yetu, kutuzunguka pande zote na pia atakuwa ndani yetu kutulinda na kutuhudumia. Kwahiyo hakuna mashambulizi yoyote yanaweza kutokea nje ya miili wala hakuna mashambulizi yoyote yanayoweza kutokea ndani ya roho. Kwa mtu aliyejiunganisha na Mungu kwa namna hiyo, Kitakachokuwa kinaendelea nje ndicho kitakachokuwa kinaendelea ndani. Hakuna tofauti.

Hakuna kiumbe chochote kilichopo kinachoweza kutoa huduma kama hiyo, hakuna! Kiumbe chochote hata shetani kinachoweza kukupa uhakika wa mwilini na rohoni,..shetani atakupa furaha ya utajiri lakini hatakupa furaha ya rohoni, atakupa utajiri wa nje lakini hatakupa utajiri wa ndani. Mwanadamu atakupa tumaini la ulinzi wa nje lakini hatakupa tumaini la ulinzi wa roho yako, mali zitakupa ulinzi wa nje, lakini hazijuli lolote kuhusu roho yako, ikiwa kuna wachawi au majeshi ya mapepo yanakuvamia mali haziingilii kati.

Daktrari atakutibu mwili lakini hataweza kutibu roho iliyovunjika na kukata tamaa, atatibu majeraha ya nje lakini hatatibu majeraha ya ndani, watatibu mifupa iliyopondeka lakini hawataweza kutibu moyo uliopondeka. Wanadamu watakuondolea hofu ya nje kwa muda, lakini hawatakuondolea hofu ya kifo na magonjwa. Wanadamu watakata kiu na njaa ya miili yetu, lakini hawatakata njaa au kiu ya kutaka kuishi milele.

Yupo mmoja tu! Ambaye ni mtaalamu wa mambo yote ya rohoni..aliyetiwa mafuta na Mungu mwenyewe ambaye anaweza kushughulika na mambo ya rohoni yaliyokosewa ufumbuzi, ambaye anaweza kutegua vitendawili vigumu vya moyo, ambaye anaingia ndani ya mtu, na kumtengeneza na kutatua matatizo yake yote yaliyomo ndani yake, anapenya hata kutenganisha nafsi na roho, na mafuta yaliyoko ndani yake, ni mwepesi wa kutambua fikra za mtu na matamanio ya mtu hata kabla mtu huyo hajayawaza.. Yeye mwenyewe anasema maneno haya..
Isaya 61: 1 “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.
2 Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao;
3 kuwaagizia hao waliao katika Sayuni, wapewe taji ya maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito; wapate kuitwa miti ya haki, iliyopandwa na Bwana, ili atukuzwe”
Huyo ni YESU KRISTO PEKE YAKE na wala hakuna mwingine. Asifiwi kwa ushabiki wa kidini kama wengine wanavyodani lakini hiyo ndio sifa yake, sio tu Mungu kamuhakiki hata wanadamu sisi wenyewe tumemwakiki na kujua kweli hakuna mwingine kama yeye,na hakuna jambo lolote linalomshinda ndivyo alivyo. 

Dada/Kaka unayesoma ujumbe huu, habari za Yesu Kristo hazitaachwa kutangazwa popote pale, Roho Mtakatifu anatenda kazi kila siku na kila mahali, kama hutasikia hapa utasikia pale habari za Yesu Kristo,

Kwa faida yako na yangu alijitoa kwa ajili yetu, ili sisi tupate msamaha wa dhambi na tupate mema yote ya nchi, hivyo anakuita leo kwa mara nyingine.Una masononeko, suluhisho sio daktari wala sio mimi, una uchungu, una dhambi, una hofu, una shida, una huzuni,una mashaka, umekata tamaa ya kuishi, unahofu ya kukataliwa, Nataka nikuambie Wanadamu wala shetani bado hatujaifikia hiyo sayansi yakutibu hayo mambo magumu ya rohoni, hakuna daktari wala mganga awezaye kutibu hayo mambo na hivyo hata ukienda kwao hawatakusaidia..

Dawa ya hayo mambo Ni YESU KRISTO KUINGIA NDANI YAKO..Basiiii!!!! Huyo ndiye atakayeondoa shida ulizonazo, huzuni, hofu, mashaka, mateso na mambo mengine yote. Mimi nilikuwa na mashaka mengi, mpaka ikafikia wakati nikajua kuwa nini dhambi ya kutokuwamehewa, na hivyo sifai tena.Lakini Kristo aliniponya na ndio maana leo hii nakuandikia ujumbe huu Ni Yesu peke yake ndiye atakayeikata kiu yako.

Unasubiri nini usimpe leo Kristo maisha yako?...anabisha mlangoni leo, mlangoni mwa moyo wako,.Unachopaswa kufanya ni kumfungulia aingie akugange moyo, na yeye akiingia ndani yako haishii kukaa ndani yako anakuzingira pia nje yake..kama glasi iliyoko ndani ya ndoo ya maji.

Ukiwa unatamani kufanya hivyo, hapo hapo ulipo yupo, anza kutafakari maisha yako ya nyuma..maisha uliyoyapitia, dhambi ulizozifanya, shida ulizozipitia, magonjwa, huzuni uliyonayo, hofu uliyonayo, mashaka uliyonayo, na kila kitu ambacho huwezi hata kumweleza mtu. Nyenyekea chini yake na mwelezee, na mwambie akusamehe na kukusafisha, mwambie akutue mizigo ya dhambi na yeye ni mwaminifu atakusaidia.
   

Hauhitaji kwenda kwa mchungaji, au kwa mtumishi hapo hapo ulipo anakusikia atakusamehe. Na baada ya kufanya hivyo fanya hima ukabatizwe..hayo ni maagizo aliyoyatoa Bwana Yesu kwa ajili ya ondoleo la dhambi, kama tu daktari anapokupa maagizo ya kuweka dawa kwenye maji na kuyaogea ili ugonjwa wako wa ngozi uondoke wote, huwezi kwenda kuweka kwenye glasi na kujipaka, utakuwa umevunja masharti na pengine ugonjwa wako unaweza usipone ..na Yesu alitupa maagizo ya kuondolewa dhambi ambao ndio ugonjwa wa pekee wa roho zetu, na hayo maagizo ni kwenda kubatizwa katika maji mengi kwa jina la Yesu Kristo, ili dhambi zetu ziondolewe kulingana na (matendo 2:38). Na kisha baada ya hapo Bwana atafanya yaliyosalia, atahakikisha anakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi, na kukutia katika kuielewa kweli yote ya maandiko..

Hapo utakuwa umezaliwa mara ya pili, na kuingizwa katika ukuhani wa kifalme, watu wa milki ya Mungu, uzao mteule utakaourithi uzima wa Milele, Na Kristo atakuwa yupo ndani yako na nawewe utakuwa ndani yake, na hivyo lolote utakaloomba utapewa kwasababu wewe tayari ni mmoja wa familia halali ya Mungu, unayejulikana Mbinguni. Atakufariji kwa faraja zote alizokuahidia kwenye Neno lake. Kama Bwan Yesu alivyosema katika.
Yohana 15.7 “Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.
8 Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu”

Yohana 14:20 “Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu”.

Bwana akubariki.

No comments:

Post a Comment