"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, January 16, 2019

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 52


SWALI 1: Je! ni vibaya kutaja Huduma kwa kujipa cheo? Mfano Mighty Prophet??
JIBU: Biblia haikatazi  mtumishi  yeyote wa Mungu kutambuliwa kwa karama aliyo nayo. Kwamfano kuitwa mchungaji, au mwinjilisti au mtume, au mwalimu au nabii au askofu n,k. Hakuna mahali ilipokataza, Lakini kuongeza Neno hapo juu yake mfano “mkuu” au “kiongozi ” “mighty” “chief” “lead” “great” n.k. hiyo ni roho ya kujiinua na ni roho ya mpinga-kristo yenyewe. Kwani vyeo hivyo vinamuhusu Bwana wetu YESU KRISTO mwenyewe.. Yeye ndiye mchungaji mkuu biblia inasema hivyo..yeye ndiye mtume mkuu, yeye ndiye nabii mkuu, Yeye ndiye Bwana wa mabwana, na yeye ndiye Mfalme wa wafalme.

Na ndio maana utaona hakuna Mtume yeyote wa Kristo alijiita kuwa yeye ni mtume mkuu,  bali cheo hicho walikitambua kuwa ni cha Kristo mwenyewe.

Waebrania 3:1 “Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini sana MTUME NA KUHANI MKUU wa maungamo yetu, Yesu, aliyekuwa mwaminifu kwake yeye aliyemweka, kama Musa naye alivyokuwa, katika nyumba yote ya Mungu.

Waebrania 3:
20” Basi, Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu MCHUNGAJI MKUU wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu,”

Unaona? Hivyo hao watu wote wanaojivika hivyo vyeo vya juu zaidi ya walivyopewa, utatambua kuwa dhima yao ni kuvuta watu kwao, wawafuate wao na si Kristo, na ndio maana utaona hawaoni hata haya kujivuka vyeo vya juu kama hivyo. Lakini biblia inasema ajikwazaye atashushwa..Watu wa namna hiyo Bwana mwenyewe atawashusha, kwasababu yeye kasema Utukufu wake hatagawana na mwingine yeyote.


SWALI 2: WAEBRANIA 6:1-3 hapo kwenye mstari wa pili, anamaanisha nini?.
JIBU: Waebrania 6:1-3 Inasema.. “1 Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu,
2 na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele.
3 Na hayo tutafanya Mungu akitujalia.”

Ndio Bwana anatuonyesha kwamba ukristo ni safari isiyoishia tu pale mtu anapotubu na kubatizwa na kumwamini Mungu, bali ni jambo endelevu siku baada ya siku tunakua, na ndio maana mtume Paulo anasema hapo TUKAZE MWENDO ili tuufikilie huo utimilifu. Hatupaswi kila siku tu tukae kwenye mafundisho yanayohusu ubatizo sahihi, au kutubu au kumwamini Mungu, au ziwa la moto, hayo ni mafundisho ya chini sana, kwamba pindi tu pale mtu alipompa Bwana maisha yake alipaswa ayatambue. Na hivyo anakuwa na wajibu wa kusonga mbele kujifunza mambo mengine ya muhimu zaidi.

Lakini inasikitisha kwamba utakuta mtu anadai yeye ni mkristo wa muda mrefu lakini bado suala la ubatizo sahihi linampiga chenga, mwingine haamini kabisa mambo hayo, mwingine hata ubatizo anaona hauna umuhimu kwake, anaamua kuendelea kubaki hivyo hivyo tu kwa muda mrefu, angali akijua kabisa biblia inafundisha kuwa pale tu mtu anapoamini , bila kupoteza muda anapaswa akabatizwe, kuukamilisha wokovu wake, lakini bado kwake anaona ni jambo linaloweza kusubiri tu, halina umuhimu sana .(Matendo 8:35-38) .

Sasa kama mambo hayo machanga yanakuwa bado ni mitihani kwa watu unategemea vipi Mungu aachilie neema kwa watumishi wake kufundisha mambo mengine ya ndani zaidi yatakayomfanya mtu akomae kiroho?. Ikiwa mtu haweza kuhesabu moja mpaka kumi, ya nini kufundishwa milinganyo?.
Hivyo yatubadilishe mienendo yetu kwanza, ili Bwana aachilie neema ya kutufundisha mambo mengine ya ndani yahusuyo ufalme na na siri zimuhusuzo Bwana wetu YESU KRISTO.

Vinginevyo tukiendelea kumzimisha Roho ndani yetu kwa kutokutaka kutii maagizo madogo, tutatii vipi yale makubwa, tutaendelea tu kubaki katika hali ile ile ya uchanga kwa muda mrefu bila mabadiliko yoyote, hatutastahili kupata chakula kigumu cha kutufanya tukue. Kama Mtume Paulo alivyosema kwa Waebrania..

Waebrania 5: 11 “..Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia.
12 Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu.
13 Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga.
14 Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa
kupambanua mema na mabaya”
 SWALI: 3 Nitamjuaje nabii wa Uongo?.
JIBU: Manabii wa Uongo hatutaweza kuwajua kama hatutawajua manabii wa Kweli,..kwanza Nabii wa Kweli ni lazima awe Mkristo, aliyempa Bwana maisha yake kikweli kweli, aliyesafishwa maisha yake kwa damu ya Yesu Kristo, na anayedhihirika kwa maisha yake matakatifu anayoishi yanayolingana na Neno la Mungu, anapaswa awe sio mtu wa kupenda fedha, sio mtukanaji, sio mwasherati ana mke/mume mmoja, hali rushwa, ana upendo, mtu wa amani, anayemheshimu Mungu na kumpa Utukufu yeye, hajitukuzi yeye, anajali watu wa Mungu, na asiyependa mambo ya ulimwengu huu. Hayo ndiyo matunda ya roho yanayotajwa katika Wagalatia 5:22 ambayo yanapaswa yaonekane kwa Nabii wa Kweli na sio Nabii tu bali hata mchungaji wa kweli, mwalimu wa kweli, askofu wa kweli, shemasi wa Kweli, muimbaji wa Kweli na muumini wa kweli. Na ndio maana Bwana YESU alisema kwa matunda yao mtawatambua..sasa matunda yenyewe ni yapi?. Ndio haya tunayoyasoma katika wagalitia 5:22.

Mtu yeyote anayejiita Nabii asipoonyesha hayo matunda ni ishara mojawapo kuwa tayari ni nabii wa uongo.
Pili nabii wa Kweli anapaswa atoe unabii unaolingana na NENO LA MUNGU au BIBLIA TAKATIFU, Kama vile alivyo mwalimu wa Ukweli, au askofu wa kweli, ni lazima afundishe kitu kinacholingana na Neno la Mungu (yaani Biblia takatifu), Mwalimu yoyote akitufundisha kitu chochote kisichohusiana na Biblia basi huyo atakuwa ni mwalimu wa mambo mengine lakini sio wa Biblia. Kadhalika na Nabii, anapaswa atoe Unabii unaolingana na Biblia, Unabii mwingine utakaotupeleka kwenye mambo mengine yasiyohusiana na Biblia Takatifu basi huyo ni Nabii wa mambo mengine, pengine mwana-mazingaumbwe au Mtabiri wa nyota.

Nabii wa Kweli anapaswa atoe Unabii unaoturudisha sisi kumfahamu sana Mwana wa Mungu (Yesu Kristo) na sio kumfahamu yeye, anapaswa atoe Unabii utakaotufanya sisi tumwamini na kumpenda Yesu, na kuyashika maneno ya Yesu zaidi ya kuyashika maneno yake binafsi, anapaswa atoe Unabii utakaotufanya tuwe watakatifu na kuchukia dhambi, unabii utakaotufanya tutubu dhambi zetu kwa kumaanisha kuziacha, unabii utakaotufanya tuanze kuutafuta ufalme wa Mbinguni zaidi ya mambo ya ulimwengu huu, Unabii utakaotufanya tutazamie mambo ya ulimwengu ujao,Unabii utakaotufanya tumpe Mungu utukufu zaidi ya kumpa yeye utukufu, unabii utakaotufanya tuwe na upendo na tuwe wakamilifu kama Mungu alivyo mkamilifu, Unabii utakaotufanya Tusiabudu Miungu mingine zaidi ya Mungu wa Mbinguni.

Lakini kama Nabii, au Mchungaji, au askofu, au Mwalimu..Hatufundishi, au kutupa Unabii wa Mambo yanayohusiana na mapenzi ya Mungu, hata kama atafanya ishara kiasi gani, hata kamaatatenda miujiza mingi kiasi gani, hata kama anaona maono na yanakuja kutimia kiasi gani..Huyo Biblia imesema ni Nabii wa Uongo na tusimsikilize.

Kumbukumbu 13: 1 “Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,
2 ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;
3 WEWE USIYASIKIZE MANENO YA NABII YULE, AU YULE MWOTAJI WA NDOTO, KWA KUWA BWANA, MUNGU WENU, YUAWAJARIBU, APATE KUJUA KWAMBA MWAMPENDA BWANA, MUNGU WENU, KWA MIOYO YENU YOTE NA ROHO ZENU ZOTE.
4 Tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye.
5 Na yule nabii, au yule mwotaji wa ndoto, na auawe, kwa kuwa amesema yaliyopotoka juu ya Bwana, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, akakukomboa katika nyumba ya utumwa, apate yule mtu kukupotoa katika njia aliyokuamuru Bwana, Mungu wako, uiendee. Ndivyo utakavyouondoa uovu utoke katikati yako”.

Unaona hapo? Kwahiyo Ishara na miujiza sio alama ya msingi ya kumtambua Nabii wa Kweli, alama ya Msingi ya kumtambua nabii wa kweli ni Anaturejeshaje kwenye Neno la Mungu (kuzishika Amri za Mungu zilizopo kwenye biblia takatifu), Nabii akitoa unabii kwamba kesho kutatokea kimbunga cha mvua ya mawe na kweli kesho kimbunga hicho kikitokea kama alivyotabiri, na akasema kwa ishara hiyo Mungu kaniambia watu wote wawaache wake zao, na waume zao, au waongeze idadi ya wake/waume walionao au Nabii yule akasema watu wote wakaasujudie jua kwa siku tatu, biblia inatuonya mtu huyo tusimsikilize; NI NABII WA UONGO, kwasababu Neno la Mungu, linasema Tusiabudu miungu mingine zaidi yake yeye Mungu aliye hai aliyeziumba Mbingu na nchi, aliyeko mbinguni, wala tusisujudie kitu chochote, Kadhalika Biblia inasema “ndoa ni ya mume mmoja na mke mmoja” na amwachaye mkewe na kuoa mwingine azini, Na yeye anatupeleka kwenda kuongeza idadi ya wake, na kufanya uzinzi.

Mfano mwingine, Nabii akatoa unabii fulani na huo unabii ukaja kutimia na akasema Mungu haangalii mavazi anaangalia roho, hivyo wanawake waendelee kuvaa nguo zao wanazovaa siku zote, vimini, suruali,n.k wajipambe kama watakavyo, au anasema Yesu haji leo wala kesho, au anasema Mungu hatawahukumu watenda dhambi na mashoga. Huyo ni wakujitenga naye mbali kwasababu ni Nabii wa Uongo (roho ya Mpinga-kristo inatenda kazi ndani yake), Biblia imekwisha tuonya.

Kwahiyo Ni muhimu kulifahamu Neno la Mungu, na kulishika ili tusidanganyike kwasababu Roho hizi za manabii wa Uongo kipindi hichi cha siku za mwisho ndio zinatenda kazi kwa nguvu zimeachiwa duniani kote,na kuwadanganya wengi yamkini hata wale waliowateule. 
 
Mungu akubariki.

No comments:

Post a Comment