Pale tu mtu anapogeuka na kuacha maisha yake ya dhambi, na kukusudia kutoka rohoni kumfuata Kristo siku zote za maisha yake, kisha akabatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kama biblia iagizwavyo kwa ajili ya ondoleo la dhambi zake (Matendo 2:38), basi kuanzia huo wakati na kuendelea Mungu humpa kipawa cha Roho Mtakatifu, kama msaidizi na kumwongoza katika kuijua kweli yote. Na zaidi ya hayo mtu huyo hupewa zawadi nyingine nayo ni kuhudumiwa na malaika watakatifu wa Bwana, anakuwa anatembea na malaika wa Bwana.
Waebrania 1:14 “Je! Hao wote [malaika] si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?”
Sasa malaika hawa hutumwa kuhakikisha usalama wa huyu mtu kwa kila namna, kuhakikisha uzima wa huyu mtu, kuhakikisha mapenzi yote ya Mungu yanatendekea kwa huyu mtu bila ya kuongezwa au kupunguzwa. Ikiwa Mungu amependa mwanawe kwa kipindi fulani apitie katika bonde la uvuli wa mauti kwa muda, lakini asidhuriwe wala asife, basi malaika hawa wanaotembea naye ndio watakao hakikisha kuwa hadhuriki kwa namna yoyote ile katika majaribu yoyote atakayokumbana nayo, anaweza kukutana na hatari hata ya kufa lakini wengine wote wanaweza wakafa yeye akabaki mzima. Sasa hii kazi inafanywa na hawa malaika watakatifu wa Mungu.
Tunamwona mfano Daudi, ulifika wakati Mungu aliruhusu, awindwe na maadui zake, mpaka wakati mwingine anaona hakuna mlango wa kumkwepa Sauli, lakini mara zote hizo alizokuwa katika shida na hatari za kufa hakuwahi kudhuriwa na lolote.
Kadhalika Ikiwa ni mapenzi ya Mungu kumbariki mwanawe na kumfanikisha katika jambo aliloikusudia au aliloombwa na mwanawe kwa wakati huo basi wale malaika watahakikisha njia zote za mafanikio zinamfikia yule mtu kwa wakati husika, watatengeneza mifereji yote ya mafanikio ili tu kufanikisha lile kusudi waliloitiwa kulifanya, ambalo ni kuwahudumia watakatifu. Hivyo tunaona faida ni nyingi sana kwa mtu yule aliyezaliwa mara ya pili na kumfanya Mungu kuwa tegemeo lake.
Na ndio maana Mungu anaitwa BWANA WA MAJESHI,.Analo jeshi kubwa sana la malaika wa kila namna, na wote hao ni kwa kusudi la kuwahudumia tu watakatifu. Lakini kama hujawa mtakatifu kwa kuzaliwa mara ya pili basi ni kinyume chake, ufalme mwingine utakuwa unakuongoza na huo si mwingine zaidi ya ufalme wa giza, na kundi la roho chafu litakuwa ndio limekuzunguza muda wote, hilo ndilo linalolokuhudumia wewe, ili kukupa nguvu ya kuendelea kutamani mabaya, kuendelea kuzini, kuendelea kukupa kiu ya pombe na sigara, kutazama pornography, kufanya mustabation, kuendelea kuwa shoga, kuendelea na usagaji,kuendelea kula, kuendelea kuiba, kutukana,kula rushwa..n.k.. Unaweza ukawa unatamani kuacha hayo mambo lakini huwezi kwa nguvu zako kwasababu ufalme wenye nguvu zaidi yako upo juu yako na MKUU WA ANGA hili amekufanya kuwa mfu kwa habari ya mambo mema..
Waefeso 2: 1 “Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu;2 ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata MFALME WA UWEZO WA ANGA, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;3 ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine.”
Lakini leo tutaona malaika watakatifu jinsi wanavyotenda kazi kwa wale watu wanaojiona kuwa ni wakristo lakini ni vuguvugu, wale ambao Mungu alishawakomboa, wale ambao wameshaonja vipawa vyote vya Mungu lakini bado hawataki kusimama imara, wale ambao wameshadumu katika imani kwa muda mrefu lakini ukitazama maisha yao ni mguu mmoja ndani, mguu mmoja nje, leo wapo kwa Mungu kesho wapo kwa shetani, ni mkristo anaye itangaza injili kwa njia ya uimbaji lakini ni mwasherati, kwa siri na anakunywa pombe, na huyo huyo bado anashiriki meza ya Bwana na kutawadhana miguu, anahudhuria ibadani, anajisitiri lakini kwasiri ni mtukanaji na anakwenda kwa waganga wa kienyeji. Yani kwa ufupi mtu ambaye ni vuguvugu.
Sasa kumbuka watu wa namna hiyo mwanzoni walianza vizuri, na kwa jinsi Mungu alivyomwaminifu wa ahadi zake, siku ile walipokata shauri kuokoka Bwana alilituma jeshi la malaika zake watakatifu watembee nao. Hivyo siku zile za kwanza ukiwauliza wokovu kwako ulikuwaje watasema nilikuwa namwona Mungu sana katika maisha yangu akinipigania. Ni kweli ni lazima uone hivyo kwasababu jeshi la Mungu aliye mkuu sana linatembea na wewe. Lakini baadaye kidogo alipoanza kukengeuka kumchanganya Mungu na dunia, mguu mmoja huku na mwingine kule ndipo hali yake ikaanza kuwa mbaya sana, anaona hasongi tena mbele kwa habari ya wokovu, anaenda mbele anarudi nyuma, magonjwa sasa yanamwandama, taabu na masumbufu asiyoelewa chanzo chake ni nini!. Hajui kuwa ni wale wale malaika watakatifu ambao walitumwa na Bwana kumuhudimia wamegeuka sasa na kuwa KUNDI LA MALAIKA WALETAO MABAYA.
Wana wa Israeli walipokuwa Misri Mungu aliwatumia malaika zake, kuwapigania, unaona yale mapigo yote yaliyokuwa yanatokea Misri, maji kuwa damu, nzige, giza, mvua ya mawe, pigo la mzaliwa wa kwanza n.k. Ilikuwa ni kazi ya malaika waliotumwa kutekeleza maagizo ya Mungu kwa ajili ya kuwakomboa watoto wake.
Zaburi 78: 45 “Aliwapelekea mainzi wakawala, Na vyura wakawaharibu.46 Akawapa tunutu mazao yao, Na nzige kazi yao.47 Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, Na mikuyu yao kwa mawe ya barafu.48 Akaacha ng'ombe zao wapigwe kwa mvua ya mawe, Na makundi yao kwa umeme.49 Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, KUNDI LA MALAIKA WALETAO MABAYA.50 Akiifanyizia njia hasira yake; Wala hakuziepusha roho zao na mauti, Bali aliiachia tauni uhai wao;51 Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri, Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu.”Lakini pindi tu walipovuka bahari ya Shamu, baada ya kubatizwa kwao, Mungu aliwaonya mapema kabisa na kuwaambia maneno haya.
Kutoka 23: 20 “Tazama, mimi namtuma MALAIKA AENDE MBELE YAKO, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea.
21 Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; WALA MSIMTIE KASIRANI; maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake.”
Unaona hapo?, wana wa Israeli walionywa mapema sasa mmeokoka, na mimi nawatumia malaika wangu kuwahudumia mbele yenu, kuweni makini kwasababu mkifanya makosa hatawasamehe kwasababu maagizo yangu yapo ndani yake. Lakini wana wa Israeli hawakulitilia hilo maanani kama walivyo wakristo wengi leo hii, wanakwenda kubatizwa, wakidhani lile ni jambo la kimasihara tu, isitoshe wanakwenda kushiriki meza ya Bwana, lakini wakitoka hapo wanarudia mambo yale yale waliyoyaacha huko nyuma..Sasa unadhani ni jambo gani litamkuta mtu wa namna hiyo? Wale malaika waliokuwa wanatembea naye watampinga..Na ndio maana hata siku za Mwisho Mungu atakapoikuhumu dunia nzima, atatumia malaika zake, kuleta mapigo juu ya nchi, wataipiga bahari na kuwa damu, milima na visiwa vitahamishwa, watalitia jua giza wakati wa adhuhuri, Na hao hao ndio watakaowakusanya waovu wote pamoja na shetani na kuwatupa katika lile ziwa la Moto.
Kama vile wana wa Israeli walivyotumiwa lile jeshi la malaika waletao mabaya, ndivyo itakavyokuwa kwa mtu yule asiyemama imara mbele za Mungu. Wana wa Israeli mapigo ambayo yangewapasa yawakute adui zao ndio yaliyowakuta wao, kwa manung’uniko yao, kwa zinaa zao, kwa anasa zako, kwa kuabudu kwao sanamu, kwa ulevi wao, ndipo walipokuta na wale nyoka wa moto kule jangwani, tauni, ardhi kupasuka na kuwameza, n.k. Hivyo ndivyo kizazi kile chote kilichomchukiza Mungu jangwani kilivyoishia, hakuna hata mmoja aliiona nchi ambayo Mungu aliyokuwa amewaahidia. Isipokuwa Yoshua na Kelebu miongoni mwa wale wote waliotoka Misri.
Na ndivyo ilivyo hata kwetu sisi tutakaposhindwa kuupambanua mwili wa Kristo, na kujiaumulia kufanya tunayotaka kwa kivuli cha wokovu, na ndio maana biblia inasisitiza NI HERI KUWA MOTO AU BARIDI KULIKO KUWA VUGUVUGU. Wakati mwingine maisha ya mtu yanaweza kukatizwa, anaweza kukumbwa na magonjwa yasiyoponyeka, anaweza kukutana na mikosi ya ajabu akidhani ni shetani kamletea, kumbe hajui ni mwenendo wake wa uvuguvugu, ndio unaomtia Mungu wivu.(Soma 1Wakorintho11:17-14 utathibitisha jambo hilo ).
Lakini Wale wa nje hawawezi kumtia Mungu wivu kwasababu hawajakombolewa hivyo si wa Mungu, hawajanunuliwa kwa damu ya Kristo. Ni sawa sawa na wale wamisri, Mungu hakushughulika baada ya Wana wa Israeli kutoka Misri, waliendelea na miungu yao wala Mungu hakuizungumzia tena baada ya pale, bali alishughulika zaidi na watu wake (Wana wa Israeli) aliokuwa amekwisha kuwakomboa.
Waebrania 3:16 “Maana ni akina nani waliokasirisha, waliposikia? Si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa?17 Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka arobaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao ilianguka katika jangwa?18 Tena ni akina nani aliowaapia ya kwamba hawataingia katika raha yake, ila wale walioasi?19 Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.
Waebrania 4 : 1 “Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa.
2 Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanganyika na imani ndani yao waliosikia.
3 Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile; kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu:”
Hivyo Kaka/Dada Biblia inatuagiza tuutimize wokovu wetu KWA KUOGOPA NA KUTETEMEKA, kwa maana ni Mungu ndiye atendaye kazi ndani yetu.(wafilipi 2:12), Hivyo Mungu hasemi hivyo kwa kututisha lakini badala yake anataka kutubariki.
Tufurahie wokovu wetu pamoja na lile kundi kubwa la Jeshi la mbinguni linapotembea na sisi kutuhudumia. Tutaishi bila hofu, tutaisha bila wasiwasi tutaishi kwa amani tutaishi kwa furaha tukijua kuwa hakuna nguvu yoyote itakayoweza kushindana nasi kwasababu sisi ni uzao mteule wa kifalme, watu wa milki ya Mungu mwenyewe.
Hivyo nikutie moyo wewe ambaye umeokolewa na unaendelea kumcha Mungu na kutembea katika njia zake, uwe na uhakika kuwa hakuna chochote kitakachoweza kwenda kinyume chako kwasababu jeshi la Mungu wa Miungu YESU KRISTO linatembea na wewe daima, kukiongoza na kukulinda na kukuhudumia.
Ubarikiwe sana.
Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na Mungu atakubariki.
No comments:
Post a Comment