Zipo karama tofauti tofauti zilizogawanywa na Bwana katika kanisa, hizo tunazisoma katika kitabu cha 1 Wakoritho 12:4-12
4 “Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.5 Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule.6 Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.7 Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.8 Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule;9 mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja;10 na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha;11 lakini kazi hizizote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.12 Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo.”
Vipawa vyote hivi Mungu hugawa kwa jinsi apendavyo yeye..hakuna mtu anayechagua awe hivi au vile, hicho huwa mtu anazaliwa nacho Mungu anakishusha juu yake yeye mwenyewe.
Na vipawa vimegawanyika katika sehemu mbili, mwilini na rohoni, vipawa vya mwilini vinapimwa katika … nguvu,ushupavu, wepesi,akili, uzuri, mbio, uwezo Fulani wa kipekee katika michezo au darasani, uchoraji, au uandishi, ubunifu, au uimbaji, wengine uongozi, wengine ualimu, n.K kuna maelfu ya vipawa hivi na kila mtu anacho cha kwake…na wakati mwingine sio lazima mtu akijue kipawa chake anaweza akawa anakifanya hata pasipo yeye kujijua…Pia wengine wamepewa viwili viwili, wengine kimoja wengine vitano..Mungu ndiye agawaye jinsi apendavyo..
Lakini leo hatuzungumzii vipawa hivyo vya mwilini tutazungumzia vipawa vya rohoni, kama tunavyosoma katika kitabu hicho cha 1 Wakorintho 12..Kumbuka vipawa vya rohoni pia mtu anakuwa anazaliwa navyo, kama tu vipawa vya mwilini, isipokuwa kama mtu hajampa Kristo maisha yake kipawa kile kinaweza kuzimwa na shetani au shetani akakitumia kwa manufaa yake mwenyewe.
Kwamfano mtu anaweza akawa amezaliwa na kipawa cha unabii, lakini kwa kuwa maisha yake ya utotoni hayakuwa ya kikristo au wazazi wake sio wakristo, au wamemweka wakfu katika madhabahu za miungu, sasa kwa kuwa shetani anakuwa na hati miliki naye asilimia 100, basi anakuwa na uwezo wa kuizima ile karama isifanye kazi yoyote…ndio hapo baadaye mtu akishakuja kumpa Kristo maisha yake na kubatizwa anajikuta anaanza kuona maono n.k ambayo hapo kwanza alikuwa hayaoni, sasa, hiyo karama sio kwamba aliipata baada ya kumpa Kristo maisha yake, hapana bali alikuwa nayo tangu alipozaliwa, isipokuwa shetani alikuwa ameizuia. Au pia shetani anaweza asiifukie bali anainyakua na kuitumia kupitisha maono yake ya uongo, mara nyingi watu wa namna hiyo wanaishia kuwa waganga wa kienyeji,wenye roho za utambuzi.
Mwingine unakuta amezaliwa na karama fulani ya uongozi, lakini kwasababu bado hajampa Kristo maisha yake, shetani anaweza akaifukia ile karama, au akaitumia kwa mambo yake, ndio hapo unakuta mtu anakuwa ni kiongozi wa vikundi haramu, au kiongozi wa mambo maovu…Na siku anakuja kumpa Kristo maisha yake kikamilifu anajikuta anachukia zile kazi mbovu na kutafuta uongozi katika kazi za Mungu, ndio hapo unakuta anaenda kuwa Mchungaji, au Shemasi n.k.
Na karama nyingine za rohoni ndio hivyo hivyo kama uimbaji, imani, uinjilisti, ualimu,uponyaji, lugha n.k. Ndio maana kuna umuhimu sana wa Mtu kumpa Yesu Kristo maisha yake na kuzingatia ubatizo sahihi ili Roho Mtakatifu apate nafasi ya kumsafisha maisha yake na kufufua kile kipawa alichokiweka ndani yake.
Sasa wapo wengi wanapenda kujua karama zao, utasikia mtu anakwambia nitaijuaje karama yangu?..mimi sijui karama yangu? Nimejaribu kumwomba Mungu anionyeshe hajanionyesha, nimefunga sana na kusali bado sijaijua n.k
Nitaka nikuambie ndugu, karama yako hutaijua kwa kuichunguza chunguza, wala Mungu hatakwambia una karama hii wala ile, ni mara chache sana Mungu mwenyewe ndio anamwambia mtu karama yako ni hii au ile, wengi wanajipachikia karama kwasababu tu wanaipenda ile karama, lakini karama ya rohoni Mungu anampa kila mtu kwa jinsi anavyotaka yeye sio kwa jinsi anavyotaka mtu. Toa kabisa kwenye akili yako hiyo karama unayodhania ni yako, kwasababu inawezekana ikawa sio yako.
Namna ya kuifahamu karama yako ni rahisi sana…Kwanza kanuni ni ile ile, kumpa Yesu Kristo maisha yako kikamilifu, ikiwa na maana kumwamini Bwana Yesu Kristo kwa ufunuo wa Roho kuwa ni Mwokozi wa Maisha yako,na kwamba alikufa na akafufuka na akapaa mbinguni, na pia anaweza kukuokoa na wewe na kukufanya kiumbe kimpya.
kisha baada ya hayo ni kufuata maagizo yake ya kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo, upate ondoleo la dhambi zako na kuzingatia kuishi maisha matakatifu kuanzia huo wakati na kuendelea…Kwa kufanya hivyo utakuwa umeweza kujinasua kutoka kwenye nguvu za giza ambazo zilikuwa zimeshika karama Mungu aliyokuwa amekuwekea ndani yako.…kumbuka shetani hataki ujue karama uliyo nayo kwasababu anajua itamletea madhara makubwa sana katika ufalme wake wa giza..Kwahiyo kitu cha kwanza hatakutumia wachawi wakuloge hapana! Ondoa kabisa hiyo akilini. Bali atakutumia mapepo yatakayohakikisha wewe humpi Kristo maisha yako kikamilifu. Au yatakayo kufanya usisimame imara kwa Mungu. Mapepo YATAKAYOKUFANYA USIMWELEWE YESU KRISTO NI NANI ili yapate uhakika kuwa hutakaa uijue karama yako daima.
Pili baada ya kuzaliwa mara ya pili kwa kumpa Kristo maisha yako, bado usianze kujichunguza chunguza karama yako ni ipi…Subiri!! Usianze kusema aa labda mimi ni mchungaji, au mwalimu au nabii…usifanye hivyo hata kidogo!!! Unachotakiwa kufanya ni kwenda kujiunga na kikundi cha wakristo wenzako kanisani, au mahali unapoishi, au popote pale…kile roho anachokusukuma kukifanya pale kwenye lile kusanyiko pasipo kumwiga mtu mwingine, wala pasipo kusukumwa wala kushuritishwa kifanye hicho…na kama kinakupa amani, na endapo ukijaribu kukiacha kukifanya kinakukosesha raha..hicho hicho kifanye, msukumo huo usiuzimishe endelea nao huo huo…
Baada ya muda Fulani, labda mwezi, au mwaka, au miaka kadhaa Bwana mwenyewe atakufunulia…na atakufunulia kwa namna hii: utaanza kusikia watu wanaanza kukuita mchungaji, au wengine wataanza kukufata na kukuomba uwaongoze katika sala au katika uimbaji…au wengine wataanza kukwambia tunaomba utuombee ukiona watu wengi wanakufuata hata usiowajua wanakuomba uwaombee ni kwasababu hapo nyuma wamekuona kwa muda mrefu kila ukiombea watu wanapona..Hivyo kwa kupitia hao unajua Bwana kakupa karama ya UPONYAJI.
Wengine watakuja wakikuomba uwaongoze katika kuabudu na kusifu, utaona mara kwa mara wanakutaka wewe ufanye hivyo, ni kwasababu wameona kila unapowaongoza kwenye sifa na kuabudu uwepo wa kipekee unashuka juu yao, uponyaji unatokea, faraja zinatokea, na watu wanageuka maisha yao..kwahiyo kwa kupitia hao unajua Bwana kakupa karama ya UIMBAJI.
Wengine watakuja na kukuomba uwaulizie Neno kutoka kwa Bwana, ni kwasababu wamekuona muda mrefu unatoa unabii na unakuja kutimia,unaona maono mara kwa mara nayo ni ya kweli, kwahiyo wakajua lazima utakuwa ni nabii…hivyo kwa kupitia hao ndio utajua kuwa Bwana kakupa karama ya kinabii.
Wengine utaanza kuona wanaanza kukuita mwinjilisti..ni kwasababu wameona mazao mengi uliyoyaleta kwa Kristo katika kuhubiri kwako, tofauti na wengine, hata kama watahubiri kutwa kuchwa, hawawezi kulinganisha na uinjilishaji wako unaoweza kuwavuta watu haraka kwa Kristo. na kama ukiwachunguza utaona hawakuiti hivyo kama kwa kujipendekeza kwako au kwa kutaka kukupa sifa bali utaona ni kama kwa kumaanisha hivi.… kwahiyo hapo utaelewa kwamba Bwana alikuchagua kabla ya kuzaliwa uwe mwinjilisti wake kwa kazi yake maalumu, ya kuvuna roho za watu na kusafisha ghala la shetani.
Wengine watakuja na kukwambia tunaomba utufundishe, ni kwasababu hapo nyuma wamekuchunguza kwa muda mrefu wakajua ukiwafundisha wewe wanaelewa zaidi kuliko mwingine ndio maana wanakufuata uwafundishe, kwahiyo kwa kupitia hao unajua Bwana kakupa karama ya UFUNDISHAJI au UELEKEZAJI.
Wengine watakufuata na kukwambia tunaomba ushauri, utashangaa kila anayekufuata hataki kuombewa, wala kuwekewa mikono hata kama anatatizo kubwa kiasi gani, anataka tu umshauri, anataka tu kukusikiliza umweleze njia impasayo akitoka huyu anakuja mwingine..ujue kwamba wamekuchunguza kwa muda mrefu na kujua kwamba wewe una Hekima..Hivyo wamepata mahali panapostahili..kwahiyo kwa kupitia hao utagundua umepewa karama ya NENO LA HEKIMA. Kwaajili ya kuwajaza hekima watoto wa Mungu.
Wengine watakufuata, wengi tu hawataki kuombewa wanataka faraja tu, na wanakufuata wewe tu, hawaendi hata kwa wachungaji wala manabii, wanakutaka wewe tu, ujue ni kwasababu wameona Maneno ya faraja ndani yako…kwa kupitia hao utajua kuwa kakupa karama ya FARAJA ndani yako. Hivyo ile silaha ya Bwana katika kuwaganga wale waliovunjika mioyo imo ndani yako.
Na karama nyingine zote ndio hivyo hivyo, utazijua kutokana na ushuhuda wa watu, wanakushuhudia wewe ni nani? Mtu hawezi kwenda kwenye duka la madawa kununua unga wa ngano, au hawezi kwenda hardware kununua dawa ya meno kila duka na bidhaa za aina yake..wateja ndio watakaosema pale utapata hichi, na pale kile…Usitafute kujipachikia karama kwa kujitazama au kwa kutafuta sifa Fulani au kwa kuona kwasababu karama ile inapendwa na wengi ngoja na mimi nijipe. Huko ni kujikweza ambapo Bwana Yesu alisema ajikwezaye atashushwa na ajishushaye atakwezwa.
Kila mmoja Mungu kamuumba na upekee wake, sio lazima sauti yako ifanane na ya Yule, kuhubiri kwako kuwe sawa na kwa Yule, hata Mungu japo alituumba kwa mfano wake, lakini lakini alimpa kila mmoja sura yake tofauti japo wote ni wanadamu. Vivyo hivyo na katika karama zake, alimpa kila mmoja wetu karama tofauti na hata ikitokea wawili au watatu au mia wanakarama moja, basi biblia inasema upo utofauti wa utendaji kazi, utendaji kazi wa huyu hauwezi ukawa sawa na wa Yule kwamba kila kitu wafanane hapana ukiona hivyo basi ujue ipo roho ya ufuasi nyuma ya huyo mtu.
Na lengo la hizo karama za rohoni ni tofauti za zile za mwilini, karama za mwilini nyingi zina lengo la kumpatia mtu riziki au kumfanya aishi katika dunia hii, au kumpa Mungu utukufu, mtu anakuwa na kipaji cha kukimbia ili akimbiapo apate tuzo itakayokuwa kama ni sehemu yake ya kupatia kipato, lakini karama za rohoni hazipo kwa lengo hilo…karama zote za rohoni ni kwa kusudi la kulijenga kanisa, kuwafanya watakatifu wawe wakamilifu, na kuwahudumia roho zao, na zote zinakuwa na lengo moja la kuwasafisha watu na kuwatengeneza kwa ajili ya kwenda mbinguni.
Kwahiyo ukiona msukumo wowote ndani yako unakuja kwa lengo la kwenda kujipatika kipato! Hiyo siyo karama ya Roho Mtakatifu, achana nayo ni kutoka kwa Yule mwovu. Karama za Mungu ni kwaajili ya kuujenga mwili wa Kristo na kuwatengeneza watakatifu. Utauliza hilo tunalipata wapi katika maandiko..soma.
Waefeso 4.11”Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;
12 KWA KUSUDI LA KUWAKAMILISHA WATAKATIFU, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;
13 hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;
14 ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu”
Na Karama ambayo shetani anapenda sana kuwanasa watu wengi ni karama ya kinabii na uimbaji.. Hizi karama mbili ndizo karama ambazo shetani anajua watu wengi wanazipenda, wengi wanapenda kuitwa nabii nabii na wengi wanapendwa kuitwa waimbaji maarufu…. Kwasababu wanapenda umaarufu pamoja na fedha..nataka nikuambie ndugu yangu, asilimia kubwa ya wanaoimba miziki inayoitwa ya injili na manabii…ni waimbaji wa uongo na manabii wa uongo..
Kwanini ni manabii wa uongo na waimbaji wa uongo?? Jibu lipo hapo juu kwenye waefuso 4:12…je! WANAWAKAMILISHA WATAKATIFU??...au wanawaharibu watakatifu kwa mavazi yao na mienendo yao, na mafundisho yao?? JE! WANATUFIKISHA KATIKA CHEO CHA KIMO CHA UKAMILIFU WA KRISTO??...au wanatupeleka katika cheo cha kimo cha kumfahamu shetani? Wanachoimba na wanachokiishi kinawafanya watu watubu, au kuwafundisha watu chuki?
Ni matumaini yangu kuwa Bwana atakujalia kuyafahamu haya na zaidi ya haya. Na hatimaye kuifanya kazi yake kwa uaminifu katika Karama sahihi aliyoiweka ndani yako.
Mungu akubariki.
No comments:
Post a Comment