Kutokujizuia ni kitendo cha kukosa uwezo wa kutawala kitu fulani kisitokee kisichopaswa kufanyika kwa wakati huo. Kwa mfano mtu anapokuwa mlevi wakati mwingine anajikuta amejisaidia pale pale, au kinywa chake kinaanza kuzungumza maneno yasiyokuwa na maana, pengine ataanza kutukana au kufoka..Huko ni kutojizuia..mambo ambayo mfano angekuwa na akili timamu, asingeweza kuyafanya hadharani.
Biblia inasema moja ya dalili kubwa itakayotuonyesha kuwa tunaishi katika siku za mwisho ni kuwepo kwa wimbi kubwa la watu wasioweza KUJIZUIA. Na kutojizuia kunakozungumziwa hapo sio kujizuia kutokutokwa na haja, hapana bali kutojizuia kutenda maovu hadharani mbele za watu, hivyo si watu wema wanaozungumziwa hapa bali wanazungumziwa wale walio waovu, ili kutofautisha uovu ule wa nyuma na huu wa siku za mwisho, kumbuka waovu wa zamani walikuwa na kitu kinachoitwa Kujizuia, lakini waovu wa siku za mwisho biblia inaweka wazi kuwa hicho kitu hakitaonekana ndani yao kabisa.
2Timotheo 3:1-171 Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.2 Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,3 wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, WASIOJIZUIA, wakali, wasiopenda mema,4 wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;5 wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.
Ilikuwa zamani, mwanamke kahaba ni mtu wa kujificha, anafanya ukahaba wake kwa siri hata ni ngumu kumtambua, mavazi yake ya kikahaba alikuwa anayavaa usiku tu tena katika eneo la shughuli zake,nje ya hapo huwezi kumkuta, ilikuwa huwezi kumwona hadharani ovyo ovyo eti anazunguka na uwazi wake barabarani, haikuwahi kutokea hivyo wakati wowote. lakini angalia sasa, makahaba wanashindwa kujiuzia kufanya mambo yao, wanakosa ule uwezo wa kutawala tamaa zao, ile hofu ya watu kuwaona na kuwachukulia hivi au vile haipo tena ndani yao, wapo tayari kupiga picha za uchi, na kutengeneza video za zisizofaa ambazo hazistahili kabisa kuwepo, na kwa ujasiri kabisa wana zi-post katika mitandao, ili watu wote wawaone, na kibaya zaidi wanaofanya hivyo wengi wao ni watu wanaojulikana, ili kusudi kwamba uchafu wao uweze kuwafikia watu wengi zaidi kwa muda mfupi, hizi ndizo ishara madhubuti za siku za mwisho.
Sio kana kwamba hayo mambo yalikuwa hayafanyiki zamani, hapana yalifanyika kwani biblia inatuambia hakuna jambo jipya chini ya mbingu, lakini kwanini unaona kama siku hizi maovu yameongezeka zaidi ya zamani,? Jibu ni kwamba hayajaongezeka kwa kiwango kile unachofikiri bali kinachoendelea sasa ni kwamba wafanyao maovu wa sasa wamepoteza kile kitu kinachoitwa kujizuia ndani yao..Roho ya kutokujali lolote imewavaa, roho ya “fuata mambo yako”, roho ya “ishi maisha yako”..roho ya “kutokujali” ndio inayotawala maisha yao. Na ndio maana hushangai hata kuona watu wa karne hizi watu waki-tengeneza video wanazini na wanyama n.k..Si ajabu tena kwao, kudhihirisha aibu zao wazi. Inasikitisha sana!
Kutukana hadharani hakukuwepo zamani, lakini sasa viwango vya matusi vimekithiri, mabarabarani, kwenye nyimbo za kidunia, kwenye mitandao, si watu wazima si watoto wadogo, maneno yanayozungumzwa huwezi kuamini kama marika kama hayo yanaweza kutoa maneno magumu kama hayo katika vinywa vyao.
Mashoga na wasagaji, wanajitangaza hadharani, hawajali tena hata vyombo vya dola na huku wanajua kabisa kwamba Sheria za nchi haziruhusu vitendo hivyo na kwamba mtu anayefanya hivyo adhabu yako ni kali, wao hilo wanalolioana kabisa hawalijali sembuse Mungu wasiyemwona?. KUTOJIZUIA.
Washirikina waendao kutafuta mali kwa waganga wa kienyeji, zamani walikuwa hawadhubutu kuiathiri jamii hadharani kama wafanyavyo sasa hivi, lakini angalia leo, mtu anafikia hatua hata ya kwenda kukata viungo vya watu wasio na hatia (ma-albino, na mtatiti ya mabinti wadogo) kwa tamaa tu za mali.
Kutokujizui, Biblia inasema pia hapo juu siku za mwisho watatokea watu WAKALI, Wasiopenda mema, ile dhambi inapata nguvu mpaka sasa hawezi kutulia ndani, inajidhihirisha nje bila kujali kitu chochote wala mtu yoyote..
Dalili nyingine inayozungumziwa hapo juu ni “KUSINGIZIA”..Tafsiri halisi iliyotumika hapo, kusingizia maana yake, ni “kumzunguzia mwingine vibaya”, au “kumsengenya mtu” kwa lugha nyepesi iliyozoelewa sasa Ni ‘’Umbea”. Kusengenya ni KIU mtu anakuwa nayo ya kutaka kupakua habari za maisha ya mtu mwingine kwa nia ya udadisi ili kupata huko mambo ya kumzungumzia yasiyopendeza mbele za Mungu..
Haya mambo zamani yalikuwepo lakini sio kwa kiwango cha uwazi kilichopo sasa, utakuta mtu anashindwa kujizuia kabisa, Anashindwa kufanya mambo yake mwenyewe, anashindwa kuwazungumzia watu kwa wema, anajikuta kutwa kuchwa ni kudadisi maisha ya watu wengine kwa ubaya. Sasa ukiona wimbi la watu wa namna hii linaongezeka basi fahamu kuwa tunaishi katika majira ya mwisho wa Dunia.
Ndugu yangu. Kama vile hilo andiko linavyosema “siku za mwisho kutakuwako na nyakati za HATARI ”. Fahamu kuwa nyakati zenyewe ndio hizi tunazoishi..Ikiwa utashindwa kujizuia mwenyewe na kuona kila kitu kufanya ni SAWA TU!...Zamani ulikuwa unaona aibu kuvaa vimini na kutembea navyo barabarani lakini sasa unaona hakuna shida yoyote! Ujue kuwa upo katika hatari kubwa sana..roho ya kutokujali umekuingia.
Ukiona zamani ulikuwa ukitukana unajisikia vibaya lakini sasa matusi yamekuwa ni sehemu ya maisha yako. Ujue kuwa ile roho ya kutokujali imekuvaa..Kama vile wale watu wa sodoma na gomora, jinsi walivyokuwa na tabia ya kutokujizuia hata kufikia hatua ya kutaka kulala na wageni wale (malaika wa Mungu) waliokuja yamkini kusitiri uovu wao,lakini wao wakashindwa kujizuia. Jambo gani lilitokea muda mfupi baada ya pale?. Kwanza kabla hata maangamizi hayajawafikia walipigwa upofu. Na upofu ule ni wa daima..Vivyo hivyo na kwa watu wasiojizuia sasa, Upofu unakuja, na upofu huo ni wa daima, ukishamkuta tu mtu, basi huyo mtu hata afanyeje ni wa kuangamizwa tu! hawezi kutubu tena, neema inakuwa haipo tena juu yake, hata ahubiriweje injili.
Zamani ulikuwa unajisikia vibaya kula rushwa, na kufanya utapeli lakini sasa yote yamekuwa sawa kwako, zamani uliogopa hata kusogelea msonge wa waganga wa kienyeji lakini siku hizi pamekuwa kama nyumbani kwako, namba za waganga na wataabiri wa nyota zimejaa kwenye simu yako ya mkononi. Upo katika hatari kubwa sana.
Hujizuii mwili wako, unatembea nusu-uchi barabarani na ku-post picha chafu mitandaoni, humwogopi tena Mungu kama hapo zamani, unakuwa ni sababu ya watu wengi kumkosea Mungu, kwa kutazama vitu unavyovipost na mavazi unayoyavaa..Dada upo katika HATARI kubwa sana. Hukumu yako haitakuwa sawa na wale wengine..siku ile fahamu tu utapigwa sana, kama usipotubu, kwasababu uliijua kweli na bado ukaendelea kufanya kwa makusudi. Kuzimu ipo ni kitu halisi kabisa, mtu yeyote asikudanganye kuwa hakuna kuzimu, ipo kabisa.
Tukiyajua hayo, basi ni wajibu wetu kumrudia muumba wetu, kabla ya huu uharibifu mkubwa ambao utaikumbuka dunia nzima haujatukuta sisi.. Tubu dhambi zako sasa, ukabatizwe upate ondoleo la dhambi zako.
Mwenye sikio asikie Neno hili, ambalo Roho wa Mungu anatuonya watu wa kizazi hiki. Kwamba tujihadhari nacho.
Ubarikiwe.
Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.
No comments:
Post a Comment