"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, January 29, 2019

MAOMBI YA YABESI.


Shalom mwana wa Mungu, karibu tujifunze habari njema za Yesu Kristo ziletazo tumaini la maisha yetu ya sasa na ya baadaye. Leo tutajifunza habari za mtu mmoja anayeitwa Yabesi, Pia tutaona jinsi alivyomwomba Mungu kwa bidii na dua yake kusikiwa. Habari hizo tunazisoma katika kitabu cha 1Nyakati 4:9-10, Tusome.

“Naye Yabesi alikuwa mwenye heshima kuliko nduguze; na mamaye akamwita jina lake Yabesi, akisema, Ni kwa sababu nalimzaa kwa huzuni.
10 Huyo Yabesi akamlingana Mungu wa Israeli, akisema, Lau kwamba ungenibarikia kweli kweli, na kunizidishia hozi yangu, na mkono wako ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda na uovu, ili usiwe kwa huzuni yangu! Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba. “(1Nyakati 4: 9).
Yabesi kama tunavyomsoma hapo, mwanzo wa maisha yake haukuwa mzuri kabisa, inawezekana yeye alikuwa mtoto ni wa mwisho kati ya ndugu zake, na wakati alipokuwa anazaliwa kama biblia inavyotuambia mama yake alikuwa katika hali ya huzuni nyingi, pengine alikuwa anapita shida za kiafya hatujui, au pengine kiuchumi, au pengine wakati Yabesi anazaliwa mama yake alikuwa katika misiba mizito ya kufiwa na ndugu zake, yote hayo yanawezekana. Hivyo kutokana na kuwa katika hali ile ya huzuni nyingi jambo hilo lilimfanya aione mimba ya Yabesi kuwa ni tofauti na za watoto wake wengine aliowazaa, pengine wale wangine aliwazaa katika furaha, katika mafanikio, hakuugua sana, aliletewa zawadi nyingi, tofauti na kwa huyu Yabesi, ni wakati wa huzuni na majonzi tu! na ndio hiyo ikampelekea hata kumpa mtoto wake jina la Yabesi. Ikiwa na maana ya HUZUNI.

Na unafahamu zamani zile mfano mtu akipewa jina ni lazima libebe maana kubwa sana juu ya maisha yake ya baadaye. Hivyo Yabesi kuitwa lile jina iliashiria kuwa maisha yake yote yatakuja kuwa ni maisha ya huzuni, uchungu, mtu wa kulemea wengine, mtu wa nuksi na mikosi, tabu, majonzi n.k. Hakuna mtu aliyeweka tumaini lolote jema la Yabesi mbeleni.. Lakini Yabesi aliendelea kukua na hilo jina akiona kuwa hakuna mtu mtaani kwao aliyeitwa kwa jina kama hilo. wakati watoto wengine wanaitwa majina mazuri kama Furaha, Amani, Upendo, Tumaini, Faraja, Godbless, Neema, Rehema n.k. yeye anaitwa, huzuni, msiba, Matatizo, masumbuko, shida, tabu, majuto. Hilo lilimwingia sana moyoni mwake, pengine lilimpa mawazo mengi maishani kufikiri juu ya hatma yake itakavyokuwa, kuwa atakuwa mtu wa huzuni siku zote za maisha yake.

Lakini tunaona biblia inatuambia Yabesi alikuwa na heshima kuliko ndugu zake wote. Aliwazidi wote kwa tabia njema, japo wengine walimwona kuwa ni mtu wa laana tu lakini yeye aliona njia pekee ni ya kutafuta kibali machoni pa Mungu na katika maneno ya watu. Ndipo akaanza kuutafuta uso wa Mungu kwa bidii na kuanza kumuomba dua hizi akisema..

” Lau kwamba ungenibarikia kweli kweli, na kunizidishia hozi yangu, na mkono wako ungekuwa pamoja nami, NAWE UNGENILINDA NA UOVU, ILI USIWE KWA HUZUNI YANGU!”
Unaona alikuwa anautafuta uso wa Mungu alikuwa anatafuta kufanya mapenzi ya Mungu, na biblia inatuambia “Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba.”.. Bwana anasema ni baba yupi mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe, au akimwomba samaki atampa nyoka?..Yabesi alimlilia Mungu na Mungu akasikia dua zake, alimjalia kutanuka kwa himaya yake kama alivyoomba, hata zaidi ya ndugu zake Mungu alimjali kutembea naye wakati wote kama alivyomwomba. Lakini kikubwa zaidi tunaona alichomwomba Mungu ambacho kingeweza kuiondoa ile laana yake ya nyuma ni “Mungu amlinde na UOVU”.
“NAWE UNGENILINDA NA UOVU, ILI USIWE KWA HUZUNI YANGU!”. Unaona ? Alifahamu jambo ambalo litakaloweza kuifanya ile laana iwe na nguvu juu yake ni UOVU tu!. Na ndicho alichomwomba Mungu amwepushe nacho, hivyo Mungu akahakikisha anamlinda na Uovu siku zote za maisha yake.Alijua kuwa jambo ambalo litakaloweza kumfanya awe na majuto katika maaisha yake ni OUVU, jambo ambalo litakalomfanya awe na masikitiko, masononeko, bahati mbaya, nuksi, mikosi, tabu, sio mambo aliyotamkiwa huko nyuma, sio majina ya kuzimu aliyoitwa huko nyuma, sio maneno ya laana aliyoambiwa na watu, bali ni Uovu utakaokuwa ndani yake. Na ndio maana Yabesi alijitunza sana tangu zamani, akawa na heshima kuliko ndugu zake zote, heshima inayozungumziwa hapo sio heshima ya kutii watu tu peke yake hapana, bali ni heshima iliyojumuisha vyote, alijiheshimu yeye mwenyewe kwanza kwa kila kitu katika matamshi yake, mwenendo wake, mwili wake aliutunza, na kazi yake,.Na zaidi ya yote akazidi kumwomba Mungu aendelee kumwepusha na Uovu, hivyo Mungu akamsikia na kumwepusha na hayo yote. Hata na yale mengine pia akamjalia.

Kaka/Dada, mwanzo wako inawezekana ulikuwa mbaya ulizaliwa katika vifungo vya giza pale wazazi wako walipokuweka chini ya maagano ya kiganga na kupewa majina ya mizimu, na hivyo hilo jambo limekuwa likikusumbua sana, inawezekana maisha yako ya nyuma yalikuwa ni mabaya sana, mwenendo wako ulikuwa hauvutii, hata mbele za watu wanaokuzunguka, mpaka imefikia hatua ya kupewa majina mabovu, huko mtaani unajulikana kama kibaka, au muhuni, jambazi, au kahaba fulani, au shoga, au teja.. wakati mwingine umelaaniwa na wazazi wako na unajiona wewe hufai tena, au ulipewa majina yasiofaa au ulirithishwa. Nataka nikuambie usiogope! ikiwa utaamua kuanza maisha yako upya sasa kwa Bwana, pamoja na laana hizo zote kuambata na wewe zitageuzwa na kuwa baraka, Yabesi alibebeshwa mzigo mzito kama huo lakini baada ya kuamua kuutafuta uso wa Mungu na kufanya UOVU kuwa ni adui yake aliguezwa na kuwa mtu mwingine zaidi hata ya wale waliokuwa wanajiona ni watakatifu mbele za Mungu.

Na wewe leo hii ikiwa utataka kutubu, kwa kumaanisha kabisa kuacha dhambi zako, na kuuchukulia kuwa UOVU ni kama ukoma, ni kama chanzo cha laana hizo zote ulizonazo sasa. Ukiamua kabisa kutoka moyoni kumkabidhi Bwana maisha yako leo, kuanzia sasa na kuendelea,kisha ukaenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kimaandiko ambao ni wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO, kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako kama ishara ya kusafishwa makosa yako kwa damu ya Yesu Kristo iliyomwagika pale msalabani. Basi Kuanzia huo wakati ndipo Bwana atakapokupa Roho wake mtakatifu kukusaidia kuishinda dhambi, kwa nguvu zako hautaweza, kwasababu hakuna awezaye kuishinda nguvu ya dhambi isipokuwa Roho Mtakatifu peke yake ndani ya Mtu.

Na dua yako utakayomwomba Mungu akulinde na uovu itakuwa na nguvu sana..Utashangaa unaweza kushinda kunywa pombe, unashinda kuvuta sigara na madawa ya kulevya, unashida uasherati, na ushoga, unashinda pornography, masturbation,unashinda ukahaba,wizi, unashinda usengenyaji, unaishinda hasira, chuki, wivu, majigambo n.k. Na mwisho wa siku unaitwa mbarikiwa mbele za Mungu na ufalme wa mbinguni unakuwa ni wako.Na yale mengine ya maisha yaliyosalia Bwana atakupa.

Hivyo unapoisikia sauti ya Mungu sasa kubali kuitii, na Mungu atakusaidia.

Ubarikiwe sana.

No comments:

Post a Comment