"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, April 1, 2019

MWILI NA DAMU YA YESU KRISTO.


Shalom, karibu katika kujifunza Neno la Mungu, ambapo leo tutajifunza juu ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu…kama maandiko yanavyotuambia.. “tumfahamu sana mwana wa Mungu hata kufikia cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo Waefeso 4:13. Yaani kwa lugha rahisi ni kwamba “tunapaswa tumfahamu na kumwelewa Yesu Kristo mpaka kufikia kile kiwango ambacho yeye anataka sisi tumfahamu”…Ndio jukumu pekee tulilopewa hapa duniani, Ili kwamba tusipelekwe na kuchukuliwa na kila aina ya upepo wa elimu zilizozagaa za kidini.

Kwahiyo kuna umuhimu sana wa kumwelewa Yesu Kristo, ni dhahiri kuwa usipomwelewa mtu fulani, huwezi kutembea naye, wala huwezi kuishi naye…hata mazungumzo yenu mnaweza msielewane au mkapishana. Kila mmoja asielewe nia ya mwenzake ni ipi hiyo ni kwasababu hamfahamiani. Na kwa Yesu Kristo ndio hivyo hivyo tusipomwelewa vizuri tutapishana naye tu kwa kila kitu.

Kuna maneno mengi ambayo Bwana Yesu aliyaongea ambayo pasipo Roho kumjalia mtu kuyaelewa, kamwe hatayaelewa na mwisho wa siku ataishia kutafsiri kwa akili tu.

Kwamfano kuna mahali Bwana Yesu alimwita Herode Mbweha.
 
Luka 13: 32 “Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika”.

Kwa sentensi hiyo ni rahisi kusema Bwana kamtusi Herode, Nimewahi kukutana na watu wanasema Bwana alimtusi Herode, na hivyo Mungu gani anatukana.

Kadhalika kuna mahali Bwana alisema..

Luka 14.25 “Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia, 26 Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”.
 
Kwa maneno hayo, pasipo msaada wa Roho, unaweza ukasema Bwana anahalalisha chuki kwa wazazi na ndugu.
 
Sentensi nyingine tena ya Bwana yenye utata mkubwa ni pale aliposema maneno haya
Yohana 6:52 “Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi MWILI wake ili tuule?
53 Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.
54 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.
55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.
56 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake.”

Kwa maneno hayo, hata wewe unaweza ukasema Bwana anahalalisha unywaji wa damu..na ulaji wa nyama ya mtu.
Na yapo maneno mengine mengi sana, katika maandiko ambayo pasipo msaada wa Roho-Mtakatifu ni rahisi kutafsiri kivingine..

Lakini hebu tuzichambue baadhi ya hizi sentensi kwa ufupi kisha tujifunze kitu..

Pale Bwana alipomwita Herode Mbweha..hakumaanisha kumtusi kwamba Herode ni Mbweha..kama sisi wanadamu tunavyotukanana na kuvunjiana heshima…Hapana Bwana alimwita Herode Mbweha kufunua tabia yake ya ndani..tabia yake ya ndani ya kurarua na kuwinda vitu vidogo vidogo aliifananisha na Mbweha, kwasababu Mbweha ndio anatabia hizo…Kwahiyo alikuwa anaangalia tabia ya rohoni ya Herode na kuifananisha na aina Fulani ya mnyama…Ndio maana yeye Bwana mwenyewe pia alijifananisha na Mwana-kondoo na sio tu yeye alijifananisha na mwana-kondoo bali hata Yohana Mbatizaji alimwita Bwana Yesu “mwana-kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu”…Yohana alimwita Bwana kondoo kwa kuiona tabia ya Bwana ya Upole kama kondoo na ya unyenyekevu….sasa kama Bwana alimtukana Herode na yeye mwenyewe atakuwa anajifanyaje?..maana kama ni matusi basi ni heri uitwe Mbweha kuliko kondoo..wafugaji wanawaelewa kondoo walivyo..Nimewahi kukutana na mfugaji mmoja akaniambia mtu anitukane matusi yote duniani, lakini asiniite mimi kondoo…kwao ni kama tusi kubwa sana.

Tukirudi kwenye mfano wa pili Bwana alisema… “mtu akija kwangu naye hamchukii Baba yake na Mama yake hawezi kuwa mwanafunzi wangu”..Na sentensi hii pia ni sentensi yenye utata sana..lakini Hebu tafakari…Inawezekanaje Bwana Yesu aseme sehemu moja, “wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi”…halafu na hapa ajisahihishe tena aseme “mtu akija kwangu ahakikishe amemchukia Baba yake na Mama yake”..unaona hiyo inawezekana kweli??..Ni dhahiri kuwa haiwezekani kwasababu Bwana Yesu hawezi kusema hapa hivi na baadaye ageuke aseme vile…kwasababu yeye sio kigeugeu..Kwahiyo hapo Bwana alikuwa haizungumzii chuki ya kuwachukua wazazi au ndugu, hapana bali chuki inayozungumziwa hapo ni chuki ya mapenzi ya wazazi..mfano mzazi mapenzi yake ni wewe usimfuate Bwana, hayo mapenzi unapaswa uyachukie…mzazi mapenzi yake ni wewe kuwa mlevi na mtu wa kidunia vuguvugu, mapenzi yake ni wewe uwe mganga, au mvaaji kama wanawake wa kidunia, hayo mapenzi ndio ya kuyakataa, na kuyafuata mapenzi ya Mungu, na kwa kuyakataa ndio kuyachukia kwenyewe huko.

Lakini sio kwenda kumtukana mzazi, au kumchukia kabisa na kukataa kuongea naye na kumwekea uadui…hapana hiyo sio maana yake..Tunapaswa tuwapende wazazi na kuwaombea…lakini kuna mipaka ya uhusiano wetu na Mungu, wasiyopaswa wao kuyaiingilia.

Na tukimalizia na huo mfano wa Mwisho Bwana aliousema Mtu asipoula mwili wangu na damu yangu hana uzima ndani yake hapa ndipo kiini cha somo letu kilipo…Hapo Bwana hakuhalalisha tukamshike na kumchinja na kuila nyama yake na kuinywa damu yake kama wachawi wanavyofanya..
 
Hapana bali alimaanisha kuula mwili wake katika roho na kuinywa damu yake katika roho kama yeye alivyosema…

Kwasababu katika roho tunakula na kunywa kama tunavyokula na kunywa katika mwili.. Na hivyo kumla Bwana Yesu Kristo ni KUYASIKIA MANEO YAKE NA KUYAAMINI NA TAFAKARI MANENO YAKE, NA KUYAISHI..na maana ya kuinywa damu yake ni KUTAFAKARI UWEZO ULIOPO KATIKA DAMU YAKE NA KUUTUMIA.. Hiyo ndiyo maana ya kuula mwili wa Yesu na kuinywa damu yake…Na kwa nje tunashiriki kama ishara tu! Ambayo ndio ule MKATE na DIVAI. Ambao ni ishara tu ya nje kuelezea mlo unaoendelea rohoni.

Sasa hata leo wapo watu wanaokula nyama ya Bwana Yesu na kuinywa damu yake, hao ndio wale watu wanaojifunza Neno lake na kulitafakari usiku na mchana na kuishi katika hilo na kuna watu wanakula nyama za watu wengine na kuna wengine wanakula nyama za miili yao wenyewe..Kama tulivyotangulia kusema…nyama ya mwili wa Bwana Yesu ni MANENO YAKE, kadhalika nyama za watu wengine ni Maneno ya hao watu…Na nyama za mtu binafsi ni maneno yake mwenyewe.

Kuna kipindi mwanzoni mwanzoni tu wakati nimempa Bwana maisha yangu..kuna vitu nilikuwa navitafakari halafu navipatia majibu mwenyewe pasipo kutumia mrejesho wa Biblia..Ilikuwa hivyo tu, na nilikuwa nayaamini majibu yangu zaidi kuliko kitu kingine..Na kwasababu nilikuwa bado ni mchanga kiroho, nilikuwa sielewi hata namna ya kuisikia sauti ya Mungu, wala kuithibitisha..Kwahiyo ilikuwa nikisoma mstari mmoja kwenye maandiko nilikuwa nauchukua huo na kuutafakari kwa jinsi niuelewavyo na kisha kuupatia tafsiri..

Siku moja usiku nilisoma mstari mmoja katika kitabu cha Mwanzo, na kuupatia tafsiri mwenyewe na kuiamini hiyo tafsiri nikaenda kulala…Usiku nikaota ndoto nimekaa kwenye kiti halafu miguu yangu ipo kwenye sufuria inayotokota maji….sasa wakati ile miguu yangu inachemka kule majini nilikuwa sisikii maumivu hata kidogo, na maji yale yalikuwa yamechemka mpaka miguu imekuwa meupe, na kuna mtu nilikuwa kama naongea naye mbele yangu ninayemfahamu…wakati tunaongea nikajikuta kama kuna sahani imeletwa mbele yangu yenye nyama..nikawa nakula zile nyama…na nikataka kama kumkaribisha Yule mtu niliyekuwa naongea naye..kabla hajaanza tu na yeye kuila ile nyama.. nikaangalia chini..nikaja kugundua kuwa zile nyama nilizokuwa ninazila zilikuwa zinatoka kwenye miguu yangu mwenyewe hiyo iliyokuwa inachemka hapo chini..na nilikuwa nimeshaanza kuila nakaribia kuimaliza..nikaacha!. Na ghafla nikashtuka usingizini…Nikawa natafakari maana ya ndoto hiyo nikiwa pale pale kitandani, Niliogopa sana.

Wakati naitafakari hiyo ndoto Nikasikia kama maelezo Fulani yamekuja kichwani yanayosema “nisizifuate akili zangu bali niliangalie Neno la Mungu”…Saa hiyo hiyo nikapata tafsiri ya ile ndoto nikikumbuka na mistari niliyokuwa nasoma jana usiku ambayo nilijitengenezea tafsiri yake mwenyewe…Kuwa ile nyama niliyokuwa naila ni nyama ya mwili wangu mwenyewe..Na kama unavyojua mtu ukijikata mguu na kuula, na ukajikata mkono nakuula maana yake, ni unajimaliza mwenyewe na mwishowe utakufa…Kwahiyo siku hiyo ndio nikaelewa madhara ya kuyafuata na kuyaamini maneno yangu mwenyewe ambayo hayana mrejesho wa kutosha kwenye maandiko…mwishoni yataniletea mauti ya kiroho. Nikamshukuru Mungu kwa kunionyesha hilo, Kwahiyo nikabadilika kuanzia siku hiyo na kuanza kuisoma biblia kwa undani sana…kitabu kwa kitabu, sura kwa sura, Kabla ya ufunuo wowote kuuamini ni lazima niuhakiki kwenye maandiko kwa nguvu zote, na niwe na mistari ya kutosha kuisimamia Roho Mtakatifu akiwa ni msaidizi wangu wa pembeni..Na nikaja kuelewa kuwa nilikuwa najipoteza mwenyewe, kwa kujiaminisha mwenyewe na mitazamo yangu..Nikaja kugundua nilivyokuwa nawaza ni tofauti kabisa na Maneno ya Mungu..ingawa katika kile kipindi nilikuwa najiona nipo sawa..

Kwahiyo ndugu Maneno ya Yesu Kristo ndio maneno ya Uzima, yanayotupa afya mwilini mwetu. Tunapoula mwili wake (Maneno yake) na Damu yake ipasavyo ndivyo tunavyojiongezea afya katika roho zetu, na tusipoula mwili wake na damu yake ndivyo tunavyojidhoofisha wenyewe kwasababu yeye mwenyewe anasema… “AMIN, AMIN, NAWAAMBIENI, MSIPOULA MWILI WAKE MWANA WA ADAMU NA KUINYWA DAMU YAKE, HAMNA UZIMA NDANI YENU”…Na zaidi ya yote unapotegemea maneno yako mwenyewe ndivyo unavyojimaliza mwenyewe na mwishowe utakufa…

Ifuatayo ni mifano michache tu ya mtu anayekula nyama ya mwili wake mwenyewe.(mawazo yake).

1) Imani ya kuamini kuwa Mungu hawezi kuiteketeza dunia na watu wote hawa..ndugu hiyo ni unajilisha nyama ya mwili wako mwenyewe.
 
2) Imani ya kuwa utakwenda mbinguni kwa kutenda mema tu pasipo kumwamini Bwana Yesu Kristo.
 
3) Imani ya kuwa ubatizo ni ubatizo tu, uwe wa maji mengi au machache haujalishi.
 
4) Imani ya kuwa siku moja Mungu atamsamehe shetani.
 
5) Imani ya kuwa hakuna Mungu wala shetani.
 
6) Imani ya kuwa Mungu haangalii mavazi yangu wala mwonekano wangu bali anaangalia roho yangu peke yake.
 
7) Imani ya kuwa Yesu Kristo harudi leo wala kesho, 
 
8) Imani ya kuwa hakunaga Jehanum ya moto mtu akifa amekufa tu.
 
9) Imani ya kuwa Biblia ni kitabu kilichotungwa na wanadamu. N.K
 
10) Imani ya kujiona wewe huna dhambi nyingi sana kustahili kuzimu kama yule.

Na unapotegemea maneno ya watu wengine ambao Hawamhubiri Kristo katika utimilifu wa Neno lake, ndivyo unavyokula nyama zao zilizotengenezwa kuzimu…Na mwisho wa siku unazizoelea hata unapoletewa chakula cha kweli cha uzima (yaani maneno ya Yesu Kristo) hutaki tena kusikia..Kwasababu umenenepeshwa kwa nyama hizo.

Na ifuatayo ni baadhi tu ya mifano ya Nyama zinazotengenezwa kuzimu watu wanazolishwa pasipo wao kujijua.

1) Ibada za Sanamu, hizo ni nyama kutoka kwa Yule adui…haihitaji mtu awe mchawi ndio ale nyama hiyo..Ibada hizo tu tayari ni uchawi.
 
2) Mafundisho ya kwenda toharani ni nyama za Yule adui. Watu wanalishwa mchana na usiku.
 
3) Ubatizo wa vichanga ni nyama za Yule adui.
 
4) Mafundisho ya ndoa za Mitara (mwanamume mmoja wake wengi).
 
5) Mafundisho yasiyolenga utakatifu wala Toba, badala yake yanalenga tu mafanikio na elimu za kichawi…Ni nyama za Yule adui. N.k.

Kwahiyo ndugu yangu kama umeshalishwa NYAMA zozote za aina hiyo, zieupuke sasa, na kama hujampa Yesu Kristo maisha yako, Nakushauri ufanye hivyo leo, kabla wakati wa hatari haujafika..Na yeye anakupenda na hataki upotee ndio maana anakuhitaji leo utubu, akupe uzima wa Milele. Akupa chakula chake cha uzima bure. Akupe mwili wake na damu yake halisi…Na sio nyama za mashetani.

Hivyo unachopaswa kufanya ni KUTUBU KWANZA KWA KUDHAMIRIA KUACHA DHAMBI Zako zote. Unadhamiria kuacha uasherati, uwongo, ulevi, rushwa, pornography, wizi, uvaaji mbaya, utukanaji, utoaji mimba, anasa na mambo yote uliyokuwa unayafanya yasiyompendeza Mungu, Na baada ya kufanya hivyo nenda ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kimaandiko wa kuzamishwa mwili wako wote kwenye maji na kwa jina la YESU KRISTO kulingana na (Matendo 2:38, 8:16, 10:48, na 19:5,) ili upate ondoleo la dhambi zako..Na kisha Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi na kukuongoza katika kuijua kweli yote ya kimaandiko..

Usikubali kulishwa nyama za watu wengine watakaokuambia utaokoka siku ile tu pasipo Yesu Kristo, au wanaokuambia kwamba ubatizo sio wa muhimu..Wala usikubali kula nyama za mwili wako mwenyewe zinazosema hakuna Mungu, wala hakuna jehanum,wala Yesu Kristo harudi..

Badala yake uule mwili wa Yesu Kristo unaosema… “Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa Luka 16:16” na unaosema “ Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu upamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. 13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho”.
Ufunuo 22:16 “Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung'aa ya asubuhi. 17 Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure”.

Bwana akubariki sana.

No comments:

Post a Comment