"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, January 5, 2019

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 49


SWALI 1: Biblia inasema Kaini baada ya kumuua ndugu yake Abeli, alikimbilia katika nchi ya Nodi, Je! Huko alipatia wapi mke na kuzaa naye watoto? (Mwanzo 4:16).
JIBU: Ukisoma Mwanzo 5:1-5 utaona inasema....

1Hiki ndicho kitabu cha vizazi vya Adamu. Siku ile Mungu alipoumba mtu, kwa sura ya Mungu alimfanya;
2 mwanamume na mwanamke aliwaumba, akawabariki akawaita jina lao Adamu, siku ile walipoumbwa.
3 Adamu akaishi miaka mia na thelathini, akazaa mwana kwa sura yake, kwa mfano wake, akamwita jina lake Sethi.
4 Siku za Adamu baada ya kumzaa Sethi zilikuwa miaka mia nane, AKAZAA WANA, WAUME NA WAKE
5 Siku zote za Adamu alizoishi ni miaka mia kenda na the lathini, naye akafa.

Sasa kwenye Mstari huo wa 4 utaona kuwa kumbe mbali ya Kaini na Abeli kuzaliwa na Adamu kulikuwa na wana wengine wa kike na wakiume waliokuja kuzaliwa kwenye familia yao pia, na ndio huko huko Kaini alipojitwalia mke.

SWALI 2: Kama KAINI alitwaa mke ambae alizaliwa na Adamu na Hawa ambao ni wazazi wake kwahiyo alimuoa dada yake je,kwahiyo nihalali kumuoa mwanamke ambae ni dada yangu wa damu?''.
JIBU: Kumbuka hata Adamu mwenyewe hakwenda kumtwaa mke kutoka kwenye familia nyingine, bali katika ubavu wake mwenyewe, hivyo kama ni undugu basi Adamu na hawa wana undugu mkubwa zaidi ya Dada na kaka...

Unaona? Mungu aliruhusu iwe hivyo mwanzoni kwa ajili ya uzazi, ili watu waongezeke, lakini baadaye Mungu alitoa maagizo kuwa ni makosa mtu kutwaa ndugu wake wa karibu na kumfanya kuwa mke wake..

Mambo ya walawi 18:6 Mtu ye yote aliye wa kwenu asimkaribie mwenziwe aliye wa jamaa yake ya karibu ili kumfunua utupu; mimi ndimi Bwana.

Na pia mstari wa 9 unasema...

9 Utupu wa umbu lako, binti ya baba yako, au binti ya mama yako, kwamba alizaliwa nyumbani mwenu au kwamba alizaliwa kwengine, utupu wa hao usifunue.

Kwahiyo ni machukizo kuoa ndugu yako yoyote yule wa karibu.


 SWALI 3: Ni kwa nini tunasema tunamwabudu MUNGU aliye hai ,je,wale wanaomwabudu shetani sio mungu wao aliye hai?
JIBU: Embu tutafakari mfano huu, utatusaidia kupata majibu ya maswali yetu. Tunajua kuwa Dunia tunayoishi sasa hivi ni dunia ya utandawazi na kugunduliwa kwa Kompyuta kumefanikisha kurahisisha mambo mengi sana, Komputa sasa inaweza kufanya mambo ambayo mwanadamu pekee angeweza kufanya, unaweza ukaiuliza swali lolote na ikakusaidia kupata sehemu kubwa ya majibu yako, inaweza kukusaidia kufanya mahesabu yako, inaweza ikakusaidia kuwasiliana na mtu mwingine aliye mbali, inaweza ikakuonyesha picha, inaweza ikakuhifadhia kumbukumbuku zako, inaweza ikakusaidia kutafiti, na hata kufanya kazi n.k. Kwa ufupi komputa sasa tunaweza kusema ni chombo ambacho kina ufanisi mkubwa karibia na mwanadamu, tunaweza kusema kina uhai fulani, Na uhai huo ni wazi kabisa hakijapewa na mwingine zaidi ya mwanadamu.

Lakini pamoja na hayo tunajua hata kiwe na ufanisi mkubwa kiasi gani, bado tu uhai wake hauwezi kuwa halisi kama wa mwanadamu mwenyewe, vipo vitu vingi kitashindwa kufanya ambavyo mwanadamu angeweza kufanya, kwamfano Komputa haiwezi kufariji, haiwezi kupima hisia za mtu, komputa haiwezi kuonyesha fadhili, komputa ukiiomba chakula haiwezi kukupa, komputa haiwezi kuona mambo ya mbeleni ili kuchukua tahadhari n.k..yenyewe inaongozwa na kwa yale tu mwanadamu aliyoyapachika ndani yake, nje ya hapo haiwezi kujichagulia mambo yake yenyewe.

Vivyo hivyo tukirudi kwa Mungu wetu. Tunajua sisi sote tumeumbwa kwa mfano wa Mungu, na kama vile alivyo hai, na sisi basi tutakuwa hai, lakini uhai tulionao si kama ule wa kwake, sisi ni mfano wa Komputa zilizotengenezwa na Mungu, tunaouwezo wa kuonyesha tabia zote za Mungu lakini haimaanishi tutakuwa na ule uhai halisi kabisa kama wa Mungu mwenyewe, wa kufikia hatua ya kuweza hata kuumba, kufanya kila kitu, kuona mambo yote ya mbeleni yanayokuja, kuchipusha chakula ardhini, hatuwezi pia kujihakikishia uzima wetu wa milele kama sio kutoka kwake.

Hivyo tunavyosema Tunamwabudu Mungu aliye HAI, tunamaanisha Mungu awezaye kufanya mambo yote, Mungu anayetoa uhai katika mambo yote, Mungu ambaye hashindwi na lolote,Shetani hawezi kuumba chochote,japo anaishi, hajui hata kesho yake itakuwaje sasa ataitwaje mungu aliye hai? Yeye kapewa tu sehemu ya uhai kama sisi tulivyopewa, hawezi kusema sasa nataka jua lizime, au leo mimea yote duniani ikauke,hana uwezo huo hivyo hawezi kuitwa Mungu aliye hai.. Neno zuri labda linaweza kumstahili yeye kuitwa nao hao wanaomwabudu ni “mungu aliyepewa pumzi”, lakini sio Mungu aliye hai aliye hai ni mmoja tu! anayekaa mbingu za mbingu.

Ubarikiwe.
SWALI 4: Wala msimwite mtu baba duniani;..Hapo Bwana wetu Yesu anamaanisha nini ndugu zangu?
JIBU: Neno hilo halimaanishi kuwa hatupaswi kabisa kumwita mtu yeyote baba duniani hata wazazi wetu, hapana kama ni hivyo basi Mungu angekuwa anapingana na Neno lake pale aliposema “Waheshimu baba yako na mama yako (Kutoka 20:12)” unaona?. Lakini tunapaswa kufahamu maneno hayo Bwana aliwalenga watu wa namna gani, ukisoma mistari hiyo kuanzia juu utaona kuwa aliwalenga wale mafarisayo na masadukayo ambao wao, walipenda kuchukua nafasi ya Mungu duniani kwa kila kitu, walitaka watu wawaone kama pasipo uwepo wao, hawawezi kumjua Mungu, pasipo watu kuongozwa na wao hawawezi kumfikia Mungu, yaani kwa ufupi walikuwa wanachukua nafasi ya Kristo duniani. Na ndio maana tukisoma tangu juu tunaona Bwana akiwaambia maneno haya..

Mathayo 23: 1 “Kisha Yesu akawaambia maku
tano na wanafunzi wake, akasema,
2 Waandishi na Mafarisayo WAMEKETI KATIKA KITI CHA MUSA;
3 basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao,
msitende; maana wao hunena lakini hawatendi.
4 Wao hufunga mizigo
mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa
kwa kidole chao.
5 Tena matendo yao yote huyatenda ILI KUTAZAMWA NA WATU; kwa kuwa hupanua hirizi zao,
huongeza matamvua yao;
6 hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele
katika masinagogi,
7 na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi.
8 Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu.
9 WALA MSIMWITE MTU BABA DUNIANI; MAANA BABA YENU NI MMOJA, ALIYE WA MBINGUNI.
10 WALA
MSIITWE VIONGOZI; MAANA KIONGOZI WENU NI MMOJA, NAYE NDIYE KRISTO”.

Mambo hayo hayo ndio tunayoweza kuyaona leo hii katika Kanisa la kirumi (Katoliki), ofisi ya kiPapa inajulikana kama “ofisi ya baba mtakatifu” na watu humweshimu yeye kama mpatanishi wa dhambi zao, na anaonekana kama ni mtu aliye na kibali cha karibu zaidi kwa Mungu zaidi ya watu wengine wote, hivyo amepewa heshima ya kipekee, anaketi mbele katika masinagogi (Katika umoja wa makanisa) ili atazamwe na ulimwengu wote kuwa yeye ni baba mtakatifu. Sasa Heshima kama hizo ambazo zinazohusianishwa na uhusiano na vyeo mbele za Mungu kwamba mtu Fulani ni mwenye cheo Fulani cha kipekee mbele za Mungu zaidi na wengine, ndizo Kristo alizokuwa anazikemea, kwamba tusimwite mtu yeyote Baba kwa namna hiyo, au kiongozi, au Rabi. Kwasababu sisi sote ni ndugu na hakuna aliye juu ya mwenziwe.

Pale Mtume Paulo alipomwita Timotheo na Tito wanae, alikuwa anaonyesha uhusiano aliokuwa nao kama mtumishi wa Mungu aliyewazaa katika injili, na kuwalea, kwa mfano wa Baba kwa mwanawe, lakini hakuwa na maana kuwa yeye yupo juu ya mwenzake, wala hakutanua hirizi zake wala kuongeza matamvua yeye, kiasi cha kukaa masokoni kupewa heshima na watu, kwamba ni sharti aanze yeye mbele za Mungu kisha wao, na kwamba pasipo yeye hawawezi kumfikia Mungu, Hapana na hakuna mahali popote Paulo alisisitiza yeye aitwa aitwe Baba.

Utaona nyaraka zake zote Mtume Paulo, alianza na “Mimi Paulo, mfungwa na Mtumwa wa Yesu, sehemu nyingine anasema mimi Paulo mtume wa Yesu Kristo”..Lakini hutaona sehemu yoyote anaanza kwa kusema “Mimi Paulo, Baba Mtakatifu wa kanisa takatifu korintho”..hapana hutaona hicho kitu.

Lakini inasikitisha zaidi kusikia leo hii watu wanagombania kuitwa baba, na wengine kwa nguvu, hata kama huyo mtu hana mahusiano yeyote ya kiiamani na yeye anayetaka amwite, bado atataka aitwe tu baba, hayo ndiyo Kristo aliyoyakataa, hiyo ni roho ya mpinga-kristo.

Lakini ikiwa ubaba wowote hautahusianishwa na kuchukua nafasi yoyote ya Kristo, huo hauna shida yoyote, ni kama tu vile unavyomwita mzazi wako baba au mama, hiyo haikuchukui nafasi yeyote linapokuja suala la kumwabudu Mungu, kwasababu unajua Baba yako aliye mbinguni ndiye anayestahili kupewa heshima zote za ibada na za kiungu.
Vivyo hivyo ikiwa utatoa heshima yako kwa kiongozi wako yeyote, au mwalimu wako, kanisani, hakikisha kuwa hilo halichukui nafasi ya Kristo, mnapokuja kwenye suala la kumwabudu Mungu basi sisi wote ni ndugu na tunapaswa kupeleka heshima zote, shukrani zote, na maombi yote kwa Mungu na sio kwa mwanadamu yeyote kama kanisa katoliki lifanyavyo kwa mapadre wao na Papa, na baadhi ya makanisa ya kiroho ambayo yanamfanya mtu mmoja kama ndio kila kitu kwao, huku wakimwita baba na pasipo yeye wanajihisi hawawezi kumwabudu Mungu. Hizo ni ibada za sanamu.

Ubarikiwe sana.

No comments:

Post a Comment