"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, January 5, 2019

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 50


 SWALI 1: Marko16. 15.{Bwana Yesu}Akawaambia Enendeni ulimwenguni mwote,MKAIHUBIRI INJILI KWA KILA KIUMBE.Ndugu zangu hapo Bwana wetu anamaanisha tuhubirie kuku,mbuzi,ngo 'mbe,kobe Nakadhilika? au Bwana Yesu Anamaanisha nini kusema MKAIHUBI INJILI KWA KILA KIUMBE?.
JIBU: Wakati ule Mtume Petro alipokuwa kule Yafa katika nyumba ya Yule mtu mtengenezaji ngozi, siku moja aliumwa na njaa sana, na alipotaka kwenda kuandaa chakula biblia inasema alizimia na kuona maono, na ndani ya maono yale aliona kitu kama nguo kubwa ikishuka kutoka juu na ndani yake imebeba viumbe vya aina zote duniani, wanyama wa kila namna. Na Bwana akamwambia Petro aende kuwachinja ale. Lakini kama tunavyosoma Petro alimjibu Mungu na kumwambia tangu azaliwe hajawahi kula vitu vilivyo najisi. Na ndipo hapo Mungu akamwambia nilivyovitakasa mimi usiviite wewe najisi.(Matendo 10).

Sasa pale ni jambo gani BWANA alikuwa anataka kumwonyesha Petro, Tukisoma ile habari, kuanzia mwanzo utaona kuwa kulikuwa na mtu mmoja mcha Mungu aliyeitwa Kornelio, Ni mtu ambaye hakuwa myahudi, wala hakujua sheria zozote za kiyahudi, Ni Mtu wa mataifa, lakini kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu alipewa neema ya kuwa mmojawapo wa wateule wa Mungu. Sasa kumbuka kabla ya hapo watu wa mataifa kule Israeli walijulikana kama najisi, hivyo hawakuruhusiwa kuchangamana na wayahudi kwa namna yoyote ile ya ibada. Lakini Mungu alimwambia Petro nilivyovitakasa mimi usiviite wewe najisi najisi, Ondoke uende katika nyumba ya Kornelio akawahubirie injili, akawabatize na wao pia wapokee habari njema za Yesu Kristo waokoke.

Hivyo vile viumbe vya aina tofauti tofauti alivyoviona Petro, najisi, na visivyo najisi, vitambaavyo, virukavyo, vyenye miguu minne, nguruwe, bundi, popo, mbuzi, pweza,karungu-yeye, kivunja-chungu n.k. Vilikuwa vinawakilisha jamii tofauti tofauti za watu waliopo duniani. Na ndio maana baada ya Petro kupata ufunuo huo ndio utaona kuanzia huo wakati nao pia wakaanza kuhubiri injili kwa watu wa mataifa pia, jambo ambalo hapo kabla walikuwa hawafanyi, walikuwa wakihubiri wa wayahudi tu peke yao. Japo YESU alishatangulia kuwapa maagizo hayo kabla lakini hawakumwelewa.

Sasa ndio tukirudi kwenye huo mstari ambao Bwana aliwaambia mitume wake siku ile aliyokuwa anapaa kwenda mbinguni akisema “Enendeni ulimwenguni mwote,MKAIHUBIRI INJILI KWA KILA KIUMBE.” Alimaanisha waende wakahubiri injili kwa kila jamii ya watu waliopo ulimwenguni bila kuchagua hawa ni wayahudi, hawa si wayahudi, bila kujali rangi, dini zao, utamaduni wao, taifa lao, lugha zao n.k. Ilimradi ni mwanadamu basi injili ni lazima imfikie. Lakini Bwana hakumaanisha tukawahubirie kuku, na panya, na mijusi, na konokono injili. 
 
SWALI 2: Warumi 8:18-25 Viumbe vinatazamiaje kwa shauku kufunuliwa kwa Mwana wa MUNGU?
JIBU: Jambo lisilofahamika na wengi ni kwamba, viumbe navyo vitakuwepo katika ulimwengu ujao (Mbingu Mpya na nchi Mpya)..Mungu alipoiumba dunia hakuwaumba wanadamu peke yao, bali aliwaumba pamoja na wanyama na ndege, Na Mwanadamu alipoasi, laana aliyolaaniwa haikumpata Mwanadamu peke yake bali hata na wanyama, mwanadamu alipoambiwa atakufa, na wanyama pia walikufa, Mwanadamu alipoambiwa atazaa kwa uchungu wanyama nao pia walizaa kwa uchungu.

Mungu alipoiangamiza dunia kwa gharika, wanyama nao waliangamizwa..na kadhalika Mungu alipowaokoa baadhi ya wanadamu wachache katika safina (Nuhu na wanawe) pia kulikuwepo na baadhi ya wanyama waliookoka na gharika. Hivyo mahali popote mwanadamu alipo wanyama nao wapo, kwasababu waliumbwa kwa ajili ya mwanadamu.

Kwahiyo kama vile sisi wanadamu tunavyotamani siku ya kufunuliwa kwetu, yaani siku tutakayoiingia Mbingu Mpya na Nchi Mpya, siku ambayo hatutakiona tena kifo, wala uchungu, wala shida na wanyama na viumbe vyote vivyo hivyo vinatamani kama sisi. Navyo vinatamani kutoka katika laana hii ya dhambi, na kuingia uhuru wa Umilele.

Biblia inasema katika ulimwengu ujao ulimwengu utakuwa na Amani, kutakuwa hakuna dhiki kwa wanyama, wala tabu. Wanyama hawatakulana tena, simba atakula majani kama ng’ombe, na mbwa mwitu atakaa pamoja na mwanakondoo.

Isaya 11: 6 “Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.
7 Ng'ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng'ombe.
8 Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira.
9 Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari”.

Kwahiyo wanyama na viumbe vyote vinatamani siku ya kuwekwa kwao huru kufike, kama sisi tunavyotamani siku hiyo ifike.

Mungu akubariki.

No comments:

Post a Comment