"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, January 16, 2019

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 53

 SWALI: Nitamjuaje nabii wa Uongo?.
JIBU: Manabii wa Uongo hatutaweza kuwajua kama hatutawajua manabii wa Kweli,..kwanza Nabii wa Kweli ni lazima awe Mkristo, aliyempa Bwana maisha yake kikweli kweli, aliyesafishwa maisha yake kwa damu ya Yesu Kristo, na anayedhihirika kwa maisha yake matakatifu anayoishi yanayolingana na Neno la Mungu, anapaswa awe sio mtu wa kupenda fedha, sio mtukanaji, sio mwasherati ana mke/mume mmoja, hali rushwa, ana upendo, mtu wa amani, anayemheshimu Mungu na kumpa Utukufu yeye, hajitukuzi yeye, anajali watu wa Mungu, na asiyependa mambo ya ulimwengu huu. Hayo ndiyo matunda ya roho yanayotajwa katika Wagalatia 5:22 ambayo yanapaswa yaonekane kwa Nabii wa Kweli na sio Nabii tu bali hata mchungaji wa kweli, mwalimu wa kweli, askofu wa kweli, shemasi wa Kweli, muimbaji wa Kweli na muumini wa kweli. Na ndio maana Bwana YESU alisema kwa matunda yao mtawatambua..sasa matunda yenyewe ni yapi?. Ndio haya tunayoyasoma katika wagalitia 5:22.

Mtu yeyote anayejiita Nabii asipoonyesha hayo matunda ni ishara mojawapo kuwa tayari ni nabii wa uongo.
Pili nabii wa Kweli anapaswa atoe unabii unaolingana na NENO LA MUNGU au BIBLIA TAKATIFU, Kama vile alivyo mwalimu wa Ukweli, au askofu wa kweli, ni lazima afundishe kitu kinacholingana na Neno la Mungu (yaani Biblia takatifu), Mwalimu yoyote akitufundisha kitu chochote kisichohusiana na Biblia basi huyo atakuwa ni mwalimu wa mambo mengine lakini sio wa Biblia. Kadhalika na Nabii, anapaswa atoe Unabii unaolingana na Biblia, Unabii mwingine utakaotupeleka kwenye mambo mengine yasiyohusiana na Biblia Takatifu basi huyo ni Nabii wa mambo mengine, pengine mwana-mazingaumbwe au Mtabiri wa nyota.

Nabii wa Kweli anapaswa atoe Unabii unaoturudisha sisi kumfahamu sana Mwana wa Mungu (Yesu Kristo) na sio kumfahamu yeye, anapaswa atoe Unabii utakaotufanya sisi tumwamini na kumpenda Yesu, na kuyashika maneno ya Yesu zaidi ya kuyashika maneno yake binafsi, anapaswa atoe Unabii utakaotufanya tuwe watakatifu na kuchukia dhambi, unabii utakaotufanya tutubu dhambi zetu kwa kumaanisha kuziacha, unabii utakaotufanya tuanze kuutafuta ufalme wa Mbinguni zaidi ya mambo ya ulimwengu huu, Unabii utakaotufanya tutazamie mambo ya ulimwengu ujao,Unabii utakaotufanya tumpe Mungu utukufu zaidi ya kumpa yeye utukufu, unabii utakaotufanya tuwe na upendo na tuwe wakamilifu kama Mungu alivyo mkamilifu, Unabii utakaotufanya Tusiabudu Miungu mingine zaidi ya Mungu wa Mbinguni.

Lakini kama Nabii, au Mchungaji, au askofu, au Mwalimu..Hatufundishi, au kutupa Unabii wa Mambo yanayohusiana na mapenzi ya Mungu, hata kama atafanya ishara kiasi gani, hata kamaatatenda miujiza mingi kiasi gani, hata kama anaona maono na yanakuja kutimia kiasi gani..Huyo Biblia imesema ni Nabii wa Uongo na tusimsikilize.

Kumbukumbu 13: 1 “Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,
2 ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;
3 WEWE USIYASIKIZE MANENO YA NABII YULE, AU YULE MWOTAJI WA NDOTO, KWA KUWA BWANA, MUNGU WENU, YUAWAJARIBU, APATE KUJUA KWAMBA MWAMPENDA BWANA, MUNGU WENU, KWA MIOYO YENU YOTE NA ROHO ZENU ZOTE.
4 Tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye.
5 Na yule nabii, au yule mwotaji wa ndoto, na auawe, kwa kuwa amesema yaliyopotoka juu ya Bwana, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, akakukomboa katika nyumba ya utumwa, apate yule mtu kukupotoa katika njia aliyokuamuru Bwana, Mungu wako, uiendee. Ndivyo utakavyouondoa uovu utoke katikati yako”.

Unaona hapo? Kwahiyo Ishara na miujiza sio alama ya msingi ya kumtambua Nabii wa Kweli, alama ya Msingi ya kumtambua nabii wa kweli ni Anaturejeshaje kwenye Neno la Mungu (kuzishika Amri za Mungu zilizopo kwenye biblia takatifu), Nabii akitoa unabii kwamba kesho kutatokea kimbunga cha mvua ya mawe na kweli kesho kimbunga hicho kikitokea kama alivyotabiri, na akasema kwa ishara hiyo Mungu kaniambia watu wote wawaache wake zao, na waume zao, au waongeze idadi ya wake/waume walionao au Nabii yule akasema watu wote wakaasujudie jua kwa siku tatu, biblia inatuonya mtu huyo tusimsikilize; NI NABII WA UONGO, kwasababu Neno la Mungu, linasema Tusiabudu miungu mingine zaidi yake yeye Mungu aliye hai aliyeziumba Mbingu na nchi, aliyeko mbinguni, wala tusisujudie kitu chochote, Kadhalika Biblia inasema “ndoa ni ya mume mmoja na mke mmoja” na amwachaye mkewe na kuoa mwingine azini, Na yeye anatupeleka kwenda kuongeza idadi ya wake, na kufanya uzinzi.

Mfano mwingine, Nabii akatoa unabii fulani na huo unabii ukaja kutimia na akasema Mungu haangalii mavazi anaangalia roho, hivyo wanawake waendelee kuvaa nguo zao wanazovaa siku zote, vimini, suruali,n.k wajipambe kama watakavyo, au anasema Yesu haji leo wala kesho, au anasema Mungu hatawahukumu watenda dhambi na mashoga. Huyo ni wakujitenga naye mbali kwasababu ni Nabii wa Uongo (roho ya Mpinga-kristo inatenda kazi ndani yake), Biblia imekwisha tuonya.

Kwahiyo Ni muhimu kulifahamu Neno la Mungu, na kulishika ili tusidanganyike kwasababu Roho hizi za manabii wa Uongo kipindi hichi cha siku za mwisho ndio zinatenda kazi kwa nguvu zimeachiwa duniani kote,na kuwadanganya wengi yamkini hata wale waliowateule. 
Mungu akubariki.
Ukiwa na swali, lolote unaweza ukatutumia, kwa neema za Bwana tutalijibu na kukutumia. Weka jina lako, na swali lako, tutakutumia kwa njia ile iliyorahisi kwako (inbox, e-mail, au whatsapp.)

No comments:

Post a Comment