"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, February 4, 2019

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 55


 SWALI 1: Je! Kufanya masturbation (Punyeto) ni dhambi?. Na je! Kuoa ni suluhisho la kuzuia tamaa kama biblia inavyosema katika 1 Wakorintho 7:9?.
JIBU: Bwana Yesu alisema amtazamaye mwanamke kwa kumtamani amekwisha kuzini naye nafsini mwake. Sentensi hiyo inaonyesha kuwa dhambi haianzii nje ya mwili bali inaanzia moyoni, hivyo zinaa pia inaanzia moyoni, ikishafanyika moyoni ndipo inatoka nje, kwahiyo chochote kinachofanyika mwilini ni matokeo ya kitu kilichofanyika tayari rohoni, hivyo uasherati, masturbation (punyeto), utazamaji wa pornography hayo yote ni matokeo ya uasherati ambao tayari yalishafanyika ndani ya moyo wa mtu.

Ndio masturbation ni dhambi. Na suluhisho pekee la kuikwepa hiyo dhambi ni kumkabidhisha Bwana Yesu maisha yako ki-kweli kweli, na kudhamiria kuanza maisha mapya katika Kristo, na kuamua KUACHA!! Wengi wanatafuta kuombewa waache kutazama pornography au kufanya masturbation lakini hawajadhamiria kuamua kuacha hivyo vitu,..wanasubiria miujiza ishuke wajikute wameacha na huku bado mioyo yao inaelekea kwenye zinaa…Nataka nikuambie ndugu yangu unayemtafuta Mungu,Hakuna maombi yoyote ya kuondoa hicho kitu ndani ya mtu, ili hivyo vitu viondoke ni kuamua kwanza kuchukua uamuzi wa kuacha hayo mambo ndipo Bwana anakuongezea UWEZO wa kushinda hayo mambo,. Kumbuka na Biblia inasema waasherati wote sehemu yao ni katika ziwa la moto.

Na pia kuhusu kuoa biblia imeweka wazi katika kitabu cha 1 Wakorintho7 :1 “Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke.2 Lakini kwa sababu ya ZINAA kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe”.

Ukisoma kwa makini huo mstari wa 2 anasema kwasababu ya ZINAA kila mtu mwanamume awe na mke wake mwenyewe…sio kwasababu ya KUEPUKA TAMAA…bali kwasababu ya ZINAA…na zinaa maana yake ni kufanya mapenzi nje ya ndoa au kabla ya ndoa, Hii ikiwa na maana kuwa, kuwa na mke hakumzuii mtu kulipuka tamaa…kama tabia ya mtu ni kutamani! Hiyo tabia hataiacha hata akioa au akiolewa..pengine ataepuka zinaa tu baada ya kuoa/kuolewa kwasababu atakuwa na mke/mume wake ndani!.... Lakini tama ya kutazama wanawake wengine itakuwa palepale kama atakuwa hajabadilishwa.

Kwahiyo suluhisho pekee la kuzuia tamaa kwa aliyeoa au asiyeoa, ni kumkabidhi Kristo maisha kwanza, na kukusudia kuacha dhambi, (kumbuka Mungu hawezi kumsaidia mtu ambaye hajakusudia kwa dhati kuacha kile kitu kibaya anachokifanya)..mtu akishakusudia kuacha kwa vitendo tabia ya kutamani, kujitenga na vichochezi vyote vya uasherati, muvi zenye vimelea vya ngono ndani yake, pornography, matusi, maneno ya mizaha yasiyokuwa na maana, ndipo Roho Mtakatifu anakuja juu yake na kumsaidia na hivyo anajikuta vile vitu havimsumbui tena maishani mwake. Tofauti na yule anayetamani tu kuacha lakini haonyeshi jitihada yoyote ya kutaka hivyo vitu viondoke ndani yake.

 SWALI 2: Naomba nisaidie kwanini Yesu alibatizwa, kulikuwa na umuhimu wowote wa yeye kufanya vile?
JIBU: Mojawapo ya kazi iliyomleta Bwana Yesu duniani ni KUTUONYESHA SISI NJIA ya kumfikia Mungu ambayo ili ilikuwa imesitirika tangu zamani biblia inatuambia hivyo. Na sababu nyingine ilikuwa ni UKOMBOZI na UTAKASO.

Sasa katika kipengele cha kutuonyesha sisi njia ilipaswa kwa kupitia maisha yake atufundishe sisi maisha makamilifu mwanadamu anayotakiwa ayapitie na kuyaishi...kwamba kwa kupitia maisha yake sisi tujifunze namna ya kuishi maisha makamilifu.

Ndio hapo unaona ilimlazimu Bwana kwenda kubatizwa, ili kutufundisha kuwa na sisi tunapaswa tukabatizwe...ingawa yeye hakustahili kubatizwa, lakini ili awe mwalimu mwema ilipasa aonyeshe kielelezo jinsi ya kufanya.... ndio maana Yohana alimwambia maneno yafuatayo…

“Mathayo 3:13 “Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe.
14 Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?
15 Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali.”

Kingine unaona ilimpasa pia Bwana Yesu kuumega mkate na kushiriki meza ya Bwana ingawa yeye hakustahili kuishiriki ile meza ya Bwana lakini alifanya vile kutuonyesha sisi kwamba tunatakiwa kufanya vile kila tunapokutana kwa kumbukumbuku lake, embu fikiria kama mambo yale yalikuwa yanamuhusu yeye basi tujiulize alikuwa anaumega mkate kwa mwili wa nani? Au anashiriki divai kwa damu ya nani?. Na huku sisi tunafahamu kuwa ishara ile ya kuumega mkate na kushiriki kikombe, ni ishara ya mwili na damu ya Yesu Kristo, sasa yeye ni damu ya nani tena na mwili wa nani alikuwa anaushiriki? Unaona hapo, hiy ilikuwa ni kwa ajili ya kutupa sisi kielelezo cha jinsi ya kufanya ili tutembee katika njia za Mungu...

Kingine unaona ilimpasa awatawadhe wanafunzi wake miguu ingawa yeye haikumpasa kuwatawadha wanafunzi wake miguu...hii yote ni ili kutupa sisi kielelezo kwamba tunapaswa tutawadhane miguu sisi kwa sisi.(Yohana 13:15). Tunyenyekeane sisi kwa sisi,

Kwahiyo mambo hayo yote Bwana Yesu aliyafanya, kusudi lilikuwa ni kutuonyesha sisi kielelezo...kwamba sisi ndio tunaotakiwa kuyafanya hayo mambo yote sio yeye...Na hata ubatizo na mambo mengine yote.

Ubarikiwe!
SWALI 3: Je! Mungu anaupendeleo zaidi kwa wanaume zaidi ya wanawake?.
JIBU: Ndivyo inavyodhaniwa na wengi, hususani linaposomwa lile andiko lisemalo 1Timotheo 2:13 “Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye.” Maneno hayo yanathibitisha kuwa Adamu ndiye aliyepewa kipaumbele cha kwanza kuliko mwanamke..

Lakini ifahamike kuwa Mungu ni Mungu wa utaratibu. Tunapotaka wote tufanane, wote tuje kwa wakati mmoja, na wote tuwe na mamlaka yanayofanana, basi maisha yangekuwa hayana maana. Hivyo Ili Mungu kutimiza kusudi lake, na kuweka mambo yote katika utaratibu ilimpasa aweke ngazi lakini hilo halimaanishi kuwa mmoja ni bora zaidi ya mwingine..Kwasababu kama tukichukulia kigezo cha kuumbwa kwa mwanaume kwanza zaidi ya mwanamke ndio tiketi..Kumbuka pia wanyama na mimea yote iliumbwa kwanza kabla hata ya Adamu kuumbwa..Sasa hapo tuseme wanyama wamepewa upendeleo mkubwa zaidi ya sisi?.

Jibu ni hapana, lakini tatizo kubwa linakuja pale wanaume wanapotaka kuwa kama wanawake na wanawake wanapotaka kuwa kama wanaume, katika utendaji kazi wao Mungu aliowawekea, hususani pale katika suala la UONGOZI katika kanisa, na nyumbani. Biblia inasema je! MAUMBILE NAYO HAYATUFUNDISHI? (1Wakorintho 11:14). Tujifunze katika maumbile ya kila mmoja, jinsi alivyoumbwa, ili tupate kulijua kusudi la Mungu katikati yetu, jaribu kufikiria suala la uleleaji wa mtoto, baba hata aweze kufanya shughuli zote za ndani namna gani, hata aonyeshe upendo kwa mtoto mkuu dizaini gani bado hataweza kumtolea mtoto chakula mwilini mwake.

Hiyo shughuli nzito na jukumu la kipekee namna hiyo ameumbiwa mwanamke tu (mama). Shughuli nzito ya kumlea akiwa kijusi tumboni, mpaka kiumbe kipya duniani na changamoto zake zote, wakati mwingine hata wengine kupoteza maisha yao kwa changamoto hizo, ni mama peke yake ndiyo aliyeumbiwa, mwanaume hata awe shujaa kiasi gani,..akijaribu kufanya hivyo atakuwa anapoteza muda wake…..hawezi kufanya hivyo hata atamanije!!….Kadhalika kazi ya ulinzi, uangalizi wa nyumba, kazi za kutumia nguvu nyingi, mwanamke hata akijitahidi vipi kwenda kubeba viroba vya michanga atakuwa anajiumiza tu mwenyewe. Shughuli hizo na taabu hizo Mungu kamuumbia mwanaume. Japo zipo zinazofanywa na wote hilo lipo wazi, lakini tatizo linakuja ni pale kila jambo, ambalo mwanaume ametawazwa na Mungu kulifanya mwanamke naye anataka kulifanya..asilimia 50 kwa 50..Na hilo ndio limekuwa tatizo kubwa.Ambao ni mpango mkamilifu wa shetani, mwanaume anavaa suruali mwanamke naye anataka kuvaa suruali, mwanaume anavaa kaptura mwanamke naye anataka kuvaa kaptura, mwanaume ananyoa nyewe zake, mwanamke naye ananyoa kipara afanane na mwanaume.

Kwa mfano tukirudi kwenye kanisa: Biblia inasema

1Wakorintho 14.34 “Wanawake na wanyamaze katika kanisa, maana hawana ruhusa kunena bali watii, kama vile inenavyo torati nayo..”
Na pia inasema 1Timetheo 2: 12 “Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu”.

Utakuta Baadhi yao wanaona kama Mungu kawaweka nyuma katika kazi yake, na hivyo wanaamua kuyahalifu kwa makusudi maagizo ya Mungu na kwenda kufundisha makanisani, na kuwatawala waume zao. Wakidhani kuwa ndio wanajenga, kumbe hawajui kuwa wanabomoa. Hekima ya Mungu ni kubwa zaidi ya mwanadamu, akisema hivi anamaanisha hivyo, yeye anajua ni jinsi gani mwanaume atatenda vizuri katika eneo hilo zaidi ya mwanamke na ndio maana akasema hivyo..

Lakini kwa anayemwona Mungu hapo kakosea kuweka ngazi, na mamlaka katika kazi yake mwenyewe aliyoibuni duniani biblia ipo wazi yanasema hivi:

1Wakorintho 14: 37 “Mtu akijiona kuwa ni nabii au mtu wa rohoni, na ayatambue hayo ninayowaandikia, ya kwamba ni maagizo ya Bwana.
38 LAKINI MTU AKIWA MJINGA, NA AWE MJINGA”.

Baki katika nafasi uliyoitiwa, Biblia haina mfumo dume hapana bali ina utaratifu. Na utaratibu huo ni Mungu mwenyewe ndio kauweka kulingana na jinsia.

Ubarikiwe.

No comments:

Post a Comment