"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, February 6, 2019

JE! UMECHAGULIWA KABLA YA KUWEKWA MISINGI YA ULIMWENGU?

Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze Maneno ya Mungu, kwa Neema zake, leo tutajifunza somo linalosema, Kuchaguliwa kabla ya kuwekwa misingi ya Ulimwengu. 
Tunajua kuwa Mungu tunayemwabudu, yaani Yule aliyekuwa anaabudiwa na wana wa Israeli ambaye sasa tunamwabudu na sisi watu wa Mataifa, Mungu muumba wa Mbingu na nchi hana mwanzo wala hana mwisho, sentensi hiyo tu! Inatosha kutujulisha yeye ni Mkuu kiasi gani, yeye ni zaidi ya upeo wetu wa kufikiri. Kwasababu kitu kisichokuwa na mwanzo wala kisichokuwa na mwisho ni kitu cha namna gani hicho?.

Hivyo basi kama hana mwanzo wala hana mwisho ni dhahiri kuwa atakuwa na uwezo wa kufahamu mwanzo wa ulimwengu na mwisho wa Ulimwengu mzima, ndio maana katika Neno lake anatabiri yatakayotokea katika siku za mwisho maelfu ya miaka nyuma kabla hata ya hiyo siku kutokea…Anasema siku za mwisho kutatokea hiki na kile, anaendelea kusema, baada ya dunia kuisha kutakuja utawala wa miaka 1000, anaendelea kusema baada ya utawala wa miaka 1000 kuisha kiti cheupe cha hukumu kitawekwa, ambapo wafu wote watafufuliwa na kuhukumiwa n.k n.k..Mambo hayo yote Bwana tayari anayajua.

Na kama anajua mwisho wa dunia katika mtiririko wote, ni dhahiri kuwa atakuwa anajua pia mwanzo na mwisho wa kila mwanadamu katika mtiririko wote…ikiwa na maana kuwa anajua ni yupi ataokolewa na yupi hataokolewa, ni yupi ataingia mbinguni na ni yupi hataingia mbinguni siku ya mwisho…Na kama anayajua hayo ni dhahiri kuwa ni yeye huyo huyo ndiye anayechagua ni yupi ataokolewa na yupi hataokolewa..Kwasababu Bwana Yesu mwenyewe alisema “Hakuna awezaye kuja kwangu asipovutwa na Baba yangu aliyenipeleka (Yohana 6:44)”. Kwahiyo ni Roho Mtakatifu ndiye anayemvuta mtu kwa MUNGU na sio mtu mwenyewe anayejipeleka kwa Mungu.

Kama Mungu yupo hivyo pengine utasema, kwanini aumbe wengine hivi wengine vile? Huo ni kama vile udhalimu Fulani hivi…Jibu la swali hilo, Mtume Paulo alilitoa kwa uweza wa Roho akasema.. Tusome:

Warumi 9:13 “Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia.
14 Tuseme nini basi? Kuna udhalimu kwa Mungu? Hasha!
15  Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye.
16 Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.
17 Kwa maana maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote.
18 Basi, kama ni hivyo, atakaye kumrehemu humrehemu, na atakaye kumfanya mgumu humfanya mgumu.
19 Basi, utaniambia, Mbona angali akilaumu? Kwa maana ni nani ashindanaye na kusudi lake?
20 La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi?.
21 Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?”.
Umeona hapo? Hakuna awezaye kushindana na kusudi la Mungu, anafanya yote kama atakavyo yeye… “HILO LINAOGOPESHA SANA.” Sisi wanadamu hatuwezi kumwuliza Mungu kwanini anafanya vile au kwanini anafanya hivi.. Ulishawahi kuaamka asubuhi na kuanza kumwuliza Mungu kwanini hakutuumba na mabawa, kama alivyowapa malaika? nasi tuwe tunaruka juu kama ndege?... Au kuku amwulize Mungu kwanini yeye kaumbwa kuku na wala si mtu? Ndivyo ilivyompendeza yeye tuwe hivi tulivyo…
Sasa swali linakuja nitajuaje kuwa mimi nimekusudiwa wokovu, na tena Nimechaguliwa kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu?.

Jibu la swali hilo hatuwezi kulipata kwa kufunga na kuomba Mungu atufunulie, wala hutuwezi kulipata kwa kukisia tu! Wala hatuwezi tukasema kwa kukisia tu Kwamba mimi nitakuwa ni miongoni wa waliochaguliwa kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu. Ili tujue kwamba sisi ni miongoni wa waliochaguliwa Jibu la swali hilo tutalipata katika BIBLIA TU!
Neno la Mungu linasema hivi katika kitabu cha.
 Waefeso 1: 3 “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo;
4 kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.
5 Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake”.
Ukitafakari kwa makini mstari huo wa nne utagundua vigezo vya kuchaguliwa tangu asili ni vipi?...hapo anasema “kama alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu ILI TUWE WATAKATIFU, WATU WASIO NA HATIA MBELE ZAKE KATIKA PENDO”…Zingatia hili neno “ILI TUWE WATAKATIFU”…hii ikiwa na maana kuwa mtu aliyechaguliwa kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu..alama yake ni UTAKATIFU. Kama Yesu Kristo alivyokuwa mtakatifu tunapaswa tufanane naye ndio tuwe na uhakika kwamba na sisi ni miongoni mwa lile kundi lililochaguliwa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu..
Na kama tunavyojua UTAKATIFU chanzo chake ni ROHO MTAKATIFU kama jina lenyewe lilivyo..roho chafu matunda yake ni uchafu, roho ya uzinzi matunda yake ni uzinzi, kadhalika na Roho takatifu matunda yake ni utakatifu. Kwahiyo kwa ufupi mtu yeyote ambaye maisha yake ni ya UTAKATIFU katika Kristo Yesu,huyo mtu asilimia 100 amechaguliwa kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu. Hakuna alama nyingine zaidi ya hiyo. Kwasababu anafanana na Yesu Kristo na kama maandiko yanavyosema pia katika kitabu cha waebrania.
Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, NA HUO UTAKATIFU, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao” 
Unaona hapo? Tiketi ya kumwona Mungu ni UTAKATIFU. Kwahiyo kwa hitimisho namna ya kujichunguza kama umechaguliwa tangu asili ni kujichunguza maisha yako je! Ni ya utakatifu? Au sio ya utakatifu, hapo ndipo utakapojijua wewe upo kundi gani na ndipo utakapoijua roho iliyopo ndani yako? Je ni roho chafu au ni roho mtakatifu?..je! maisha yako yanafanana na maisha ya Yesu Kristo au Yuda eskariote, maana maandiko yanasema.

Warumi 8: 29 “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. 30 Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita,hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza”.

Je! Na wewe ni mtakatifu kama mwana wa Mungu, Yesu alivyokuwa mtakatifu, umefananishwa na yeye?..au ni mla rushwa?, au ni msengenyaji?, au ni mzinzi, au Ni mwasherati? au ni mtazamaji wa pornography au mfanyaji masturbation? Au wewe ni msagaji? Na kahaba? Je! Ni mlawiti?, je! Ni mvaaji wa nguo fupi na suruali zinazokuonyesha maungo yako? je ni muuaji au mhudhuriaji kwa waganga na disko? Je! Ni mtukanaji. Kama hayo yote  unayafanya na bado unakwenda kanisani na kujiita mkristo na kujifariji kwamba upo katika mstari wa watakaoenda mbinguni..napenda nikuambie ndugu yangu “ichunguze hiyo roho iliyopo ndani yako” sio roho mtakatifu bali ni roho nyingine ya Yule adui, inayokuongoza kwenda katika ziwa la moto. Roho wa Mungu aletaye utakatifu ndani ya mtu huyo ndio MUHURI AU ALAMA ya kukutambulisha kwamba wewe ni umechaguliwa tangu asili au la! Kwamba wewe umekusudiwa wokovu au la! Maandiko yanasema hivyo. (Waefeso 4: 30 “Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye MLITIWA MUHURI hata siku ya ukombozi”).

Wagalatia 5:19 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, KATIKA HAYO NAWAAMBIA MAPEMA, KAMA NILIVYOKWISHA KUWAAMBIA, YA KWAMBA WATU WATENDAO MAMBO YA JINSI HIYO HAWATAURITHI UFALME WA MUNGU.”

Ndugu yangu, naamini na wewe ni mmoja wa waliochaguliwa kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ndio maana Roho Mtakatifu aletaye utakatifu hajakuacha kabisa yupo nje! Anagonga mlango wa moyo wako anataka kuingia ndani yako AKUTIE MUHURI WA UTAKATIFU, ili uwe na tiketi ya kumwona Mungu.

Lakini kama huisikii sauti yake wala kwako haina maana basi wewe sio miongoni mwa walio wake..kama biblia inavyosema katika Warumi 8:9 “Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. LAKINI MTU AWAYE YOTE ASIPOKUWA NA ROHO WA KRISTO, HUYO SI WAKE.”.

Swali linarudi lile lile..Je! wewe ni miongoni mwa walio wake au wasio wake??..je! wewe ni miongoni mwa watakaoenda mbinguni au watakaoenda katika lile ziwa la moto? Je! Unaisikia sasa sauti ya Roho mtakatifu anayekutaka utubu na uwe mtakatifu au huisikii?.. Jibu unalo wewe.
Ikiwa unataka leo hii Roho Mtakatifu aingie ndani yako, uwe miongoni mwa waliochaguliwa kabla ya msingi wa ulimwengu, unachopaswa kufanya hapo ulipo, tenga sio chini ya dakika 10 au zaidi hapo ulipo Tubu! mwambie Bwana akusamehe maovu yako yote, mweleze yote usifiche hata moja maana yeye anakujua kuingia kwako na kutoka kwako?..na kisha baada ya kufanya hivyo dhamiria kuacha hayo maisha ya dhambi uliyokuwa unaishi..usiende kulewa tena, usiende kufanya uasherati tena, achana na kampani mbovu n.k Kisha hatua ya pili inayofuata Nenda katafute ubatizo sahihi wa kweli wa kimaandiko nao ni wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo, ili kumbukumbu la dhambi zako zifutwe kabisa kabisa… na baada ya hapo Roho Mtakatifu ataingia ndani yako na kukupa wewe nguvu na uwezo wa kushinda dhambi na kuishi maisha ya utakatifu. 

Uwezo huo au nguvu hiyo haiji isipokuwa kwanza umedhamiria kuacha njia zako mbaya za nyuma, wengi wanasema wametubu na kukoka lakini bado mioyo yao ipo Misri, na ndio maana wanashindwa kuishinda dhambi kwasababu hiyo.. Ile nguvu ya Roho Mtakatifu haijashushwa ndani yao kutokanana na mioyo yao kutokuwa thabiti kwa yeye waliyemtubia dhambi zako.

Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja KWA JINA LAKE YESU KRISTO, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.”

Hivyo fanya hivyo leo na Bwana atakuangazia Nuru yake.Hapo ndipo utapata uhakika ya kuwa umechaguliwa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu. Kesho si yako, hizi ni siku za mwisho.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na Bwana azidi kukubariki.

No comments:

Post a Comment