Tunasoma Bwana wetu Yesu Kristo alikuwa akizunguka mahali na mahali, kuhubiri injili, kwa marika yote na kwa watu wa aina zote, matajiri kwa maskini, wasafi kwa wachafu, wakubwa kwa wadogo hakuchagua kundi fulani tu! bali alienenda kwa wote..Ikifutufundisha na sisi pia kwamba tunapopeleka injili hatupaswi kubagua kundi fulani… kuna watu hawapeleki injili kabisa kwa maskini, na kuna watu pia hawapeleki injili kabisa kwa matajiri, ..hilo Bwana yeye hakulifanya, kwasababu nia yake yeye ilikuwa sio kutafuta faida fulani bali kutafuta roho za watu.
Lakini tunasoma, alipokuwa anaingia kila mahali, kila mtu alikuwa anamdhania tofauti…alipoingia kwa maskini na wenye dhambi alionekana kama mlevi na mtu asiyekuwa na maana…alipoingia kwa matajiri alionekana anatafuta faida fulani labda fedha kutoka kwao…Lakini nia yake haikuwa kutafuta fedha bali kuwafanya watu watubu wamgeukie Mungu..
Mathayo 9:10-13 “Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake.11 Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?12 Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi.13 Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, NATAKA REHEMA, WALA SI SADAKA; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi”.
Unaona hapo Bwana anasema “NATAKA REHEMA, WALA SI SADAKA;”…Nia ya kuingia kwa watoza ushuru ambao walikuwa ndio matajiri kwa wakati huo sio kutaka fedha au zawadi kutoka kwao, hapana bali kutaka rehema…
kwamba wajione kuwa ni wenye dhambi na hivyo watubu!!.
Wengi wetu tunadhani, Bwana ana haja sana na mali zetu tulizonazo…au ana huzuni sana na umaskini tulionao…Nataka nikuambie ndugu yangu, Bwana haji kwako ili kutaka fedha au kukupa fedha, Bwana anakuja kwako kwa ajili ya roho yako, hauzuniki kwasababu ya umaskini wako wa mwilini bali anahuzunika sana kwasababu ya umaskini wako wa rohoni, ahufurahii sana utajiri wako wa mwilini bali anaufurahia sana utajiri wako wa rohoni…
leo hii anazungumza na wewe hapa!! Ni sawa tu na amekutembelea nyumbani mwako, ANATAKA REHEMA NA WALA SI SADAKA…ndio maana alisisitiza na kusema “nendeni mkajifunze nini maana ya maneno haya”…..sentensi hiyo ina maana kuwa hawakumwelewa nia yake ya kuingia kwenye nyumba za maskini na matajiri…hivyo wanapaswa wakakae chini wakajifunze kwa utulivu, wamwombe na Mungu awafunulie, nia ya Kristo ni nini kuwaendea, vinginevyo wataishia kutokumwelewa maisha yao yote…….. Ndugu Kristo anataka utubu uache dhambi, umgeukie yeye ili akupe uzima wa Milele, hataki sadaka yako, Yeye kila kinatoka kwake,
Anataka roho yako kwasababu kuna hukumu mbeleni inakuja kwa watu wote wasiomcha Mungu, na yeye hapendi mtu yeyote apotee kama maandiko yanavyosema. Kaa chini ujifunze ujue anataka nini kwako.
Mfano mwingine tunaweza kujifunza ni wakati Bwana anaingia kwenye nyuma ya mwanamke mmoja anayeitwa Martha, Martha hakuwa Tajiri alikuwa ni mtu wa kawaida tu, na alikuwa na dada yake anayeitwa Miriamu ambaye alikuwa anaishi naye…Siku moja akasikia Bwana anataka kuja kumtembelea nyumbani kwake…Kama tunavyojua wanawake wataanza kuhangaika huku na kule mambo ya jikoni, mara kusafisha sebule, mara kufagia uwani, mara kupika mboga hii na ile, mara kutengeneza kachumbari n.k n.k unakuta shughuli zinakuwa ni nyingi mpaka wakati mgeni anafika zinakuwa bado hazijaisha…Ndivyo ilivyokuwa kwa Martha alikuwa na shughuli nyingi mpaka Bwana anafika bado zilikuwa hajazimaliza…Na mdogo wake Miriamu alipomwona Bwana kaingia akaacha kumsaidia dada yake kazi na kwenda kuketi miguuni pa Bwana akisikiliza maneno ya uzima, wakati huo Martha bado ana vishughuli shughuli vingi huko jikoni..
Pengine akawa anajaribu kumwonyesha Miriamu viishara fulani atoke pale sebuleni , ili aje akashughulike kule jikoni na wenzake..lakini yeye kakazana kumsikiliza Bwana na maneno yake. Martha akashindwa kujizuia akaanza kuzungumza na Bwana..tunasoma habari hiyo katika …
Luka 10: 38 “Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake.39 Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake.40 Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie.41 Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi;42 lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa”.
Unaona jibu la Bwana hapo??...wengi hata mimi ningeweza kusema Bwana angemkemea Miriamu kwa uvivu..lakini haikuwa hivyo kwa Bwana badala yake alimsifia mbele ya dada yake Martha…Neno ni lile lile.. “Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, NATAKA REHEMA, WALA SI SADAKA”… Bwana hatafuti chakula kizuri, wala maandalizi mazuri, wala sadaka za mtu, wala huduma ya mtu, wala hapendezwi sana na sifa za mtu anazompa zaidi ya Rehema, anataka Toba!! Anataka uzima wa rohoni wa mtu, Hicho ndio cha kwanza anachokihitaji!...kwa ufupi laiti Martha angeanza kwanza kwa kukaa chini na kumsikiliza maneno yake, ndipo baadaye ampikie yeye na wanafunzi wake ingekuwa sawa…lakini yeye alitanguliza huduma kabla mtoa huduma hajatoa huduma yake..na matokeo yake alimwambia “unahangaika na kujisumbua kwa mambo mengi na wakati linalohitajikwa kwa sasa ni limoja tu REHEMA!”..Kaa chini kwanza sikiliza maneno ya uzima na hayo mengine yatafuata baadaye.
Ndugu yangu jifunze ni kitu gani Kristo anataka kwako. Usihangaike, wala usihangaishwe na kutoa sadaka wakati maisha yako ni machafu, ni kupoteza muda tu!! Kristo hajaja kukitafuta hicho kwako, usijisumbue kuhakikisha hukosi kutoa fungu la kumi kila siku na hali ndani ya moyo wako kumejaa kutokusamehe, kumejaa usengenyaji,kumejaa rushwa, kumejaa uasherati, kumejaa ulevi, anasa, pornography, ndani ya moyo wako kumejaa kutokujisitiri, kumejaa masturbation, kumejaa ibada za sanamu na miungu, kumejaa safari za waganga, kumejaa wivu na mambo yote mabaya.. Usijaribu kumfanyie yeye huduma kabla yeye hajakufanyia huduma…utaishia kumhuzunisha badala ya kumfurahisha, anachotaka kwako kwanza ni moyo safi…hiyo ndiyo sadaka ya kwanza anayoikubali mbele zake, Ndio maana Bwana aliwakemea mafarisayo kwa mambo hayo hayo..
Mathayo 23:23 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache”. 24 Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia.
25 Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi.
26 Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi”.
Usitafute kufunga siku nyingi, au miezi mingi…wakati ndani yako hujataka wala kukusudia kuacha dhambi (kusamehe wale wote waliokukosea na mambo mengine yote)..hiyo siyo saumu Bwana anayoitaka..swaumu Bwana anayoitaka ni hii…
Isaya 58: 3 “Husema, Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu.4 Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu.5 Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana?6 JE! SAUMU NILIYOICHAGUA, SIYO YA NAMNA HII? KUFUNGUA VIFUNGO VYA UOVU, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?7 Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe?8 Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde.9 Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu;”
Ni maombi yangu Bwana atakujalia kuyafahamu hayo na zaidi ya hayo na kuyatendea kazi. Kama hujampa Bwana maisha yako kikweli kweli, mlango upo wazi lakini sio siku zote, njia ya mlango huo inazidi kuwa nyembamba kwa kadri siku zinavyozidi kwenda, njia hiyo inazidi kusongwa siku baada ya siku, jana ilikuwa rahisi kwako kuokolewa kuliko leo na itafika wakati njia itakuwa nyembamba mpaka hakutakuwa na nafasi tena ya kupita na mlango utafungwa..
Hivyo ni vyema unapoyasikia haya leo uzingatia kumrudia Mungu wako kwa kutubu na kumaanisha kuacha dhambi zako..na maisha ya kale uliyokuwa unaishi yasiyompendeza Mungu, na Bwana atakusamehe na kukukaribisha kwake. Na baada ya kutubu katafute ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako (Matendo 2:38), huo ni muhimu sana, kila aliyeamini alizingatia kubatizwa. Na baada ya hapo Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu, atakayekusaidia kushinda dhambi na kukutia katika kweli yote ya kuyafahamu maandiko. Na kwa kufanya hivyo utakuwa na uhakika wa uzima wa Milele.
Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na Bwana atakubariki!
No comments:
Post a Comment