"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, February 11, 2019

ROHO ZILIZO CHINI YA MADHABAHU:

Ufunuo 6:9 “Na alipoifungua muhuri ya tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao.
10 Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi?
11 Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vilevile kama wao.”
Shalom! Mpendwa wa Bwana. Leo ni siku nyingine Bwana ametupa, hivyo usikubali siku ya leo ipite bila kupata maarifa mapya yahusuyo maandiko hususani katika siku hizi za hatari tunazoishi.

Na leo tutatazama juu ya hizi roho zinazoonekana hapo zikiwa chini ya madhabahu zikilia kwa nguvu na kuugua kutaka zilipiziwe kisasi juu ya hao wakaao juu ya nchi, Leo tutaona hizi roho ni wakina nani.

Kama hufahamu bado juu ya ufunuo wa Mihuri saba ambayo habari yake inaanzia kutokea ule mstari wa kwanza, basi ni vizuri ukatenga muda wako kupitia maelezo yake {kama utataka utani-inbox nikutumie} ili ukifika hapa ikusaidie pia kupate picha kamili ya kitu kinachoendelea katika huu muhuri wa tano tunaokwenda kuutazama.

Watu hao wanaoonekana hapo si wengine zaidi ya wayahudi ambao waliuawa katika kipindi cha Holocaust, kilichotokea kati ya kipindi cha mwaka 1941-1945, Ambapo wayahudi wengi zaidi ya milioni 6 waliuawa kikatili chini ya utawala wa kidicteta wa NAZI Ujerumani..Historia inarekodi Mbili ya tatu ya wahayudi wote waliokuwa wanaishi bara la ulaya waliuliwa. Na Leo tutatazama kwa ufupi baadhi ya mateso waliyokuwa wanayapitia mpaka kupelekea kuwaona hapa chini ya madhabahu wakilia na kuuga kuomba kisasi kisikawie kulipizwa juu ya adui zao.

1) CHEMBA ZA GESI:

Wakati huo waayahudi wengi walikusanywa kutoka katika vijiji na miji mengi katika majimbo yote yaliyokuwa yanatawailiwa na Nazi, na kuahidiwa kuwa wanapelekwa mahali pa kutunzwa mbali na vita penye nyumba nzuri na utulivu.. Lakini badala yake walichukuliwa na kuwekwa katika treni, na kusafirishwa umbali mrefu kwa siku kadhaa bila hata maji wala chakula mbali na makazi ya watu, na kumbe huko kulikuwa tayari wameandaa kambi za mateso na kazi tu kwa ajili ya wayahudi. Sasa Walipokuwa wanawasili kwenye kambi, wanaume na wanawake na watoto walikuwa wanatengwa tofauti,.

Wale wanaume wenye nguvu walichukuliwa na kupelekwa kufanyishwa kazi ngumu za ujenzi wa reli na kukata magogo, lakini wale wanawake na watoto pamoja na wazee wote, walikuwa wanadanganywa kuwa kabla ya kwenda kupangiwa majukumu yao ya kazi inawapasa kwanza waende kuogeshwa kwa pamoja katika mabafu ya moto ili kuzuia magonjwa ambayo yamekuwa yakilipuka mara kwa mara katika kambi nyingi za ki-NAZI.

Hivyo bila kujua chochote wale wanawake na watoto wanakubali kuvua nguo zao, pamoja na kukatwa nywele zao. Kisha wanawachukulia kwa upole na kuwapelekwa kwenye vyumba maalumu vinavyoonekana kama mabafu yenye mabomba ya mvua.

Wakishawaingiza wote huko, kuhakikisha kuwa hakuna nafasi hata kuzunguka huku na kule kwa mtu yeyote kutokana na kubanana kwao, ghafla mlango wa chumba hicho kisichokuwa hata na sehemu ya kupitisha hewa kinafungwa kwa nyuma..Na taa zote kuzima eneo lote linakuwa giza kwa muda fulani.

Wakati wale watu kule ndani wanashangaa ni jambo gani linaendelea, ghafla tundu la chumba hicho kwa juu linafunguliwa kuruhusu mwanga wa jua kupita kwa muda mfupi, wakidhania kuwa wanafunguliwa maji kwa juu kumbe hapo juu anakuwa amesimama mtu ameshika makopo maalumu ya gesi mbaya ijulikanayo kama “ZYKLON B”, kitu anachofanya ni anaitaupa hiyo gesi chini kwa haraka kwenye hicho chumba cha shimo walichomo hao watu kisha anafunga mlango wa tundu.

Baada ya muda mfupi, kinachosikika huko nje ni ni kilio na mahangaiko ya watu, gesi ile ni mbaya kwasababu inaua oxgen yote, halafu inachoma mapafu mtu akiivuta anasikia kama moto unawaka kwenye kifua chake, damu zinaanza kutoka puani na midomoni, sasa kwa kuwa hakuna sehemu ya kutokea, basi watu kwa kujaribu kuokoa maisha yao wanarukiana huku na kule kama vile kuku aliyechinjwa wakijaribu kutafuta walau hata sehemu ya kuokoa maisha yao. Lakini kwa kuwa gesi ile ni kali sana mtu hafi kifo cha raha bali cha mateso makali na mahangaiko yasiyoelezeka, wengi wao wanakutwa wamekufa huku wametokwa na haja zote mbili. Na ndani ya muda wa dakika chache tu, kila mmoja anakuwa ameshakufa, kisha baadaye kidogo kama baada ya dakika ishirini hivi, askari wa ki-NAZI anakuja kufungua mlango wa ile chemba, na kuvuta miili yote nje. Na wakitoka hao wanaingizwa wengine.

Sasa kwa kuwa kambi hizi zipo mbali na makao ya watu, wale askari wanakuwa tayari wameshachimba mashimo makubwa na marefu, kwa ajili ya kuichomea miili ile,na kwa jinsi gesi ile ilivyo mbaya miili ikitoka pale hata kuitambua tena ni ngumu kwa jinsi ilivyoaribiwa na gesi ile. Moshi ule hauishi kwasababu kila siku idadi ya watu wasiopungua watu “ELFU SITA” walikuwa wanaingizwa katika chemba za gesi. Na hiyo ni takwimu ya kambi moja, na kulikuwa na kambi kama hizi nyingi tu za mateso.
Jaribu kufikiria ni unyama kiasi gani huo anafanyiwa mwanadamu mwenzako. Kumbuka wayahudi hawakufanya kosa lolote listahilio mateso hayo makali, walichukiwa kwasababu wao ni WAYAHUDI tu! Uzao wa Mungu basi!..wala hakuna sababu nyingine yoyote, iliyowafanya watende mambo ya kinyama kama hayo. Mamilioni ya wayahudi waliuawa kwa namna hii ya kuwekwa katika chemba za gesi.

Huo ni mfano wa mambo madogo sana yatakayokuja kutokea huko mbeleni kwa watu wale watakaoukosa unyakuo.

2) UCHUNGUZI WA KIMAABARA:
Sasa wale ambao watanusurika kwenda kwenye chemba za gesi, baadhi yao wanachukuliwa na kwenda kufanywa “SAMPULI” kwa majaribio katika mahabara. Wengine wanachukuliwa na kwenda kufungiwa katika vyumba maalumu, na ndani ya vyumba hivyo hawapewi maji wala chakula. Bali maji ya chumvi tu tena yale ya baharini, ili kutafiti ni jinsi gani wanadamu anaweza kuishi kwa muda mrefu kwa kutegemea tu maji ya bahari.

Hivyo kama wewe umesoma unaelewa ni jinsi gani chumvi inavyofonyonza maji mwilini, unakaukiwa maji kabisa, kiasi kwamba hata mate yanaisha mdomoni.. Jaribu kufikiria watu hao wanawekwa katika hali hiyo ya maji tu ya chumvi mpaka kufa kwao. Mfanyakazi mmoja wa kambi hizo anasema alishuhudia watu wale wakilamba sakafu kwa ajili ya maji yanayochuruzika wakati wa usafi katika sakafu. Lakini walikufa wote baada ya kipindi Fulani.

Wengine walichukuliwa na kuwekwa katika vyumba vya baridi vyenye barafu, uchi, kama majaribio wakifanyiwa utafiti kuona ni jinsi gani mtu anaweza kutibiwa kwa haraka kutoka katika ugonjwa wa Hypothermia, huu ni ugonjwa utokanao na mtu kupigwa na baridi sana na kupoteza fahamu kuwa kama kichaa..Lakini wengi wao hawakuweza kustahimili walikufa baada ya kipindi Fulani na wengine wale waliostahimili waliishia kupata mtindio wa ubongo wa kudumu.

Wengine walichukuliwa na kutolewa misuli yao mwilini wakishuhudia kwa macho yao na kuong’olewa mifupa yao bila hata ya ganzi yoyote, na kujaribu kuupandikizwa kwa mwengine ili wajaribu kuona kama kuna uwezekano wa kuamisha viungo kutoka kwa mwanadamu mmoja hadi kwa mwanadamu mwengine kwa muda mfupi na kuendelea kufanya kazi..Wengi wao kutokana na maumivu makali walikufa na baadhi ya walipata ulemavu wa kudumu na wale waliokuwa dhaifu waliuliwa au walipelekwa katika chemba za gesi.

Walikuwa wanawachukua vijana wadogo umri katika ya miaka 11-12 na kuwafunga mahali wasipoweza kuhangaika kisha wanafungiwa nyundo juu ya vichwa vyao na ile nyundo inaachiwa ishuke juu ya vichwa vyao kila baada ya dakika kadhaa, kupima kiwango cha ustahimiliji wa mtu anapojeruhiwa maeneo ya vichwani..wengi wa hao kama wasipokufa basi wanaishia kuwa vichaa.

Wanawachukua mapacha katika pea. Na kumfanyia utafiti aidha mmoja wao, huku mwingine akimtazama, wanaweka “dai” kwenye macho ya mmoja, kupima mabadiliko ya vina saba kwa mwingine..baadaye Yule akishamaliza kufanyiwa utafiti na kuonekana kuwa hafai tena ni kufa tu, basi wanamalizia kumuua na yule mwenzake, kwasababu hana kazi tena hapo.

Waliwahasi wayahudi wengi kwa njia tofauti tofauti wengine kwa x-ray, au upasuaji au kwa madawa makali n.k. kuona ni ipi iliyonyepesi ya kuwahasia watu kwa haraka bila kupoteza muda na gharama za matibabu. Wayahudi waligeuzwa kuwa wanyama.,.Na HITLER alikuwa na kauli mbiu yake inayosema “ hawa watu wasife tu kifo cha kawaida, bali wahakikishe wanakufa vifo vya mateso”. Mambo haya unaweza ukadhani ni hadhithi au yalitokea zamani sana lakini ni mambo yaliyotekea miaka 76 tu iliyopita!. Wapo watu baadhi ambao bado hawajafa walioshuhudia hizo kambi za mateso..

Wengine walichukuliwa juu kwenye kwenye helikopta za jeshi na kupelekwa juu sana na kisha kutupwa chini, pasipo parachuti na wanajeshi wale waliruka na maparachuti kujaribu kujijaribu uwezo wao wa kuokoa watu endapo wataanguka kutoka kwenye helikopta au ndege, wengi wa wayahudi hao waliishia kuanguka chini na kufa papo kwa hapo, na wale wanajeshi wakitua chini na parachuti wakiwa salama.

Wengine walichukuliwa na kufungiwa kwenye mabehewa, na magari ya mizigo, na huko ndani inapitishwa mirija yenye gesi ya carbon-monoxide..ile ya mkaa ambayo inamuua mtu kwa haraka sana. Kisha baadaye wanafunguliwa na kutupwa kwenye mashimo huko misituni.

Na Wale wanaosalia kufanya kazi ngumu, maisha yao ni ya viboko viboko na kazi, chakula ni supu tupu mchana, na kipande cha mkate kidogo usiku..hayo ndio maisha yako ya kila siku huku ukiwa kwenye kazi ngumu..ukionyesha udhaifu wowote kule kambini uliuliwa au ulinyongwa. Ndivyo ilivyokuwa katika kambi zote.

Kaka/dada hayo ni baadhi tu mateso ndugu zetu hawa wayahudi waliyoyapitia, katika kile kipindi cha vita ya pili ya dunia, na ndio hao wanaoonekana hapo chini ya madhabahu wakisema

“Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi? Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vilevile kama wao.”

Unaona? Biblia inasema “WAKAAMBIWA WASTAREHE BADO MUDA MCHACHE”.

Mpaka itimie idadi ya wajoli wao watakaouawa vile vile kama wao. Na hiyo ndugu itakuwa si wakati mwingine zaidi ya wakati wa DHIKI KUU ambayo ipo karibuni kutokea..bado muda mfupi sana. Ni dhiki ambayo Bwana Yesu anasema haijawahi kutokea wala haitakaa itokee tena kama hiyo baada ya hapo,.Yaliyowakuta wayahudi kipindi cha Hitler ni mfano mdogo sana kulinganisha na yatakayokuja kuwakuta tena wakati wa ile dhiki kuu mpinga-Kristo atakaponyanyuka kupambana na uzao wote wa Mungu .

Mpinga-Kristo atawaua watu wote ambao watakataa kuipokea ile chapa ya mnyama, lakini wale wote ambao watakubali kuipokea hatawaua,na watakuwa ni wengi sana watakaoikubali chapa ile, kwasababu haitakuja kwa wazi kama wengi wanavyodhani, na kwa pamoja wataingoja ile siku ya Bwana inayotisha ambayo itatokea kipindi kifupi tu baada ya dhiki kuu kuisha.

Na safari hiyo haitakuwa kwa wayahudi tu peke yao, bali pia kwa wale wakristo watakaochwa kwenye unyakuo. Na hawa hawatauliwa ovyo ovyo tu barabarani kama wengi wadhanivyo, bali watapelekwa pia katika makambi ya siri ya mateso, huko ndio kutakuwa na kilio na kusaga meno. Usitamani uwepo ndugu!

Bwana ameshatuonya, Dalili zote zinaonyesha Kristo yupo mlangoni kurudi, unyakuo ukipita leo je! Utakuwenda na Bwana katika karamu ya arusi ya mwanakondoo? Au utabakia hapa? Jibu unalo ndugu. Ni maombi yangu utaanza kuyatengeneza maisha yako tena upya.

Tubu dhambi zako sasa, ili usamehewe. Kisha ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamwishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO, upate ondoleo la dhambi zako, na baada ya hapo uendelee kuishi maisha ya kumtazama Bwana na utakatifu mpaka siku unyakuo utakapokukuta.

Maran Atha!

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na Bwana atakubariki, kwani utakuwa umeshiriki kuifanya kazi ya Mungu.

2 comments: