"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, February 19, 2019

BABA YANGU ANATENDA KAZI HATA SASA!.


Shalom! Mwana wa Mungu, Karibu tujifunze Neno la Mungu…ambapo leo tutajifunza mambo machache yahusuyo utendaji kazi wa Mungu. Tutajifunza ni wakati gani Mungu anatenda kazi kwa watu wake.

Swali ambalo limekuwa ni changamoto kueleweka, na linaloulizwa na wengi ni kuhusu siku gani inayopasa iwe ni ya kuabudia au ya kukutana na Mungu, je! ni jumapili, jumamosi au lini?...miongoni wa wanaosema jumamosi ndio siku ya kuabudu mstari mama wanaousimamia ndio huu:
Mwanzo 2: 3 “Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya”
Hali kadhalika pia miongoni mwa wanaosimamia kuwa jumapili ndio siku ya kuabudu, mstari huu ndio msingi wao.
 
Marko 16: 9 “Naye alipofufuka alfajiri siku ya kwanza ya juma, alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, ambaye kwamba alimtoa pepo saba”..

Kulingana na mstari huo siku ya kwanza ya juma ni jumapili, Hivyo hiyo ndio siku ya kupumzika na kuabudia kulingana na wao kwasababu ni siku ambayo walipata ushindi wao kwa kufufuka kwa Bwana Yesu.

Kumekuwa na kushindana kusikoisha kati ya makundi haya mawili, kila moja likitetea hoja zake..Lakini Biblia inasema Mungu ni Roho nao wamwabuduo imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.

Kwahiyo Mungu aliruhusu watu waishike sabato katika agano la kale, kufunua sabato halisi itakayokuja huko mbeleni (yaani pumziko la roho), kadhalika aliruhusu wana wa Israeli katika agano la kale wakati wanatoka Misri waishike pasaka (ile siku waliyotoka Misri), kufunua pasaka wetu halisi atakayekuja huko mbeleni yaani (Bwana wetu Yesu Kristo), ambaye kwa yeye tunapata ondoleo la dhambi na kutolewa kutoka katika utumwa wa dhambi. 1 Wakorintho 5: 7 “Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo;”

Kwahiyo katika agano jipya hatuna sheria yoyote ya lazima ya kushika sabato wala pasaka, wala sikukuu yoyote ile..Kwasababu tumepata ufunuo kamili wa mambo hayo yalikuwa yanamaana gani.

Wakolosai 2:15 “akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.16 Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo”
 
Pia jambo lingine la muhimu la kujua ni kuwa, Mungu hana siku maalumu ya kupumzika, kwa sababu yeye hachoki, Neno linaposema “katika siku ya saba aliacha kufanya kazi zake zote akapumzika” haimaanishi kuwa katika siku ya saba..shughuli zake zote alizisimamisha au zilisimama hapana!! bali alimaanisha kuwa katika siku hiyo “aliacha kufanya kazi ya kuumba vitu vipya”..
Kwasababu kama katika siku ya saba shughuli zake zote zilisimama basi mwanadamu pia angeacha kupumua kwasababu na yeye ni kazi ya Mungu, wanyama pia wangesimama kupumua, na kila kitu kingesimama, hata jua lingesimama..lisingekuchwa,na mito nayo ingesimama, kwasababu vyote hivyo ni kazi ya Mungu, unaona! lakini tunaona vitu vyote viliendelea kama kawaida hata katika hiyo siku ya saba, maji yaliendelea na mizunguko yake, jua liliendelea kusogea, miti iliendelea kuota n.k..kwahiyo kazi ya Mungu ilikuwa iliendelea…na inaendelea mpaka leo, yeye hapumziki anaendelea kutenda kazi.

Ndio maana wakati Fulani mafarisayo walitaka kumkamata Bwana Yesu kwa habari hiyo hiyo ya kuishika sabato, wakitaka kumwonyesha kuwa katika siku ya saba hapaswi mtu yoyote kufanya kazi kwasababu hata Mungu mwenyewe alistarehe katika siku hiyo akaacha kufanya kila kitu alichokuwa anakifanya..Lakini Bwana alikuwa na ufunuo mkubwa zaidi ya huo na kuwaambia…

Yohana 5:14 “Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi.
15 Yule mtu akaenda zake, akawapasha habari Wayahudi ya kwamba ni Yesu aliyemfanya kuwa mzima.
16 Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwudhi Yesu, kwa kuwa alitenda hayo siku ya sabato.
17 Akawajibu, BABA YANGU ANATENDA KAZI HATA SASA, NAMI NINATENDA KAZI”.

Umeona hapo?..Bwana anawaambia wale waliokuja kumshitaki kuwa siku ya saba hapaswi kufanya kazi…lakini Bwana akawaambia, BABA YAKE ANATENDA KAZI HATA SIKU HIYO, NA YEYE ANATENDA KAZI. Umeona hana siku ambayo anapumzika. Wao walitaka kumwambia siku ya saba Mungu alipumzika, lakini yeye akawaambia Baba yake anatenda kazi hata sasa. Kazi zake bado zinaendelea.

Bado anaendelea kuumba kimiujiza, bado anaendelea kutengeneza wanadamu kwenye matumbo ya wanawake, bado anaendelea kulitembeza jua kwa amri yake, bado anaendelea kutushushia mvua, bado anaendelea kuiumba miti na mimea, ndio maana ukiukata mti leo baada ya muda Fulani utaukuta umekua tena, hiyo ni kazi ya Mungu iliyo katika mwendelezo wake, haina pumziko, kama Bwana Yesu alivyosema “Baba yangu anafanya kazi hata sasa nami ninatenda kazi” kadhalika na sisi pia tunatakiwa tuseme maneno hayo Kama Baba yetu wa mbinguni anavyotenda kazi nasi pia TUNAZITENDA.
Na kazi hizo ni zipi?..Si nyingine zaidi ya zile zile Bwana Yesu alizozifanya.

Yohana 14 : 12 “Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, KAZI NIZIFANYAZO MIMI, YEYE NAYE ATAZIFANYA; NAAM, NA KUBWA KULIKO HIZO ATAFANYA, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba.
13 Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.
14 Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya”
Sasa Bwana Yesu alifanya kazi gani?; aliponya wagonjwa wa kila aina (wa mwilini na wa rohoni). Kama Baba naye anavyojishughulisha kuiponya dunia kila siku, hapumziki, Bwana Yesu alirudisha uhai wa mtu aliyekufa, aliumba macho ya mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa kwake n.k, aliwahubiriwa watu injiii, na sisi Bwana katuambia kazi hizo tunaweza kuzifanya kwa jina lake.

Kwahiyo nataka nikuambie wewe unayesoma ujumbe huu, hakuna UGONJWA, WALA SHIDA, WALA KIFUNGO CHOCHOTE CHA SHETANI Kitakavyoweza kusimama mbele yako kuanzia leo hii kama umeuelewa ujumbe huu, kama umemwamini Yesu Kristo kwa dhati kabisa kutaka moyoni mwako.
Kama ni ugonjwa Kristo anao uwezo wa kukuponya sasa hivi, sio kesho, na ametupa uwezo wa kuombeana sisi kwa sisi na kupokea uponyaji wetu. Kwahiyo kama una ugonjwa wowote sasahivi hapo ulipo, Weka mkono wako mahali penye tatizo na uambie huo ugonjwa maneno haya kwa sauti na kwa Imani  
“EWE UGONJWA!!, BABA YANGU WA MBINGUNI ANATENDA KAZI HATA SASA, NAMI NATENDA KAZI KAMA YEYE, ONDOKA KWANGU NA USIRUDI TENA KWA JINA LA YESU”
 
Baada ya kusema hivyo AMINI! Na uhai wa huo ugonjwa utakuwa umeishia hapo hapo.

Utasema mbona sijawahi kumuona Baba akiniponya leo iweje aniponye kwa dakika moja? Nataka nikuambia ulishawahi kumwona akikuponya isipokuwa ulikuwa hujui tu kama ameshawahi kukuponya mara nyingi! Chukua mfano siku ile ulipojikata na kisu mkononi na baada ya wiki mbili ile ngozi ikajirudia tena vile vile, kama ilivyokuwa mwanzo huoni huo tayari ulikuwa ni uponyaji?..Hapo ni Baba yako anafanya kazi yake ya kukuponya kila siku, unapokata nywele na baada ya wiki mbili zinaota tena huoni huo ni uumbaji tayari… sasa kwanini na wewe usifanye kazi ya kutamka uponyaji juu yako na kwa watu wengine, hiyo ndio sababu iliyomfanya Kristo akafanye miujiza kila mahali pasipo kizuizi chochote sio cha sabato wala cha sikukuu yoyote, kwasababu aliona Baba hana mipaka kila siku anafanya kazi zake.

Kila siku katika maisha yako, likumbuke hilo neno, Mungu hapumziki katika kazi zake na wala hachoki,anafanya kazi kila dakika na kila sekunde…na hivyo nasi pia hatupaswi kupumzika katika kuzifanya kazi zake..Kila siku tunapaswa tuumbe jambo jipya moyoni mwetu na maishani mwetu, kama yeye anavyoumba watu wapya kila siku kwenye matumbo ya wanawake. Kwasababu huo uwezo tumepewa..Tukitamka tu! Kwa IMANI TUSIPOKUWA NA MASHAKA, Hilo tulilolisema ni lazima litokee..

Ndugu nakuambia hilo kwasababu mimi binafsi Bwana kanitendea katika maisha yangu, watu kadha wa kadha nimewaombea nao wamepona! Na mimi mwenyewe Bwana ameniponya mara nyingi kwa njia hiyo. Hivyo mwamini Mungu.
 
Bwana akubariki sana..

Tafadhali “share” ujumbe huu na wengine.

No comments:

Post a Comment