"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, January 19, 2019

JE! ULEVI NI DHAMBI?.

Shalom, mtu wa Mungu, karibu tujifunze Neno la Mungu, ambapo leo tutajifunza kwa ufupi juu ya unywaji wa Pombe (au ULEVI). Kumekuwa na mgawanyiko wa makundi mengi katikati ya Wakristo; ambapo wapo wanaoamini kuwa unywaji wa pombe sio dhambi na wapo wanaoamini kuwa pombe imehalalishwa katika maandiko. Na kila kundi linadai kuwa na maandiko ya kusimamia.

Lakini ni muhimu kufahamu kuwa “kuielewa Biblia sio kusoma kile kilichoandikwa pale na kwenda kukushikilia kama kilivyo”..Hapana bali ni kuelewa “ufunuo wa kile kilichoandikwa pale kwa uongozo wa Roho Mtakatifu na kukifanyia kazi”.. Vinginevyo biblia utaiona kuwa inajichanganya mahali na mahali, na kukiona kama ni kitabu cha Uongo, lakini tunajua Biblia ni Kweli wala hakuna chochote kilichokosewa wala cha uongo.. Kama tunaona kuna mahali inajichanganya basi tujue kwamba si biblia inayojichanganya bali ni ufahamu wetu ndio unaojichanganya juu ya kile tunachokisoma.
Biblia Takatifu imegawanyika katika sehemu mbili: AGANO LA KALE na AGANO JIPYA. Utendaji kazi wa Mungu katika Agano la kale ni tofauti kidogo na utendaji wake katika Agano jipya ingawa Mungu ni Yule Yule. Hata katika maisha ya kawaida utendaji kazi wa Serikali iliyokuwa mwaka 1990 ni tofauti na hii iliyopo awamu hii, Ingawa Serikali ni ile ile, isipokuwa tu imerekebisha sera zake, katiba yake, na Huduma zake kwa wananchi. Na madhumuni ya kubadilika utendaji kazi wa serikali ni ile kumfanya mwananchi akae katika hali iliyo bora zaidi kuliko ile aliyokuwa hapo kwanza.

Kadhalika katika Ufalme wa Mbinguni, baada ya Adamu kuasi, Mbingu zilishusha mwongozo wa Kwanza wa namna mwanadamu anavyotakiwa kuishi huo mwongozo ndio unaoitwa Agano la Kale, na Baada ya Muda Fulani, Mbingu zikaleta mwongozo mwingine mpya (katiba mpya )itakayomkamilisha mwanadamu katika ukamilifu wote na hiyo katiba ndio inayoitwa AGANO JIPYA. Kwahiyo Agano jipya ndio utimilifu wa Mwanadamu..Agano la kale halikuweza kumkamilisha mwanadamu..Lakini Mungu ni Yule Yule hajabadilika.

Kwahiyo yapo mambo ambayo Mungu aliyaruhusu katika Agano la Kwanza (yaani Agano la kale) ambayo hayakuwa mapenzi yake kamili, kwamfano Bwana Mungu aliruhusu katika agano la kale, kuwepo na ndoa za mitara (yaani ndoa za mwanaume mmoja kuoa wake wengi)…Lakini katika Agano jipya tunaona Bwana anasema mambo hayo yaliruhusiwa lakii haikuwa hivyo tangu mwanzo (ndoa inapaswa iwe ya mume mmoja na mke mmoja), na hivyo sio sahihi kuwa na mke zaidi ya mmoja.

Kadhalika tunaona pia Katika agano la kale, Bwana aliruhusu Mwanadamu kuua mtu yoyote anayeenda kinyume na maagizo yake aliyoyatoa katika torati, mfano mtu katika Israeli akionekana anaabudu sanamu, au miungu mingine sheria ilikuwa ni kuuawa..Lakini katika agano jipya hilo jambo halipo, tumeambiwa tusiue kabisa, na wala tusilipize kisasa, Mungu mwenyewe ndiye atakayelipa.

Katika agano la kale pia Mungu aliruhusu talaka, yaani aliruhusu Mwanamume kutoa hati ya talaka kwa mkewe endapo wamekosana, lakini katika Agano jipya Hatujapewa ruhusa ya kutoa talaka ya namna yoyote ile, wala kuachana isipokuwa kwa habari ya uasherati tu. Na vivyo hivyo kuna mambo mengine mengi ambayo Agano la kale iliruhusu lakini agano jipya imezuia.

Na pia tunaona katika agano la kale, damu iliyokuwa inatumika kuondoa dhambi ilikuwa ni damu ya wanyama, lakini katika agano jipya lililo bora zaidi ilitumika damu ya mtu mmoja mtakatifu kwa ajili ya ondoleo la dhambi, kwasababu damu za wanyama zisingeweza kuondoa dhambi bali zilifunika tu.
Na leo tutazungumzia jambo moja ambalo Mungu aliliruhusu katika agano la kale na akalizuia katika Agano jipya. Kwasababu halikuweza kumkamilisha mwanadamu.
Hebu tusome mstari ufuatao..
Mithali 31: 1 “Maneno ya mfalme Lemueli; mausia aliyofundishwa na mama yake.
2 Ni nini, mwanangu? Tena ni nini, mwana wa tumbo langu? Tena, ni nini mwana wa nadhiri zangu?
3 Usiwape wanawake nguvu zako; Wala moyo wako usiwape wal
e wawaharibuo wafalme.
4 Ee Lemueli, kunywa mvinyo hakuwafai wafalme, hakuwafai wafalme; Wala haifai wakuu waseme, Ki wapi kileo?
5 Wasije wakanywa na kuisahau sheria, Na kuipotosha hukumu ya mtu aliye taabuni.
6 Mpe kileo yeye aliye karibu na kupotea;
Kampe divai yeye aliye na UCHUNGU NAFSINI.
7 Anywe akausahau umaskini wake; Asiikumbuke tena taabu yake”
Ukisoma huu mstari kwa haraka pasipo kujua utendaji kazi wa Mungu katika nyakati tofauti tofauti unaweza ukasema “Mungu kahalalisha unywaji wa Pombe”…Na pia ukisoma mstari huu haraka haraka unaweza ukasema Mungu kahalalisha uuaji “Usimwache mwanamke mchawi kuishi (kutoka 22: 18)”., au usomapo mstari huu unaweza ukasema Mungu kahalalisha visasi “Walawi 24: 19 Na mtu akimtia mwenziwe kilema; vile vile kama alivyofanya, naye atafanyiwa vivyo; jeraha kwa jeraha, jicho kwa jicho, jino kwa jino; vile vile kama alivyomtia mtu kilema, naye atalipwa vivyo”

Kwahiyo unaona mistari hiyo Mungu alihalalisha mambo yasiyo sahihi yafanyike miongoni mwa watu wake ili wakae kwa utulivu na ustaarabu, ndio maana unaona alihalalisha visasi, alihalalisha mauaji kwa waabudu sanamu, n.k

Lakini pia alihalalisha UNYWAJI WA DIVAI, (kumbuka, ni divai tu ndiyo iliyohalalishwa sio kilevi chochote nje na hicho) na ilihalalishwa kwa watu walio katika UCHUNGU na walio katika shida, na umaskini mkali, ili wanywapo wakausahau Umaskini wao…Lakini kama tunavyosema agano la kwanza halikumkamilisha mwanadamu..Mtu anaweza kweli kunywa divai, akalewa akausahau umaskini wake kwa wakati ule aliokuwa amelewa tu, lakini akili yake itakaporudi atakuwa bado ana kumbukumbu la umaskini wake na uchungu wake katika maisha yake (shida zake zipo palepale).

kwahiyo kilevi hakingeweza kumweka huru mtu mbali na uchungu nafsini, au hali ya kukosa raha nafsini, kama tu vile damu ya ng\ombe na Mbuzi isivyoweza kuondoa dhambi bali kufunika kwa kipindi kifupi tu, na baada ya muda kunakuwa na kumbukumbu la dhambi ndivyo ilivyo kwa divai. Na tunaona pia mbali na divai kumfanya mtu asahau umaskini wake kwa kitambo, bado pia ilikuwa inamfanya mtu kwa sehemu asahau sheria za Mungu..Kwahiyo haikuwa ni dawa kamili ya makosa. Ni sawa madaktari watoe dawa ya kwanza ya kutibu ugonjwa Fulani, lakini dawa hiyo haitibu bali inapunguza tu makali, na zaidi ya yote inayomadhara ya pembeni lakini baada ya muda wagundue dawa nyingine ambayo haina madhara kabisa ya pembeni na inatibu ugonjwa wote kabisa.

Hivyo agano la kale lilivyokuwa, tunaweza kulifananisha na dawa hiyo yenye kupunguza makali lakini haiondoi ugonjwa, na zaidi ya yote ina madhara ya pembeni kwa mtumiaji,
Lakini lilivyokuja, agano jipya,yaani agano la Yesu Kristo hilo ndilo tunaloweza kulifananisha na dawa mpya yenye uwezo wa kuondoa ugonjwa kabisa kabisa na isiyokuwa na madhara ya pembeni.Agano hili jipya ndilo lililo na uwezo wa kuondoa dhambi kabisa kabisa, na ndilo lenye uwezo wa kumfanya mtu aliye na uchungu nafsini mwake kupata tumaini, furaha na raha isiyoisha kwasababu pombe inampa mtu tu faraja ya kitambo lakini, Yesu akiwa moyoni mwa mtu anampa raha ya milele isiyoisha.Ndio maana Bwana Yesu alisema..
Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; NANYI MTAPATA RAHA NAFSINI MWENU;
30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.
Unaona! Pombe yetu kwasasa ambayo inaweza kutufanya tusahau shida zetu na uchungu wetu, Ni kuwa na Yesu Kristo ndani yetu, na sio ULEVI. Huyo ndiye atakayekata kamba za mateso, shida, ya huzuni, uchungu na umaskini,…Yeye ndiye Maji yaliyo hai ambayo mtu akiyanywa hataona kiu tena. Divai sio maji yaliyo hai kwasababu mtu akiinywa baada ya muda atakwenda kuitafuta tena.

Lakini utasema mbona Mtume Paulo alihalalisha pombe katika agano jipya na kusema..katika 1 Wakorintho 11: 22 “Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa ajili ya hayo”

Hapo aliposema “hamna nyumba za kulia na kunywea ” hakumaanisha kuhalalisha ulevi,..tafakari mfano huu> umepanda gari la umma labda akaingia mtu na sigara yake mdomoni na kuanza kuivuta ndani ya lile gari, na wewe ukamwambia samahani tunaomba ukavutie sigara zako nje” je! Kwa sentensi hiyo utakuwa umehalalisha sigara?? Ndicho Mtume Paulo alichokuwa anajaribu kuwaambia hapa, watu baadhi walioko kanisa Koritho ambao walikuwa wanaidharau meza ya Bwana, kwa kunywa divai ile pasipo kiasi mpaka kufikia kulewa.

Kadhalika wapo wanaosema Mtume Paulo alimwambia Timotheo anywe pombe 1Timotheo 5: 23 Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara..
Kumbuka zamani hawakuwa na piriton, au panadol tulizonazo sisi leo, hivyo tiba ya karibu ambayo ilikuwa inaweza kumfanya mtu atulize magonjwa madogo madogo ilikuwa ni divai tena kwa kiwango kidogo sana. Lakini kwasasa mtu huwezi kutumia divai kutuliza homa zipo dawa nyingi hospitalini zilizobora kushinda hizo na zenye uwezo mkubwa.. Kwahiyo utaona hapo haikunywewa kama kitu cha kujiburudisha mpaka kulewa, bali kama dawa.

Kwahiyo kama maandiko pia yanavyotuambia Waefeso 5: 18 “Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho”.
Hivyo ndivyo Mungu anavyotaka, usikubali kwa namna yoyote kushawishika kwamba Mungu kahalalisha unywaji wa pombe katika nyakati hizi, Ulevi ni dhambi inayowapeleka maelfu kuzimu leo, Ulevi na Uasherati. Jiepushe na hivyo vitu ndivyo vinavyouharibu mwili wa Mtu ambao biblia imesema ni hekalu la Roho Mtakatifu.
1 Wakoritho 6: 9 “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,
10 wala wevi, wala watamanio, WALA WALEVI, wala watukanaji, wala wanyang'anyi”.
Kama hujampa Bwana Maisha yako, fanya hivyo sasahivi, tubu kutoka ndani ya moyo wako, na dhamiria kabisa kuacha dhambi na maisha ya kale uliyokuwa unaishi, anza maisha mapya na Kristo kisha, katafute ubatizo sahihi kulingana na maandiko,wa maji mengi na kwa Jina la Yesu Kristo na Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu, atakayekusaidia kushinda dhambi na kukuongoza katika kuijua kweli yote ya Biblia.

Bwana akubariki.

No comments:

Post a Comment