"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, February 12, 2019

UTAMBUE UJUMBE WA SAA UNAYOISHI.


Shalom! Mtu a Mungu, Karibu tujifunze Neno la Mungu, ambalo ndio uzima wetu, wa miili yetu, nafsi zetu na roho zetu…Leo tutajifunza somo lenye kichwa kinachosema UTAMBUE UJUMBE WA SAA UNAYOISHI.

Kwanza kabla ya kuuzungumzia ujumbe wa saa ni muhimu kujifunza baadhi ya njia Mungu alizoziweka katika kukamilisha kusudi lake chini ya mbingu…Na mojawapo ya njia Mungu aliyoiweka katika kutimiz akusudi lake ni KUZALIANA NA KUONGEZEKA. Pale Edeni Mungu hakutuumba wanadamu wote kwa wakati mmoja, hakutuumba mimi na wewe na ndugu zetu wote na Adamu na kutuweka pamoja pale Edeni…Kwa ufupi hakuijaza dunia kwa siku moja na kwa wakati mmoja…hapana bali tunaona alimwumba Mwanamke mmoja tu na mwanamume mmoja tu!! akamaliza kazi yake akapumzika…umewahi kujiuliza ni kwanini hakutuumba wote siku ile ile, badala yake sisi wengine tunakuja kutokea duniani miaka zaidi ya 6,000 baadaye?? Na zaidi ya yote hatujatokea kwa kuumbwa kama Adamu alivyoumbwa, badala yake tunazaliwa? Umewahi kujiuliza ni kwanini?.

Ni kwasababu Mungu ni wa utaratibu, ilimpendeza yeye kila mtu awe chini ya mzazi, kwamba huyu atamzaa huyu na yule atamzaa yule, hivyo hivyo kwa vizazi vyote ili pawepo na heshima ulimwenguni pamoja na utaratibu wa kuishi. Endapo wote tungetolewa mavumbini kama Adamu kusingekuwa na mtu wa kumweshimu mwenzake, wala kumjali, kila mtu angefuata mambo yake, kusingekuwepo na unyenyekevu, kusingekuwa na kitu kinachoitwa familia, wala upendo usingekuwepo, n.k Lakini Mungu kwa kulijua hilo akatuumba sisi sote ndani ya Adamu Baba yetu wa kwanza.

Sasa Mungu habadiliki na wala hajabadilika, kwa njia hiyo hiyo ya kuzaliana kwa mwili, na katika roho ndio anayoitumia hiyo hiyo…Mara nyingi Mungu anapowatengeneza watoto wake kiroho, hawezi kumpa kila mtoto siri zake za ufalme wa mbinguni, hapana! Huwa anatumia njia hiyohiyo ya kuzaliana, anamchagua mtu mmoja kisha anampa ufunuo wa kutosha kuhusu jambo fulani, na huyo mtu anakwenda kuwafundisha wengine mambo ambayo ameambiwa na Mungu, na ikiwa anaokwenda kuwafundishwa wakiamini, wanakuwa ni kama watoto wake wa kiroho. Na hao watoto wanapokuwa watu wazima kiroho nao pia wanakwenda kuzaa watoto wengine kupitia injili waliyojifunza kutoka kwa Baba zao wa kiroho, inaendelea hivyo hivyo kwa vizazi na vizazi.

Wengi wetu tunapenda Mungu atufundishe yeye mwenyewe siri zote za ufalme wa mbinguni, kama alivyoongea na Musa na Adamu.. lakini hatujui kuwa huo sio utaratibu wa Mungu wa kuwatengeneza watoto wake, njia ya kututengeneza sisi ndio hiyo hiyo ya kuzaliana, ni lazima wakati fulani tuhubiriwe injili mahali fulani, na watu waliotutangulia katika imani, kisha tutakapofikia kiwango fulani cha kukua nasi pia tutakwenda kuwafundisha wengine.
Warumi 10:13 “kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.
14 Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje PASIPO MHUBIRI?
15 Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!”.
Unaona MHUBIRI Ni lazima awepo, Nakumbuka siku ya kwanza kusikia neno “Mungu”, nilikuwa nina umri wa miaka kama 6 hivi, sitaisahau hiyo siku, nilikuwa na mtu fulani ambaye ni mtu mzima sana, sasa nikawa natazama baadhi ya nyumba za hapo mtaani, nikawa ninamwuliza yule mtu, nyumba moja moja,mahali pale anakaa nani?..ananitajia fulani, namwuliza tena na pale anakaa nani? Ananiambia fulani…baada ya nyumba zote kuisha nikatazama juu mawinguni nikamwuliza na kule juu anakaa nani?..akanijibu KULE ANAKAA MUNGU, baada ya kuniambia vile nikamwuliza Mungu ni nani? Akaniambia ndiye aliyetuumba sisi sote na kila kitu unachokiona!!..baada ya kuniambia vile..nilihisi kama kuna sauti inaniambia ndani yangu, umeshajua! Hutasema hukusikia. Nilijihisi mzito sana siku hiyo, akili yangu ikageuka..

Sasa tukichukua mfano kwa tukio kama hilo, Mungu hakunitokea na kuniambia mimi ni Mungu na nipo juu!! Hapana! Bali alimleta muhubiri na kwa kupitia huyo muhubiri ndio nikamjua Mungu…kwahiyo huyo muhubiri ni kama Baba yangu aliyenizaa katika kumjua Mungu. Kwahiyo utaona tabia ya Mungu ni kutumia watu kutengeneza watu! Mfano anatumia tumbo la mwanamke kutengeneza mwanadamu mpya…hamtengenezi tena kutoka kwenye udongo kama alivyofanya kwa Adamu,kadhalika pia anatumia hao hao watu(au wahubiri) kuwatengeneza watoto wake wa kiroho. Kwanini anafanya hivyo jibu ni NDIVYO ILIVYOMPENDEZAAA!! Na pia anataka tuishi katika utaratibu na heshima.

Ndio maana ukirudi katika kipindi cha Musa, utaona Mungu anamteua mtu mmoja tu Musa, ambaye atauona uso wa Mungu, na kuzungumza na Mungu ana kwa ana, na kumpatia huyo maagizo yote ya nini cha kufanya na nini cha kuwaambia wana wa Israeli.. huoni Mungu akimtokea mtu mmoja mmoja katikati ya wana wa Israeli na kuanza kumpa maagizo kama alivyompa Musa. Hapana! Alimteua mtu mmoja tu Musa, hao wengine watasikia kutoka kwa Musa. Watakuwa watoto wa Musa katika roho! Ndio maana utaona wana wa Israeli wote kwa vizazi vyote iliwapasa waishike sheria ya Musa, kwasababu ndiye aliyekuwa kama Baba yao katika roho.

Kadhalika tunapokuja katika agano jipya. Bwana alipopaa alitoa mitume wake 11 akawatuma wakahubiri injili kote duniani, siri za YESU KRISTO kwamba ndiye Mkombozi wa Ulimwengu na Masihi aliyetabiriwa kuja..Na kwa kupitia mafundisho yao wao ndio wakalizaa kanisa, WAO NDIO WAKAWA MABABA WETU SISI. Hata tungefanyaje sisi watoto tusingemjua Kristo kwa mapana pasipo kupitia wao!! Na ndio maana tunaona kanisa lote lilikuwa linadumu katika mafundisho ya Mitume.
Matendo 2: 40 “Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi.
41 Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu.
42 WAKAWA WAKIDUMU KATIKA FUNDISHO LA MITUME, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali”.
Unaona, fundisho la Mitume, ndilo likawa fundisho la Mababa. Bwana aliwachagua Mitume wake akiwemo Paulo ndani yake kuwapa ufunuo wa Yesu Kristo ni nani??..tusingejua kama Yesu Kristo ni Mungu kama Mtume Yohana asingesema “hapo mwanzo kulikuwako Neno naye Neno alikuwako kwa Mungu naye Neno alikuwa ni Mungu” na pia tusingefahamu siri hiyo kama Mtume Paulo asingesema maneno haya..

1 Timotheo 3:16 “Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu.”
Kadhalika tusingejua kama kuna kitu kinachoitwa unyakuo kama Mtume Paulo asingesema kwa mapana katika mistari hii.
1 Wathesalonike 4: 13 “Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini.
14 Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye.
15 Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti.
16 Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.
17 Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele”.
Mungu aliwafunulia hao kwanza ili wao watuzae sisi katika roho baadaye kwa kupitia injili hiyo. Mungu asingeweza kutupa sisi ufunuo huo kila mtu mmoja mmoja, kwasababu sheria yake ya kuzaliana ingevunjika, ilimpasa awachague hao na kuwapa ufunuo huo, ili sisi tuje kuusikia baadaye kutoka kwao na kuuamini.

Sasa tangu kipindi hicho cha mababa wetu ambao ndio MITUME mpaka sasa imepita miaka zaidi ya 2,000, na kulingana na unabii wa kibiblia kanisa la Kristo tayari limeshapitia nyakati tofautitofauti saba (7) zinazojulikana kama nyakati saba za Kanisa.

Na biblia inatabiri nyakati za mwisho maasi yataongezeka sana, kabla ya kuja ile SIKU YA KUOGOFYA YA HASIRA YA MUNGU MWENYEZI, ambapo dunia yote itafumuliwa na wanadamu wataangamizwa kutokana na maasi yao!!...
Sasa naomba usikiliza hapa kwa makini mtu wa Mungu!!!
Biblia ilisema pia kipindi kifupi sana karibia na Hiyo siku ya kutisha kuilijia ulimwengu wote! Mungu atamtuma ELIYA NABII, na Kazi kubwa ya huyo ELIYA itakuwa ni KUIGEUZA MIOYO YA WATOTO IWAELEKEE BABA ZAO!!!!!. Yaani kuwarejesha watoto wayageukie mafundisho ya mababa ambao ni MITUME WA YESU KRISTO!..Tunasoma hayo katika kitabu cha….
Malaki 4:5-6 “Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya Bwana, ILIYO KUU NA KUOGOFYA.
6 Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, NA MIOYO YA WATOTO IWAELEKEE BABA ZAO, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.”
Sasa swali linakuja Huyu Eliya aliyetabiriwa atakuja katika hizi siku za mwisho ni nani??.
Wengi hapa ndipo walipokwama na kufikiri kuwa Siku za Mwisho Mungu atamrudisha tena yule Eliya aliyechukuliwa juu na magari ya moto! Hapana! Mungu hana utaratibu huo wa kuwarudisha watu walioondoka duniani kuhubiri tena..hana utaratibu huo, ni mmoja tu! ndiye aliyetabiriwa atarudi na mawingu, huyo si mwingine zaidi ya YESU KRISTO, MKUU WA MAJESHI…wengine wote watabaki huko waliko,

Sasa Biblia iliposema “nitawapelekea Eliya nabii” haikumaanisha Eliya mtishbi bali ilimaanisha roho iliyokuwepo juu ya Eliya ndiyo itakayorudi, na hiyo roho si nyingine zaidi ya roho Mtakatifu mwenyewe, kwasababu Roho aliyokuwepo juu ya Eliya alikuwa ni Roho Mtakatifu. Sasa kumbuka kitu kimoja! utendaji kazi wa Roho Mtakatifu juu ya Musa ulikuwa ni tofauti na utendaji kazi juu ya Danieli, na pia utakuwa ni tofauti juu ya Eliya, Nabii Danieli alihubiri lakini hakuwarudisha watu kwa Mungu, yeye Mungu alimtumia kutoa unabii tu juu ya siku za mwisho, Musa hakutoa unabii juu ya siku za mwisho kama Danieli lakini yeye Roho alimtumia kutangaza sheria za Mungu…Kadhalika Eliya hakutoa unabii juu ya siku za mwisho kama Danieli lakini yeye aliwageuza watu mioyo waigeukie torati ya Musa ambayo ndiyo ilikuwa sheria ya Mababa! Kwa ishara na miujiza..Kwahiyo roho alikuwa ni mmoja juu ya manabii wote isipokuwa utandaji kazi ni tofauti.

1 Wafalme 18: 36 “Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako.
37 Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na YA KUWA WEWE UMEWAGEUZA MOYO WAKURUDIE.
38 Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji.

Sasa hiyo roho ya Eliya ya kuigeuza mioyo ya watoto iwageukie mababa! Ndiyo hiyo iliyoahidiwa kurudi tena duniani, kipindi kifupi kabla ya dunia kuangamizwa.

Kwahiyo kama alivyomtia Mafuta Musa, kipindi cha wana wa Israeli, na kama alivyomtia mafuta Eliya mtishbi kipindi cha sanamu za Ahabu na Yezebeli ili kwamba wana wa Israeli waigeukie torati ya Musa waliyoiacha.. vile vile Bwana alimtia mafuta pia mtu fulani katika kizazi hichi anayeitwa WILLIAM MARRION BRANHAM, Mwenye ujumbe unaofanana na ule wa ELIYA kwamba..”watoto warudi katika mafundisho ya mababa(yaani mafundisho ya Mitume)”. Roho Mtakatifu katika utendaji kazi kama uliokuwa juu ya Eliya, ulikuwa pia juu ya huyu mtu (William Branham). Hatuna muda wa kutosha kumzungumzia hapa! Lakini kama ukipata nafasi unaweza ukafuatilia mafundisho yake katika mitandao. Hakika utajifunza mengi sana.

Kwa ishara nyingi na miujiza Mungu alimthibitisha, na ujumbe wa kuirudia IMANI YA MABABA, Kurudi kwenye Neno, kuishi kulingana na Neno, Mababa walituambia…”mtu asiyekuwa na Roho Mtakatifu huyo sio wake warumi 8:9” hivyo na sisi tunapaswa tuwe na Roho Mtakatifu.

Mababa walituambia “tutubu kila mmoja wetu tukabatizwe kwa jina lake Yesu Kristo tupate ondoleo la dhambi, Matendo 2:38” hivyo tusipo tubu! Na kwenda kubatizwa sahihi kwa jina lake Yesu Kristo, kwaajili ya ondoleo la dhambi, dhambi zetu hazitaondolewa..na hatutaokoka na ghadhabu inayokuja hapa mbeleni.

Mababa walituambia..”waasherati, wazinzi, waabudu sanamu, walafi, watukanaji hawataurithi ufalme wa Mbinguni” hivyo ni wajibu wetu kujiweka mbali na hayo mambo.
Mababa walituambia siku za mwisho watu watajitenga na Imani wakisikiliza mafundisho ya mashetani, 1 Timotheo 4:1, siku hizo ndio hizi. Madhehebu yanayowafundisha watu ndoa za wake wengi ni halali, kuombea wafu ni halali, kuabudu sanamu ni sio sahihi, kuna nafasi ya pili ya kuokoka na moto wa milele baada ya kufa(mafundisho ya toharani) n.k.

Mababa walituonya juu kunyanyuka kwa roho ya mpinga kristo itakayotenda kazi ndani ya kanisa katika siku za mwisho, na kwamba tujiepushe na kutoka katikati ya yao..

2 Wakoritho 6: 14 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?
15 Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?
16 Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
17 Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.
18 Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,”
Ndugu yangu, Roho Mtakatifu sasa anazungumza nasi kwa Roho ya Eliya, kwamba tokeni kwake enyi watu wangu,!! Tutoke wapi? Tutoke kwenye mifumo na kamba za kimadhehebu ambazo ndani yake kumejaa upotevu na roho ya mpinga-kristo na turudi kwenye Neno kama lilivyohubiriwa na Mababa wetu Mitume. Madhehebu yote yaliyoacha uongozi wa Roho Mtakatifu na kupachika vyeo vya kibinadamu badala yake, biblia imetabiri hayo ndiyo yatakayokuja kuiunda ile chapa ya Mnyama.
Roho ya Eliya Bwana aliiachia juu ya huyu ndugu WILLLIAM MARRION BRANHAM, na kujaliwa kuyaeleza hayo yote, Na sasa Bwana ameiachilia juu yetu kutambua, nyakati tunayoishi na UJUMBE WA SAA HII.
 
Ujumbe wa saa hii ni kutoka katika mapokeo ya ki-Madhehebu? Na kurudi katika Neno kama lilivyohubiriwa na Mababa (Mitume watakatifu). Toka katika mapokeo yanayokwambia ubatizo wa maji mengi au maji machache haujalishi! Hiyo ni roho ya Mpinga-kristo. Toka katika dhehebu linalokuambia tunaweza kuwaombea wafu watoka katika mateso huko waliko, hilo ni sinagogi la shetani!! Toka katika dhehebu linalokuambia Bikira Mariamu anaweza kutupatinisha sisi na Mungu. Hiyo ni injili iliyotengenezwa kuzimu kabisa ndugu yangu…Mpatanishi wa sisi na Mungu ni mmoja tu!!! YESU KRISTO, Usidanganyike na mafundisho ya mashetani!!.. Toka katika madhehebu yanayokuambia Mwanamke anaruhusiwa kuvaa suruali!! Na nguo fupi..hayo ni madhehebu ya mashetani!! Kwa nje ni mazuri lakini ndani Kristo ameyakataa!..hawakwambii ukweli kwasababu anayeabudiwa humo ni shetani! Na shetani analohitaji ni kuipeleka nafsi yako kuzimu! Hilo tu!! Toka katika madhehebu yanayokuambia bado miaka mingi Kristo aje!, ni roho zinazoshawishi kukulewesha ili siku ile ikujie kama mwivi.
 
Je! unaishi katika ujumbe wa saa hii?? Au nje ya saa hii??, je! bado unautumainia ulimwengu ambao unapita? Ni matumaini yangu kuwa, Roho Mtakatifu ni sehemu ya maisha yako.

Kama hujamkabidhi Yesu Kristo maisha yako, ni vyema ukafanya hivyo leo, kabla mlango wa Neema hujafungwa, kabla unyakuo haujapita na ukaachwa, kabla ya mpinga-kristo kunyanyuka ulimwenguni na kulazimisha watu kuipokea ile chapa ya mnyama. Unachotakiwa kufanya hapo ulipo ni kutenga dakika chache angalau sio chini ya dakika 15, funga mlango wako kaa peke yako zungumza na Mungu wako, mweleze maisha yako ya nyuma, tubu kwa ajili ya hayo, usifiche chochote, mwambie akusamehe na pia mwahidi hutafanya hayo tena, na baada ya kutubu usifanye tena hayo uliyokuwa unayafanya, Bwana atakusamehe yeye ni mwenye rehema na atakukubali tena, haijalishi umemkosa kiasi gani!. Kisha usikawie nenda katafute ubatizo sahihi kulingana na imani ya mababa(Mitume)..huo utaupata katika kitabu cha Matendo 2:38, Matendo 8:16, Matendo 10:48 na Matendo 19:5, ubatizo huo ni wa maji mengi na KWA JINA LA YESU KRISTO..Na baada ya kubatizwa Bwana atakupa kipawa chake cha Roho Mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi na hapo utakuwa umezaliwa mara. Kumbuka hakuna mtu atakayeurithi ufalme wa Mbinguni kama hajazaliwa mara ya pili.

Mungu akubariki sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na Mungu atakubariki.

Kwa mtiririko mzuri wa mafundisho haya usiache kutembelea website yetu |wingulamashahidi.org|

No comments:

Post a Comment