"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, March 28, 2019

MADARAKA YA WAKATI MKAMILIFU.


Shalom mtu wa Mungu, ni kwa rehema za Bwana tumeiona siku ya leo, hivyo hatuna budi kumshukuru sote pamoja kwa mema anayotutendea na pia kushiriki katika kujifunza maagizo yake kila iitwapo leo. Hivyo nakukaribisha tutafakari kwa ufupi juu ya haya “madaraka ya wakati mkamilifu” yanayozungumiwa kwenye maandiko, tutayaona ni yapi, na yatakuja wakati gani?.
Biblia inasema.
Waefeso 1:9 “akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo.
10 Yaani, KULETA MADARAKA YA WAKATI MKAMILIFU atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu VYA MBINGUNI na vitu VYA DUNIANI pia. Naam, katika yeye huyo;
11 na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake.”
Sasa Kama ukisoma huo mstari wa 10 kwenye tafsiri nyingine za biblia kwa lugha iliyo nyepesi unaweza kusomeka hivi,
“Wakati mkamilifu utakapofika, basi vitu vyote ya mbinguni na duniani vitajumuishwa pamoja kwa yeye huyo..Au wakati uliokusudiwa (wa Mwisho) basi mambo yote ya mbinguni na ya duniani yataletwa pamoja katika yeye huyo (KRISTO YESU)..
Ndugu tukimjua Kristo, na ukuu wake na uweza wake, basi hatutaishi maisha ya kutokujali tu, tukiwa hapa duniani, hatutauchukulia ukristo wetu kama kitambulisho cha dini tu kama wengine wanavyofanya badala yake tutaishi kwa mitume wa zamani walivyoishi,..Leo Tunaishi maisha ya uvuguvugu na machafu kila siku na huku bado tunajiita ni wakristo, ni kwasababu tumekosa ufunuo wa kumjua Yesu Kristo ni nani katika maisha yetu, tumekosa shabaha ya kufahamu ni mambo gani na gani yalimfanya Yesu kuja duniani, tunadhani alikuja kufa tu msalabani halafu basi, na sasa ameketi mkono wa kuume wa Mungu mbinguni akisubiria kurudi tena kuja kunyakua watu wake….Hatujui mengine zaidi ya hayo.

Hiyo ndio sababu inayotufanya tunaishi maisha ya kuukinai wokovu, tunaposoma habari za watu ambao walijitoa maisha yao, watu ambao hawakupenda maisha yao hata kufa kwa ajili ya Bwana, tukisoma habari ya Ibrahimu ambaye japo Mungu alimpa kila kitu lakini aliishi kama mpitaji hapa duniani kukaa kwenye mahema, akiutazamia mji wenye misingi (YERUSALEMU MPYA),sio hii ya sasa inayoharibika,(Waebrania 11:8)…watu ambao Mungu aliwapa kila kitu lakini hawakupumbazwa na vitu walivyopewa, macho yao wakati wote yalielekea juu, mfano wa Ibrahimu na Ayubu…Sio kana kwamba walikuwa hawajipendi hapana bali waliona mbele, walipokea ufunuo wa mambo yanakuja na hivyo wakaanza kujijengea misingi mizuri kuanzia hapa duniani ili wakifika kule, iwe heri kwao. Lakini sisi tunaona wokovu ni kama kitu-baki, ni kitu tu cha ziada, na sio kila kitu katika maisha yetu.

Hatujui kuwa Kristo sasa yupo katika hatua za mwisho kabisa za kutimiliza mambo yake yote, na yeye mwenyewe hakutuficha siku anakwenda kwa Baba alisema, “ninakwenda kuwaandalia makao”,

Sasa ni vizuri kufahamu kuwa Kristo alipokuwepo duniani alikuja kufanya upatanisho wa kitu vikuu vitatu.

1) UPATANISHO KATI YA SISI KWA SISI

2) UPATANISHO KATI YA SISI NA MUNGU

3) UPATANISHO KATI YA MBINGU NA DUNIA.

Kristo alikuja kutupatanisha sisi kwa sisi, kumbuka hapo mwanzo wayahudi (yaani Waisraeli) walikuwa hawachangamani na mataifa kabisa, Israeli limekuwa likijulikana ni Taifa teule la Mungu, Mungu alilolibariki kupitia Ibrahimu. Ilikuwa hakuna namna yoyote ile sisi watu wa mataifa tungeweza kumfikia Mungu, lakini kwa kupitia Bwana Yesu, sisi ambao tumezaliwa mara ya pili ni mamoja sawa na wayahudi, mbele za Mungu hakuna aliye juu ya mwenzake, bali wote tunakubaliwa sawa kwa kupitia damu ya Kristo. Hiyo ni nafasi kubwa sana ya upendeleo..Jaribu kufikiria taabu walizozipata wengine kwa muda mrefu sisi tunakuja kuzila kiuwepesi namna hiyo. Ni neema kubwa sana. Jambo hilo unaweza kulipata katika kitabu cha Waefeso..

Waefeso 2: 11 “Kwa ajili ya hayo kumbukeni ya kwamba zamani ninyi, mlio watu wa Mataifa kwa jinsi ya mwili, mnaoitwa Wasiotahiriwa na wale wanaoitwa Waliotahiriwa, yaani, tohara ya mwilini iliyofanyika kwa mikono;
12 kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani.
13 Lakini sasa, KATIKA KRISTO YESU, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo.
14 Kwa maana yeye ndiye amani yetu, ALIYETUFANYA SISI SOTE TULIOKUWA WAWILI KUWA MMOJA; AKAKIBOMOA KIAMBAZA CHA KATI KILICHOTUTENGA.
15 Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani.
16 AKAWAPATANISHA WOTE WAWILI NA MUNGU KATIKA MWILI MMOJA, KWA NJIA YA MSALABA, AKIISHA KUUFISHA ULE UADUI KWA HUO MSALABA.
17 Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu.
18 Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja.
19 Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu”.

Hali kadhalika Kwa kumwamini tu Yesu na uweza katika damu yake, basi moja kwa moja tunakuwa tumepatanishwa na Mungu na hivyo tunakuwa na uwezo wa kupakaribia patakatifu pa patakatifu mahali Mungu alipo juu sana, na kuzungumza naye uso kwa uso katika roho, na kupokea rehema itokayo kwake. mambo ambayo hapo mwanzoni hayakuwepo, ilikuwa ni kuhani mkuu tu, alipelekea maombi yake katika maskani iliyofanywa na wanadamu huku chini mfano wa ile ya mbinguni, kisha Kerubi wa Mungu pale chini ndiye aliyekuwa anayachukua hayo maombi na kuyasogeza mbele ya kiti cha enzi cha Mungu huko juu mbinguni, lakini sasa kwa kupitia damu ya Yesu, sisi wenyewe tuingia moja kwa moja mbinguni kwa damu ya Yesu, na kupeleka haja zetu na majibu ya maombi yetu, sawa tu na makerubi na malaika wa Mungu walio mbinguni, sisi na wao hatuna tofauti yoyote, mbele za Mungu tukiwa ndani ya Kristo ni kitu kimoja.

2 Wakorintho 5: 17 “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.
18 Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, ALIYETUPATANISHA SISI NA NAFSI YAKE KWA KRISTO, NAYE ALITUPA HUDUMA YA UPATANISHO;
19 yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho”.

Na Jambo lingine la mwisho Kristo aliloleta NI KUIJUMUISHA MBINGU NA NCHI KUWA KITU KIMOJA..vitu vya mbinguni na vitu vya dunia, Sasa Hakuna yoyote ambaye angeweza kufanya jambo hili, inahitaji nguvu ya ajabu inayovuka viwango vya fikra za kibinadamu, inahitaji iwe muumba kufanya shughuli hii..
 
Wakolosai .1:9 “Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; 20 na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; KWA YEYE, IKIWA NI VITU VILIVYO JUU YA NCHI, AU VILIVYO MBINGUNI”.

Sasa jambo hilo ndilo linalokuja kutokea katika WAKATI MKAMILIFU ULIOKUSUDIWA, Yesu aliposema naenda kuwaandalia makao, ili nilipo mimi na nyinyi muwepo, na makao hayo yamegawanyika katika sehemu tatu, ya kwanza ni makao ya roho zetu ambayo hata sasa sisi tuliopokea Roho Mtakatifu tupo ndani yake, Waefeso 2: 6 “Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu;

Na makao ya pili ni MIILI MIPYA ambayo tutaipokea tukifika mbinguni miili isiyoharibika, na makao ya tatu ndio hiyo NCHI MPYA NA MBINGU MPYA…Ambayo hiyo sasa itashuka kutoka mbinguni na kutua hapa duniani…Itashuka Hapa hapa duniani hatutaishi mbinguni milele, makao yetu yatakuwa ni hapa maandiko yanasema hivyo.

Na ndio hapo hilo neno linalosema “atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia.” Ndipo litakapotimia,

Ndugu yangu Kristo anayo nafasi kubwa sana maishani mwetu, kwanza kati yetu sisi wanadamu, pili kati yetu sisi na Mungu na tatu kati ya makao yetu ya sasa na ya yale ya baadaye..Embu jaribu kufikiria, ikiwa leo hii hutaweza kuzishiriki Baraka za Ibrahimu tu ambazo Mungu alimwahidia yeye na uzao wake (Wayahudi) kuwa watakuja kuirithi nchi, japo kweli walikuwa vile lakini bado hawakuweza kumkaribia Mungu, sasa wewe ambaye sasa ni mtu wa mataifa na bado huna habari na Kristo siku ile utaonekania wapi?..Itawezekanikaje kumfikia Mungu, au utamshawishi vipi Mungu hata akusikie maombi yako sasa wewe ambaye unasua sua katika mawazo mawili.

Hujapatanishwa, na Wayahudi, hujapatanishwa na Mungu, bado hujapatanishwa na hayo makao mapya yanayokuja huko mbeleni, unatagemea vipi, Mbingu utaiona ndugu?. Matumaini yako ni nini?, tegemeo lako lipo kwa nani?...
 
Muda umekaribia wa madaraka ya wakati mkamilifu kuanza, Kristo kuvileta vitu vyote pamoja, chini ya mikono ya MUNGU..lakini wale wote wanaopinga, biblia inasema kitakachosalia kwao ni kuangamizwa milele.

Yesu yupo mlangoni ndugu yangu, fanya uamuzi sasa, wakati ndio huu, pokea kuponi yako sasa ya kuwa na uhakika wa maisha baada ya kufa, ulimwengu huu unaousumbukia unakuahidia nini miaka yako 100 mbeleni kama sio ukomo wa mauti?. Kwanini usikubali NEEMA HII YA UPATANISHO inayokuja kwako bure, ingekuwa ni wanadamu ungejaza fomu ngapi ili ukubaliwe tu uwe raia wa taifa fulani?, ungejaza fomu ngapi ili ukubaliwe kuwa mrithi wa taifa fulani?, ungejaza form ngapi ili ufikie tu kigezo cha kumfika raisi wa taifa fulani?. Lakini kwa Mungu haipo hivyo, vyote hivyo ni bure, na vinapatikana hata hapo ulipo sasa hivi.

Chukua maamuzi sasa, kabla ya mlango wa neema kufungwa. Unachopaswa kufanya hapo ulipo ni kutubu kabisa dhambi zako kwa kukusudia kuziacha,..unakusudia kuacha ulevi, anasa, wizi, uasherati uongo, uvaaji usio na maadili, na kila aina ya uchafu, Kisha hatua inayofuata ni kwenda kubatizwa, hakikisha unabatizwa katika ubatizo ulio sahihi wa kimaandiko, yaani ni ule wa kuzamishwa katika maji mengi, na kwa jina la YESU KRISTO, (zingatie hilo uwe ni kwa jina la YESU) sawasawa na maandiko (Matendo 2:38, 8:16, 10:48, 19:5), ili upate ondoleo la dhambi zako. Na baada ya hapo Mungu mwenyewe atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu, atakayekusaidia kushinda dhambi na kukuongoza katika kuijua kweli yote ya maandiko Yohana 16:13.

Na kuanzia hapo utakuwa na nafasi ya kuwa mshirika wa mambo yote ya kimbinguni Mungu aliokusudia kuwafunulia watoto wake.

1Wakorintho 2:9 “lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.”

Ni maombi yangu utafanya hivyo sasa.
 
Tafadhali “SHIRIKI” ujumbe huu na wengine.Bwana akubariki sana.

No comments:

Post a Comment