Kama unakumbuka Isaka wakati anawabariki wanawe Esau na Yakobo, Yakobo alimnyang’anya ndugu yake mbaraka wake, kwasababu ya yeye kutokuujali ukubwa Mungu aliompa. Hivyo ikatengeneza aina fulani ya chuki kati ya hao ndugu wawili, yaani Esau na Yakobo, na Baba yao tunasoma baada ya kumbariki Yakobo alimwambia Esau maneno haya…
Mwanzo 27: 38 “Esau akamwambia babaye, Una mbaraka mmoja tu, babangu? Unibariki mimi, mimi nami, Ee babangu. Esau akapaza sauti yake, akalia.39 Isaka, baba yake, akajibu, akamwambia,Angalia, penye manono ya nchi patakuwa makao yako,Na penye umande wa mbingu unaotoka juu.40 Kwa upanga wako wewe utaishi, nawe utamtumikia nduguyo; NA ITAKUWA UTAKAPOPONYOKA, UTALIVUNJA KONGWA LAKE KATIKA SHINGO YAKO.41 Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo”.
Kwahiyo unaweza kuona hapo hizo Baraka, hazikuwa kwa Esau na Yakobo tu peke yao, bali ni kwa vizazi vyote vya Esau na vizazi vyote vya Yakobo,.Kwamba Israeli atakuwa akimshinda Esau lakini endapo Israeli atalemaa katika roho basi Esau atampiga na kulivunja kongwa lake katika shingo yake.
Sasa hapa baada ya miaka mingi sana zaidi ya miaka 400 Kupita..tunaona uzao wa Yakobo ambao ndio wana wa Israeli unakutana tena katika mapambano na uzao wa Esau ambao ndio hao Waamaleki. Hivyo Israeli walijua kabisa endapo tusipokuwa makini, na hawa wakiwa na bidii basi unabii unaosema hatutamshinda Esau utatimia juu yetu..Hivyo ile vita haikuwa ya kawaida palikuwa na changamoto kubwa sana katika, Israeli hawakuwa na namna nyingine zaidi ya kumgeukia Mungu na kumtegemea yeye…
Ndipo tunasoma Musa baada ya kupata hizo habari kuwa waamaleki wamewazunguka alikwenda kumwomba Mungu wa Israeli na Bwana akampa maagizo ya kufanya kama tunavyosoma katika…
Kutoka 17: 8 “Wakati huo Waamaleki wakatokea, wakapigana na Israeli huko Refidimu.9 Musa akamwambia Yoshua, Tuchagulie watu, ukatoke upigane na Waamaleki; kesho nitasimama juu ya kilele kile, na ile fimbo ya Mungu nitakuwa nayo mkononi mwangu.10 Basi Yoshua akafanya kama Musa alivyomwambia, akapigana na Amaleki; na Musa na Haruni na Huri wakapanda juu ya kile kilima.11 Ikawa, Musa alipouinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda.12 Lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito; basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa.13 Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa ukali wa upanga”.
Hapa tunaona mkono wa Musa ndio uliowapa ushindi waisraeli, alipounyanyua juu, ndivyo waisraeli walivyokuwa wanapata nguvu vitani, na alipoushusha waamaleki waliwapiga waisraeli..Lakini kama tunavyosoma mwisho wa siku Israeli walishinda kutokana na Mikono ya Musa kusimama juu muda wote.
Ni nini tunachoweza kujifunza katika habari hii ??
Wakristo sisi ni uzao wa Mungu, ambapo tumefanyika kuwa uzao wa Mungu kweli kweli, kupitia Yesu Kristo Bwana Wetu, Mkuu wa Uzima, sisi tunafananishwa na Uzao wa YAKOBO ambao umebarikiwa…Lakini pia upo uzao wa yule Adui, huo unafanana na uzao wa ESAU, na huo kazi yake ni kupambaba na sisi kila siku kutupinga katika safari yetu ya kwenda mbinguni,..Na Bwana alitoa unabii kama alivyotoa kwa Yakobo na Ndugu yake kwamba Yakobo atampiga Esau lakini pia Esau akiponyoka atamvunja kongwa Yakobo katika shingo yake {Kwa tafsiri iliyo nyepesi ni hii: Esau akijitahidi na kupata nguvu, basi ataweza kuondoa utawala wa ndugu yake juu yake}..Na pia Bwana alizungumza juu yetu, na kusema.
“nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.Mwanzo 3:15”
Wengi tunaishia hapo kwamba, uzao wako utamponda kichwa, lakini tunasahau kuwa pia uzao wa nyoka umepewa mamlaka ya kutuponda sisi kisigino, tusipokuwa makini”
Kwahiyo katika ulimwengu wa Roho ni vita vikali vinaendelea, hivyo inahitajika umakini mkubwa sana, na msaada ya Mungu.
Sasa Biblia inasema… “kama vile Musa alivyomwinua nyoka wa shaba jangwani” ili kila amtazamaye yule nyoka wa shaba apone, ndivyo hivyo hivyo Mwana wa Adamu alipaswa ainuliwe msalabani ili kila mtu amtazamaye aokolewe..
Kadhalika kama Musa alivyounyanyua mkono wake juu ili kila Mwisraeli aliyeko vitani apate kupona na kuteka na kupata ushindi dhidi ya Maadui zake..NA WAKRISTO VIVYO HIVYO HATUNA BUDI KUMWINUA YESU KRISTO KATIKA MAISHA YETU ili tuweze kupata ushindi dhidi ya maadui zetu (yaani roho ya uadui inayotenda kazi ndani ya watu na majeshi ya mapepo wabaya).
Na kumbuka kumwinua Kristo katika maisha yetu sio kumwimbia mapambio na nyimbo za kuabudu, hiyo ni sehemu mojawapo, Lakini sehemu kubwa ya kumwinua Mungu katika maisha yetu ni kumaanisha kumwamini kwa kuzitubia dhambi na kuzicha, na kubatizwa na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu na kuishi maisha ya utakatifu yanayoonekana mbele za watu kuanzia huo wakati na kuendelea, huko ndiko kumwinua Kristo kunakozungumziwa.
Kumbuka pia hakuna ushindi pasipo Yesu Kristo kuinuliwa juu ya maisha yetu. Musa alipoishiwa nguvu watu walikuja kumsaidia kuitegemeza mikono yake ili isishuke…Na sisi katika maisha yetu ya kikristo ya vita, tunapoishiwa nguvu…tunapaswa tufanye juu chini tusiiangushe imani yetu kwa Kristo tuishikilie kwelikweli kwa bidii zote maana hiyo tumekabidhiwa mara moja tu!…Biblia inasema “Mpende Bwana Mungu wako kwa nguvu zako zote, kwa akili zako zote, na kwa moyo wako wote”.
Vinginevyo tukisema tuiache Imani, shetani yupo na amepewa amri ya kutuponda visigino. Amri hiyo kapokea kutoka kwa Mungu.
Ndugu unayesoma ujumbe huu, Yesu Kristo ni muhimu sana katika maisha haya…kama ulimsikia kwa juu juu tu!! kanisani, au mahali popote pale, kama umehubiriwa ni wa-mafanikio-ya-kibiashara Yesu ni zaidi ya hapo!…. jaribu tena kutenga muda umtafakari, hakuna tumaini, wokovu, hakuna maisha, hakuna mafanikio yoyote nje ya Yesu Kristo!...Waliomwamini ndio wanaoitwa wabarikiwa. Huwezi kumpendeza Mungu wala kumwelewa Mungu, wala kumshinda shetani nje ya Yesu Kristo!...Kama ule mkono haujanyanyuliwa juu (Yesu Kristo) hata kama unajiona unatenda wema kiasi gani kama hujamnyanyua juu ni kazi bure! Ni sawa na mtu anayefanya kazi katika shirika ambalo hajaajiriwa, wala hawamjua akitumai kupata mshahara mwisho wa mwezi kutoka huko.. mipango yako ni mizuri lakini nje! Ya Yesu Kristo ni bure!...
Suluhisho ni kumtamani aje aingie katika maisha na kuanza maisha mapya katika yeye..
Bwana akubariki sana.
Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.
No comments:
Post a Comment