"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, March 28, 2019

UFUFUO WA UZIMA NA WA HUKUMU.


Shalom, Mtu wa Mungu karibu tujifunze Injili, uweza wa Mungu uuletao wokovu, leo tutajifunza kwa ufupi juu ya NGUVU YA UFUFUO ILIYOPO NDANI YA YESU KRISTO. Katika kitabu cha Yohana tunasoma maneno yafuatayo aliyoyazungumza Bwana Yesu.

Yohana 5: 25 “Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja,na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai.
26 Maana kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake.
27 NAYE AKAMPA AMRI YA KUFANYA HUKUMU KWA SABABU NI MWANA WA ADAMU.
28 Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini WATAISIKIA SAUTI YAKE.
29 Nao watatoka; wale waliofanya MEMA KWA UFUFUO WA UZIMA, na wale WALIOTENDA MABAYA KWA UFUFUO WA HUKUMU”.

Katika mistari hiyo Biblia inasema Mwana kapewa amri na Baba ya kufanya hukumu na tena amepewa uwezo wa kufufua wafu kama vile Baba alivyo na uwezo wa kufufua wafu, tunayasoma hayo juu kidogo katika Yohana 5: 21 “Maana kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na MWANA AWAHUISHA WALE AWATAKAO”.

Kama wengi wetu tunavyofahamu kuwa kuna ufufuo utakaokuja baada ya maisha haya kuisha ambapo wale wote waliotenda haki watafufuliwa na kuurithi uzima wa milele, na wale wote waliotenda mabaya watafufuliwa kwaajili ya hukumu, na kila mmoja atahukumiwa kulingana na matendo yake na wale waovu watatupwa katika lile ziwa la moto, lenye moto usiozimika, waangamie milele.

Sasa jambo la kujiuliza hapa ni kwanini, Bwana Yesu awafufue wale waovu na kisha awahukumu na awatupe katika ziwa la moto…kwanini asingewaacha huko huko mautini, awahukumu huko huko na kuwatupa kwenye lile ziwa la moto wakiwa huko huko mautini, kuna umuhimu gani au haja gani ya wao kufufuliwa na tena wakati kuzimu wataenda tu??.
 
Kuna siri nzito sana hapo. Lakini kwa ufupi ni kwamba, siku ile ya hukumu watu wote waovu watavaa miili yao waliyokuwa nayo hapa duniani..yenye damu na mifupa na macho na moyo, na kusimama mbele za Bwana, na kisha kuongea naye ana kwa ana, kutoa hesabu kwa kila jambo na kila uovu waliokuwa wanaufanya, mbele ya kiti cha Hukumu…Jambo hilo halitafanyika mtu akiwa katika roho, hapana bali litafanyika mubashara kabisa katika mwili kama tulivyo hapa duniani…Na katika ziwa la moto mtu hatatupwa katika roho, bali atatupwa akiwa na mwili wake wa damu na nyama, na utaungua kule na ukiisha ndipo roho itaendelea nayo kuteseka milele kwenye huo moto milele.

Kwahiyo leo hatutaingia sana huko, lakini napenda tujifunze Nguvu ya ufufuo.
Ukiutafakari kwa makini mstari huo utakuja kugundua kuwa Kumbe Ufufuo sio tija. Kwasababu watu wote watafufuliwa, waovu na wema..kinachojalisha ni sababu ya kufufuliwa kwako. Kama mtu alikuwa mcha Mungu basi ufufuo kwake utakuwa wa maana, lakini kama alikuwa mwovu basi ufufuo kwake utakuwa ni laana.

Na ufufuo maana yake, ni “kukirudishia tena uhai au maisha kitu kile kilichokuwa kimekufa”..hiyo ndio maana ya ufufuo.
 
Sasa kuna ufufuo wa roho ambao unaendelea sasahivi, ambapo watu wote WANAISIKIA SAUTI YA MWANA WA ADAMU, na wanafufuka kutoka kwa wafu katika roho…Na sauti ya mwana wa Adamu ni Habari njema inayohubiriwa duniani kote leo, habari za msalaba na wokovu uliopo katika Kristo Yesu, sasa wapo ambao wanafufuka kwaajili ya uzima wa milele na wapo ambao wanafufuka kwaajili ya hukumu.

 
Wako ambao pindi tu wanapoisikia injili macho yao yanafumbuliwa (wanafufuka katika roho), hii inatokea pale ambapo wanachomwa dhamiri zao ndani ya mioyo yao, na kujijua kuwa njia zao sio sawa, hivyo kwa moyo mnyoofu wanaitii injili na kuokoka kikamilifu,wanaacha njia zao mbaya za kale, na kuzaliwa mara ya pili wakati huo huo na kuwa viumbe vipya.

Na wapo pia ambao wanapoisikia tu injili macho yao yanafunguka (wanafufuka) na kujua kabisa ndani ya mioyo yao Neno la Mungu ni kweli, na Roho Mtakatifu anawashuhudia kabisa kuwa Njia ya wokovu ni hii, na njia wanayoiendea wao sio sawa…Roho anawafufua katika roho zao, lakini kwasababu wanapenda giza kulika Nuru wanaikataa ile njia ya kweli,..na kwa makusudi, hawataki kugeuka na kutubu, wanaendelea na njia zao mbaya, hawa ndio wanaofufuliwa sasa kwa ajili ya hukumu. Wanayafumba macho yao kwa makusudi ingawa wamepewa neema ya kuona..Wanafahamu kabisa hata wakifa sasa hivi wanastahili Jeahanum ya Moto, lakini bado hawataki kutubu. Hawa wamefufuliwa kwa ajili ya Hukumu.

Kwahiyo ndugu unayesoma ujumbe huu, usifurahie tu Roho wa Mungu anapokushuhudia ndani yako kuwa KRISTO ndiye njia ya kweli na uzima, huo ni ufufuo tu! Ambao hata waovu wanapewa…hata waovu katika nyakati hizi za mwisho wanapewa neema hiyo mioyoni mwao kujua kuwa Kristo ni njia ya kweli na uzima, na kwamba hakuna uzima wowote nje yake yeye.. Hiyo ni neema ya ufufuo ambayo watu wote wanapewa waovu na wema..Lakini swali ni je! Unafufuliwa kwa sababu gani?.

Kama unaisikia injili kila siku inayokuambia ulevi, uasherati, utukanaji, rushwa,uvaaji mbaya ni dhambi, mustarbation, usagaji, na pornography…na ndani ya moyo wako unajua kabisa ni kweli ni dhambi kufanya mambo hayo..fahamu tu! Ufufuo uliopewa ni wa hukumu na sio wa uzima wa milele, haijalishi unayajua maandiko kiasi gani, au umezungumza na malaika kiasi gani,au umemwelewa Kristo kiasi gani, au umeponywa na Yesu kiasi gani,

Mtume Paulo kwa uwezo wa Roho aliandika habari za watu hawa wafanyao dhambi kwa makusudi huku wakijua kabisa wanayoyatenda sio sawa…Wameisikia injili (wakapata ufufuo katika roho zao)..lakini ufufuo wao ukawa ni wa mauti.

Warumi 1: 18 “Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu.
19 Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, KWA MAANA MUNGU ALIWADHIHIRISHIA.
20 Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; HATA WASIWE NA UDHURU
21 kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.
22 Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika;
23 wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo.
24 Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao.
25 Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina.
26 Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili;
27 wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.
28 Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.
29 Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya,
30 wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao,
31 wasio na ufahamu, wenye kuvunjamaagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema;
32 ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao”.
Unaona Biblia inasema..”kwa maana walipomjua Mungu hawakumtukuza” na inasema “Mungu aliwadhihirishia ndani yao”..ikiwa na maana kuwa watu hawa, nuru ya haki iliwazukia ndani yao, au kwa lugha nyepesi tunaweza kusema ufufuo ulipita ndani ya roho zao, wakaiona kweli na kuiamini lakini walipoiamini hawakuifuata!..Hilo ndio jambo la kuogopesha, mtu anauona ukweli lakini haufuati…Nimewahi kuona madaktari bingwa ambao wanajua elimu yote ya biolojia ya ini na figo, na ni washauri wazuri wa kushauri watu wasitumie pombe na sigara kwani ni hatari kwa afya zao, lakini wao ndio watumiaji wakubwa wa mambo hayo, na wanakufa kwa magonjwa hayo hayo…Na ukiwauliza kwanini wanafanya hivyo na hali wanajua kwa kina na mapana madhara ya hivyo vitu katika mwili, zaidi hata ya watu wengine wanavyojua…wanakujibu basi tu! Nimeamua na nimependa kufanya hivyo, na atazidi kukuambia yupo tayari kufa na wala haogopi.

Sasa watu wa namna hii pia wapo katika Kanisa la Kristo, wanajua kabisa uzinzi ni dhambi, kwamba waasherati wote sehemu yao ni katika lile ziwa la moto, na wengine wamepewa maono na ndoto za jehanamu wameonyeshwa mahali wanawake wanaovaa vimini na suruali walipo lakini hao hao utawakuta wanaendelea kufanya hivyo bila uoga wowote. Ni kwasababu gani wanafanya hivyo? Ni kwasababu wapo katika ufufuo wa hukumu. Mpaka unaweza ukasema kwanini Mungu awafunulie mioyo yao waiamini injili halafu na bado wasiifuate si ni bora asingewapa kabisa neema hiyo..kuliko kuwapa halafu wasiifuate?..Jibu ni rahisi… “kila mtu lazima aisikie sauti ya mwana wa Adamu na kutoka kaburini aliko”.

Kadhalika pia usifurahie kwasababu kazi yako iliyokuwa imekufa ikafufuliwa tena, kwasababu huo unaweza ukawa ni ufufuo wa mauti kwako, furahia kazi yako kufufuka kwa ajili ya ufufuo wa uzima..

Unapokwenda kuombewa kazi yako au afya yako na kupona, na kisha maisha yako hayageuki hata kidogo, zaidi ya yote ndio unakuwa mbaya kuliko ulivyokuwa hapo kwanza, hujisikii vibaya kuendelea na uasherati wako, wala kiburi chako, nataka nikuambie hiyo ni dalili moja wapo ya kazi yako kufufuliwa kwa ajili ya hukumu yako mwenyewe,..hiyo kazi yako yako itakuwa kitanzi kwako cha kukuua na hatimaye kukupeleka katika ziwa la moto…Biblia inasema “…Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza Mithali 1:32”.

Kwahiyo furahia pale kazi yako inapofufuka na kustawi na inazidi kukufanya kuwa mtakatifu na mkamilifu mbele za Mungu, mali zako zinapoongezeka ndipo na kiwango chako cha usafi kinavyozidi kupaa..hapo kazi yako itakuwa imefufuliwa kwa ufufuo wa uzima. Haitakupeleka jehanamu.

Bwana akubariki sana, kama hujampa Yesu Kristo maisha yako…usikawie kawie, kama amezungumza nawe moyoni mwako zaidi ya mara moja na kukushuhudia kuwa njia unayoiendea sio sawa, na wewe mwenyewe umehakikisha jambo hilo moyoni mwako, usijaribu kwenda kutatufa visababu vya kujihalalishia njia zako. Mtii leo, yeye anawakubali wakosaji, na anasamehe dhambi, akikusamehe amekusamehe kweli kweli hana visababu sababu vidogo vidogo vya kukushitaki tena au kukulaumu..Unakuwa mpya kabisa mbele zako.

Waefeso 5.14 “Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza.”

kwahiyo Hapo ulipo tubu, dhamiria kuacha dhambi zote ulizokuwa unazifanya nyuma, Fufuka sasa katika ufufuo wa Uzima katika jina La Yesu, na sio ufufuo wa Mauti, mfanye Bwana kuwa tumaini lako kuanzia leo na kuendelea.. Na baada ya kutubu katafute ubatizo kwani ni wa umuhimu sana kukamilisha wokovu wako na ni maagizo ya Bwana mwenyewe aliyoyatoa kwamba ni lazima kila mtu aliyempokea yeye akabatizwe, na ubatizo sahihi ni wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kulingana na Matendo 2:38, na Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi na kukuongoza katika kuijua kweli yote ya maandiko.

Bwana akubariki.

No comments:

Post a Comment