"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, February 20, 2019

PENGINE MUNGU ALISHASEMA NAWE KWA NJIA HII.


Mbali na mtu kuona maono au kuota ndoto Kuna mambo mengine ambayo nimeshawahi kuona yakitokea kwa watu wengi, na wengine walikuwa wakiniuliza ni nini maana yake lakini wasifahamu, hata mimi mwenyewe yamenitokea mara nyingi, na sikujua maana yake mpaka Bwana alipokuja kunipa ufahamu wa kuelewa...

Na hata pengine yalishawahi kukutokea na wewe, kuna wakati Fulani labda umekaa mahali unazungumza na watu, au unafanya kitu Fulani, na mara kunatokea tukio mbele yako ambao linalohusiana na tukio hilo, pengine katikati ya mazungumzo au shughuli mfanyayo na hapo hapo unapata ufahamu wa kujua kama vile tukio hilo ulishawahi kuliona mahali fulani, na sasa linatimia, ni kama vile linajirudia hivi au unaona tukio fulani na ghafla unajua hatma yake ni nini, na kweli inatokea hivyo, na hiyo huwa haidumu sana, ni kitendo cha sekunde mbili tatu, imekwisha..

Au inatokea tena wakati mwingine, ukitazama kitu chochote cha asili aidha mbingu, miti, milima, bustani, habari,wanyama, watu n.k.. hapo hapo unajikuta kuna hisia nzuri inakujia ndani yako usijue ilipotoka inakuwa kama ulishawahi kuishi sehemu Fulani nzuri yenye amani na furaha na utulivu kam hiyo hapo kabla n.k. na hiyo nayo huwa haidumu muda mrefu ni kitendo cha sekunde kadhaa tu imekwisha.

Sasa kama hautaelewa maana ya hayo mambo, utabakiwa na maswali mengi kichwani. Lakini hujui kuwa ni Mungu ndiye anayezungumza na wewe na kukuonyesha uhalisia wa mambo jinsi ulivyo.

Kuna siku moja nilikuwa ninacheza na mtoto wa Dada yangu nje, nilikuwa ninamrusha rusha juu na kumkamata, lakini baada ya muda kidogo mawazo yangu yalihama nikawa ninafikiria mambo mengine, nikawa kama nimepoteza amani kama vile mtu aliyeachwa kwenye unyakuo…na mara Yule mtoto ambaye nilikuwa ninacheza naye pale nje, akatulia kwa muda mfupi, halafu akawa anaangalia mbinguni pale pale mbele yangu. Kisha akazungumza maneno haya mara tatu “HUKUMU, HUKUMU, HUKUMU”..na baada ya hapo akaendelea na michezo yake, kama kawaida. Nikapata wasiwasi kidogo huyu mtoto mdogo wa miaka mitatu haya maneno ya ndani kayajulia wapi na huku hata kuongea vizuri alikuwa hawezi ni mzito hata wa kuongea..

Yale maneno yaliniingia ndani ya moyo wangu, nikafiria sana na tena linaendana na jambo nililokuwa ninawaza muda huo huo, hapo ndipo nikajua kuwa ni Mungu alikuwa anazungumza na mimi.

Sasa kwanini ninasema hivi, ndugu zipo njia nyingi sana usizozidhania tofauti na ulizizoe Mungu kusema nawe kila siku, na hizo pia zitatuhukumu katika siku ile ya mwisho. Unaweza kuikwepa Injili ya msalaba, unaweza ukakwepa mahubiri ya Neno la Mungu,akasema sikujua, Mtu atakwepa kila kitu kwa kisingizio cha kuwa hajasikia injili lakini hatakwepa SAUTI ya Mungu inayosema naye kila siku katika maisha yake kwa namna ambazo asizozitazamia yeye.

Sasa ni kwanini mtu anapata hisia kama hizo za kuona vitu vinavyoweza kutokea muda mfupi au sekunde chache mbeleni, ni kwasababu Mungu anamwonyesha kuwa pia una ouwezo wa kuona mambo yatakayokuja kutokea huko mbeleni kabisa hata baada ya kifo, kama hatopuuzia. Ikiwa umeona ya muda mfupi kidogo mbeleni kwanini usione ya muda mrefu yanayokuja huko mbeleni?. Kwanini usione ipo dhiki kuu inakuja huko mbeleni, Kwanini usione lipo ziwa la moto mbeleni?. kwanini usione ipo mbingu imeandaliwa kwa wale watakaoshinda, kama ikiwa kuna wakati mwingine unapata hisia nzuri kama alishawahi kuishi mahali Fulani kuzuri?, Kwanini asijue kuwa upo utawala wa amani wa miaka 1000 unakuja huko mbele wa Kristo na bibi-arusi wake na umilele ujao..

Ndugu Kila mwanadamu ameumbwa ni kiwango Fulani cha Imani, haijalishi awe ni mwenye dhambi, au mwema, haijalishi awe ni mwaminio au sio mwaminio, hata mtu anayeamini kuwa hakuna Mungu imemgharimu Imani, kuamini kuwa Mungu hayupo. Hivyo hakuna ambaye atanusurika siku ile ya Hukumu, hakuna hata mmoja.

Sikia maneno ya Mungu yanavyosema:
Isaya 65: 12 “mimi nitawaandikia kuuawa kwa upanga, na ninyi nyote mtainama ili kuchinjwa; kwa sababu NILIPOITA HAMKUITIKA; NILIPONENA, HAMKUSIKIA; bali mlitenda yaliyo mabaya machoni pangu, mlichagua mambo nisiyoyafurahia.

Unaona Mungu amekuwa akinena na wewe kwa njia mbalimbali, wakati mwingine ulipokuwa katika shughuli zako na mihangaiko umeshawahi kusikia sauti kama mtu akuita jina lako kwa nguvu, na ulipotazama usione mtu, Sauti kama hizo ni kukuonyesha kuwa Mungu anakuita umtazame yeye, lakini wewe husikii, hata leo hii anazidi kunena na wewe lakini bado unataka kuufanya moyo wako mgumu usitubu dhambi zako na kumgeukia Mungu. Kumbuka Kuna wakati Mungu kauandaa wa kuuawa kwa waovu wote, na huko si kwingine zaidi ya kwenye ziwa la moto.

Usisubiri hizo nyakati mbaya zikukute, usiitamani hukumu ya Mungu,ambayo hakuna mtu hata mmoja aliye mwovu atapona, itii sauti yake leo, mpe Bwana maisha yako, anza mwanzo mwema, weka mbali maisha ya dhambi, yanakusaidia nini hayo? utubu kabisa kwa kumaanisha kuacha dhambi zako, kisha haraka iwezekanavyo katafute mahali utakapoweza kwenda kubatizwa ubatizo sahihi kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako kama hujabatizwa, wengi shetani kawapofusha macho na kufikiri ubatizo haujalishi, au hauna maana sana, ndugu yangu usidanganyike. Ubatizo ni wa umuhimu sana, biblia inasema “aaminiye na kubatizwa ataokoka” sio aaminiye tu! peke yake hapana! Bali aaminiye na kubatizwa…utasema mbona Daudi hakubatizwa? ina maana hataokoka?..Daudi hakubatizwa kwasababu yeye hakuifahamu hii neema ingawa alitamani kuijua, hivyo yeye na watu wote ambao hawakuijua hii neema ya Ubatizo, Bwana atawapa neema ya wokovu kwasababu hawakujua, kadhalika Daudi aliua maadui zake kwasababu hakuijua hii neema tuliyonayo sisi ya kufahamu kuwa hata kumwonea hasira ndugu yako ni sawa na kuwa muuaji, hali kadhalika Daudi alioa wake wengi kwasababu hakuijua hii neema ya kuwa mtu anapaswa awe na mke/mume mmoja tu!! Lakini leo hii wewe unayesikia haya, ukiua na umeshaufahamu ukweli kwa kisingizio cha kujilinganisha na Daudi, utakwenda kwenye ziwa la moto, vivyo hivyo ukimwacha mume wako/mke wako na kwenda kuoa mwingine au kuongeza wake wengi kwa kisingizio cha kujilinganisha na Daudi, utakwenda katika ziwa la moto, kadhalika wewe unayesema leo ubatizo sio wa lazima sana kwa kujilinganisha na Mfalme Daudi na yule mtu aliyekufa na Bwana pale msalabani utaenda kwenye ziwa la moto. Kwasababu umeujua ukweli na bado ukaukataa. Na leo hii umeusikia ukweli hapa siku ile hutasema hukuusikia.

Na ubatizo sahihi sio wa kunyunyiziwa, ni wa kuzamishwa mwili wote katika maji mengi na ni kwa jina la YESU Kristo kama maandiko yaagizavyo katika (Matendo 2:38, 8:16, 10:48, 19:5).Jina la Yesu ndio jina la Baba,Mwana, na Roho Mtakatifu, hakuna lingine Wengi wanapuuzia maagizo hayo lakini wewe usiwe hivyo, suala la wokovu wa roho yako usilichukulie kidini, au kiwepesi wepesi hayo ni maandiko kabisa na ni maagizo ya Mungu kwa ajili ya uzima wa roho yako. Mtu yeyote anayemaanisha kumfuata Kristo hataona ni masharti magumu, lakini waliovuguvugu ndio watatoa udhuru.Na ndio hao mwisho wa siku wokovu wao hauthibitiki.

Lakini wewe ukizingatia hayo kwa moyo mweupe Bwana atakupa kipawa cha Roho wake na huyo ndiye atakayekuongoza siku zote katika kuijua kweli. Na kubatizwa si lazima kupitia mafunzo yoyote ya muda mrefu, halafu baadaye upokee cheti Fulani, kama dini zinavyofanya..tiketi ya kubatizwa ni KUAMINI NATOBA BASII!!. Pindi tu mtu anapoamini na kutubu dhambi zake na kuamua kumwishia Kristo wakati huo huo anapaswa akabatizwe.

Na pia kama umempa Bwana maisha yako tayari na umebatizwa na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu, ni wajibu wetu sote kuwahubiria wengine habari njema za ufalme, hivyo popote pale ulipo waambie wengine kuhusu wokovu ulio katika Bwana wetu Yesu Kristo

Ikiwa kama hujabatizwa na hujui mahali utakapopata huduma hiyo, unaweza pia kuwasiliana nasi, tukuelekeze mahali karibu nawe.

Ubarikiwe sana.

No comments:

Post a Comment