2 Wakorintho 5: .17 “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.18 Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, ALIYETUPATANISHA sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho;19 yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho.20 Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu.
Kuna sababu kadha wa kadha kwanini
Yesu Kristo Bwana wetu, anajulikana kama Mwana wa Mungu, hiyo ni moja ya sifa
yake kuu..Ingawa yeye alikuwa ni MUNGU katika mwili, lakini hilo halikuwa na
umuhimu mkubwa sana kwetu kulifahamu , kuliko kumfahamu yeye kama mwana wa
Mungu, ndio maana huoni mahali popote akitafuta kujionyesha yeye kuwa ni MUNGU.
Hakutaka hilo, kwasababu hiyo sio sababu kubwa iliyomleta duniani, hakuja
kutafuta kuabudiwa duniani…bali kutafuta kilichopotea. Kama ingekuwa amekuja
kutafuta kuabudiwa kama Mungu, basi angekaa huko huko mbinguni kwenye utukufu
wake angekuwa hana sababu ya kushuka huku duniani kwenye mavumbi..
Raisi anapokutana na familia yake
cheo chake kinabadilika na kuwa Baba na MWANA-FAMILIA na sio raisi tena,
hatamwadhibu mwanawe kwa kutumia vyombo vya dola, bali atatumia fimbo kama
ikiwezekana, na Yesu Kristo alivyokuja duniani cheo chake cha kimungu
kilibadilika na kuwa MWANA. Kwahiyo ilimpasa awe kama mwanadamu, ndio maana watu
wasiomwelewa Bwana YESU wanapinga vikali kuwa yeye sio Mungu, Mungu gani
anakufa? Analia? Anakula na kunya?...Ni kweli kwa kumchunguza tu pasipo kuwa na
ufunuo wa utendaji wake kazi hutaweza kuona uungu wowote ndani yake. Lakini
akikujalia kupata ufunuo utamwelewa vizuri yeye ni nani. ukisoma Wafilipi
2:5-8, pamoja na 1Wakorintho 2:6-8, na Tito 2:13 na Timotheo 3:16, Utapata picha halisi ya kuwa yeye ni nani. Na kwamba
alikuja katika SIRI KUU SANA, ijulikanayo kama Siri ya utauwa..Na biblia
inasema siri hiyo haijulikani kwa kila mtu bali kwa wakamilifu tu peke yao ya
kwamba Kristo YESU ni MUNGU.
Lakini Bwana Yesu alipokuja duniani
alitamani sana sisi tumjue yeye kama Mwana wa Mungu kuliko kumjua yeye kama
Mungu, ndio maana aliwauliza wakati Fulani wanafunzi wake..”watu husema ya kuwa
mimi ni nani?” wakasema wengine Eliya, wengine Yohana mbatizaji, wengine
Yeremia n.k akawauliza na wanafunzi wake, na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni
nani? “PETRO AKAJIBU WEWE NDIWE KRISTO, MWANA WA MUNGU ALIYE HAI.
Unaona? Bwana Yesu alimsifia Petro kwa ule ufunuo
alioupata wa kumtambua Kristo kama mwana wa Mungu..
“Yesu akajibu, akamwambia, HERI wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 16:16-19)Zingatia hilo neno “HERI” Ikiwa na maana kuwa amebarikiwa yeye alifahamuye hilo, unaweza ukajiuliza kwanini Bwana hakumrekebisha Petro na kumwambia hapana! Mimi si mwana wa Mungu, bali ni Mungu mwenyewe niliyekuja katika mwili. Unaona jambo ni lile lile, Yeye anataka tumwelewe ni kitu gani kilichomleta Duniani zaidi ya kuelewa ni kitu gani alichokiacha mbinguni.
Alifanyika kuwa MWANA WA MUNGU, ili
kutuonyesha sisi NJIA ya jinsi mwana wa Mungu anavyotakiwa awe, ili siku
atakapoondoka duniani, sisi tuliosalia kwa kuyaangalia maisha yake, tujifunze
kwake, alikuja kutengeneza njia iliyoharibika..ili kwa kumtazama yeye tuyarekebishe
maisha yetu. Ili yafanane na ya kwake ili nasi tuwe WANA WA MUNGU kweli kweli.
Kama yeye alivyomtegemea Baba nasi tumtegemee Baba asilimia 100, kama yeye
alivyokuwa mtakatifu hata akashuhudiwa mbinguni nasi tuwe hivyo hivyo, kama
yeye alivyovumilia nasi tuvumilie majaribu, kama yeye alivyokuwa na upendo nasi
tuwe na upendo.n.k Hizo ndio tabia za kuwa MWANA WA MUNGU. Sio kusema sisi ni
wana wa Mungu lakini maisha yetu hata kidogo hayafanani na ya kwake, yeye
ametupa kielelezo, kama yeye alivyofanya na kuishi na sisi pia tufanye na
kuishi vilevile kama yeye..
Ni sawa na mwalimu aliyeona
wanafunzi wake hawamwelewi akaamua kuvua cheo chake cha ualimu na kuvaa uniform
za kiuanafunzi na kwenda kuketi pamoja na wanafunzi, na kujifanya yeye ni
mwanafunzi na kusoma nao na kujiweka chini ya changamoto zote za kiuanafunzi
ili tu kuwaonyesha njia bora ya kusoma inavyopaswa na kumwelewa mwalimu
anapofundisha. Ndivyo na Bwana Yesu alivyofanya kuacha enzi na mamlaka kuja
duniani. Ni kutuonyesha tu sisi njia!
Lakini tukiachana na hayo, tunaweza
kujifunza pia sifa nyingine kuu ya KUWA MWANA WA MUNGU, Na sifa hiyo si
nyingine zaidi ya UPATANISHO, Sifa hii ndio iliyobeba kiini cha somo letu leo…
Sasa sababu nyingine kubwa
iliyomfanya Bwana Yesu kuwa mwana wa Mungu na si malaika ni KUTUPATANISHA SISI
NA MUNGU. Kumbuka sisi tulikuwa tumepotea dhambini, na tulikuwa tayari wote ni
wa kwenda kuzimu, hakuna hata mmoja wetu angepona hata Musa, hata Eliya, hata
Yohana Mbatizaji hata Adamu mwenyewe wote walikuwa ni wakupotea…Lakini kwa
kupitia damu ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu tumepatanishwa na Mungu. Tunakwenda
mbinguni bure endapo tukimwamini yeye na kuyaishi maneno yake.
Hivyo basi ili na sisi tuwe wana wa
Mungu ni lazima tuwe wapatanishi kama yeye. Utauliza? Na sisi kwahiyo inatupasa
tumwage damu kama yeye?? Jibu! Damu ya Yesu inatosha!
ilishamwagika mara moja, lakini
alitupa kielelezo kama yeye alivyotufanyia sisi na sisi tuyafanye kwa wengine,
kwahiyo ndio wakati mwingine kama inabidi inatupasa na sisi kumwaga damu au
kutoa uhai wetu kwaaajili ya wengine..maandiko yanasema hivyo katika kitabu cha
1 Yohana 3:16” Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake
kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu” HUO
NDIO UPATANISHO, Na kwa kufanya hivyo tutaonekana tumekuwa WANA WA MUNGU,kwa
macho yakimbinguni, tutafananishwa na MWANA WA MUNGU,Yesu Kristo aliyetoa uhai
wake kwa ajili yetu. Biblia inasema katika kitabu cha Mathayo..
Mathayo 5:9 “HERI WAPATANISHI; Maana
hao WATAITWA WANA WA MUNGU”
Upatanishi unaozungumziwa hapo juu,
sio kuwapatanisha watu wanaogombana au watu waliokosana hapana! Bali kujitoa kwa
hali na mali kwa ajili ya kuwapatanisha watu na Mungu wao, KWA KUWAPELEKEA
HABARI NJEMA za wokovu na hata kugharimika kufa, ilimradi tu umpatanishe mtu na
Muumba wake, kama Bwana Yesu alivyofanya. Maandiko yanasema..
Umeona hapo? Ndugu…Kristo,Mwana wa Mungu alitupatanisha sisi na Mungu ndio maana akaitwa Mwana wa Mungu, kwasababu heri walio wapatanishi hao wataitwa wana wa Mungu, na sisi Bwana ametupa huduma ya upatanisho..Ndiyo haya maneno yanayosema nawe sasa,…kama maandiko yanavyosema hapo katika mstari wa 20 “KANA KWAMBA MUNGU ANASIHI KWA VINYWA VYETU; twawaomba ninyi kwa ajili ya KRISTO MPATANISHWE NA MUNGU.”2 Wakorintho 5: 17 “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.18 Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, NAYE ALITUPA HUDUMA YA UPATANISHO;19 yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; NAYE AMETIA NDANI YETU NENO LA UPATANISHO.20 Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, KANA KWAMBA MUNGU ANASIHI KWA VINYWA VYETU; twawaomba ninyi kwa ajili ya KRISTO MPATANISHWE NA MUNGU.
Biblia inakusihi ndugu unayesoma
ujumbe huu ambaye hujawa kiumbe kipya bado, ambaye ni vuguvugu katika imani,
ambaye bado unaupenda ulimwengu, ambaye bado hujaacha anasa, wala usengenyaji,
wala ulevi, wala tamaa mbaya…inakuomba upatanishwe leo na Mungu.
Mgeukie yeye leo ukanywe maji ya
uzima, kama Bwana mwenyewe alivyosema katika Ufunuo 22:17 “Naye mwenye kiu na
aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure.”..Ni bure kabisa
yanapatikana…Utafika wakati haya maji hutayapata bure wala kwa fedha, yatakuwa
hayapo…Na unajua madhara ya kukosa maji ya uzima baada ya kifo??..ni mabaya
sana usitamani uyakose huko.
Kama hujatubu dhambi zako, bado
hujachelewa, mwambie Bwana akusamehe, mahali popote ulipo, jitenge peke yako
kwa muda kisha tubu! Mwambie Bwana kuanzia leo unahitaji kuwa kiumbe kipya,
unahitaji kupatanishwa naye, wewe mwenye dhambi na kama umemaanisha kufanya
hivyo yeye “anakubali wakosa” atakusamehe na atakupa amani ya ajabu moyoni
mwako, hiyo amani ndio uthibitisho wa kusamehewa dhambi zako, na bila kupoteza
muda haraka sana nenda katafute ubatizo sahihi wa kimaandiko, wa maji mengi na
kwa JINA LA YESU KRISTO(kulingana na Matendo 2:38) ili dhambi zako ziondoke
kabisa kabisa, Baada ya kufanya hivyo Bwana Yesu Mwenyewe atakupa kipawa cha
Roho wake Mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi na kuilewa biblia vizuri..
Kwa kukamilisha hatua hizo utakuwa
umezaliwa mara ya pili na kuwa kiumbe kipya…kama maandiko yalivyosema hapo
juu..” MTU AKIWA NDANI YA KRISTO YA KALE YOTE YAMEPITA TAZAMA YAMEKUWA
MAPYA”..Bwana mwenyewe atayafanya mapya maisha yako kwa kila NYANJA!
Mungu akubariki sana…Na kama tayari
ulishakuwa ndani ya Kristo, yaani umeshazaliwa mara ya pili, Neno linasema
TUMEPEWA HUDUMA YA UPATANISHO, hivyo ni wajibu wako pia kwenda KUWAPATANISHA
WENGINE NA MUNGU WAO, yaani kwenda kuwaambia habari za Neema zilizopo ndani ya
Yesu Kristo na Raha na Tumaini, na toba!. Huo ndio uthibitisho wa kuwa kweli
umefanyika kuwa mwana wa Mungu, kumbuka Neno hili “heri wapatanishi maana hao
wataitwa wana wa Mungu”.
Ubarikiwe sana.
Tafadhali “share” ujumbe huu kwa
wengine,
No comments:
Post a Comment