"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, March 28, 2019

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 58


SWALI 1: Biblia inasema usiape kabisa, lakini ni kwanini watu wanaapa mahakani na katika kufunga ndoa?
JIBU: Ni vizuri kuelewa aina ya viapo mbalimbali vinavyozungumziwa katika biblia, ili usichanganyikiwe unapokutana na baadhi ya vifungu vinavyoonyesha wengine wakiapa lakini Biblia haiwahesabii kosa lolote kwa mfano pale mtume Paulo aliposema.

2Wakorintho 1: 23 "Lakini mimi NAMWITA MUNGU AWE SHAHIDI JUU YA ROHO YANGU, ya kwamba, kwa kuwahurumia sijafika Korintho".

Warumi 1: 9 "Kwa maana Mungu, nimwabuduye kwaroho yangu katika Injili ya Mwana wake, NI SHAHIDI wangu jinsi niwatajavyo pasipo kukoma",

Hivyo kwa maelezo mafupi Vipo viapo vya aina mbili..aina ya kwanza ni viapo vya uaminifu, mfano wa hivi ni maagano au nadhiri.. Kwamfano Nadhiri ni kiapo, kinachomfunga mtu kwa Mungu wake kwamba unakuta mtu anamwambia Mungu ukinitendea hivi nitakutendea hivi, au sitafanya kitu fulani kwa wakati fulani mpaka nimalize kutimiza kusudi fulani..Hivi vyote mbele za Mungu ni viapo, na mtu anafungwa katika hivyo mpaka avitimize, asipovitoa kwake mtu huyo inakuwa ni dhambi.

Hali kadhalika na pale wenzi wawili wanapofunga ndoa mbele za Mungu sawasawa na maagizo yake, moja kwa moja wanaingia katika viapo kwamba hakuna chochote kitakachowatenganisha mpaka kifo kitakapowakuta..Sasa iwe wamekiri hadharani au hawajakiri hadharani, wakishaingia kwenye ndoa tu, tayari maandiko yameshawafunga.

Hali kadhalika na mahakamani au katika mikataba ya kidunia: Ili mtu kujiridhisha na wewe uaminifu wako, huwa unaapishwa, kwamba unalolisema ni kweli, na kwamba utafanya sawasawa na mkataba au makubaliano mliyoingia..Sasa viapo kama hivyo vyote haviji kwa lengo la kujihesabia haki, au kujiona wewe uko sawa mbele za mtu, au kujifanya wewe ni mkamilifu hapana bali ni vya kuthibitishwa tu.

Lakini sasa vipo viapo ambavyo vinakuja nje ya utaratibu wa Mungu, kwa mfano mtu pale anaposema HAKI YA MUNGU vile!!, au naapa juu ya kaburi la babu yangu, au naapa kwa kichwa changu, au naapa juu ya kiti cha enzi cha Mungu, n.k…Unaona Vyote hivi ni viapo vinavyokuja kwa shinikizo fulani, au vinavyotokana na kiburi fulani, na mara nyingi viapo vya namna hii vinatoka katika kinywa cha mtu kwa makosa ya kushutumiwa, na si vinginevyo, hivyo watu wa namna hii mara nyingi hata bila kufikira anatoa maneno makuu kama hayo yaliyovuka mipaka, maneno ambayo hawezi hata kuyasimamia, kwamfano anaposema ninaapa kwa kichwa changu, utadhani kama yeye anajua hata hicho kichwa kiliundwaje undwaje, au mwingine anasema ninapa mbele ya kiti cha enzi cha Mungu utadhani yeye na Mungu ni mtu na mdogo wake, na hivyo ana uwezo sawa au unaokaribiana na Mungu n.k.

Viapo vya namna hii ndivyo Mungu kavikataa kwasababu vinatoka moja kwa moja kwa yule mwovu, Mungu hapendi watu wanaojikweza na wenye viburi..Hivyo mtu akijikuta katika hali kama hiyo ya kushutumiwa hapo maneno yake ndio yanapaswa yawe Ndio ndio, au Siyo siyo.. Basi,

Lakini ikiwa ni kama vitu kama nadhiri, au maagano,au mapatano ya ndoa, au mikataba, au mahakamani..Hayo hayaji kutokana na kushutumiwa au kiburi bali yanakuja kwa lengo la kujiridhisha, kukiri uaminifu wako tu, na si zaidi ya hapo, na hiyo huwa mtu hafikii hatua ya kujikweza au kujihesabia haki, au kujihalalishia mamlaka ya kutendewa alichosema kama imethibitika kuwa hajasimamia alichosema.


 SWALI 2: Mfalme Daudi aliwahesabu wana wa Yakobo apate kujua idadi yao kamili, 1mambo ya nyakati 21:7, jambo lililoonekana chukizo kwa bwana, mpaka kusababisha watu elfu sabini waangamie kwa tauni. SWALI. ni uovu gani hapo Daudi aliufanya ulete madhara hayo yote? au torati ilisemaje kuhusu watu kuhesabiwa?
JIBU: Hakukuwa na uovu wowote mkubwa kivile katika kuhesabu watu, japo Daudi alifahamu hakupaswa kufanya vile kwa wakati ule lakini yeye aliendelea kufanya ndio maana baadaye alikuja kujutia makosa yake, na kumwomba Mungu msamaha!.

Lakini sasa swali linabaki pale pale ni kwanini kwa kosa lake mwenyewe lisababishe zaidi ya watu ya elfu 70 kuangamia kwa tauni? Mpaka kufikia hatua Daudi mwenyewe kumlalamikia Mungu, na kumwambia kwanini unawaadhibu watu wengine wasio na hatia kwa kosa langu mwenywewe? Kwanini Mungu afanye vile? Kwanini awaadhibu na watu wasio na hatia kwa kosa la mwingine?...

Daudi hakufahamu sababu ya Mungu kufanya vile. Sasa ukisoma vizuri biblia, hiyo habari katika kitabu cha Samweli utaona jambo fulani pale la kuzingatia … Tusome

2 Samweli 24: 1 “TENA HASIRA YA BWANA IKAWAKA JUU YA ISRAELI, AKAMTIA DAUDI NIA JUU YAO, akisema, Nenda, ukawahesabu Israeli na Yuda. 2 Basi mfalme akamwambia Yoabu, jemadari wa jeshi la askari, waliokuwa pamoja naye, Zunguka sasa katikati ya kabila zote za Israeli, tangu Dani mpaka Beer-sheba, mkawahesabu watu, nipate kujua jumla ya hao watu”.

Unaona hapo ukisoma mstari wa kwanza utaona, kuna jambo wana wa Israeli walilifanya hapo kabla mpaka kupelekea hasira ya Mungu kuwaka juu yao..Kama ukisoma huko nyuma utagundua kuwa Mungu alikuwa hapendezwi na njia zao tangu siku nyingi, na ndio maana wakati mwingine alikuwa anawatia katika mikono ya wafilisti, na hapa pia vivyo hivyo, kuna mambo maovu walikuwa wanayafanya pengine kwa siri au hadharani (japo biblia haijaeleza hapo ni mambo gani) lakini ni dhahiri kuwa matendo yao yalimudhi Mungu sana, mambo kama kuabudu miungu migeni, rushwa, kudhulumu watu, mauaji yasioyo na hatia, kuhalifu sabato, kupitisha wana wao motoni, kuwaonea wajane na mayatima ni miongoni mwa vitu walivyokuwa wanavifanya wana wa Israeli kwa wakati ule..Hivyo Mungu akaamua kumtumia Daudi nia kama sababu ya kuwaadhibu makosa yao… Na ndio hapo tunakuja kuona Daudi anaingiliwa na shetani kufanya vile, kama tu vile Mungu alivyotaka kumwangamiza mfalme Ahabu akaruhusu Pepo la uongo likawavae wale manabii wake 400, kadhalika na Daudi naye aliingiwa na shetani kufanya mambo ambayo Mungu hakumwagiza , na baadaye tunaona tauni inakuja kuachiliwa juu ya Israeli ili Mungu kujilipizia kisasi juu yao wote waliomuudhi..

Hivyo wakati mwingine hata sisi kama taifa au mtu binafsi, tunaweza kufanya makosa, na Mungu akakusudia kutuadhibu kwa kupitia viongozi wetu, na ndio hapo unaweza kushangaa viongozi wanaonyesha tabia za ajabu kwetu au kwako, anakuwa mkatili au dikteta,sisi tukidhani kuwa yule kiongozi ndio kakengeuka, lakini kumbe nyuma yake ni Mungu kasimama kumruhusu kwa makusudi kabisa mtu yule atumiwe na ibilisi ili au kutufundishwe sisi adabu. Mfano unaweza kuona Mfalme Nebkadneza alikuwa ni diktekta, aliteka mataifa yote ulimwenguni kwa nguvu na akayatawala kwa mabavu..na hata Taifa la Mungu Israeli liliwekwa chini wa utawala wa Nebkadneza lakini ukiisoma biblia kwa makini utaona kuwa Mungu ndiye aliyemtia Nebkadneza nia ya kwenda kuteka mataifa yote ulimwenguni pasipo hata yeye Nebkadneza kufahamu chochote…Na Mungu alifanya vile ili kujilipizia kisasi kwa mataifa yote yaliyomwacha ikiwemo na Taifa la Israeli watu wake.

Hivyo tunapaswa tuwe makini na njia zetu tumwombe Mungu kila siku..Ili wengine wasifanyike kuwa fimbo ya Mungu kutuadhibu sisi.
SWALI 3: Baba mmoja Ananisimulia akisema, "Mimi hapa huwa ninasikia watu wanaosema wanakuja kunikamata.akaniuliza je! Na wewe unawasikia? Nikamwambia hapana mimi siwaskii[saa hiyo ni yeye tu anawaskia]. Akanichukua akanishika mkono Akaniambia"Unaskia hiyo nyimbo yangu wanaimba?(Mimi siisikii yeye peke yake anasikia)"Nikamwambia hapana" ANAOGOPA SANA. Sasa Juzi juzi Usiku nikamkuta amesimama hapa nje nyumbani kwetu Akiwa ameshika panga mkononi mwake akaniambia "Unamsikia bibi mmoja kule ng'ambo anasema nimebaka mjukuu wake[Kwa bibi huyo ni mbali na hapa kwetu]?"Nikamwambia hapana.Akarudi nyumbani na panga lake.[Wakati huo anaongea yuko siriazi kabisa].Wakati mwingine ananiambia aliowaona watu wamesimama mlangoni kwake.

Sasa Swali:Ndugu kwa nyinyi Muonavyo Hicho ni kitu gani?? KARIBUNI___ [Nilijaribu kumueleza habari ya kumpa Bwana maisha akasema ATAPAMBANA KIJESHI[Nilijuwa anamaanisha kwa waganga],Lakini namuona sasa hawezi kupambana kijeshi alivyosema].Hali yake inazidi kuongezeka Ikifika mahali Si ajabu akawa kichaa kabisa.
JIBU: Shalom, Mambo yanayoendelea katika roho ni mengi, na shetani naye kila kukicha anaongeza mapana ya maarifa yake…mtu akizama katika maarifa ya shetani (mfano uchawi)..anakuwa anauwezo wa kufanya vitu ambavyo kwa namna ya kawaida haviwezekani kufanyika…sasa kwa mtu kama huyo aliyekuja kukusimulia kuwa anasikia sauti za nyimbo, na ana uwezo wa kusikia mtu akizungumza akiwa mbali, ni wazi kuwa kuna roho ipo ndani yake na hiyo ni roho ya yule adui.

Kwanini ni roho ya adui, na si ya Mungu? kwasababu matunda ya hiyo roho ni ya yule adui, kumpeleka kwenye uovu na kumweka katika vifungo vya uoga,wasiwasi na mkandamizo… Kwasababu matunda ya Roho Mtakatifu sio hayo…ingekuwa ni Roho Mtakatifu yupo ndani ya huyo mtu ungeona matunda ya Roho ndani yake kama yalivyoandikwa kwenye kitabu cha Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”

Umeona hapo? Roho Mtakatifu akiwa ndani ya mtu hivyo vitu hapo juu lazima vionekane, amani, furaha,upendo n.k…Lakini roho iliyopo ndani ya huyo mtu haijamsukuma kwenye upole, wala haimpeleki kwenye furaha, wala uvumilivu, wala amani…zaidi ya yote umempeleka kwenye hofu, mashaka na ghadhabu…hivyo hiyo ni moja kwa moja roho ya yule mwovu ipo ndani yake.

Sasa Roho Mtakatifu akiwa ndani ya mtu huwa ni lazima atoe na kipawa fulani juu ya huyo mtu, ndio hapo anawapa wengine vipawa vya unabii, wengine lugha, wengine miujiza,ishara,uchungaji, ualimu,uinjilisti n.k [kumbuka vipawa vya Roho ni tofauti na matunda ya Roho].

kadhalika na roho za mashetani ni hivyo hivyo, mtu akiwa na pepo fulani la utambuzi, ni lazima litampa uwezo fulani,(ni kama karama yake fulani hivi) watu wengine shetani anawapa uwezo wa kufanya utambuzi, wanakuwa na uwezo wa kutambua siri za watu, au kuona vitu vinavyoendelea sehemu nyingine mbali na mahali walipo, hata wakati mwingine wanakuwa na uwezo wa kusikia sauti na mazungumzo ya watu waliopo mbali kama huyo mzee, wengine wanakuwa na uwezo wa kufanya viishara ishara fulani (mazingaumbe mazingambwe) wengine wanakuwa hawana huo uwezo lakini wanakuwa wanauwezo mwingine mkubwa wa ushawishi…wanaweza kumshawishi mtu au jamii na wakafanikiwa kuleta vitu vyenye madhara kwa kutumia hivyo vipawa walivyonavyo vya nguvu za giza.

Kwahiyo kwa habari ya huyo mzee ni kwamba kafungwa na nguvu za giza, aidha kwa kujua au kwa kutokujua, na kwasababu hamjui Yesu Kristo, inawezekana yeye akajihisi anakipawa kutoka kwa Mungu cha uwezo wa kujua na kuwasikia maadui zake mahali walipo, lakini ni roho ya adui ipo ndani yake, pasipo yeye kujijua,hivyo nakushauri, tenga muda umhubirie injili, ili macho yake ya rohoni yafumbuke,umweleze uwezo uliopo katika Yesu Kristo, na tumaini lililopo ndani ya Yesu Kristo, na Bwana akimpa Neema ya kuamini injili na kuipokea, mwekee mikono na kumwombea kwa Jina la Yesu na hizo roho zitamwacha atakuwa huru kabisa. Na akizingatia kutubu kwa kuacha dhambi zake kabisa na kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi, basi Bwana atampa kipawa cha Roho wake Mtakatifu kwasababu yeye mwenyewe alisema ahadi hiyo ni kwa watu wote waliompokea..Na akiisha pokea Roho Mtakatifu basi yale matunda ya Roho yataambata naye..atapata amani isiyokuwa ya kawaida, furaha ya ajabu, upendo wa ajabu, uvumilivu usioelezeka, upendo usiokuwa na mipaka na fadhili nyingi.

Bwana akubariki

No comments:

Post a Comment