"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, February 16, 2019

MJI WENYE MISINGI.


Ibrahimu tunamwita ni Baba wa Imani, kutokana na Imani tunayoiona aliyokuwa nayo kwa Mungu wake licha ya kukaa kwa muda mrefu bila kupata mwana Mungu aliyekuwa amemuahidia akizingatia na huku umri umeshakwenda yeye na mke wake, hakukata tamaa kumwamini Mungu badala yake aliendelea kusubiria mpaka Mungu alipotimiza alichomuahidia na hata alipopata mwana, zaidi ya yote tunasoma katika uzee ule Mungu alimjaribu tena amtoe mwanawe kuwa sadaka ya kuteketezwa, Nalo hilo Ibrahimu halikumtikisa bali alidhubutu kumtoa, ndipo Mungu akavutiwa sana na Imani ya Ibrahimu..

Lakini hilo pekee tu pekee lingetosha Mungu kumfanya Ibrahimu kuwa baba wa imani na mtu wa kuigwa kwa vizazi vyote? Watu watakaokuja kumwamini yeye baadaye?..Lipo jambo lingine la ndani zaidi tunapaswa tulijue ambalo ndilo tutaligusia siku ya leo.
Tukisoma kitabu cha Waebrania tunapata kuona tabia nyingine tofauti ambayo Ibrahimu aliionyesha kwa Mungu wake. Tunasoma:
Waebrani 11:8 “Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako.
9 KWA IMANI ALIKAA UGENINI KATIKA ILE NCHI YA AHADI, KAMA KATIKA NCHI ISIYO YAKE, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.
10 Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu”.
Sasa ukiyachunguza hayo maandiko kwa makini utaona kuwa Ibrahimu alikuwa na jicho lingine la mbele zaidi hata ya lile alilokuwa ameahidiwa na Mungu katika mwili..Na ndio maana siku zake zote maisha yake yote hakusumbuliwa na mambo yanayopita, hukusumbuliwa na kukawia kwake kupata mtoto,hakusumbuliwa na hata kutoa mwanawe Isaka kuwa sadaka kwa Mungu wake…

Embu Soma tena hapo anasema. 9 KWA IMANI ALIKAA UGENINI KATIKA ILE NCHI YA AHADI, KAMA KATIKA NCHI ISIYO YAKE,..Kumbuka Mungu alimtoa Ibrahimu nchi ya mbali sana huko Uru ya Ulkadayo na kumleta Kaanani, mahali ambapo Mungu alimwahidia kumpa kila kitu ambacho ni chema, alimwahidia kuwa atamfanya kuwa taifa kubwa sana, atamfanya kuwa uzao hodari, uzao ambao utamiliki malango yote ya adui zake wote..Atamfanya kuwa taifa tajiri, na lenye nguvu sana..

Sasa embu jaribu kutengeneza picha ingekuwa hiyo nafasi umepewa wewe, Mungu anakuambia utakuwa na uzao hodari katika nchi fulani na kwa kupitia wewe mataifa yote duniani yatabarikiwa, hivi utajisikiaje?...Ni wazi kuwa utajiona kuwa ni mtu wa kipekee mbele za Mungu kuliko wengine wote, utatanua mbawa kidogo, utajiona kuwa wewe ni mtu muhimu sana mbele za Mungu kuliko wengine..Hata ukifika katika hiyo nchi Mungu aliyokuahidia utaimiliki pengine kwa kiburi fulani, utaishi kama mfalme fulani au chief fulani hivi kwani Mungu tayari ameshakuridhia na kukupa wewe..hata watu wote wa huo mji wakitaka kupigana na wewe hutaogopa, kwasababu Mungu alishakupa wewe milki hiyo.

Lakini kwa Ibrahimu haikuwa hivyo, alikuwa na jicho la mbali zaidi, hakutazama Baraka hizo Mungu alizomwahidia za kitambo tu, hakutazama wingi wa uzao atakaokuwa nao duniani, hakutazama ukuu wa taifa atakalolizaa duniani, hakutazama utajiri wa kimwilini, kwa hili jicho la kimwilini, bali aliyatafakari maisha yake kwa utulivu sana, akiangalia jinsi Mungu alivyomtoa Nchi ya Ulkadayo na kumleta pale Kaanani, na jinsi Mungu alivyomwepusha katika taabu zote zile, za kungojea nchi ambayo Mungu amemwahidia, akajiuliza kama Mungu anao uwezo wa kunifanya taifa kubwa ndani ya dakika moja, kwanini anakawia hivi kunipa mwana? Sababu nini?..Ibrahimu alitaka kujua kusudi la maisha, nyuma ya haya yote kuna nini?.. Na ndipo akafahamu kuwa maisha yake ni picha ya mambo yatarajiwayo mbeleni yajayo baada ya ulimwengu huu kupita. Alifahamu kuwa maisha yake ni somo, maisha yake ni sauti Mungu anayozungumza naye juu ya mambo ya mbeleni sana..ng’ambo ya pazia..

Na ndio maana tunasoma Ibrahimu licha ya kupewa utajiri wote ule wa kimwilini, bado aliendelea kuishi katika nchi ile ambayo ni kweli ilikuwa ni haki yake kustarehe na kujifurahisha lakini biblia inatuambia aliishi mule kama vile siyo nchi yake, aliishi katika milki yake kama vile sio milki yake, kama vile mgeni nyumbani kwake mwenyewe..aliisha na mke wake Sara kwenye mahema, fikiria Ibrahimu alikuwa ni mtu tajiri sana mwenye mali nyingi alizopewa na Mungu lakini hakuishi kwenye makasri,..hiyo inafunua nini?..Inaonyesha ni jinsi alivyoishi kama mpitaji hapa duniani?.

Unadhani alikuwa hajipendi?. Hapana..Biblia inatuambia ni kwasababu alikuwa anautazama mji ulio bora, alikuwa anautazamia mji wenye misingi, sio ule wa Kaanani aliopewa ambao Mungu kweli alimpa kuwa milki yake, lakini huo ingempasa aweke misingi yeye iliyodhaifu, ingempasa aubuni yeye..Lakini badala yake Ibrahimu hakufanya hivyo bali aliutazamia mji wenye misingi ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu mwenyewe.. Na mji huo si mwingine zaidi ya YERUSALEMU MPYA ya mbinguni HALELUYA!!.

Jambo hilo ndilo lililomfanya Mungu apendezwe na Ibrahimu na kumfanya awe kielelezo cha kuigwa kwa watu wote, ikiwemo mimi na wewe.

Ndugu leo hii, umekuwa ukimsubiria Mungu aje kukufanikisha katika jambo fulani ambalo alikuahidia atakufanyia zamani, au tayari ameshakufanyia, pengine ulikuahidia kukupa mtoto kwa muda mrefu na sasa amekupa, pengine alikuahidi utakapa mali amekupa, ulisubiria nyumba amekupa, ulingojea hiki au kile kwa muda mrefu sasa amekupa, Je! unadhani hayo ndio mapenzi ya Mungu kwako?.

Usipokuwa makini utakuwa unaona kila siku pale Mungu anapokufanikisha katika mambo yako ndio anapendezwa na wewe,ndio mrithi wake, utaona kila unalomwomba anakupa na wakati mwingine hata umetolewa unabii utakuja kuwa raisi, au mtoto wako atakuja kuwa bilionea wa kwanza duniani, Mungu kakuotesha utakuja kuwa kichwa cha ukoo wako mzima, wote wasiokupanda watakuja kukuinamia, ukadhani kuwa hayo ndio mapenzi ya Mungu kwako!!.

Ni kweli Mungu atatimiza Neno lake kwa alichokuahidia,lakini usipokuwa naUFAHAMU kama wa IBRAHIMU, Jua tu siku ile ikifika, hutaingia katika mji ule YERUSALEMU MPYA BIBI-ARUSI WA KRISTO. Siku ile kama Bwana Yesu alivyosema watatoka watu kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni; 12 bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. ( Mathayo 8:11)..Unaona hapo, wataketi na Ibrahimu, na Bwana hawezi kuwaketisha pamoja na Ibrahimu watu wasiofanana na Ibrahimu katika mienendo.

Hiyo Yerusalemu mpya, kwa tafsiri nyingine ni BIBI-ARUSI wa Kristo, yaani watakatifu wa Kristo, sasa sio kila mtu anayejiita ni mkristo atakuwa bibi-arusi wa Kristo, hapana, kama vile biblia inavyosema hawawi wote waisraeli walio wana wa Israeli, Vivyo hawawi wote wakristo, walio wa-kristo. Kuna tofauti kati ya suria na mke, wanawali wenye busara na wanawali wapumbavu, magugu na ngano. kadhalika mbele za Mungu, si kila mkristo ni bibi-arusi wa Kristo, si kila mtu ataujenga YERUSALEMU WA MBINGUNI. Bali ni wale tu waliokamilishwa katika wokovu.
Biblia inatumbia mji huo hakitaingia kilicho kinyonge, wala kidhaifu, ndugu ukiona umekosa tu unyakuo basi ufahamu kuwa wewe si miongoni mwa mji mtakatifu wa Mungu. Ukiona umekosa tu karamu ya mwanakondoo siku ile ya unyakuo basi hali yako ni itakuwa mbaya sana.

Ukisoma kitabu cha ufunuo sura ya 21 utaona ni jinsi gani hawa watu walivyo wa tofauti sana, wenye imani hii ya Ibrahimu, kundi hili dogo sana wanavyofananishwa na uzuri wa mji ule , ulipambwa ushukao kutoka mbinguni kwa Mungu mwenyewe..Watu ambao Mungu amewajenga katika misingi iliyo imara..Na tunasoma misingi yenyewe ni mitume na manabii,(Biblia takatifu) na sio misingi ya pesa na mafanikio..sio misingi ya utajiri na ufahari, sio misingi ya urembo na umaarufu, sio misingi ya elimu ya dunia hii kama wengine wanavyodhani.

Mji huo unaonekana ukiwa na vipimo sahihi kabisa, urefu wake, na mapana yake, na kwenda juu kwake ni sawa sawa, kuonyesha uimara wake na umakini wa ujenzi wake, kuonyesha jinsi ulivyo FITI, kwa vifaa vilivyotumika kuujengea mji huo..jinsi watakatifu hao walivyostahili kwa utakatifu wao kujengwa juu ya misingi ya mitume na manabii (yaani BIBLIA) na sio katika mapokeo ya kibinadamu na madhehebu.

Mji huo unaonekana ukiwa umejaa dhahabu kote, ikiashiria utakatifu wa wateule..Unaonekana ukiwa umepambwa kwa vito vya thamani vya kila namna, ikiwakilisha wito na utumishi tofauti tofauti wa wateule wa Mungu.

Embu tusome kidogo tabia za mji huu..
Ufunuo 21:9 “Akaja mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na vile vitasa saba vilivyojaa yale mapigo saba ya mwisho, naye akanena nami, akisema, NJOO HUKU, NAMI NITAKUONYESHA YULE BIBI-ARUSI, MKE WA MWANA-KONDOO.
10 AKANICHUKUA KATIKA ROHO MPAKA MLIMA MKUBWA, MREFU, AKANIONYESHA ULE MJI MTAKATIFU, YERUSALEMU, UKISHUKA KUTOKA MBINGUNI KWA MWENYEZI MUNGU;
11 wenye utukufu wa Mungu, na mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi, safi kama bilauri;
12 ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu, wenye milango kumi na miwili, na katika ile milango malaika kumi na wawili; na majina yameandikwa ambayo ni majina ya kabila kumi na mbili za Waisraeli.
13 Upande wa mashariki milango mitatu; na upande wa kaskazini milango mitatu; na upande wa kusini milango mitatu; na upande wa magharibi milango mitatu.
14 Na ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.
15 Na yeye aliyesema nami alikuwa na mwanzi wa dhahabu, apate kuupima huo mji, na milango yake, na ukuta wake.
16 Na ule mji ni wa mraba, na marefu yake sawasawa na mapana yake. Akaupima mji kwa ule mwanzi; ulikuwa kama maili elfu na mia tano; marefu yake na mapana yake na kwenda juu kwake ni sawasawa.
17 Akaupima ukuta wake, ukapata dhiraa mia na arobaini na nne, kwa kipimo cha kibinadamu, maana yake, cha malaika.
18 Na majenzi ya ule ukuta wake yalikuwa ya yaspi, na mji ule ulikuwa wa dhahabu safi, mfano wa kioo safi.
19 Na misingi ya ukuta wa mji ilikuwa imepambwa kwa vito vya thamani vya kila namna. Msingi wa kwanza ulikuwa yaspi; wa pili yakuti samawi; wa tatu kalkedoni; wa nne zumaridi;
20 wa tano sardoniki; wa sita akiki; wa saba krisolitho; wa nane zabarajadi; wa kenda yakuti ya manjano; wa kumi krisopraso; wa kumi na moja hiakintho; wa kumi na mbili amethisto.
21 Na ile milango kumi na miwili ni lulu kumi na mbili; kila mlango ni lulu moja. Na njia ya mji ni dhahabu safi kama kioo kiangavu.
22 Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake.
23 Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo.
24 Na mataifa watatembea katika nuru yake. Na wafalme wa nchi huleta utukufu wao ndani yake.
25 Na milango yake haitafungwa kamwe mchana; kwa maana humo hamna usiku.
26 Nao wataleta utukufu na heshima ya mataifa ndani yake.
27 Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.”
Unaona hapo Yohana anaonyeshwa MKE WA MWANAKONDOO ambaye ndiye YERUSALEMU MPYA, na hapo mwisho kabisa anakuambia 21.24 “Na mataifa watatembea katika nuru yake. Na wafalme wa nchi huleta utukufu wao ndani yake”.

Sasa mwisho kabisa Mungu akishamaliza kuujenga huu mji ambao mpaka sasa anaujenga katikati ya watu wake na unakaribia kuisha, hapo ndipo maskani ya Mungu itakapokuwa na wanadamu, Hapo ndipo Mungu atakaposhuka na kukaa katikati ya wanadamu kwenye maskani yake..Na maskani yake ndio huu mji Yerusalemu mpya, ambayo inamwakilisha bibi-arusi kwa Kristo tu peke yake.Hivyo Mungu atakaa ndani ya hawa watu... Hawa watakuwa ni watu wa-kipekee sana mbele za Mungu, kama vile sisi tuwaonavyo malaika, ndivyo itakavyokuwa watu watakaopewa neema ya kuingia kule watakavyowaona hawa bibi-arusi wa Kristo..

Huo ndio mji ambao Ibrahimu alikuwa anautazamia.. licha ya kuahidiwa kuwa taifa hodari duniani hakujisumbua kulitazama hilo kama alivyolingojea hili kwa saburi zote..Swali ni je! Wewe nawe ni miongoni mwa mji mtakatifu wa Mungu ambao Mungu anauandaa sasa?..Yerusalemu mpya, bibi-arusi wa Kristo?..Je! Kristo akirudi leo unao uhakika wa kwenda naye?. Je! unaishi maisha ya kutazama mbinguni, au mambo tu ya duniani?.
 Je! umeoshwa dhambi zako, na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi, kama Neno lenyewe “ubatizo” linavyomaanisha, na kwa jina la YESU KRISTO?. na ikiwa umefanya hivyo vyote je! maisha yako yanauhakisi utakatifu? (Waebrania 12:14), maana biblia inasema hakuna mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao huo.

Ikiwa hayo hayapo ndani yako.. unao muda, sasa mji ule unakaribia kuisha ujenzi wake, fanya bidii uingie kabla mlango wa neema haujafungwa. Ulimwengu huu na mali zisiwe kisingizio siku ile. Kwasababu wapo waliokuwa na mali zaidi yangu na yako na waliokuwa na mafanikio kupita ya Ibrahimu lakini waliishi kama wapitaji tu hapa dunia.
Isaya 35: 8 “Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; WASAFIRIO, WAJAPOKUWA WAJINGA, HAWATAPOTEA KATIKA NJIA HIYO.
Ni matumaini yangu utatubu leo na Bwana akujalie kuishi katika utakatifu na usafi.
Ubarikiwe sana.

No comments:

Post a Comment