Mathayo 12:20 “Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hata ailetapo hukumu ikashinda. 21 Na jina lake Mataifa watalitumainia.”
Wakati nautafakari huu mstari nikakumbua tukio lilotokea mahali nilipokuwa ninaishi kipindi cha nyuma, Nakumbuka wakati fulani tulipanda migomba. Na kila siku jioni na asubuhi nilikuwa na desturi ya kwenda kuimwagilia,.mpaka ikakua kiasi cha kuanza kuzaa ndizi,.Lakini siku moja usiku upepo ulivuma, usiokuwa wa kawaida, na tulipoamka asubuhi tulikuta migomba mingi kati ya ile imelala chini, na kibaya zaidi yote iliyovunjika ilikuwa ni ile iliyokuwa imeanza kutoa Ndizi, nadhani kutokana na kulemewa na uzito wa ile mikungu ndio maana ikashindwa kustahimili upepo na kuanguka, ilibaki michache tu ambayo haikuanguka na hiyo ilikuwa ni ile ambayo haijazaa..Haikuwa migomba ya hapo tu, bali mpaka ya majirani pia ilianguka..
Sasa Kitu tulichokifanya ni kujaribu kuinyanyua ili kuisapoti na mirunda ya miti, lakini mingi ilivunjia vibaya kiasi kwamba hata ukiunyanyua upande huu, unaangukia upenda ule, hata mfano uweke mirunda 6 kuusapoti mgomba mmoja bado hauwezi kusimama, na kuikata hatuwezi, tutakosa ndizi na ndizi bado ni changa. Hivyo ilitubidi kupambana nayo hivyo hivyo kujaribu kuisimamisha au kuigemeza kwa namna ambayo haitaweza kukauka mpaka hapo ndizi zitakapokomaa.Tulipitia changamoto Fulani mfano Leo utaisimamisha hivi, kesho utakuta umeanguka tena, leo utauweka hivi kesho utaikuta ipo vile. Lakini japo iliendelea kuwa katika hali mbaya ya kusua sua, lakini hatukukosa kabisa kupata ndizi, tulivuna ndizi zilizokomaa kabisa zisizo na matatizo.
Sasa ndio najiuliza kama sisi hatukuweza kuikatia tamaa migomba ile,ambayo sio kwamba ilikuwa ndio chakula pekee tulichonacho, hapana lakini hatukupenda tu kuiona katika hali ile ya kuanguka,..lakini hatukuikatika tamaa kabisa mpaka ilipofika wakati wa kutoa matunda mazuri kabisa yaliyokomaa,..UNADHANI MUNGU ATATUKATIAJE TAMAA SISI ?. Embu yatafakari tena haya maneno yaliyonenwa juu ya Bwana Yesu.
“Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hata ailetapo hukumu ikashinda.21 Na jina lake Mataifa watalitumainia.”
Mwanzi, ni shina lolote la mmea, inaweza ikawa ni mti, mchicha, mgonga n.k. Lakini anasema ukipondeka huo, hata kufikia hatua ya kukosa matumaini kabisa yeye anasema hatamalizia kuuvunja..Utambi utoao moshi ni kama umeshazima, yaani utambi ukishafikia hatua ya kutoa moshi tu, ni wazi kuwa huo tayari umeshazima huo, lakini yeye anasema hataumalizia kuuzima, moyo ambao wewe huwezi kuwa nao, huwezi kuwa na tumaini na utambi ambao unatoa moshi tu, tena kikubwa utakachofanya hapo ni kuuzima haraka usiendelee kukotelea moshi. Lakini kwa YESU haikuwa hivyo, yeye bado aliutazama, na kuuhangaikia..Na utambi huo ni sisi, mwanzi huo ni mimi na wewe!
Inawezekana maisha yako ni sawa na mwanzi uliopondeka, umefika hatua, unaona kabisa tayari ulishakosea njia, na hakuna matumaini tena ya kumrudia Mungu, umekuwa mlevi wa kupindukia, unatumia madawa ya kulevya mpaka yamesha kauthiri huwezi tena kuacha.,Umekuwa mwasherati mpaka imefikia hatua umepata UKIMWI, na wewe bado ni kijana mdogo tu na hivyo umekata tamaa ya kuishi, unaona kama jamii haiwezi kuwa na wewe tena, wala Mungu kukupokea kwa mambo uliyoyafanya. Umekuwa katika magonjwa yasiyoponyeka, huna tumaini tena. Nataka nikuambie, YESU yupo, sio marehemu,kutaka kukusimamisha tena, na kukunyanyua tena uwe mwana Mungu BUREEE!!.
Yeye ndiye aliyetabiriwa maneno haya
Isaya 61: 1 “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu BWANA AMENITIA MAFUTA niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao".
Unaona? Unaweza ukawa ni mdhaifu wa Imani, imefikia wakati unataka kusema Mungu hayupo umekuwa utambi unaotoa moshi,ni hatua moja tu imebaki ya wewe na kukata tamaa ya maisha, umekuwa katika vifungo vya giza, umeingia katika ushirikina, na uchawi, maisha yako unaona kabisa yapo hatarini kutoweka, hujui kama hata kesho utaishi kwa jinsi ulivyo katika vifungo vya hofu, wewe ni utambi unaotoa moshi, pengine unaweza ukawa ulianza vizuri na Kristo huko nyuma ulikuwa moto kweli kweli utambi wako ulikuwa unawaka vizuri huna shida yoyote , lakini wakati ukafika shughuli za dunia na udanganyifu wa mali na anasa vikakusonga, sasa umepoa huna tofauti na watenda dhambi wengine..Yesu ni wa rehema bado unatamani kukuwasha tena uangaze upya. Ametiwa mafuta kwa kazi hiyo.
Ulimwengu utakukatia tamaa, lakini Kristo anakutazama haijalishi umedondoka mara ngapi, Upo katika masononeko ya roho, upo katika tabu na maumivu mbali mbali, Njoo kwa Yesu. Leo hii sema ni mwisho naanza tena na Bwana naye atakupokea,..
Ukisoma pale mbele kidogo utaona anaendelea kusema Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, HATA AILETAPO HUKUMU IKASHINDA..Unaona? Hukumu inayozungumziwa hapo, ni kusudi la Mungu, au mapenzi ya Mungu juu ya mtu huyo…Ikiwa na maana kuwa Yesu atahakikisha mtu Yule ampokeaye..japo atakuwa ameharibika kiasi cha kutokuweza kutengenezwa tena, yeye mwenyewe atahakikisha anamfanya upya maisha yake na kuhakikisha mapenzi yote ya Baba yake aliyokusudia juu ya huyo mtu yanatimia. Na ndio maana anasema:
Mathayo 11: 28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; 30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
Ndugu ni nani awezaye kukuahidi mambo mema kama haya kama sio YESU peke yake.?Kwanini kila siku unasikia YESU ni rafiki wa wengine, Na asiwe rafiki yako? Hata sisi tulipokuwa walevi, na wazinzi, na watukanaji, wa endaji disco,watazamaji pornography, tulikuwa katika hofu,japo mbele za watu tulijifanya wenye furaha siku zote, na wenye ujasiri..Lakini siku YESU alipotupa raha nafsini mwetu ndipo tulipojua hakika raha halisi ipo wapi?..Kwahiyo tunafahamu vizuri hali unayopitia wewe uliye katika dhambi, kwasababu na sisi tulikuwa huko, lakini tumeonja huku, na tumejua hakika Bwana ni mwema.
Njoo! Kwa mwokozi wako ambaye ni mwokozi wetu pia, muda unazidi kwenda, moja ya siku hizi UNYAKUO utapita, au kama hautapita basi KIFO kitakukuta, sasa huko uendako ni nani atakuwa mtetezi wako? Kama umemkataa mtetezi wako angani u hai?..Ukimpokea leo atakuwa ni rafiki mwema kwako.
Bwana akuangazie rehema zake.
Ubarikiwe na Bwana.
No comments:
Post a Comment